Presha Gavana Joho aseme Shahbal tosha

Na FARHIYA HUSSEIN

GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho, ana mtihani mgumu kuhusu chaguo lake la mrithi wa kiti hicho mwaka 2022.

Kwa muda mrefu Bw Joho amekuwa mwandani wa Mbunge wa Mvita, Abdulswamad Nassir, anayemezea mate kiti hicho.

Hata hivyo, idadi ya wandani wake wanaohamia upande wa mfanyabiashara Suleiman Shahbal, imeibua maswali kuhusu msimamo halisi atakaochukua.

Bw Joho amepanga kujitosa katika siasa za kitaifa atakapokamilisha kipindi chake cha pili cha ugavana mwaka ujao.

Imebainika kuwa madiwani wa chama cha ODM ambao wanaegemea upande wa gavana, wameanza kumuegemea Bw Shahbal.

Awali, kikundi cha wataalamu na washauri wa kisiasa Pwani, ambao walishirikiana na Bw Joho miaka iliyopita, pia walikuwa wameelekeza macho yao kwa Bw Shahbal.

Taifa Leo imebaini kuwa madiwani hao wa ODM wanaonyesha nia ya kutaka kufanya kazi na Bw Shahbal kuelekea uchaguzi mkuu.

Kati ya wawakilishi 41 wa wadi akiwemo Spika wa Bunge la Kaunti ya Mombasa, ni watatu pekee ndio walichaguliwa kupitia tiketi isiyo ya ODM.

Mmoja ni wa Ford Kenya, mwingine wa Wiper na wa tatu alichaguliwa kama mgombeaji wa kujitegemea.

“Wengi wetu wanamuunga mkono Bw Shahbal kuwania kiti cha ugavana. Tunataka kiongozi atakayeendeleza miradi iliyoanzishwa na Bw Joho, si anayetafuta huruma kwa umma,” akasema mmoja wa madiwani, ambaye aliomba jina lake kufichwa.

Alizidi kusema kuwa kwa sasa bado ni mapema Bw Joho kutangaza msimamo wake kwani mawimbi ya kisiasa yangali yanabadilika, lakini akiwa tayari atafanya hivyo.

Maoni yake yaliungwa mkono na wanachama wengine wa ODM katika bunge hilo, ambao walidai kuwa tayari wamewasilisha chaguo lao kwa gavana huyo.

Katika miezi michache iliyopita, Bw Joho ameanza pia kuonekana akiwa karibu na Bw Shahbal, kuliko awali walipokuwa mahasimu wakubwa kisiasa.

Mfanyabiashara huyo anaonekana kuungwa mkono na asilimia kubwa ya madiwani kuliko mbunge wa Mvita, Bw Nassir.

Hali hii huenda ikamweka pazuri Bw Shahbal endapo kutakuwa na kura ya mchujo kuamua mpeperushaji bendera ya ODM katika kinyang’anyiro cha ugavana Mombasa.

Bw Shahbal alishindwa kupata kiti hicho katika chaguzi mbili zilizopita, alipowania kupitia chama cha Wiper mwaka 2013 na Jubilee mwaka 2017.

Alitangaza kuhamia ODM hivi majuzi. Msimamo wa madiwani wa Mombasa umezidisha idadi ya wandani wa Bw Joho ambao wanazidi kuvutia upande wa Bw Shahbal.

Mapema 2021, ilifichuka kuwa wanasiasa waliohusika pakubwa katika kampeni za Gavana Joho wakati wa chaguzi zilizopita, tayari wamejiunga na kikosi cha kampeni za Bw Shahbal.

Miongoni mwao ni meya wa zamani wa Mombasa, Ahmed Mohdhar, mshauri wa kisiasa wa Gavana Joho, Idris Abdirahman, pamoja na aliyekuwa mbunge wa Kisauni, Rashid Bedzimba.

Nassir na Shahbal walilia ‘tosha’ ya Raila uagavana Mombasa

VALENTINE OBARA na ANTHONY KITIMO

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, alikwepa kumwidhinisha mwanasiasa yeyote kuwania ugavana Mombasa kupitia chama hicho mwaka ujao alipozuru kaunti hiyo.

Wanasiasa wawili wanaomezea mate tikiti ya chama hicho kuwania ugavana Mombasa mwaka ujao walionekana kuzidisha juhudi za kusaka ‘baraka’ za Bw Odinga.

Wawili hao ambao ni Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir na mfanyabiashara Suleiman Shahbal, walionekana kung’ang’ania sikio la Bw Odinga alipozuru kaunti hiyo Alhamisi.

Bw Nassir na Bw Shahbal hawakukutana ana kwa ana hadharani katika hafla mbili ambazo Bw Odinga alihudhuria akiandamana na Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho.

