Vijana wataka vyuo vya kiufundi vianzishe masomo ya kidijitali

Na STEPHEN ODUOR

VIJANA katika Kaunti ya Tana River, wametaka mafunzo ya kisasa yatolewe katika taasisi na vyuo vya kiufundi ili kushawishi wengi wao kujiunga navyo.

Kulingana nao, taasisi hizo huchukuliwa kuwa za watu waliofeli katika elimu za msingi kwa vile mafunzo yanayotolewa yamejikita katika mbinu za zamani za utendakazi ilhali jamii ya sasa ni ya kidijitali.

“Hakuna mtu ambaye angependa kujifunza mambo ambayo yamepitwa na wakati katika enzi hizi,” akasema kiongozi wa vijana, Bi Asha Shehe.

Alidai kuwa, baadhi ya vijana waliopokea mafunzo kuhusu masuala ya umeme waliamua kufanya kazi ya bodaboda baada ya kukosa ajira zilizolingana na masomo yao, huku wengine kama vile fundi wa mifereji wakikosa ajira kwa vile mbinu walizofunzwa zilipitwa na wakati.

Waziri wa Elimu katika kaunti hiyo, Bw Abbas Kunyo alisema utawala uliopo unazingatia masuala hayo na tayari kuna mikakati ambayo ilikuwa imeanza kutekelezwa.

Bw Kunyo alisema mojawapo ya mikakati iliyoanzishwa ni kuwapa wahadhiri mafunzo ya kidijitali, ndipo wawe na uwezo wa kufunza mbinu za kisasa za utendakazi.

“Ukweli ni kuwa idadi ya wanafunzi katika taasisi zetu imekuwa ikiongezeka katika miaka ya hivi majuzi ikilinganishwa na zamani. Katika miezi ijayo, mtashuhudia wenyewe kozi mpya ambazo tutaanzisha,” akasema.

FAUSTINE NGILA: Usilie ughali wa mafuta, nunua gari la kielektriki

NA FAUSTINE NGILA

MAGARI mengi yanayomilikiwa humu nchini na duniani kote yanatumia dizeli au petroli, mafuta ambayo yanachafua mazingira na kutishia maisha ya vizazi vijavyo.

Najua pia kwa wale ambao bado wana ndoto ya kumiliki gari, wanapanga kununua gari linalotumia mafuta kwa kuwa hayo ndiyo magari wanayoona kwenye barabara.

Hawaoni magari ya kielektroniki kwa wingi.Ni kweli kuwa magari ya kielektroniki ni machache, lakini tangu yaingie humu nchini kuanzia 2015, kumekuwa na mjadala muhimu kuhusu iwapo madereva wataendelea kununua mafuta ambayo ni ghali na yanayochafua mazingira au watanunua magari ya kielekntroniki yasiyotoa moshi na yanayohitaji kutiwa chaji kama simu.

Tunaishi katika enzi ambapo mafuta machafu yanaendelea kuchafua anga na kuchangia majanga duniani kama vile mvua kupita kiasi inayosababisha mauti kutokana na mafuriko, mioto ya kila mara kutokana na joto la kiajabu, kuongezeka kwa maji baharini na kuyeyuka kwa theluji milimani kwa kasi isiyowahi kushuhudiwa.

Nimejionea Wakenya wengi wakifurika mitandaoni kuilaani serikali kwa kupandisha bei ya dizeli, petroli na mafuta taa kila mara, lakini wanasahau kuwa mustakabali wa kawi upo kwa vyanzo visivyochafua mazingira kama vile umeme kutokana na miale ya jua, mvuke au upepo.

Ingawa kuna mbinu nyingi za kuhamia kwa magari ya kielektroniki (kielektriki, ukipenda)Kenya yahitaji sera za kudhibiti jinsi magari yanayotumia mafuta yatahifadhiwa au sehemu zake kutumiwa upya, tusije tukajaza taka za kielektroniki tunapoboresha hewa tunayopumua.

Aidha, ni Wakenya wachache tu ambao wanaelewa jinsi injini za magari haya hufanya kazi. Hawajui pia ni wapi kuna vituo vya kuchaji magari ya aina hii. Inamaanisha kuwa hamasisho linahitajika ili wananchi waelewe tija ya ninachozungumzia.

