LEONARD ONYANGO: Wakuu wa shule waliotafuna mabilioni wachukuliwe hatua

Na LEONARD ONYANGO

HATUA ya wizara ya Elimu kuanzisha mchakato wa ‘kurejesha’ kimya kimya mabilioni ya fedha zilizotumwa kwa wanafunzi na shule hewa kati ya 2008 na 2018, inafaa kushutumiwa vikali.

Katibu wa wizara ya Elimu Julius Jwan, wiki iliyopita alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PCA), alikiri kwamba wizara ya Elimu ilituma mabilioni ya fedha kwa wanafunzi na shule zisizokuwepo.

Dkt Jwan alisema hali hiyo ilisababishwa na hatua ya wakuu wa shule pamoja na wakurugenzi wa elimu kutoa taarifa za kupotosha kuhusu idadi ya wanafunzi ili kujipatia fedha za wizi.

Ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali iliyotolewa miezi mitatu iliyopita ilifichua kuwa wizara ya Elimu ilituma zaidi ya Sh3.7 bilioni kwa wanafunzi na shule hewa katika miaka ya fedha ya 2017/2018 na 2018/2019.Wakuu waliongeza idadi ya wanafunzi ili kujipatia fedha za bwerere.

Ripoti za kupotosha kutoka kwa wakuu hao wa shule ziliidhinishwa na wakurugenzi wa elimu wa kaunti kabla ya kutumwa kwa wizara ya Elimu.Shule ya zaidi ya 2,600 zilinufaika na fedha hizo za bwerere ambazo ziliishia katika mifuko ya wasimamizi wa shule.

Jumla ya Sh105.9 milioni za bwerere zilitumwa kwa wanafunzi hewa katika shule 331 za sekondari za umma katika mwaka wa fedha wa 2018/2019.Ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ilionyesha kuwa Sh369 milioni zaidi zilitolewa kwa shule 99 za msingi katika kaunti 13 mwaka huo.

Dkt Jwan aliambia Kamati ya PCA kwamba, wizara ya Elimu imefanikiwa kurejesha jumla ya Sh21.1 milioni tangu 2019.

Mfumo wa NEMIS

Kulingana na Dkt Jwan, ilikuwa vigumu kwa wizara ya Elimu kuthibitisha idadi ya wanafunzi shuleni kwani wakati huo hakukuwa na Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Elimu (Nemis) unaotumiwa sasa.

Katibu huyo wa Wizara alimbia wabunge kwamba shule zilizopokea fedha za ziada zimekuwa zikikatwa kutoka katika mgao wao.Kupunguza mgao wa shule hizo zilizotumiwa fedha za ziada kunamaanisha kwamba wanafunzi ndio wanaumia.

Haifai kwa wizara ya Elimu kuadhibu wanafunzi ilhali waliohusika na ujanja huo ni wasimamizi wa shule na wakurugenzi wa elimu.

Wakuu wa shule walioongeza idadi ya wanafunzi ili kujipatia fedha za ziada kwa maslahi yao ya kibinafsi wanapaswa kukamatwa na kufikishwa kortini.

Wakurugenzi wa elimu walioidhinisha shule hewa kutumiwa fedha pia hawana budi kuadhibiwa kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao na kufanya walipa ushuru kupoteza mabilioni ya fedha.

Wizara ya Elimu inastahili kuripoti uhalifu huo kwa Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi (EACC) na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) badala ya kujaribu kurejesha fedha hizo kimya kimya huku wahusika wakiponda raha na fedha za wizi.

Shule yakosa kupata wanafunzi wa kidato cha kwanza

Na BRIAN OJAMAA

Huku wanafunzi wa kidato cha kwanza wakiendelea kuripoti katika shule walizoitwa, shule moja katika Kaunti ya Bungoma haijasajili hata mwanafunzi mmoja.

Shule ya sekondari ya Mikokwe iliyo Kaunti-ndogo ya Bumula, Bungoma, haijapokea mwanafunzi yeyote wa kidato cha kwanza.

Shule hiyo ilitengewa wanafunzi watatu pekee na Wizara ya Elimu ambao walitarajiwa kujiunga nayo kuanzia Jumatatu.

Hata hivyo, watatu hao hawajaripoti katika shule hiyo ambayo ilianzishwa zaidi ya miaka saba iliyopita.Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Dickens Lumati aliambia Taifa Leo kwamba huenda kutengewa wanafunzi watatu kulitokana na makosa kwa kuwa ina uwezo wa kuwa na wanafunzi wengi.

“Ni wanafunzi watatu pekee waliopewa nafasi katika shule yetu na wote hawajaripoti,” alisema.

Mwalimu huyo mkuu alisema kwamba anahofia huenda shule hiyo haitakuwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka huu.

Alisema mmoja wa wanafunzi watatu waliotakiwa kujiunga na shule hiyo alipewa nafasi hiyo kimakosa kwa kuwa anatoka eneo la Webuye Mashariki ilhali shule ni ya kutwa na iko mbali na nyumbani kwao.

“Sidhani ataripoti. Ni vigumu kuwa na mwanafunzi wa kutwa anayesafiri zaidi ya kilomita 80,” alisema Lumangati.

Alisema shule hiyo ina uwezo wa kuwa na wanafunzi 60 wa kidato cha kwanza lakini kufikia Ijumaa hakuna hata mmoja aliyekuwa ameripoti.Shule hiyo ina walimu sita walioajiriwa na TSC huku wengine wakiwa wameajiriwa na bodi.

Huu ni mwaka wa nne shule hiyo kuwa na watahiniwa katika mtihani wa KSCE.Katibu Mkuu wa tawi la Bungoma Kusini la chama cha walimu Kenya (Knut) Ken Nganga alilaumu mfumo wa Wizara ya Elimu wa kuteua wanafunzi wa kidato cha kwanza akisema unafaa kunyooshwa ili changamoto zilizoshuhudiwa mwaka huu zisirudiwe mwaka ujao.

Alisema mfumo wa zamani ambao wanafunzi walikuwa wakiitwa shule walizochagua unafaa kurudiwa.

Nganga alisema kwamba katika mfumo wa sasa wa kidijitali, wanafunzi wengi waliitwa shule za kutwa za mbali ambazo hawawezi kujiunga nazo.

Alisema baadhi ya wanafunzi waliopata alama nzuri waliitwa katika shule ndogo. Pia, alikosoa kuanzishwa kwa shule bila mpango mzuri.

Shule nyingi zilianzishwa na CDF bila kuzingatia umbali na baadhi ya zilizoko kwa sasa zitakabiliwa na tatizo kama hilo,” alisema.

Covid-19: UN yarai mataifa kuanza kufungua shule zao

Na AFP

GENEVA, Uswisi

UMOJA wa Mataifa (UN) umezirai nchi ambazo bado zinaendelea kufunga shule kutokana na janga la virusi vya corona kuzifungua, ili kuwaruhusu wanafunzi kurejelea masomo yao.

Umoja huo ulisema kuwa hali hiyo inawaathiri zaidi ya watoto 600 milioni kote duniani, ikivuruga pakubwa mpangilio wa masomo yao.

“Hali haiwezi kuendelea namna hii,” akaeleza James Elder, ambaye ndiye msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Maslahi ya Watoto (UNICEF) kwenye kikao na wahahabari jijini Geneva, Uswisi.

Ingawa alikubali nchi nyingi zinakabiliwa na wakati mgumu kufanya maamuzi kuhusu njia za kukabili janga hilo, alieleza “shule zinapaswa kuwa taasisi za mwisho kufungwa na za kwanza kufunguliwa.”

Alisema ni makosa kwa nchi kufungua upya baa na vituo vya burudani kabla ya kufungua shule.

“Si lazima walimu na wanafunzi wote kupewa chanjo ndipo shule ziweze kufunguliwa,” akasema.

Alizirai nchi kutopunguza fedha zinazoitengea sekta ya elimu licha ya changamoto za kiuchumi zilizosababishwa na janga hilo.

Barani Ulaya, wanafunzi wengi wako likizoni. Hata hivyo, inakisiwa kuwa karibu nusu ya wanafunzi wote katika maeneo ya mashariki na kusini mwa Afrika wamo majumbani mwao kutokana na athari za janga hilo.

Kijumla, zaidi ya watoto 32 milioni wanakisiwa kuwa nyumbani katika maeneo hayo baada ya shule kufungwa kutokana na athari zinazohusiana na janga hilo.

Nchi nyingi zimekuwa zikilazimika kufunga shule mara tu baada ya kiwango cha maambukizi kuanza kuongezeka.

Hilo linaifanya hali hiyo kudorora kwani kabla ya janga kutokea, ilikisiwa watoto karibu 37 milioni hawakuwa wakienda shuleni licha ya kufikisha umri unaohitajika.

Katika bara Asia na eneo la Pacific, shule katika eneo hilo zimefungwa kwa zaidi ya siku 200 kutokana na janga hilo.

Katika eneo la Amerika Kusini na Carribean, nchi 18 zimefunga shule zake ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

“Kutokana na hali hiyo, nchi sasa zimelazimika kukabili visa vya ghasia za kinyumbani, hali ya wasiwasi na ongezeko la mimba za mapema miongoni mwa wasichana,” akasema Elder.

Alitoa mfano wa Uganda, ambapo kati ya Machi 2020 na Juni 2021, taifa hilo lilirekodi ongezeko la karibu thuluthi moja ya mimba za mapema miongoni mwa wasichana walio kati ya umri wa miaka 10 na 24. Kulingana na shirika hilo, idadi kubwa ya wanafunzi hawawezi kumudu gharama za kushiriki masomo kwa njia ya mtandao.

CHARLES WASONGA: Walimu wakuu wanaoendelea kutoza ada za ziada waadhibiwe

Na CHARLES WASONGA

NIMEWAHI kuandika mara si moja katika safu hii kwamba ni haki ya kila mtoto nchini kupata angalau elimu ya msingi. Elimu hii inaaza kutoka kiwango cha chekechea hadi kile cha shule ya upili.

Kwa hivyo, kuwa mujibu wa kipengele cha 43 (f) cha Katiba ya sasa, ni wajibu wa serikali kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata haki hii.

Hii ndio maana serikali imeanzisha, na inafadhili, sera mbalimbali katika sekta ya elimu kama vile elimu bila malipo katika shule za msingi na kupunguzwa kwa gharama ya elimu katika shule za upili.

Isitoshe, serikali inatekeleza sera ambapo wanafunzi wote waliofanya mitihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) wanapata nafasi ya kujiunga na shule za upili bila kuwekewa vizingiti kama alama duni au ukosefu wa karo.

Muhimu zaidi ni kwamba serikali imeweka viwango vya karo ambavyo vinapaswa kutozwa wanafunzi katika viwango mbalimbali vya shule za upili, ili kukinga wazazi dhidi ya kupunjwa na walimu wakuu walaghai.

Kwa hivyo, ningependa kumhimiza Waziri wa Elimu George Magoha kuwachukulia hatua kali zaidi walimu wakuu wanaokiuka mwongozo wa karo uliotangazwa na wizara yake mapema mwezi jana.

Kulingana na mwongozo huo wazazi ambao watoto wao wanasomea shule za upili za kitaifa watalipa Sh45,000 kwa mwaka na wale ambao watoto wao wanasomea shule za upili ngazi za kaunti na kaunti ndogo wanapaswa kulipa Sh35,000 katika mwaka ujao wa masomo.

Hii ni kwa sababu muhula ujao umepunguzwa kutoka wiki 39 hadi 30 kutokana na janga la Covid-19.Lakini kuna walimu wengine wakuu ambao tayari wameanza kukiuka mwongozo huu kwa kutoza ada zaidi haswa kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza watakaoripoti shuleni kuanzia Agosti 2, 2021.

Wanatoza kati ya Sh5,000 na Sh35, 000 kama ada ya kufadhili ujenzi wa miundo msingi, bila idhini ya wizara ya elimu inavyohitaji kisheria.