Hafla ya kwanza ambayo Bw Odinga alihudhuria ilikuwa ni uzinduzi wa kituo cha mafuta cha Hass katika mtaa wa Nyali, ambapo Bw Shahbal alikuwepo.

Baada ya kuandamana kwa karibu katika uzinduzi huo, wawili hao walienda kufanya mkutano wa faragha nyumbani kwa Bw Shahbal katika mtaa huo.

Ingawa waliyozungumzia hayakuanikwa wazi, duru ziliambia Taifa Leo kwamba, Bw Odinga alimwahidi Bw Shahbal kutakuwa na kura ya mchujo kwa njia ya haki na uwazi kuamua watakaopewa tikiti ya chama kuwania viti vyote vya kisiasa.

Baadaye, katika hafla ya kuzindua kitengo maalumu cha matibabu ya moyo katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Pwani, Bw Odinga alikumbwa na shinikizo kutoka kwa umati uliokuwa ukimrejeaja Bw Nassir kama ‘gavana mtarajiwa.’

Ingawa Bw Joho ndiye alikuwa mwandalizi wa hafla, Bw Nassir ndiye alitembea na waziri huyo mkuu wa zamani sako kwa bako walipowasili katika hafla hiyo. Bw Joho aliwafuata kwa karibu kutoka nyuma.

Katika hotuba yake, Bw Odinga alimtambua tu Bw Nassir kama mbunge mahiri ambaye amechangia mengi hasa katika wadhifa wake wa uenyekiti katika kamati ya bunge ya kuchunguza matumizi ya fedha za umma.

“Nataka kutoa shukrani kwa mbunge wa hapa kwa kazi anayofanya kufichua ufisadi katika bunge. Tunataka wabunge wetu waendelee kufanya kazi yao,” akasema Bw Odinga, huku mbunge huyo akisimama kando yake. Bw Nassir alisema kila mtu yuko huru kujiunga na ODM Mombasa lakini ana matumaini makubwa kwamba wapigakura watamchagua yeye kurithi kiti cha Bw Joho.

“Tumeona baadhi ya watu waliokuwa wakikashifu ODM katika uchaguzi uliopita wakirudi kutafuta kiti cha ugavana. wajue mimi ndiye nitakuwa gavana Mombasa” alisema Nassir.

Shahbal aonekana kufaidika na siasa za kumrithi Joho

Na MOHAMED AHMED

SIASA za urithi wa kiti cha Gavana wa Mombasa Hassan Joho zimeonekana kuchukua mkondo tofauti ambao unaonekana kumfaidi mfanyabiashara Suleiman Shahbal ambaye anawinda kiti hicho mwaka 2022.?

Kufikia sasa, kiti hicho kimevutia wagombeaji kadha wakiongozwa na Bw Shahbal pamoja na mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir ambao ndio wameonekana kuwa washindani wa juu zaidi.

Wawili hao wote wanatarajia kupata kuidhinishwa na Bw Joho wakati uchaguzi huo utakuwa unakaribia mnamo 2022.? Licha ya Bw Joho kuonyesha dalili kuwa atamuunga mkono Bw Nassir, watu wake wa karibu ambao wamehusika katika mipango yake ya siasa wameonekana kuelemea upande wa Bw Shahbal, hatua ambayo inaibua masuali mengi kuliko majibu.

Miongoni mwa watu hao wa karibu wa Bw Joho ni washauri wa kisiasa wa gavana huyo akiwemo Rashid Bedzimba ambaye alikuwa mbunge wa Kisauni na aliyekuwa mshauri wa Bw Joho, Idriss Abdurahman ambaye sasa ni mshauri wa masuala ya usalama katika afisi ya gavana.

Bw Bedzimba ambaye ana ushawishi wa kutosha katika eneo bunge la Kisauni alipanga mkutano na viongozi wa kampeni zake na kuwakutanisha na Bw Shahbal.

Hatua hiyo ni baada ya kubainika kuwa Bw Abdurahman naye ndiye aliyechukua uongozi wa mipango ya kampeni ya Bw Shahbal.? Kwa upande Bw Bedzimba analenga kumkusanyia Bw Shahbal kura za Kisauni kulingana na ufuasi alionao.

Bw Bedzimba amehudumu eneo bunge hilo kwa zaidi ya miaka 15 kama diwani na mbunge.? Hata hivyo, mwaka 2017 alipoteza kiti hicho kwa mbunge wa sasa Ali Mbogo ambaye kwa sasa analenga kiti cha ugavana.

Aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar pia analenga kiti hicho.? Siku za hivi karibuni, ni Bw Shahbal na Bw Nassir ambao ndio wameonekana kuzunguka zaidi kuuza sera zao mapema kwa wananchi.