Gharama

Kwa kawaida, gari la kieletroniki litakuondolea gharama ya kununua mafuta. Ni gari ambalo baada ya kuchaji unaweza kuliendesha kwa zaidi ya kilomita 500 ambapo ungetumia mafuta ya Sh5,000. Betri yake nayo hubadilishwa baada ya kati ya miaka minane na kumi.

Hata hivyo, itakuwa safari ndefu kwa Kenya kufikia lengo hili, ikizingatiwa kuwa umeme hata jijini Nairobi hupotea kila mara.

Hali hii sasa inahitaji matumizi ya kawi ya jua ambayo serikali tayari imependekeza sera hasi zinazozuia matumizi yake kule vijijini.

Ni sera hizi ambazo zinafaa kuondolewa ili kuwaruhusu wamiliki wa magari kujenga vituo vya kuchaji magari popote wanapotaka nchini.

Serikali inafaa kupiga jeki mpango huu kwa kujenga vituo vya kuchaji katika barabara zote kuu, na kubuni sera ya kuwataka wamiliki wa vituo vya mafuta kuweka pia mashine za kuchaji magari haya.

Tayari kuna vituo vitatu jijini Nairobi, lakini jinsi dunia imebadilika huenda vituo hivyo vikaongezeka hata zaidi huku mataifa yanayounda magari yakisema kuwa hayatauza magari ya mafuta baada ya mwaka 2030.

Hivyo basi, tunafaa kujiandaa kisaikolojia, kiuchumi na kuweka miundomsingi ifaayo mapema ili kuenda na kasi sawa na mataifa yaliyoendelea.

Iwapo unamiliki gari la mafuta, sasa fahamu kuwa soko la mafuta litaporomoka.Tusipofanya hivi, basi tutakuwa tunachafua mazingira ambayo yanafaa kutumiwa na vizazi vijavyo ambavyo pia vina haki ya kuishi maisha bora.

FAUSTINE NGILA: Tuna kibarua kukuza miji ya kibiashara na kiteknolojia

Na FAUSTINE NGILA

SUALA muhimu lililojitokeza katika ziara ya Rais Uhuru Kenyatta nchini Uingereza wiki iliyopita, lilikuwa azma ya kufanya Nairobi kuwa jiji la kibiashara kimataifa.

Ilitangazwa pia kuwa kama kituo cha biashara barani Afrika, Nairobi ingetia saini mkataba mwingine na jiji la London, Uingereza, kuwezesha Kenya kujifunza mengi kuhusu usimamizi wa miji ya kibiashara.

Lakini kama tunavyojua, tumekuwa na mipango ya kuanzisha kituo kama hicho tangu Bunge lipitishe Sheria ya Kituo cha Biashara ya Kimataifa cha Nairobi mnamo 2007. Kwenye tovuti yake, kituo hicho kinafaa kuzinduliwa rasmi mwishoni mwa mwaka huu.

Lakini sioni hilo likifanyika.Sababu kuu ni kwamba hatujaweka miundomsingi ifaayo kwa kituo kama hicho.

Ukitazama kote duniani, miji ya kibiashara imekuwa ikijengwa mahali kuna mabenki, kampuni za ufadhili wa kifedha na masoko ya hisa.Itatubidi tuwekeze pakubwa katika sekta ya ujenzi na uuzaji wa majumba na maeneo makubwa, ili kutimiza azma yetu ya kujenga kituo hicho.

Rwanda, kwa mfano, imechukua mtindo huo. Mwaka uliopita, Rwanda ilipatia benki ya Equity – ya kutoka humu nchini – kandarasi ya kujenga jumba la Kigali Financial Tower ambapo kutakuwa na Kituo Cha Kimataifa cha Fedha cha Kigali.

Hapa kwetu, tumeanza vibaya kwani tayari hatuna eneo maalum ambako tunaweza kujenga kituo cha kimataifa cha kibiashara.Hii ni licha ya serikali kusema kuwa, mwekezaji yeyote ameruhusiwa kujenga kituo kama hicho popote nchini baada ya kupewa leseni.

Dunia ya sasa pia imetufundisha kwamba wawekezaji huvutiwa na mji wa kibiashara iwapo tayari kuna shirika la serikali la kutangaza, kuendeleza na kusimamia mji huo; pamoja na kuwa na kampuni ya kutoa leseni kwa biashara zote zilizo humo.

Pili, tunahitaji halmashauri huru ya kusimamia na kudhibiti wafanyabiashara wote katika eneo hilo maalum la kiuchumi.