Haitoshi kwa Katibu wa Wizara ya Elimu Dkt Julius Jwan kuwaonya walimu wakuu kama hawa au kuwashauri wazazi kutolipa ada hizo, bali awasimamishe kazi, kwa muda, walimu wakuu kama hawa ili iwe funzo kwa wengine wenye nia ya kushiriki uovu kama huo.

Isitoshe, walimu wakuu kama hawa wanafaa kushtakiwa kwa ukiukaji wa Katiba kwani kitendo hicho cha kuwatoza wanafunzi ada hizo za ziada kinahujumu haki ya wanafunzi, hususan kutoka jamii masikini kupata elimu, kulingana na kipengele cha 43 cha Katiba.

Aidha, kinaathiri sera ya serikali ya kuhakikisha kila mwanafunzi anajiunga na shule ya msingi.

Mbunge aitaka serikali ijenge shule zilizozama

Na FLORAH KOECH

MBUNGE wa Baringo Kusini Charles Kamuren ameitaka serikali itoe pesa za ujenzi wa shule sita mpya ambazo zilisombwa na maji ya mafuriko mwaka 2020.

Shule hizo zilisombwa baada ya Mto Baringo kuvunja kingo zake na sasa zitajengwa upya katika ardhi nyingine ambayo ishatolewa na jamii ya eneo hilo kwa hiari.

Kando na shule, vituo vya kiafya, masoko, makanisa na makazi ya zaidi ya watu 10,000 pia yalisombwa na maji.

Zaidi ya shule 15 ziliathiriwa na mafuriko hayo na sasa wanafunzi kutoka shule hizo wamejiunga na wenzao kutoka shule jirani.

Kati ya shule za upili zilizosombwa ni Salabani, Ng’ambo Girls’ na shule ya mseto ya Lake Baringo. Shule za msingi za Ng’ambo, Sintaan, Leswa, Lorok,Loruk, Loropil, Noosukro, Kiserian, Loruk,Ilng’arua, Ng’enyin, Sokotei na Salabani pia zilisombwa na maji hayo ya mafuriko.

Shule hizo zilifaa kujengwa upya na serikali lakini hadi sasa bado hilo halijafanyika huku Bw Kamuren akisema kwamba shughuli za masomo zinaendelea kutatizika.

Bw Kamuren alisema hali itakuwa mbaya mno wanafunzi wa kidato cha kwanza wakitarajiwa kuripoti shuleni mnamo Julai.

“Naomba serikali itoe fedha kwa ujenzi upya wa shule zilizosombwa na maji ya mafuriko. Kwa sasa wanafunzi wanasomea mazingira magumu na hali itakuwa mbaya zaidi wakati wanafunzi wa kidato cha kwanza wataripoti shuleni,” akasema Bw Kamuren.

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo serikali iliahidi kutoa Sh10 milioni kwa ujenzi wa shule za upili na Sh5 milioni kwa ujenzi wa shule za msingi.

“Bado hatujapata fedha zozote kutoka kwa serikali mwaka moja baada ya ahadi hiyo kutolewa. Tumetumia pesa kidogo kutoka kwa Hazina ya Maeneobunge (NG-CDF) kujenga madarasa machache. Wanafunzi wetu hawawezi kuendelea kusomea chini ya miti,” akaongeza Bw Kamuren.

Taifa Leo ilibaini kwamba vyandarua ambavyo vilikuwa vimetolewa na Shirika la Msalaba Mwekundu sasa vimeraruka na havisaidii sana kuwakinga dhidi ya mvua na jua kali.

Kamishina wa Kaunti ya Baringo Henry Wafula alithibitisha kwamba pesa za kujenga upya shule hizo zinatolewa hivi karibuni.

“Serikali bado ilikuwa kutathmini hali na kukadiria gharama ya ujenzi. Pesa hizo zitatolewa hivi karibuni ila kwa sasa wanafunzi wanaweza kuendelea kusomea katika shule jirani,” akasema Bw Wafula.

Uteuzi wa Kidato cha Kwanza waahirishwa

Na DAVID MUCHUNGUH

WANAFUNZI waliofanya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) mnamo Machi mwaka huu, watalazimika kusubiri zaidi kabla ya kujua shule za upili watakazojiunga nazo.

Matokeo ya uteuzi wa wanafunzi watakaojiunga na shule mbalimbali za sekondari yalifaa kutolewa Ijumaa wiki hii, lakini imeahirishwa kwa wiki mbili hadi Juni 15.

Watahiniwa 1,179,192 waliofanya KCPE wamekuwa wakingoja kwa hamu kujua shule watakazojiunga nazo.

Wakati wa hotuba yake alipokuwa akitangaza matokeo ya KCPE Aprili 15, Waziri wa Elimu Profesa George Magoha alisema kuwa wanafunzi wangejua shule za sekondari watakazojiunga nazo Mei 28. Lakini jana, Prof Magoha hakutoa sababu zozote za kuahirisha shughuli hiyo.

“Wizara ya Elimu inaendelea na mchakato wa kuwapangia wanafunzi shule za sekondari watakazojiunga nazo. Matokeo ya mchakato huo yatatangazwa Juni 15. Nawahakikishia kuwa watahiniwa wote waliofanya mtihani huo watajiunga na shule za upili,” akasema Waziri Magoha.

Kuahirishwa huko kumepokelewa kwa hasira na wazazi wa watahiniwa hao,

“Hatujaridhishwa na hatua hiyo ya Prof Magoha. Tumekuwa tukingojea matokeo ya uteuzi wa wanafunzi ili tujue hatua inayofuatia. Hata wanafunzi waliofanya mtihani watakumbwa na msongo wa mawazo.

“Wanafunzi wanataka kujua shule watakazoenda. Waziri alifaa kutoa sababu kuhusu hatua ya kuahirisha shughuli hiyo,” akasema Bi Catherine Muthoka, mzazi kutoka jijini Nairobi ambaye bintiye anasubiri kujiunga na Kidato cha Kwanza.

Maafisa wa Wizara ya Elimu wako mjini Naivasha ambako wamekuwa wakifanya kazi ya kuhakikisha kuwa watahiniwa wote wanajiunga na shule za sekondari.

Wanafunzi watapangiwa shule kulingana na alama walizopata na shule ambazo wanafunzi walichagua kabla ya kufanya mtihani wa KCPE.

Prof Magoha mwezi uliopita alisema kuwa mfumo unaotumiwa kuwapangia watahiniwa shule ni wa kuaminika na uteuzi huo utakuwa huru na haki.

Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza na Darasa la Kwanza wanatarajiwa kuanza masomo yao Julai, kwa mujibu wa kalenda mpya ya masomo.

Kumekuwa na madai kuwa baadhi ya wazazi wamekuwa wakijaribu kutoa hongo kuwezesha watoto wao waliopata alama za chini kujiunga na shule za kitaifa.

MARY WANGARI: Wazazi watumie likizo kuwapa watoto malezi bora

Na MARY WANGARI

SHULE nyingi zilifunguliwa jana baada ya wanafunzi kuwa nyumbani kwa likizo ya zaidi ya mwezi mmoja.

Hata hivyo, wanafunzi wa madarasa mengine wakirejea shuleni, wenzao wa Gredi ya Nne watasalian nyumbani hadi Julai. Waliofanya mtihani wa Darasa la Nane piawatakuwa nyumbani wakisubiri kujua shule watakazopata ili kujiunga na elimu ya sekondati.

Hali hii ya kuwa na baadhi ya wanafunzi ambao watakuwa nyumbani wenzao wakiendelea na masomo, limeibua wasiwasi na minung’uno miongoni mwa wazazi na walezi.

Hii ni baada ya kuzuka kwa janga la Covid-19 ambalo lilivuruga mifumo ya elimu duniani huku wanafunzi nchini Kenya wakilazimika kukaa nyumbani kwa kipindi cha miezi 10.

Likizo hiyo ndefu haikukosa madhara yake huku ikiacha athari za kudumu kwa baadhi ya watoto.Kuanzia matumizi ya mihadarati, kujihusisha na ngono, mimba za mapema, hadi uhalifu, ni miongoni tu mwa maovu yaliyojitokeza katika likizo hiyo.

Baadhi wakiwa wamekata tamaa ya kurejea shule, wengine walianza kusaka riziki na hata kugeukia uendeshaji bodaboda na kuzika elimu katika kaburi la sahau.

Kwa wengine, hasa wasichana, ndoto ya kurejelea masomo yao ilitokomea kabisa huku wakiwa wahasiriwa wakuu wa dhuluma za kingono, mimba na ndoa za mapema.

Pia kulikuwa na athari za kiafya na kisaikolojia kutokana na watoto kutumia muda mwingi wakitazama televisheni, mitandao ya kijamii badala ya kucheza na kutangamana na wenzao.

Si ajabu kwamba wazazi na walezi wanahofia kuwa athari hizo huenda zikajitokeza tena kwa wanafunzi walioagizwa kuendelea kukaa nyumbani kwa muda zaidi.

Hata hivyo, kipindi cha likizo vilevile kina manufaa yake hasa kwa kuimarisha uhusiano kati ya wazazi na watoto wao.Kando na kukatiza shughuli za elimu, likizo ndefu iliyosababishwa na virusi hatari vya corona, ilidhihirisha wazi jinsi wazazi walivyotelekeza majukumu yao ya malezi na kuwaachia walimu kazi yote.

Si ajabu basi baadhi ya wazazi na walezi waligutushwa na uhalisia mchungu kwamba hawafahamu chochote kuhusu watoto wao wenyewe.

Matokeo yake yalikuwa kuongezeka kwa visa vya utovu wa nidhamu kwa watoto na visanga vya kila aina vilivyowaacha Wakenya vinywa wazi.

Likizo hutoa fursa muhimu kwa wazazi kuwa kielelezo bora kwa watoto wao, kuwashauri na kuimarisha uhusiano kati yao kwa kushiriki muda pamoja.

Pamoja na kuwasaidia kudurusu masomo waliyofunzwa shuleni, wazazi pia wanaweza kuwasaidia kujihami vilivyo kukabiliana na maisha kwa jumla kwa kutumia maarifa na tajriba zao binafsi.

Changamoto tele wanafunzi wakirejea shuleni

WANDERI KAMAU na FLORAH KOECH

WANAFUNZI wa shule za sekondari nchini wanarejea shuleni Jumatatu kwa muhula wa tatu, huku changamoto tele zikiendelea kuandama sekta ya elimu.

Licha ya serikali kutoa hakikisho kwamba kila kitu ki shwari, uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kuwa, shule nyingi katika sehemu tofauti nchini bado hazijajitayarisha kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa corona.

Kiwango cha maambukizi ya virusi hivyo nchini kingali zaidi ya asilimia tano. Katika baadhi ya maeneo, shule zina miundomsingi duni, uhaba wa walimu, ukosefu wa fedha kuziwesha kuendesha shughuli zake za kila siku na mafuriko makubwa.

Kwa mfano, katika Kaunti ya Baringo, hatima ya zaidi ya wanafunzi 4,000 haijulikani kutokana na ongezeko la visa vya ukosefu wa usalama.

Zaidi ya visa kumi vya mashambulizi vimeripotiwa katika eneo la Baringo Kusini kwa mwezi mmoja uliopita, ambapo watu wawili waliuawa.Miongoni mwa shule za msingi zilizoathirika ni Mukutani, Arabal, Kapindasum, Kasiela, Sinoni, Chebinyiny, Chemorong’ion, Noosukro, Sokotei na Kiserian katika eneo la Baringo Kusini.

Zingine ni Kagir, Yatya, Chemoe, Chepkesin, Barketiew, Kesumet, Kosile, Kapturo na Ng’aratuko katika eneo la Baringo Kaskazini.Hayo yanatokea wakati waziri wa Elimu, Prof George Magoha, anashikilia kuwa walimu wakuu hawapaswi kutoa visingizio vyovyote kuhusu changamoto zinazowaathiri, kwani serikali tayari ishatuma Sh7.5 bilioni kwa shule za msingi na upili za umma kuziwezesha kuendesha shughuli muhimu shuleni mwao bila matatizo yoyote.