Akizungumza katika ukumbi wa Sheikh Zayed eneo la Bombolulu baada ya kukutana na wafuasi hao wa Bw Bedzimba, Bw Shahbal alisema kuwa ana matumani kuwa kushikana na Bw Bedzimba kutamuezesha kunyakua kiti hicho cha ugavana.

Alisema pamoja watapigana na changamoto za utovu wa usalama, utumizi wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana na ukosefu wa kazi.

“Nataka kumshukuru Bw Bedzimba kwa nafasi hii ya kunikutanisha na majemedari wake. Mimi nawaomba tushikane mkono ili tuhudumie watu wetu wa Kisauni na Mombasa kwa jumla tukiwa pamoja,” akasema Bw Shahbal.

Bw Bedzimba kwa upande wake alisema kuwa ameaumua kumuunga mkoni Bw Shahbal kwa sababu miongoni mwa wale wote ambao wanataka kuwania kiti hicho yeye yupo mbele.

Alimtaja Bw Shahbal kuwa kiongozi mwenye maono na mwenye azma ya kuhudumia wakazi wa Mombasa kwa hali na mali..? ? ? “Mimi madhali alikuja akaniomba anataka kukutana na nyinyi nikasema tumpe nafasi. Kwa sababu hata tukiangalia kwa wote wale ambao wanataka kiti hicho Bw Shahbal yupo mbele yao tayari,” akasema Bw Bedzimba.

Hayo yalijiri huku mbunge wa Mvita Bw Nassir akionekana kuondeleza siasa zake katika maeneo bunge ya Kisauni, Nyali na Changamwe.? ? ? Bw Nassir amekuwa akifanya mikutano na kujipigia debe ili apate nafasi hiyo baada ya kumaliza hatamu yake kama mbunge wa Mvita.

Aidha, mbunge wa Kisauni Ali Mbogo naye ameonekana kushikilia siasa za mashinani ambapo amekuwa akiendesha kampeni zake za kiti cha ugavana.

Ikiwa imesalia zaidi ya mwaka mmoja, wandani wa masuala ya siasa wanatazama iwapo wale ambao wameanza mapema siasa zao watatoboa hadi mwisho wa ushindani huo wa mwaka 2022.

Hii pia ni kwa sababu inatarajiwa kuwa kutaibuka wawaniaji wengine katika kumezea mate kiti hicho.? ? Ikisubiriwa hilo, kwa sasa viongozi waliopo wamepata wasaa wa kujipigia debe na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kupata kiti hicho ifikapo mwaka wa uchaguzi.

Shahbal atetea mikutano na Raila, alenga ugavana 2022

Na MOHAMED AHMED

MFANYABIASHARA wa Mombasa, Bw Suleiman Shahbal ametetea mikutano yake ya mara kwa mara na Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga.

Huku akithibitisha azimio lake kuwania ugavana Mombasa katika uchaguzi ujao, Bw Shahbal ambaye ni mwanachama wa Jubilee alidai kwamba mikutano hiyo huwa ni ya kimaendeleo wala si kujiandaa kisasa.

“Kwa sababu ya umoja wa viongozi wetu, mimi huenda kumuona kwa sababu ya mipango ya maendeleo. Hii ni fursa ya kukutana na kiongozi kama yeye,” akasema.

Mkutano wao wa hivi karibuni ulikuwa wiki iliyopita ambapo alimtembelea Bw Odinga afisini mwake.

Kulingana na wadokezi wetu, Bw Shahbal anatazamiwa kuingia kwenye muungano wowote ambao utasimamiwa na Bw Odinga ifikapo mwaka wa 2022.

Endapo atapitishwa na Bw Odinga, inaaminika Bw Shahbal atapata mwanya mkubwa kushinda kiti hicho. Anatazamiwa kupambana na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir na mwenzake wa Kisauni Ali Mbogo.

Bw Nassir amekuwa mwandani wa kisiasa wa Gavana Hassan Joho kwa muda mrefu lakini kwa miezi kadhaa sasa, Bw Shahbal pia ameonekana akinyemelea upande wa Bw Joho.

“Mwaka wa 2022 bado uko mbali. Kwa sasa kiti hicho kina mwenyewe ambaye ni Gavana Joho, kwa hivyo ni lazima tushirikiane naye kwa ajili ya kaunti yetu,” akasema Bw Shahbal.

Alikuwa akizungumza katika Shule ya Spaki ambao alizindua mradi wa masomo.

“Tusiweke kaunti hii katika hali ya kampeni wakati kampeni bado hazijafika. Kwa sasa ni ushirikiano wa maendeleo ndio muhimu. Siasa bado miaka miwili ijayo,” akasema Bw Shahbal.