Jijini Dubai, gavana wa benki kuu ndiye pia mwenyekiti wa Kituo cha Kimataifa cha Kifedha cha Dubai.Badala ya halmashauri kama hii, tulicho nacho kwa sasa ni kamati iliyojaa wanasiasa, wasioelewa jinsi kituo kama hiki kinafaa kuendeshwa.

Pia kunahitajika mahakama maalumu ya kutatua migogoro ya kibiashara miongoni mwa wawekezaji katika mji huo, ikitilia maanani sheria za kimataifa.

Upo wakati ambapo Wizara ya Fedha ilishirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege kutoa ardhi ambapo kituo hicho cha biashara ya kimataifa kinafaa kujengwa, lakini juhudi hizo sasa zinafaa kufuata mwongozo wa miji mingine ya kimataifa duniani Singapore na Hong Kong.

Ili kuvutia zaidi wawekezaji tutahitaji kumiliki asilimia 100 ya kampuni zinazokuja, na vile vile kuondoa ushuru mwingi unaotozwa kampuni za Kenya kwa sasa.

Kwa kuendelea kufanya utafiti kuhusu vituo vya kibiashara duniani, huenda tukajijengea kituo bora zaidi hapa Afrika.

Lakini iwapo tutashikilia mkondo tunaofuata kwa sasa, huenda mradi huu ukasambaratika kwa kujenga vitu vinavyofukuza wawekezaji.

Pia mradi unaweza kuishia kukwama kama ule wa Konza TechnoCity. Lazima tuwe makini sana.

FAUSTINE NGILA: Wapi utekelezwaji wa Ripoti ya Blokcheni?

Na FAUSTINE NGILA

NI miaka mitatu sasa tangu Ripoti ya Blockcheni na Akili Bandia (AI) iwasilishwe kwa serikali kwa ajili ya utekelezaji katika miradi ya kitaifa.

Lakini hakuna chochote Wizara ya Teknohama imeambia wananchi tangu ipokee ripoti hiyo ambayo ilipigiwa upatu kubadilisha utendakazi katika sekta za umma na kibinafsi nchini.

Ingawa suala la Blokcheni lingali geni kwa Wakenya wengi, serikali haijafanya lolote kueleza wananchi maana yake na umuhimu wake kwa taifa hili.

Kwenye mapendekezo ya ripoti hiyo, wanajopo wa Tume ya Blockcheni waliirai serikali itumie teknolojia hiyo katika sekta za afya, ardhi, fedha na elimu, lakini mafunzo na warsha kuhusu matumizi yake bado hazijaandaliwa.

Kufikia mwaka huu, Wakenya wanafaa kuwa na uelewa wa ndani kuhusu jinsi teknolojia hii inaboresha huduma, kwanza kwa kuzima ufisadi na kuwanasa wanaoiba fedha za umma.

Tunaelekea msimu wa siasa na hatimaye Uchaguzi Mkuu mwaka ujao, lakini wananchi hawana habari kuwa teknolojia ya blockcheni ina uwezo wa kuzima wizi wa kura na kuwafungia nje wanasiasa na wapigakura feki.

Hii ni teknolojia muhimu ambayo ina uwezo wa kuzima ghasia za baada ya kila uchaguzi, kwa kuitumia katika mchakato mzima wa kupiga kura, kuzihesabu na kutangaza mshindi.

Ni uvumbuzi wa kisasa ambao unawazuia wadukuzi ambao hunuia kuiba pesa au data za siri za watu, kampuni na serikali kwa kuwa unatambua kila mtu anayeingia mle ndani na kumwanika kwa umma papo hapo.

Iwapo wananchi watafahamishwa kuuhusu, utaweza kutumiwa kusimamia na kufuatilia matumizi ya fedha za serikali hadi kwenye kaunti, hali ambayo itawaogopesha wezi.

Tatizo la wizi wa fedha za kaunti hutokana na hali kwamba hela hizo hutolewa kutoka Hazina Kuu ambapo huibwa kabla ya kufikia serikali za kaunti litasuluhishwa na teknolojia hii.

Kila kaunti inaweza kugawiwa hela zake na kufuatiliwa kidijitali.Itakomesha mazoea ya wanasiasa kutumia wahasibu kuiba pesa kisha kufuta rekodi za wizi huo ili kuficha ushahidi.

Pia, mtindo wa baadhi ya wafanyabiashara na kampuni kukwepa kulipa ushuru utaisha huku rekodi za Blockcheni zikitumika kortini kuhukumu mafisadi.Lakini mbona mswada haujatua bungeni kujadili jinsi blockcheni itatumika, miaka mitatu baadaye?