“Tumeweka mikakati ya kutosha kuhakikisha wanafunzi wetu hawakabiliwi na matatizo yoyote wanaporejea shuleni,” akasema Profesa Magoha Ijumaa.

Licha ya waziri kusisitiza fedha hizo zimetumwa katika akaunti za shule, walimu wakuu waliozungumza nasi walisema bado hawajapokea fedha hizo na itawabidi kungoja ili kuona ikiwa zitatumwa kama alivyoahidi Waziri.

Serikali pia inakabiliwa na kibarua cha kuhakikisha walimu wote wamepewa chanjo dhidi ya virusi vya corona, ikizingatiwa kufikia sasa, ni nusu pekee ya walimu waliopewa chanjo hiyo.

Shule za kibinafsi zalalamikia ubaguzi

Na WANDERI KAMAU

CHAMA cha Wamiliki wa Shule za Kibinafsi nchini (KPSA) kimelalamika kuwa wanafunzi katika shule hizo walibaguliwa kwenye zoezi la kusahihisha Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) mwaka uliopita.

Chama hicho kilisema uchunguzi wake umebaini kulikuwa na ubaguzi mkubwa kwenye matokeo hayo, kwa kuwa, yalitofautiana sana na utaratibu ambao kimekuwa kikitumia kutabiri matokeo hayo katika miaka ya awali.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana, mwenyekiti wa chama hicho, Bw Steve Odero, alisema wanahofia huenda mapendeleo hayo yakajitokeza tena kwenye mchakato wa kuwateua wanafunzi watakaojiunga na Kidato cha Kwanza baadaye mwezi huu.

Bw Odero alisema ni makosa kwa Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, kuwatofautisha wanafunzi wa shule hizo na zile za kibinafsi, akisema hilo linajenga taswira isiyofaa miongoni mwao.

“Ni wazi kulikuwa na mapendeleo makubwa kwenye utoaji wa matokeo ya mtihani wa KCPE mwaka uliopita. Kwa miaka mingi, tumekuwa tukitumia utaratibu maalum kubashiri vile wanafunzi wetu watakavyofanya mitihani yao ya kitaifa. Hata hivyo, hali ilikuwa kinyume mwaka huu, kwani utabiri wetu ulitofautiana kabisa na matokeo yaliyotolewa. Tunahofia huenda ubaguzi huo ukaendelezwa hata katika Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE),” akasema.

Kwenye matokeo ya KCPE mwaka uliopita, wanafunzi wa shule za umma walifanya vyema ikilinganishwa na wenzao katika shule za kibinafsi, hali ambayo imeendelea kuzua hisia miongoni mwa wadau wa elimu. Kwa mfano, miongoni mwa wanafunzi 15 bora nchini, kumi kati yao walitoka katika shule za umma, huku shule za kibinafsi zikiwa na wanafunzi watano pekee.

Taswira hiyo ni kinyume na miaka ya awali, ambapo shule za kibinafsi zimekuwa zikishikilia nafasi bora kitaifa, ikilinganishwa na wenzao katika shule za umma.

Ili kuhakikisha matakwa yake yanashughulikiwa ifaavyo, chama kililishinikiza Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNUT) kuwajumuisha wawakilishi wake kwenye bodi yake. Bw Odero alisema ni hatua hiyo pekee itakayohakikisha wana usemi wa kutosha katika masuala yanayohusu uendeshaji na usimamizi wa mitihani.

Sossion aililia serikali shule zifunguliwe Mei

Na CHARLES WASONGA

KATIBU Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) Wilson Sossion ameiomba serikali kuruhusu kufunguliwa kwa shule mnamo Mei 10, ilivyoratibiwa licha ya serikali kuweka masharti mapya ya kudhibiti msambao wa corona.

Akiongea Jumatatu asubuhi katika runinga ya Citizen TV Bw Sossion alisema kalenda ya masomo iliyotangazwa na Wizara ya Elimu Desemba, 2020 haifai kuvurugwa na vikwazo vipya vilivyotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta kuzuia maambukizi ya Covid-19.

“Tunaomba serikali kuweka mipango itakayohakikisha kuwa utaratibu wa masomo hautavurugwa tena. Tunahimiza kwamba kufikia Mei walimu watakuwa wamepewa chanjo na shule kufunguliwa. Hatutaki watoto kukaa nyumbani kwa muda mrefu zaidi kama ilivyokuwa mwaka jana ambapo wengine waliathirika pakubwa,”akasema.

“Hata ikiwezekana likizo ya wakati huu inafaa kufupishwa ili watoto warejee shuleni ili watoto wasiathirike na maovu ya kijamii yanayosababishwa na marufuku dhidi ya corona,” Bw Sossion ambaye pia ni Mbunge Maalum wa chama cha ODM.

Katibu huyo Mkuu wa Knut alielezea matumaini kuwa kufikia mwezi Mei, serikali itakuwa imelegeza masharti ya kudhibiti corona iliyoweka juzi kabla ya tarehe ambayo shule zinapaswa kufunguliwa.

Mnamo Ijumaa, Rais Uhuru Kenyatta alitoa maagizo mapya na makali ya kuzuia msambao wa corona ambapo aliamuru kusitishwa kwa masomo katika taasisi zote za masomo nchini.

Aidha, aliweka marufuku ya watu kuingia na kuondoka kaunti tano ambazo zimeshuhudia idadi ya juu ya maambukizo ya corona, miongoni mwa masharti mengine. Kaunti hizo ni Nairobi, Machakos, Kiambu, Kajiado na Nakuru.

Shule za bweni zipigwe marufuku – Kuppet

GEORGE SAYAGIE na GERALD BWISA

CHAMA cha kutetea Masilahi ya Walimu wa Shule za Upili na Vyuo (KUPPET) jana kiliendeleza wito wake wa kutaka shule za mabweni zipigwe marufuku.

Mwenyekiti wa chama hicho Omboko Milemba alisema hiyo ndio mojawapo ya njia za kukomesha visa vya fujo na utovu wa nidhamu shule.Akiongea baada ya kushuhudia uchaguzi wa tawi la Narok la Kuppet, Bw Milemba pia aliitaka serikali kusambaza vifaa kwa usawa shuleni ili kusawazisha viwango vya elimu.

“Shule za mabweni zinafaa kupigwa marufuku na vifaa viwe katika shule zote ili mwanafunzi wa hapa Narok aweze kufaidi sawa na mwenzake katika Shule ya Upili ya Alliance,” akasema Milemba ambaye pia ni Mbunge wa Emuhaya.

Alisema hayo wakati ambapo visa vya wanafunzi kuteketeza shule vimekuwa vikiongezeka, wakilenga mabweniBw Milemba pia aliitaka Tume ya Huduma za Walimu (TSC) kupandisha vyeo walimu wote waliohitimu huku akilitaka bunge kutenga fedha nyingi kwa tume hiyo.

“TSC pia inahitaji fedha zaidi ili iweze kuajiri walimu watakaotekeleza Mtaala Mpya wa Umilisi na Utendaji (CBC),” akasema.

Wakati huo huo, polisi katika kaunti ya Trans Nzoia wanawazuilia wanafunzi 14 kwa tuhuma za kuteketeza mabweni mawili wakitaka waruhusiwe kwenda nyumbani kuleta karo.

Kulingana na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Wasichana ya Heart Girls iliyoko kaunti ndogo ya Saboti, Bi Rosemary Bor, alipata habari saa sita za usiku kwamba mabweni mawili yalikuwa yakichomeka..

“Hapo kwa hapo nilipasha habari maafisa wa polisi. Walimu, wanafunzi na wanakijiji walijaribu kuzima moto huo lakini ukawalemea,” akasema Bi Bor.

Wazima moto kutoka serikali ya kaunti ya Trans Nzoia na maafisa wa polisi ndio walifaulu kuuzima moto huo.Malazi na mali nyingi ya wanafunzi iliharibiwa kabisa.

Katika kaunti ya Makueni, wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Makueni walimjeruhi mwalimu wao mkuuu Raphael Katana, walipozua fujo Ijumaa usiku.Kufuatia kisa hicho shule hiyo imewaagiza wanafunzi wote 258 wa kidato cha nne waende nyumbani kwa wiki mbili kutoka nafasi kwa uchunguzi kuhusiana na kisa hicho, akasema Bw Katana.

Hofu wanafunzi hawavai maski wakiwa shuleni

Na WAANDISHI WETU

WANAFUNZI wameacha kuvalia barakoa wakiwa shuleni au kuzivaa visivyo hatua ambayo inawaweka katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona.

Baadhi yao wanabadilishana barakoa zao. Jambo hili limeanza kuwatia wasiwasi wazazi.Hii ni tabia ya kushtua wakati ambao takwimu za wizara ya afya zinaonyesha kuwa katika muda wa wiki mbili sasa, kiwango cha maambukizi ya corona kinaongezeka nchini.

Uchunguzi wa Taifa Leo umeonyesha kuwa baadhi ya wanafunzi pia wanavaa barakoa chini ya kidefu na wengine wanabadilisha zao.Wataalamu wa afya wanasema tabia hii inaweza kusambaza virusi.

Kulingana na kituo cha kudhibiti kusambaa kwa magonjwa (CDC), kuambia wanafunzi wavae barakoa si sawa na wao kuzivaa kwa njia inayofaa.

“Barakoa inafaa kufunika pua na mdomo vyema hadi chini ya kidefu. Watoto wanaweza kuvaa barakoa moja siku nzima isipokuwa ipate unyevu au kuchafuka. Hata hivyo, wote wanafaa kuwa na barakoa mbili na wazazi wanafaa kununua barakoa maalumu kwa watoto,” ripoti ya kituo hicho inasema.

Ripoti hiyo inaeleza kwamba watoto wanaweza kupata dalili zisizo kali za corona au kutopata dalili na kwa hivyo kuna haja yao kuvalia barakoa wakiwa karibu na watu.

Mnamo Alhamisi mwanafunzi wa shule ya msingi katika kaunti ya Nairobi alienda nyumbani akivalia barakoa ya mwanafunzi mwingine.

Alipoulizwa kiini, alimwambia mama yake kwamba alibadilishana na rafiki yake ambaye rangi ya barakoa yake ilikuwa ya kuvutia kuliko yake.Katika baadhi ya shule, wanafunzi wa chekechea wanapolala baada ya chamcha, huwa wanaweka barakoa zao katika eneo moja na wanapoamka, huwa wanachukua yoyote na kuvaa.

Katika uchunguzi, Taifa Leo ilibaini kuwa wanafunzi wakiwa katika mabasi ya shule asubuhi na jioni wengi wao huwa wanazivaa chini ya kidefu.Hali hii inashuhudiwa kote nchini kutokana kauli za wazazi katika mitandao ya kijamii wakilalamika kwamba watoto wao wanabadilishana barakoa wakiwa shuleni.

“Kwa nini kila wakati mtoto wangu akitoka shuleni huwa anavaa barakoa ya rangi tofuati na anayotoka nayo nyumbani asubuhi, wanabadilishana lini barakoa zao? Walimu wanafaa kuwa makini,” mzazi kwa jina Elizabeth aliandika kwenye mtandao wa kijamii.

Mzazi mwingine kwa jina Nancy alisema kwamba mwanawe huwa anarudi kutoka shule bila barakoa. “Huwa hana habari alipoipoteza na wapi,” alisema.

“Watoto wanafaa kuvaa barakoa wakipanda mabasi ya shule, wakiingia na kutoka shuleni na wakiwa madarasani,” ripoti ya CDC inahimiza.Shirika la Afya Ulimwenguni linahimiza shule zitumie mbinu tofauti kuhakikisha wanafunzi wanazoea kuvaa barakoa.

“Shule zinafaa kuweka mabango ya kuonyesha jinsi ya kuvaa barakoa vyema katika madarasa na maeneo mbalimbali kama vile kumbi za shule,” linasema shirika hilo.

Wakakti huo huo, idara ya afya katika kaunti ya Mombasa imeanza kutoa chanjo ya homa ambayo ilikuwa imesitishwa kufuatia maambukizi ya corona.

Ripoti za Angela Oketch, Maureen Ongala na Wachira Mwangi

Wazazi wa wanafunzi wanaoteketeza mabweni walipe gharama – Serikali

DAVID MUCHUNGUH na CHARLES WASONGA

WAZAZI sasa watalazimika kulipia gharama ya ukarabati wa shule zilizoharibiwa na watoto wao huku majengo zaidi ya shule yakiteketezwa Jumatano katika wimbi la utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi nchini.

Waziri wa Elimu George Magoha Jumatano alikariri msimamo wa serikali kwamba wanafunzi wanatakaopatikana na hatia ya kuhusika katika vitendo hivyo vya uhalifu watakamatwa na kushtakiwa.

“Mtoto yeyote ambaye ana umri wa zaidi ya miaka minane ataweza kushtakiwa. Tunashirikiana na idara ya upelelezi wa jinai kufanikisha hili. Uovu huu sharti ukome. Kwa hivyo, jengo lolote lililoteketezwa litajengwa upya na wazazi,” akasema.

Miongoni mwa shule ambazo majengo yao yameteketezwa wiki hii ni Shule ya Upili ya Wavulana na Moi Nyatike ambako bweni lilichomwa na wanafunzi, Shule ya Upili ya Kigama, iliyoko kaunti ya Vihiga na Shule ya Upili ya Wavulana ya Karumandi iliyoko kaunti ya Kirinyaga ambako pia mabweni yaliteketezwa.

Wanafunzi watano wamekamatwa kuhusiana na visa hivyo.

Profesa Magoha amewaamuru wakurugezi wa elimu kuitisha mikutano ya bodi za elimu katika kaunti kufikia Februari 25, 2021 kwa lengo la kupendekeza njia za kukomesha fujo shuleni.

“Wizara imetoa taarifa kuhusu usalama katika shule za upili za mabweni, ambayo itaongoza bodi simamizi za shule katika kuweka mikakati ya kuzuia kutokea kwa visa kama hivyo shuleni,” Profesa Magoha akasema.

Alikuwa wakiongea na wanahabari alipozuru Shule ya Msingi ya Kwa Njenga katika kaunti ndogo ya Embakasi Kusini, kaunti ya Nairobi.

Awali, Profesa Magoha amewalaumu wazazi kwa kufeli kuwapa nidhamu watoto, na hivyo kuchangia ongezeko la visa vya utovu wa nidhamu shuleni.

Wiki jana alikosolewa kufuatia pendekeza lake kwamba adhabu ya kiboko inaposa kurejeshwa shuleni. Adhabu hiyo ilipigwa marafuku mnamo mwaka wa 2001, sheria Watoto ilipofanyiwa marekebisho.

Profesa Magoha aliongeza kuwa visa vya utovu wa nidhamu pia vinasababishwa na matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa wanafunzi, uovu ambao alisema umekithiri nyumbani.

Chama cha Kitaifa cha Walimu Nchini (Knut) na kile cha kutetea masilahi ya walimu wa shule za upili (Kuppet), vikisema vitawagonganisha walimu na wanafunzi.

KING’ORI: Visa vya wanafunzi kushambulia walimu lazima vidhibitiwe

NA KINYUA BIN KING’ORI

WANAFUNZI wamerejea shuleni juzi tu baada ya kukaa nyumbani kwa takriban miezi tisa kutokana na janga la corona.

Lakini katika siku za hivi punde baada ya kurejea kwao, kumekuwa na matukio ya kushangaza kutoka kwa baadhi yao.Ni suala la kusikitisha kuona kuwa mwanafunzi anaamua kubeba silaha na kuamua kumshambulia mwalimu wake.

Majuzi, mwanafunzi wa kidato cha tatu wa shule ya upili ya Kisii High alisababisha shughuli za masomo kukatizwa kwa muda alipomjeruhi mwalimu wake kwa madai ya kumwadhibu huku pia akimjeruhi mwingine aliyeenda kumsaidia mwenzake.

Pia kumekuwa na kisa cha mwanafunzi kupatikana akiwa na panga shuleni katika Kaunti ya Kwale, miongoni mwa vingine. Vitendo hivyo, japo huenda tukaviona vichache leo ni thibitisho kwamba wanafunzi huenda ikawa wamerithi tabia potovu kutoka kwa jamii au wazazi kwa muda wa miezi tisa ambayo wamekaa nje kutokana na ugonjwa wa corona.

Kibarua kigumu tulichonacho kwa sasa ni vipi tunaweza kukomesha visa vya aidha hii. Serikali inafaa kurejesha adhabu ya kiboko shuleni au ibuni mbinu mbadala ya kurejesha nidhamu shuleni, ni lazima mazingira ya mwalimu yawe salama shuleni na nje ya shule kama ya mwanafunzi yalivyo.

Usalama wa mwalimu wafaa kuboreshwa ili wasijeruhiwe na wanafunzi waliopotoka kimaadili.Walimu nchini wanataka kutekeleza wajibu wao katika mazingira bora wala si vinginevyo.

Kwa muda mrefu tumeishi kuangazia usalama wa wanafunzi na kusahau walimu. Mfano, wiki jana vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti visa mbalimbali vya walimu kujeruhiwa, Lakini inasikitisha kuona licha ya matukio hayo ya utovu wa nidhamu kutokea wazazi wamekaa kimya hawajajitokeza hadharani kushtumu visa hivyo.

Hali ingekuwa tofauti ikiwa ni mwalimu angekuwa amemdunga mwanafunzi kisu. Hata hivyo, hali hii inafaa kudhibitiwa kwani ikiwa wanafunzi wataendelea na vitendo vya kushambulia walimu wao, bila shaka viwango vya vlimu vitashuka mno, maana walimu watakuwa wakifanya kazi zao kwa uoga.

Wizara ya Elimu haipaswi sasa kunyamaza walimu wakishambuliwa, hatutaki mwalimu auliwe shuleni na wanafunzi ndio tuanze kukaa vikao kutafuta suluhu. Waziri wa Elimu, Prof George Magoha ahakikishe kuwa serikali inawalinda walimu dhidi ya visa vya aina hii.

Na ili elimu iweze kusaidia kufanikisha nchi na vizazi vijavyo, lazima wanafunzi waweze kuwa wenye nidhamu shuleni hata wakiwa katika mazingira tofauti.

Wanafunzi 170,000 waliokosa kurejea shuleni wasakwa

Na LEONARD ONYANGO

TAKRIBANI wanafunzi 170,000 hawajarejea shuleni tangu shule zilipofunguliwa wiki mbili zilizopita licha ya serikali kuagiza machifu kuwasaka.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwa wengi wa wanafunzi ambao hawajarejea shuleni wameolewa, wamejiingiza katika dawa za kulevya au wanashiriki shughuli za kuwaletea mapato.

Jana, waziri wa Elimu George Magoha alikiri kuwa baadhi ya wanafunzi ambao hawajarejea shuleni wana umri wa zaidi ya miaka 18 hivyo ni vigumu kuwalazimisha kuendelea na masomo yao.

Kwa mfano, katika shule ya Upili ya Wasichana ya Our Lady of Fatima iliyoko mtaani Kariobangi Kaskazini, Nairobi, wanafunzi 24 kati ya 900 hawajarejea.

Kulingana na waziri wa Elimu George Magoha, wanafunzi watano kati ya 24 ambao hawajarejea ni wajawazito na wanakaribia kujifungua.Prof Magoha aliyekuwa akizungumza katika ya Shule ya Wasichana ya Our Lady of Fatima, alisema kuwa idadi kubwa ya wanafunzi katika maeneo kame, ikiwemo Kaunti ya Turkana, hawajarejea shuleni kutokana na ukosefu wa chakula shuleni.

“Malori ya kusafirisha chakula katika maeneo hayo yamekumbwa na changamoto za usafiri njiani kutokana na barabara mbovu. Mwishoni mwa wiki hii shule hizo zitapokea chakula,” akasema Prof Magoha.

Alisema tangu shule kufunguliwa Januari 4, mwaka huu, asilimia 99 ya wanafunzi wamerejea shuleni.“Machifu na maafisa wengine wa serikali wanaendelea kusaka wanafunzi ambao hawajarejea shuleni,” akasema Prof Magoha.

Takwimu za wizara ya Elimu zinaonyesha kuwa takribani watoto milioni 17 wanasoma katika shule za msingi na sekondari humu nchini. Hiyo inamaanisha kuwa wanafunzi 170,000 ambao ni sawa na asilimia moja, hawajulikani waliko.

Wakati huo huo, Waziri Magoha alionya wakuu wa shule dhidi ya kuwafukuza wanafunzi wanaoshindwa kulipa karo.Aliwataka wakuu wa shule kutembelea familia za wanafunzi hao ili kuthibitisha ikiwa zina uwezo wa kulipa karo au la.

“Mna miguu na afya njema. Ni nini kinawazuia kutembelea familia za wanafunzi wanaoshindwa kulipa karo? Ni makosa kumrudisha nyumbani mwanafunzi ambaye familia yake inaishi maisha ya umaskini; hata ukiwafukuza pesa hazitaanguka kutoka mbinguni,” akasema Prof Magoha.

Agizo hilo la wizara ya Elimu limewaweka wakuu wa shule katika njiapanda kwani itakuwa vigumu kwao kutembelea familia za mamia ya wanafunzi wanaoshindwa kulipa karo.

Prof Magoha alipiga marufuku vieuzi au sanitaiza shuleni akisema kuwa huenda vikatumiwa na wanafunzi kuteketeza shule.

“Walimu wahakikishe kuwa hakuna mwanafunzi anayeenda na sanitaiza darasani au katika bweni. Wanaokuja nazo wanyang’anywe kisha wapewe wakati wa kuondoka shuleni. Hii ni kwa sababu tumeanza kushuhudia visa vya shule kuteketezwa kwa kutumia sanitaiza,” akasema.

Prof Magoha alisema kuwa wanafunzi wa Gredi 1 hadi Gredi 3 wanaosomea mitaa ya mabanda na maeneo yenye kiwango kikubwa cha umaskini watapewa uji wa bure na serikali.

Kulingana na Prof Magoha, uji huo ulio na soya, utasaidia ubongo wa watoto kukua vyema.Alisema shule zote za umma za jijini Nairobi zimepokea madawati kutoka kwa serikali.

Shule za Kaunti ya Uasin Gishu zimepokea asilimia 94.7 ya madawati ikifuatiwa na Siaya (asilimia 91.5), Vihiga (asilimia 90), Kisumu (asilimia 88.2), Nyandarua (asilimia 84.5), Nyeri (asilimia 82.8), Kiambu (asilimia 82.4), Migori (asilimia 82.2), Machakos (asilimia 81.9), Murang’a (asilimia 81.8) na Busia (asilimia 81.6).

WANTO WARUI: Huenda wanafunzi wengi wakakosa mitihani ya KNEC

Na WANTO WARUI

Baraza la mitihani nchini (KNEC) linapanga kuwapa wanafunzi wa Gredi ya 1-3 na madarasa ya 5-7 majaribio ya kutathmini kiwango chao cha uelewa kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, 22-01-2021.

Hii ni kutokana na hali iliyowakumba wanafunzi ya kukaa nyumbani kwa kipindi cha miezi tisa kutokana na mkurupuko wa ugonjwa wa Covid-19.

Kwa mujibu wa KNEC, wanafunzi wote wanatarajiwa kuwa shuleni ili waweze kufanya majaribio hayo ambayo tayari yameandaliwa na KNEC na kutumwa shuleni kupitia njia ya mtandao.

Hivi ni kusema kuwa KNEC inatarajia kila shule nchini iwe na uwezo wa kupata majaribio hayo, iweze kusimamimia wanafunzi wafanye kisha isahihishe kazi hiyo na kutuma majibu yaliyotolewa na wanafunzi kwake (KNEC) kupitia njia iyo hiyo ya mtandao. Hali ilivyo sasa, kuna wanafunzi wengi ambao bado hawajarudi shuleni na hali zao za kuendelea na masomo hazijulikani.

Miongoni mwao ni wasichana ambao walipata mimba, wengi wao sasa wakiwa katika hatua za mwisho za kupata watoto. Kwao itakuwa vigumu mno kuweza kufikia majaribio haya.

Shuleni nako changamoto ni nyingi. Wanafunzi waliorudi shuleni bado hawana madawati ya kutosha. Wengine wanasomea chini ya miti kulikojaa upepo na mavumbi.

Shule nyingi nchini hazina umeme wala kompyuta. Haitakuwa jambo rahisi kwa walimu kuweza kusimamia mitihani hii katika hali kama hizi.Kuna baadhi ya shule ambazo zilifungwa kutokana na mafuriko ya maziwa kama vile Baringo, Nakuru na Naivasha.

Sehemu kubwa ya wanafunzi hao huenda bado iko nyumbani kutokana na hali ya umaskini ya wazazi. Ni wazi kuwa wanafunzi kama hawa hawatapata fursa ya kufanya majaribio haya.

Wati ambapo wanafunzi wa kidato cha nne, darasa la nane na gredi ya nne walipokuwa shuleni, KNEC iliweza kuandaa majaribio kama haya. Ingawaje shule zilijizatiti kusimamia, kuna shule nyingine ambazo hazikutoana matokeo sahihi.

Kufikia sasa, KNEC bado haijaweza kutoa matokeo ya tathmini la Gredi ya 4 kwa walimu.Hivi ni kusema kuwa, majaribio yanayotarajiwa kuanza leo yatakuwa na changamoto kwa walimu na wanafunzi wenyewe.

Kuna wale ambao wataweza tu kufanya nusu ya majaribio hayo huku wengine wakishindwa kabisa. Ijapokuwa KNEC inafanyiza zoezi hili ikiwa na nia nia ya kutathmini kiwango cha uelewa wa wanafunzi tu, itakuwa si vyema kuwakosesha wanafunzi wengi kiasi hiki kushiriki zoezi kama hili.

Mpango huu wa KNEC wa kutathmini wanafunzi kwa njia hii ungefaulu zaidi endapo serikali kufikia sasa ingekuwa ishatekeleza ahadi yake ya awali ya kupeana kompyuta kwa wanafunzi. Hali ilivyo sasa, itabidi wanafunzi wengi waikose mitihani hii.

KING’ORI: Shule za mashinani pia zilindwe dhidi ya corona

Na KINYUA BIN KING’ORI

Wiki Jana, shule za msingi na sekondari kote nchini zilifunguliwa baada ya kufungwa kwa miezi tisa na wanafunzi kwa sasa wamo madarasani wakiendelea na masomo japo walimu wameanza kukumbana na matatizo mengi.

Waziri wa Elimu, Prof George magoha anapaswa kuhakikisha walimu na wanafunzi wanakingwa dhidi ya maambukizi ya homa hatari ya Corona.

Shule nyingi za umma zimeshindwa kuzingatia sheria zilizowekwa na wizara ya Afya na kuwalazimu walimu wakuu wa baadhi ya shule hizo kujibunia mbinu zao wenyewe kuwashughulikia wanafunzi kutegemea na idadi yao ikizingatiwa shule nyingi hazina madarasaa ya kutosha hadi sasa.

Kwa mfano, baadhi ya wanafunzi hasa wa shule za msingi wanabadilishana barakoa bila kujali maambukizi ya homa hatari ya corona. Serikali imefungua shule lakini ukweli mchungu ni kwamba haijakuwa na mipango kabambe kuzua homa hiyo hatari.

Wizara ya Elimu isambaze sanitaiza na sabuni shuleni sawia barakoa na ielekeze jinsi zitakavyowafikia wanafunzi wote hasa maeneo ya mashambani.

Tusije kusahau kuna shule zingine hazipati maji ya mifereji yanayotiririka kila wakati ikizingatiwa lazima wanafunzi na walimu wazingatie sheria za wizara ya Afya ya kunawa mikono kwa maji inayotiririka ili kuzuia kuenea kwa Corona.

Je, wanafunzi wa shule za msingi ya Kilera na Linjoka, wadi ya Ntunene, igembe kaskazini watafuata kanuni hizo kivipi wakati ambapo kupata maji ya mifereji hata manyumbani mwao ni kitendawili?

Aidha, baadhi ya shule zinaendelea kukumbana na changamoto kubwa kutokana idadi kubwa ya wanafunzi wapya, shule za umma hasa maeneo ya mashambani zimekosa nafasi zaidi kuwaruhusu watoto ambao wazazi wao walirejea vijijini kutokana na athari ya Janga la corona, tuliambiwa na waziri wa Elimu kutakuwa na nafasi toshelezi kwa watoto wote lakini hakuna madarasaa mapya yamejengwa katika shule nyingi za umma wala madawati.

Je, ikiwa watoto wamejazana darasani watarajia walimu wabuni mbinu zipi kuhakikisha usalama wao na wanafunzi wakati huu wa covid 19 umehakikishwa?

Serikali inafaa kutoa fedha za ujenzi wa madarasa kwa shule zote za umma na ununuzi wa madawati mengine. wazazi hawawezi kukubali afya ya watoto wao ifanyiwe mzaha, japo wengi wametii amri ya kuwarejesha watoto shuleni hawakufanya hivyo kwa kupendezwa na mazingira ya shule bali wengi wanataka wana wao hasa wa darasa la nane na kidato cha nne wafanye mitihani yao ya kitaifa.

Walimu wakuu ikiwa watakosa usaidizi ufaao kutoka kwa serikali huenda wakalazimika kuwaongezea wazazi mzigo zaidi kwa kuwazidishia karo ili waweze kujenga madarasa zaidi. Ikiwa hivyo, baadhi ya walimu watatumia mbinu hiyo kuwapunja wazazi ambao hata pesa za kulipa karo kuzipata ni muujiza ya Musa kutokana na hali ngumu ya uchumi.

Nimebaini, shughuli za kuimarisha shule za umma huenda zikachukua muda mrefu kwa sababu serikali inategemea wabunge watumie fedha za NG-CDF kujenga madarasa zaidi katika maeneo yao.

Wizara ya Elimu inapaswa kukubali ukweli kwamba pesa hizo haziwezi kutosha kusaidia kufanikisha uboreshaji wa shule maadamu, zinazotengewa miundomsingi shuleni huwa asilimia ndogo huku zingine zikitumika kwa basari, usalama na maendeleo mengine katika kustawisha maeneobunge.

Waziri wa Elimu, Prof George magoha, awajibikie usalama wa wanafunzi na walimu, la sivyo, huenda shule zikafungwa tena kabla ya muhula huu kukamilika ikiwa maambukizi ya Corona yatasambaa shuleni.

Afueni kwa shule 6 kufunguliwa baada ya miaka saba

NA KALUME KAZUNGU

AFUENI imepatikana kwa zaidi ya wanafunzi 400 wa shule sita zilizoko msitu wa Boni zilizofungwa kwa miaka saba, Kaunti ya Lamu baada ya serikali kupeleka walimu na kuzifungua shule hizo.

Katika kipindi cha juma moja tangu shule kufunguliwa kote nchini, wanafunzi wa shule za Bodhai, Basuba, Milimani, Mangai, Mararani na Kiangwe walilazimika kusalia nyumbani baada ya walimu kukosa kufika shuleni kufuatia changamoto ya usalama barabarani inayochangiwa na magaidi wa Al-Shabaab.

Mwishoni mwa juma, serikali ilipeleka zaidi ya walimu kumi kwenye shule hizo na kuamuru shule zote kufunguliwa ili wanafunzi wa msitu wa Boni wasome kama wengine.

Walimu hao walisafirishwa shuleni kupitia usafiri wa angani.

Katika mahojiano na Taifa Leo Jumatatu, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, alisema wameweka mikakati kabambe, ikiwemo kudhibiti vilivyo usalama kwenye vijiji vyote vya msitu wa Boni katika juhudi za kuhakikisha masomo yanaendelea eneo hilo.

Kwa zaidi ya miaka saba, shule za msitu wa Boni zimekuwa zikifungwa kila mara na kulazimu watoto kubaki nyumbani na wazazi wao kutokana na utovu wa usalama ambao umekuwa ukichangiwa na magaidi wa Al-Shabaab.

Bw Macharia aidha alishikilia kuwa msimamo wa serikali ni kuhakikisha maisha na shughuli za kawaida zinarejelewa msituni Boni, hivyo akawahimiza wazazi kuwapeleka watoto wao shuleni ili wasome kama wengine nchini.

“Tumewasilisha walimu zaidi ya kumi kwenye shule za msitu wa Boni. Kila shule inahudumiwa na walimu wawili kwani wanafunzi wengi msituni Boni ni wa chekechea hadi darasa la nne. Tumeamuru shule zifunguliwe na tunashukuru kwani wanafunzi tayari wamefika shuleni kusoma. Usalama pia umedhibitiwa vilivyo kote Boni, ikizingatiwa kuwa serikali bado inaendeleza operesheni ya usalama eneo hilo. Wazazi na wanafunzi wasiwe na shaka,” akasema Bw Macharia.

Baadhi ya wazazi,walimu na wanafunzi waliozungumza na Taifa Leo hawakuficha furaha yao baada ya shule zao kufunguliwa.

Abdallah Wakati ambaye ni mzee wa jamii ya Waboni eneo la Kiangwe alisema ombi lake ni kuona shule za eneo hilo zikiendelea kuhudumu nyakati zote ili wanafunzi wao wasome na kuhitimu kama wengine.

Kijiji cha Kiangwe kilichoko msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu. Hatimaye watoto waliokuwa wakirandaranda vijijini eneo hilo warudi madarasani baada ya serikali kuzifungua shule sita. PICHA/KALUME KAZUNGU

“Kuna watoto wengi vijijini hapa ambao walianza kusoma zamani na walistahili wawe wamekamilisha masomo yao ya shule ya msingi. Hilo halijawezekana kutokana na kwamba shule zimekuwa zikifungwa mara kwa mara. Nafurahi kwamba hatimaye shule zetu zimefunguliwa japo kuchelewa. Ni matumaini yetu kwamba shule hizi zitaendelea kuhudumu ili wanafunzi wetu wabaki madarasani kusoma hadi wahitimu kama wengine nchini,” akasema Bw Wakati.

Farida Kokane aliisisitizia serikali kuongeza idadi ya walimu wanaohudumia shule za msitu wa Boni kwani walimu kumi pekee hawatoshi.

Bi Kokane pia aliiomba serikali kuboresha miundomsingi kwenye baadhi ya shule ili wanafunzi wawe na mahali pazuri pa kusomea.

“Shule zetu hapa msituni Boni zina changamoto ya majengo na mahali pa kukalia. Madarasa yako na nyufa zinazoficha nyoka. Pia madarasa hayana milango, ambapo wanyama wa msituni wamekuwa wakitafuta makao madarasani.  Serikali irekebishe hali duni ya shule zetu wakati inapozifungua,” akasema Bi Kokane.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa shule hizo, Diwani wa Basuba, Barissa Deko alishikilia kuwa ipo haja ya serikali kuanzisha kituo cha pamoja cha elimu eneo la Kiangwe ili kuhudumia wanafunzi kutoka vijiji vyote sita vya msitu wa Boni.

Alisema anaamini kuanzishwa kwa kituo hicho ambacho kitakuwa cha bweni kutamaliza kabisa matatizo ya kielimu kwenye msitu wa Boni.

“Badala ya kila mara kufungua na kisha kufunga shule zetu, ni vyema kuanzishwe kituo cha pamoja cha elimu eneo la Kiangwe. Eneo hilo linafikika kwa urahisi ikilinganishwa na vijiji vingine eneo hili la msitu wa Boni. Walimu wa kutosha wapelekwe pale. Walinda usalama pia wasambazwe pale. Wanafunzi wawe wanasoma na kulala pale. Wakifanya hivyo sidhani watoto wa jamii yetu ya Waboni watahangaika kwa kukosa masomo kila mara kama ilivyo sasa,” akasema Bw Deko.

WANTO WARUI: Kuzuia wanahabari shuleni kunaficha maovu

NA WANTO WARUI

Hatua ya hivi juzi ya Wizara ya Elimu kupiga marufuku vyombo vya habari shuleni huenda ikasababisha hasara zaidi kuliko faida.

Ingawaje kwa upande mmoja vyombo vya habari vinaweza kuzusha hali ya taharuki shuleni hasa wakati huu tunapokumbwa na janga la maradhi ya Covid-19, lakini pia kuna maovu mengine sugu ambayo huenda yakafanyika shuleni na yakakosa kumulikwa.

Kuporomoka kwa madarasa ya shule ya Talent Academy ambapo wanafunzi kadhaa walipoteza maisha yao, kwa mfano, ni tukio ambalo lilifungua serikali macho.

Aidha wawekezaji wengine katika sekta hii ya elimu walichukua tahadhari kutokana na kisa hicho. Kama si vyombo vya habari kuangazia suala hilo, huenda kufikia leo wanafunzi wengine wengi wangekuwa wamepoteza uhai wao kutoka na ulegevu kama huo wa wamiliki wa shule.

Mfano mwingine wa maovu yanayoendeshwa shuleni ni kuadhibu wanafunzi kwa kuwatandika kinyume cha sheria. Aidha wanafunzi wengi hasa wale wa kike hupitia dhuluma za kimapenzi ambazo zahitaji kuwekwa wazi ili jamii iweze kukosoa matendo kama hayo. Kumekuwa na kesi nyingi shuleni za mioto na hata matumizi ya dawa za kulevya.

Hofu kubwa ya Wizara ya Elimu katika suala hili ni taharuki inayoweza kuzushwa na vyombo vya habari endapo kutatokea mkurupuko wa maradhi ya Covid-19 shuleni.

Bila shaka ni kweli kuwa jambo kama hilo linaweza kuzua wasiwasi mwingi sana kwa walimu, wanafunzi na zaidi kwa wazazi. Hata hivyo, mtu akificha mwiba na kutoung’oa hatimaye mwiba huo hutunga usaha na maumivu zaidi.Je, serikali imebuni mikakati bora ya kukabiliana na hali ya Covid-19 endapo ugonjwa utakurupuka shuleni?

Ni vipi wengine watajua na kuweza kuchukua tahadhari hasa jamii ambayo inaweza kuwa imezingira shule iliyoathirika?Ni kweli kama alivyosema Waziri wa Elimu kuwa wanafunzi ni wengi zaidi na hawawezi kutoshea madarasa yaliyoko katika shule zetu. Ikiwa kabla maradhi ya Covid-19 hayajaingia madarasa yalikuwa hayatoshi, sembuse sasa?

Ni wazi kuwa sheria ya kujikinga na maradhi haya ambayo ni kutokaribiana ndiyo ngumu zaidi kutekelezwa kwa wanafunzi. Sidhani kuna shule hata moja nchini ambayo itaweza kuhakikisha wanafuzi hawagusani hasa uwanjani wanapocheza.

Jambo la muhimu zaidi ambalo Wizara ya Elimu ingefanya ni kuwaita waandishi wa habari na kufikia muafaka wa mazungumzo nao ili kuwaelekeza yale ambayo wasingependa yawasilishwe hewani huku wakipatia vyombo hivyo fursa ya kukagua maendeleo ya masomo au upungufu wa kimaadili katika shule.Kwa kufanya hivyo, maovu mengi ambayo yanaweza kutokea shuleni yatapunguzwa.

Hali ilivyo sasa, huenda kuna mambo mengi sana mabaya ambao hayatajulikana au kuweza kurekebishwa.

Wamiliki wa shule zilizolemewa na makali ya Covid-19 wageuza madarasa kuwa vyumba vya biashara

Na SAMMY WAWERU

MADARASA ya shule za wamiliki binafsi nchini zilizolemewa na makali ya Covid-19 kiasi kwamba zimeshindwa kuafikia masharti ya serikali wakati huu ambapo masomo ya shuleni yamerejelewa baada ya zaidi ya miezi tisa, yamegeuzwa kuwa vyumba vya biashara.

Shule kote nchini zimefunguliwa leo Jumatatu, Januari 4, 2021 miezi tisa baada ya kufungwa kufuatia mkurupuko wa virusi vya corona.

Kwenye uchunguzi wa Taifa Leo, tayari shule zilizoathirika zimeweka vibango vya matangazo ya kukodisha madarasa kuwa maduka na ofisi, huku uga ukigeuzwa bustani.

Shule ya mmiliki binafsi ya Kastemil iliyoko eneo la Kasarani, Thika Road na Brain Stone Academy, Githurai, zimegeuza madarasa yake kuwa vyumba vya biashara.

“Mwishoni mwa 2020 tuliarifiwa tuendee chochote tunachomiliki shuleni kwa sababu haitafunguliwa tena,” Caroline Ng’ang’a mmoja wa walimu Brain Stone Academy akaambia Taifa Leo.

Sawa na shule hizo, wazazi wa Grand Kago Academy, Karatina mwaka uliopita, 2020, walitakiwa kuanza kutafutia wanao shule zingine, mmiliki akiwaarifu gharama kuafikia sheria na mikakati ya ufunguzi kudhibiti maenezi ya virusi vya corona shuleni imemlemea.

Maelfu ya watoto waliokuwa katika shule za kibinafsi zilizoathirika huenda wakafungiwa nje, kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na shule za umma.

Kulingana na chama cha shule za wamiliki binafsi nchini (KPSA), watoto wapatao 56,000 wameathirika hasa baada ya shule walikokuwa wakisomea kufungwa kwa sababu ya wamiliki kushindwa kuafikia mahitaji ya ufunguzi.

Kila shule imetakiwa kuhakikisha imeweka mikakati na mipangilio maalum kuzuia wanafunzi kuambukizwa Covid-19 shuleni.

Wanafunzi wa wazazi wasio na karo wasifukuzwe shuleni – Serikali

MWANGI MUIRURI na DIANA MUTHEU

SERIKALI imetangaza kwamba itawachukulia hatua walimu ambao watafukuza watoto shuleni kwa kukosa karo au sare mpya wakati shule zitakapofunguliwa Jumatatu.

Akizungumza akiwa Kaunti ya Murang’a jana, Waziri wa Elimu George Magoha alisema serikali inataka wanafunzi wote kurudi shuleni kwa asilimia 100.Alisema serikali imetekeleza jukumu lake la kupeleka madawati shuleni ilivyoahidi na kutoa Sh18.5 bilioni kwa shule za msingi na za upili kufadhili masomo.

Kulingana na Prof Magoha, kila idara ya serikali inatekeleza mchango wake kuhakikisha kanuni za kuzuia corona zitazingatiwa na watoto wote wamerudi shuleni.Naibu waziri wa elimu (CAS) Zack Kinuthia alisisitiza kwamba sare mpya za shule na karo hazitapewa kipaumbele wanafunzi watakaporudi shuleni kuanzia Jumatatu ijayo.

“Tumeagizwa kuhakikisha hakuna mwanafunzi atakayefukuzwa shuleni kwa sababu ya karo au kutokuwa na sare mpya kwa sababu hatufungui shule kwa mashindano ya utanashati au kuonyesha nguvu za kifedha,” alisema Bw Kinuthia.

Alisema wizara imepokea jumbe ambazo shule zimetumia wazazi kuwataka walipe malimbikizi ya karo na pesa za sare shule zikifunguliwa na kusema walimu waliotuma jumbe hizo hawakuagizwa na wizara.

Baadhi ya jumbe ambazo Taifa Leo iliona zinawaagiza wanafunzi wa shule za mabweni kulipa malimbikizi ya karo, kuwa na maski 50, pesa za kununua sare mpya shuleni na lita tatu za sanitaiza.

Ingawa aliwahimiza wale ambao hawakuathiriwa mno na janga la corona kulipa malimbikizi ya karo, waziri alisema wale ambao wanapitia hali ngumu baada ya kupoteza mapato wanaweza kulipa baadaye kwa awamu mradi tu wajue wanadaiwa.

Wakati huo huo, Baraza la Kitaifa la Ushauri kwa Waislamu (KEMNAC) limeiomba Wizara ya Elimu kuondoa karo ya muhula wa kwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Panaroma, katika kaunti ya Mombasa, mwenyekiti wa baraza hilo, Sheikh Juma Ngao alisema kama karo hiyo haitaondolewa, basi wazazi wakubaliwe kulipa karo polepole, kwani wameathirika na kuwepo kwa virusi vya corona nchini.

‘Karo ya shule ya muhula wa kwanza twaomba iondolewe. Kama haitaondolewa basi wazazi wanafaa kupewa nafasi walipe polepole pasi na watoto wao kufukuzwa nyumbani,’ akasema Sheikh Ngao.

Mwanachama wa KEMNAC, Sheikh Mohammed Juma alisema wazazi wengi bado wanahangaika kuwatafutia wanao chakula. Kulingana na Wizara ya Elimu, shule zinafaa kufunguliwa mnamo Januari 4, 2021.

Watoto mayatima wafadhiliwa kuejerea darasani

Na LAWRENCE ONGARO

WATOTO mayatima wapatao 100 wa Gatundu Kaskazini, wamefadhiliwa kwa vyakula huku wakiahidiwa kulipiwa karo shuleni mwaka wa 2021.

Kikundi cha wanawake likiongozwa na Jane Wambui kiliahidi kuwasaidia watoto hao ambao wanatoka vijiji vinne katika eneo hilo.

Watoto hao wanatoka viijiji vya Gakoe, Kanjuki, Ndiko na Kamwangi.

Bi Wambui alisema kwa muda mrefu watoto hao wamekuwa katika hali ngumu ya maisha na kwa hivyo wao kama wanawake walionelea kuwajali.

” Sisi kama kikundi cha wanawake Tutafanya juhudi kuona ya kwamba tunawasaidia watoto hao ambao kwa muda mrefu wamekuwa katika dhiki bila usaidizi wowote,” alisema Bi Wambui.

Alisema wengi wao hawakuweza kuhudhuria masomo na kwa hivyo wakaachwa katika hali ya ufukara vijijini.

“Sisi kama kikundi cha wanawake waliostaafu kama walimu tutafanya juhudi kuona ya kwamba watoto hao wanarudi shuleni na kupata masomo kamili,” alisema Bi Wambui kwa niaba ya wenzake.

Alisema wengi wa watoto hao ni wale walioachwa na wazazi wao huku wakiingilia vitendo viovu vijijini.

” Watoto wengi walioachwa yatima wamekuwa wakiingilia tabia zisizo dawa kama kuvuta sigara, na kunywa pombe haramu,” alisema mmoja wa wafadhili hao.

Alisema hawangetaka kuona watoto hao wakiingilia maovu bali ni vyema wakirekebishwa na kupewa usaidizi.

Wakati huo pia watoto hao waliathirika sana hasa wakati wa mlipuko wa homa ya covi-19.

” Wengi wao walikuwa wakirandaranda mitaani jambo ambalo ilikuwa ni hatari kwa maisha yao. Kwa hivyo tunataka kuwaleta pamoja ili wawe watoto wema,” alisema Bi Wambui.

Wanafunzi wengi zaidi kusomea chini ya miti 2021

Na WAANDISHI WETU

IDADI kubwa ya wanafunzi watakaorudi shuleni wiki ijayo, watalazimika kusoma chini ya miti baada ya serikali kushindwa kupanua madarasa ili kuepusha misongamano inayoweza kueneza virusi vya corona.

Waziri wa Elimu Prof George Magoha, Jumatatu alikiri itakuwa changamoto kuepusha mtagusano wa wanafunzi wakati shule zitakapofunguliwa Jumatatu ijayo, na hivyo itabidi walimu na wasimamizi wa shule wawe wabunifu ikiwemo kuwekea watoto madarasa chini ya miti na viwanjani.

Waziri alisema hayo huku walimu wakuu wakiitaka serikali kutoa fedha kwa shule kabla ya Jumatatu ijayo.Walimu hao wa shule za msingi wakiongozwa na mwenyekiti wao wa kitaifa Nicholas Gathemia, walisema shule nyingi hazipo tayari kwa ufunguzi kutokana na uhaba wa madarasa na vifaa vya kuzingatia kanuni za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

“Wanafunzi wote wakirudi shuleni Jumatatu hawatatoshea katika madarasa yaliyopo,” akasema Bw Gathemia. Bi Phoebe Kittoi wa Shule ya Msingi ya Magadi, alisema wanatarajia idadi ya wanafunzi katika shule za umma kuwa ya juu zaidi kutokana na kufungwa kwa shule nyingi za kibinafsi.

Kufikia sasa shule za kibinafsi 227 za msingi na sekondari zimefungwa kutokana na madhara ya Covid-19, na kuwaacha wanafunzi wapatao 56,000 bila pa kusomea.

Wengi wa wanafunzi hawa watalazimika kujiunga na shule za umma na hivyo kuongeza msongamano.Walimu hao waliokutana Nairobi walisema serikali inapasa kutenga fedha za matibabu ya walimu na wanafunzi ambao huenda wakaambukizwa virusi vya corona shule zikifunguliwa.

Katika hotuba ya kitaifa kuhusu hali ya Covid-19 nchini mnamo Novemba, Rais Uhuru Kenyatta alihimiza wabunge washauriane na bodi za Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji Maeneobunge (NG-CDF) ili kufadhili maandalizi ya shule kabla watoto wote warudi Januari.

Miongoni mwa masuala yaliyohitajika kufadhiliwa ni pamoja na kuweka sehemu za kuosha mikono, usambazaji barakoa, usafi na upanuzi wa madarasa ili kuepusha mtagusano.

MISONGAMANO

Kwa kawaida, shule za umma huwa na msongamano wa wanafunzi madarasani na vile vile katika mabweni.Katika kipindi ambapo wanafunzi wa Darasa la Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne walikuwa shuleni, baadhi ya shule zilikuwa zikitumia madarasa ya wanafunzi ambao walikuwa wangali nyumbani kuepusha mtagusano.

Kwa msingi huu, changamoto itatokea wakati watoto wote watakaporudi shuleni kuanzia Jumatatu.Serikali ilikuwa imezindua mpango wa kusambazia shule madawati 650,000 lakini imeonekana hapakuwepo mpango mahsusi kuhusu sehemu ambapo madawati hayo yangetumiwa.

Prof Magoha alisema kufikia jana, madawati takriban 500,000 yalikuwa tayari yamesambazwa kwa shule zilizo sehemu mbalimbali za nchi.Kando na ukosefu wa madarasa, serikali jana ilisisitiza haitasambazia wanafunzi wote barakoa isipokuwa milioni tatu pekee ambao wametambuliwa kutoka katika familia zisizojiweza kifedha.

“Wazazi wajue hili ni suala muhimu sana. Familia zinaweza kugharamia barakoa ya Sh100 nzuri ambayo inaweza kuoshwa. Msisubiri barakoa kutoka kwetu. Nendeni mnunulie watoto wenu,” akasema waziri.

Prof Magoha aliongeza kuwa wizara yake inaendelea kushauriana na Wizara ya Fedha ili Sh19 bilioni zinazohitajika shuleni kwa Muhula wa Pili utakaoanza Januari zitolewe haraka.Walimu wakuu wamekuwa wakilalamika hawajapokea fedha ilhali wanahitajika kukamilisha maandalizi ya kufungua shule.

Huku hayo yakijiri, foleni ndefu zilishuhudiwa katika maduka ya vitabu na sare za shule katika miji tofauti.Wamiliki wa maduka hayo walilazimika kuchukua usukani ili kuhakikisha miongozo ya idara ya afya kuhusu umbali inafuatwa kikamilifu.

Wanunuzi walipanga foleni nje ya maduka hayo ambapo idadi chache ya watu iliruhusiwa kuingia ndani kwa zamu na kuzingatia mipangilio maalum.

Maduka mengi ya sare yamekuwa wazi siku zote isipokuwa siku kuu ya Krisimasi ambapo yalifungwa kwa muda.Wamiliki walisema japo wazazi wameanza kumiminika, huenda idadi yao ikaongezeka hata zaidi mwishoni mwa wiki hii na mwezi ujao.

Maduka hayo tayari yamejazwa vifaa mbalimbali vya shule ili kutosheleza mahitaji ya wanunuzi.

Ripoti za Victor Raballa, Faith Nyamai, Valentine Obara na Phyllis Musasia

Sh19 bilioni za mpango wa elimu bila malipo kutolewa kabla ya Januari 4

Na CHARLES WASONGA

WIZARA ya elimu Jumatatu ilitangaza kuwa serikali itatuma Sh19 bilioni katika shule za msingi na za upili za umma chini ya mpango wa elimu bila malipo kabla ya shule kufunguliwa Januari 4, 2021.

Waziri wa Elimu George Magoha alisema mazungumzo yanaendelea kati ya Wizara yake na ile ya Hazina ya Kitaifa kuhakikisha kwamba fedha hizo zinatumwa “haraka iwezekanavyo”.

Profesa Magoha alisema Sh4 vilioni kati ya fedha hizo zitaelekezwa kwa shule za msingi huku Sh15 bilioni zikitumwa kwa shule za upili.

Akiongea katika shule ya upili ya Obola iliyoko eneo bunge la Seme, kaunti ya Kisumu alipokagua mradi wa msambazaji madawati, Profesa Magoha aliwataka walimu wakuu kuhakikisha kuwa fedha hizo zimetumika vizuri. Alionya kuwa wale watakaopunguza fedha hizo watachakuliwa hatua za kinidhamu bila kuhurumiwa.

“Serikali imeweka mikakati hitajika ya kuhakikisha kuwa shule zinafunguliwa ikiwamo kusambazwa kwa fedha za mpango wa elimu bila malipo kwa wakati kabla ya masomo kuanza,” akasema.

Profesa Magoha akaongeza: “Nawaomba wazazi kutowatuma nyumbani wanafunzi kwa kukosa karo, bali washughulikie mchangamoto zinazowakabiliwa wazazi, mmoja baada ya mwingine.”

Waziri alisema janga la Covid-19 limewaathiri waziri kiuchumi na kuwataka walimu wakuu kutowawekea wazazi mahitaji makubwa.

“Lakini nawaomba wazazi kuwakagua wazazi kwa sababu kuna baadhi yao ambao ni waongo na huenda wakazingizia changamoto ya kiuchumi inayoshuhudiwa nchini kukwepa kulipa karo ya watoto ilhali wanayo uwezo wa kifedha,” Profesa Magoha akasema.

Profesa Magoha alisema serikali imewatambua wanafunzi milioni 3 kutoka jamii masikini ambao watapewa barakoa bila malipo.

“Tayari tuko na maski milioni mbili ambazo zitasambaziwa watoto kutoka familia masikini. Isitoshe, tunafanya mazungumzo na kampuni ya kutengeneza ngua ya Rivatex iwasilishe maski milioni moja zilizosalia kabla ya shule kufunguliwa,” akaeleza.

Profesa Magoha alikiri kuwa itakuwa vigumu kwa shule kudumisha kanuni ya kutenganisha wanafunzi na ndipo akawataka wazazi kuhakikisha kuwa watoto wao wanavalia maski nyakati zote kuhusu msambao wa Covid-19 shule zitakapofunguliwa.

Kuhusu mradi wa madawati shuleni, Profesa Magoha alisema kufikia Jumatatu, Desemba 28, 2020, madawati 500,000 yalikuwa yamesambazwa katika shule mbalimbali za umma nchini.

“Maafisa wa serikali wakiwemo wale elimu, wenzao kutoka wizara ya masuala ya ndani na viongozi wa kisiasa watahakikisha kuwa mafundi wa Jua Kali wanaotengeneza madawati hayo wameyawasilisha shuleni kufikia Jumatatu,” akaeleza.

Wakati huo huo, Profesa Magoha ametangaza kuwa watoto ambao wamekuwa wakisoma katika shule za kibinafsi zilizofungwa watahamishwa hadi katika shule za umma.

“Na mikakati imewekwa kuhakikisha kuwa watahiniwa kutoka shule hizo wanafanya mitihani yao ya kitaifa katika vituo vya serikali,” akasema.

CORONA: Shule bado kujiandaa

WANDERI KAMAU na FAITH NYAMAI

HUKU shule zikitarajiwa kufunguliwa Jumatatu ijayo, hofu imeibuka nchini kuhusu hali na mazingira ya shule za umma ikiwemo uhaba wa madarasa na walimu katika kipindi hiki cha janga la corona.

Walimu wakuu wanasema hawajui wanafunzi watakakosomea baada ya miundomsingi katika shule nyingi kuharibika kwa kutotumiwa kwa karibu miezi kumi tangu shule zilipofungwa katika juhudi za kukabili maambukizi ya Covid-19.

Licha ya kutangaza shule zitafunguliwa wiki ijayo kwa kuzingatia kanuni za kuzuia corona, serikali haijafanikisha ujenzi wa madarasa mapya ili kuzuia misongamano ya wanafunzi.

Hofu hiyo pia inahusu usalama wa wanafunzi kiafya, kwani shule nyingi bado hazijabuni mikakati thabiti kuhakikisha wanafunzi watazingatia kanuni ambazo zimetolewa na Wizara ya Afya kuhusu maambukizi ya virusi vya corona.

Hali hiyo imezua wasiwasi miongoni mwa wazazi, ambapo wengi wameeleza kutoridhishwa na mikakati ambayo serikali imechukua kutayarisha shule kukabili hali hiyo mpya.

Hilo linajiri huku maafisa wa elimu katika vitengo mbalimbali wakiendelea na harakati za mwisho mwisho kuhakikisha wanafunzi wote wamerejea shuleni.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, wadau wengi wa elimu, miongoni mwao wazazi, walieleza kutoridhishwa na hali ilivyo katika shule nyingi.

“Inasikitisha kuwa serikali inasisitiza kuhusu haja ya wanafunzi kurejea shuleni wakati shule zenyewe ziko katika hali mbaya kimiundomsingi. Baadhi ya madarasa yameharibika. Madirisha hayapo kati ya matatizo mengine. Haya ni mambo yanayopaswa kushughulikiwa kabla ya wanafunzi kurejea,” akasema mzazi ambaye hakutaka kutajwa.

Walimu wakuu wa shule kadhaa walisema shule nyingi hazina madarasa ya kutosha kuhakikisha wanafunzi hawasongamani kwa mujibu wa kanuni ambazo zimetolewa na serikali.

Vile vile, imekuwa vigumu kwa shule nyingi, hasa zilizo katika maeneo ya mashambani na mitaa ya mabanda, kupata maji ya kutosha kuhakikisha wanafunzi wananawa mikono kila mara.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo jana, Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Wazazi (NPA), Bw Nicholas Maiyo, alisema wanafahamu kuhusu changamoto hizo, ijapokuwa wazazi wanafaa kushirikiana na serikali katika kutatua hali hiyo.

“Huu umekuwa mwaka mgumu kwetu sisi sote. Hivyo, ni muhimu wadau wote kushirikiana badala ya kuelekezeana lawama ili kuhakikisha wanafunzi wanarejelea masomo yao licha ya ugumu ambao umekuwepo,” akasema Bw Maiyo.

Hata hivyo, mshirikishi mkuu wa Vuguvugu la Elimu Yetu, Bw Joseph Wasikhongo aliilaumu serikali kwa kutochukua hatua zozote kuimarisha hali za shule kabla ya wanafunzi kurejea.

“Serikali haijachukua hatua za kutosha kuhakikisha mazingira ya wanafunzi ni salama wanaporejelea masomo. Inapaswa kuwa imeweka juhudi zaidi kuliko hali ilivyo sasa,” akasema Bw Wasikhongo.

Mnamo Septemba, Rais Uhuru Kenyatta alizindua mpango wa Sh1.9 bilioni kuziwezesha shule kupata madawati mapya yanayoziungatia kanuni za kukabilki corona.

Serikali pia ilitangaza mpango wa kuziwezesha shule kupata fedha ili kuimarisha miundomsingi yake zinapojitayarisha kuwapokea wanafunzi.

Licha ya ahadi hiyo, walimu wakuu wengi wanasema bado hawajapokea fedha hizo kumaanisha hakuna dawati za kutosha shuleni.Hata kama dawati zingekuwemo, bila madarasa ya kuhakikisha wanafunzi hawakaribiani itakuwa vigumu kuzingatia kanuni za kuzuia corona.

Licha ya malalamishi hayo, Waziri wa Elimu George Magoha amesisitiza kuwa shule zitafunguliwa kama iivyopangwa bila mabadiliko yoyote.Aliwaambia wazazi kuwatayarisha wanao kurejea shuleni, na hawapaswi kutoa visingizio vyovyote kwa kushindwa kuwanunulia vifaa kama vile barakoa.

Hata hivyo alikiri kuwa itakuwa changamoto kuhakikisha wanafunzi hawatangamani wakiwa shuleni.Aliongeza kuwa serikali itatoa usaidizi wa barakoa tu kwa wanafunzi ambao wanatoka katika familia maskini.

Prof Magoha pia aliwaambia wazazi ambao wanao walipata mimba wakati wakiwa nyumbani kuhakikisha wamerejea shuleni. Maelfu ya wasichana katika sehemu mbalimbali nchini walipachikwa mimba baada ya kuwa nyumbani kwa muda mrefu kutokana na janga hilo.

“Ujauzito si ugonjwa. Serikali itafanya kila iwezalo kuhakikisha kila mwanafunzi yuko shuleni,” akasema. Idadi ya walimu imepungua ingawa tume ya TSC ilitangaza kuwa itaajiri walimu 5,000 mwaka huu.

Matiang’i aagiza machifu kusaka wanafunzi watakaokaidi kurudi shule

Na George Odiwour

WAZIRI wa Usalama Dkt Fred Matiang’i ameagiza machifu kusaka watoto ambao watakosa kuripoti shule zitakapofunguliwa baada ya wiki mbili zijazo.

Waziri Matiang’i aliagiza makamishna wa kaunti, manaibu wao na machifu kuzuru shule zote kuanzia Januari 4, mwaka ujao ili kubaini idadi ya wanafunzi watakaokosa kuripoti.

Dkt Matiang’i aliyekuwa akizungumza alipojiunga na mke wa kiongozi wa ODM, Bi Ida Odinga, wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa maktaba katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Ogande, Kaunti ya Homa Bay, aliwataka machifu kurekodi idadi ya wanafunzi watakaokuwa shuleni kila siku.

“Machifu wanafaa kuandaa mikutano ya kuhamasisha watu katika maeneo yao kuhusu umuhimu wa elimu,” akasema.

Miongoni mwa wanafunzi wanaomulikwa na serikali ni wasichana ambao walipata ujauzito wakati wa likizo ndefu iliyosababishwa na virusi vya corona. Kwa mfano, wasichana 7,200 walipata ujauzito kati ya Machi na Desemba, mwaka huu, kulingana na Waziri Matiang’i.

Kwa mfano, wasichana 7,200 walipata ujauzito kati ya Machi na Desemba, mwaka huu, kulingana na Waziri Matiang’i.’Machifu pamoja na wasaidizi wao wanastahili kushirikiana na maafisa wa elimu kuhakikisha kuwa watoto wote wanarejea shuleni. Serikali haitakubali kisingizio cha aina yoyote,” akaongezea.

Bi Odinga aliitaka serikali kuhakikisha pia kuwa watoto wa kiume wanarejea shuleni.Alisema watoto wengi wa kiume wanajihusisha katika biashara na kazi mbalimbali na huenda wakakataa kurejea shuleni.

“Watoto wengi wa kiume sasa wanajihusisha na biashara za bodaboda. Wengine wanafanya kazi ya mjengo. Serikali ihakikishe kuwa wavulana hao wanarejea shuleni,” akasema.

Jinsi mafuriko yanavyoathiri shule zilizoko katika mitaa ya mabanda Nairobi

Na SAMMY KIMATU

skimatu@ke.nationmedia.com

SHULE nne katika mitaa ya mabanda ya Mukuru katika Kaunti ya Nairobi zitafungwa ikiwa serikali haitachukua hatua ya haraka kuzuia mafuriko yaliyosumbua kwa zaidi ya miaka mitano.

Shule hizo zinaathiriwa na mafuriko kila mwaka kutokana na unyakuzi wa ardhi katika kingo za mto Ngong.

Shule zilizoathirika ni pamoja na Shule ya Msingi St Bakhita, Shule ya Upili ya St Michael, Shule ya Upili ya Viwandani na shule ya msingi ya St Elizabeth.

Shule hizo nne ziko katika kaunti ndogo ya Makadara. Aidha, wanayakuzi wa ardhi ambao humwaga mchanga ndani ya mto na kulazimisha maji kupita kuelekea shuleni baada ya kujenga nyumba na vibanda katika kingo za mto.

“Mara tu wanapotupa tani za mchanga kwenye kingo za mto, maji husukumwa kuelekea shuleni. Hata baada ya shule hizo kulalamikia idara husika, hakuna hatua iliyochukuliwa, ’’ mwalimu mmoja ambaye hakutaka kutajwa katika vyombo vya habari alisema. Jitihada kali za bodi ya usimamizi wa shule hazijazaa matunda baada ya kuripoti kwa serikali ya kaunti ya Nairobi na Mamlaka ya Kutunza Mazingira Nchini (NEMA).

Jumatano, Taifa Leo iliona ukuta wa shule katika Shule ya Msingi ya St Elizabeth baada ya ukuta wa awali kuanguka kwa sababu ya mafuriko.

Ukuta wa shule katika Shule ya Msingi ya St Elizabeth. Picha/ Sammy Kimatu

Mwaka 2019 mafuriko yalilazimisha zaidi ya wanafunzi 1,300 katika shule hiyo kukaa nyumbani. Kina cha kilikuwa takribani futi nne katika eneo yoye ya shule.

“Kila mwaka, tunalazimika kuwarudisha wanafunzi nyumbani kwa sababu maji hujaa kote shuleni huku nayo masomo yakivurugwa,” mwalimu mmoja wa Shule ya St Elizabeth akaeleza.

Kufuatia mafuriko, shule zinakabiliwa na gharama za ziada pia. Vivyo hivyo katika shule ya upili ya St Bakhita na St Michael, mambo sio tofauti.

Wafanyakazi walikuwa na shughuli nyingi wakijenga vizuizi vya maji nje ya ua la shule hizo ili kuzuia maji kuharibu ukuta baada ya wafanyabiashara kando ya Mto Ngong uliotamba kutoka barabara ya Likoni katika sehemu kati ya Daraja la Express kuelekea mtaa wa mabanda wa Mukuru-Maasai.

Mabwanyenye wamejenga nyumba za kukodisha na yadi za wafanyabiashara wa juakali zilizojengwa juu ya mchanga.

Mto umegeuzwa na kulazimisha maji kuelekea ukuta wa shule hizo mbili.

Raha kwa wachuuzi baada ya masoko kufunguliwa

NA KEVIN ROTICH

Baada ya shule kufungwa mwezi wa Machi kutokana na mkurupuko was virusi vya Korona, uuzaji wa vyakula, vifaa vya kuandika na pia sare za shule zilitatizwa.

Kutokana na ukosefu wa wanunuzi, wasambazaji walilazimika kuuza bidhaa zao kwa bei ya kutupa ili kuzuia hasara mkubwa.

Lakini agizo la serikali la kufunguliwa kwa shule wiki hii kwa awamu, ni jambo la kufurahisha kwa wachuuzi.

Mmoja wa waliohangaika ni wauzaji wa wa vitabu, kalamu na pensili Merge Sationer katika kaunti ya Kajiado, kaunti ndogo ya Ongata Rongai.

Minica Gathesha anasema uuzaji ulipungua kwa hadi asilimia sufuri kutoka mwezi wa machi.

“Kutoka machi, hatujauza chochote kwani bidha za Januari bado zipo kwenye duka letu,” Bi Gathesha anasema.

Lakini anatarajia ununuzi kupanda kwa asilimia themanini hadi mia moja kuanzia wiki hii wanafunzi wanaporejea shuleni mwao.

“Ni wakati mdogo tu kabla ya hali ya kawaida kurejea,” anasema.

Mwezi wa Oktoba 6, serikali ilitangaza kufunguliwa kwa shule hasa kwenye madarasa ya nne, nane na kidato cha nne kuanzia wiki hii baada ya kufungwa kwa Zaidi ya miezi mitano kutokana na virusi vya korona.

Kulingana na masharti mapya yaliyotelewa na Waziri wa Elimu George Magoha, muhula wa pili utachukua zaidi ya wiki kumi na mmoja.

“Wizara ya elimu inawajulisha ya kuwa kufunguliwa kwa mashule kwa awamu itaanza na darasa la nne, nane na pia kidato cha nane wiki hii,” Profesa Magoha alisema ijuma wiki iliyopita kupitia ujumbe.

Patrick Wanjohi ambaye usambaza mboga katika mashule kwenye eneo la Kasarani mjini Nairobi anasema uuagizaji ulipungua kwa asilimia tisini.

Alikuwa akisambaza zaidi ya kabegi 5, 000 kila mwezi kwa Sh20.

“Ijapo shule zimefunguliwa, bado hatujaponea kwani uharibifu uliofanyika kwenye Uchumi ni mkubwa sana. Biashara itafunguka kidogo lakini bado tunangoea hali itakavyo kuwa,” anasema.

Muhula wa pili utaanza Oktoba 12 hadi Desemba 23 ambapo wanfunzi watrejea majumbani kwa likizo ya krismasi kutoka December 24 hadi Januari 1, 2021 kabla ya kurejealea muhula wa tatu Januari 4 hadi Aprili 16.

Mitihani ya darasa la nane na kidato cha nne vitafanyika Machi mwaka ujao.

Bwana Wanjohi alilazamika kuuza mboga zake katika soko la Githunguri ili kupunguza hasara. Lakini, ilichukua siku tatu kuyauza. “Niliuza kwa Sh10, ambayo ni chini ya asilimia 50 ambayo nilikuwa nikiuza kabla ya virusi vya korona.

“Kwa sasa, nikiuza bidhaa za Sh12, 000 ya kabegi nina furaha,” anasema.

Kwa upande wake, Wangeshi Waithaka ambaye huuza sare za shule katika soko la Uhuru Market katika barabarea ya Jogoo mjini Nairobi anasema ameuza chini ya asilimia kumi kwa ujumla na rejareja kuanzia Machi.

“Kwa wastani, ningeuza zaidi ya sare mia tano lakini kwa sasa nauza chini ya hamsini kwa mwezi,” anasema. Anasema alilazimika kutumia pesa ambazo alikuwa amewekeza katika msimu wa Januari alipopungukiwa na hela.

Niliwatuma sita kati ya waajiri saba wangu kwa kuwa uuagizaji ulishuka. “Lakini, nimewaita watatu wao na wengine nikiwatarajia kurudi siku jumatatu,” anaongeza.

Wanafunzi watakao rudi mashuleni watatarajiwa kuvaa meski, kupimwa joto mwilini na kuzingatia hali ya juu ya usafi. Kutokana na hayo, amejitosa kuunda meski uagizaji ukitarajiwa kupanda wiki hii.

“Kwa sasa natengeneza maski kwa wanfunzi kwa wingi,” anasema. Anasii mashule kupatia tenda biashara ndogo ndogo hasa sare na bidhaa kadhalika za shule.

Nguo zake huuza kutoka Sh130 hadi Sh3, 000.