Mbona serikali imenyamazia ripoti hiyo?Yamkini uroho na ubinfasi wa wanasiasa na washauri wa serikali ndio kikwazo kikuu katika mpango mzima wa kufumbia macho teknolojia yenye uwezo mkubwa.Labda wanajiuliza, tukitekeleza hii blockcheni tutaiba hela za umaa vipi? Tutanyakua mashamba vipi?

Tutaiba kura vipi? Tutatoa rushwa vipi?Yaani, kimsingi, wanasiasa walio serikalini wanaonekana kuigomea teknolojia hii kwa kuwa itawakata miguu, itawaondoa kwenye utafunaji wa mabilioni ya walipa ushuru, itawafilisisha!

Ni mwenendo ambao unafaa kukoma, na kila mfanyakazi wa serikali kuzoea kujizolea mali kwa njia halali. Bila hili, ripoti ya blockcheni itasalia tu kwa maktaba ya serikali ambapo kwa sasa inalamba vumbi.

Spika Muturi awarai madaktari watumie teknolojia kwa tiba

Na Ruth Mbula

SPIKA wa Bunge la Kitaifa, Bw Justin Muturi, amewarai wadau wa afya kuharakisha utekelezaji wa taratibu za kutumia teknolojia kutoa huduma za afya katika hospitali za humu nchini.

Bw Muturi alisema hospitali zinapaswa kukumbatia mfumo huo wa kisasa hususan wakati huu nchi inakabiliwa na janga la corona, kama njia ya kutimiza malengo ya kitaifa ya kutoa Afya kwa Wote (UHC).

Haya yanajiri huku wizara za Afya na Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) zikitangaza kuwa zinaendesha mikakati kushinikiza matumizi ya teknolojia katika sekta ya afya nchini. Wadau wanahoji hilo litapunguza mno maambukizi ya corona.

Bw Muturi alikuwa akizungumza Jumamosi alipofunga kongamano la sayansi la kila mwaka, la Chama cha Kitaifa cha Madaktari (KMA).

Kongamano hilo la siku tatu lilifanyika katika hoteli moja Kaunti ya Kisii na kuhudhuriwa na madaktari kutoka sehemu mbalimbali nchini.

Bw Muturi alisema kuwa Afya kwa Wote (UHC) ni mojawapo ya malengo makuu ya serikali yaliyo kwenye Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.

“Kutokana na idadi ndogo ya madaktari tuliyo nayo nchini, hatutaruhusu hali ambapo madaktari wetu wataendelea kuhamia katika nchi nyingine. Ni wakati tukumbatie matumizi ya teknolojia katika sekta hii ili kuboresha huduma tunazotoa,” akasema.

FAUSTINE NGILA: Jihadhari na matapeli wa sarafu za kidijitali

Wataalamu wakagua uvunaji wa bitcoin katika kituo cha Bitfarms eneo la Saint Hyacinthe, Quebec, Canada hapo zamani. Bitcoin ni sarafu ya kidijitali inayokubalika kama mbinu ya malipo kote duniani, na ndiyo sarafu kongwe zaidi ya kidijitali duniani. Picha/Maktaba

Na FAUSTINE NGILA

Katika kipndi hiki cha mahangaiko kutokana na athari za janga la corona, nimepokea malalamishi mengi kutoka kwa Wakenya kuhusu jinsi wamelaghaiwa mamilioni ya pesa wanapojaribu kuwekeza katika sarafu za kidijitali.

Ni mwaka jana tu ambapo mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda alipojitia kitanzi baada ya kupoteza Sh500,000 katika kipochi cha dijitali, na kuibua swali la ni hadi lini wawekezaji wataendelea kupunjwa kutokana na ukosefu wa maarifa kuhusu sarafu kama Bitcoin, Ethereum, Dogecoin, Ripple na Tether.

Soko zima la sarafu za kidijitali nchini limekumbwa na changamoto za ugumu wa kueleweka na mfumko wa thamani yake usioweza kubashiriwa. Lakini ripoti iliyotolewa wiki iliyopita na kampuni ya Mastercard inaonyesha kuwa asilimia 40 ya Wakenya wako tayari kuwekeza katika majukwaa haya hata ingawa hawana elimu inayohitajika.T

atizo kuu la vijana wa humu nchini ni kwamba wana tamaa ya kuitwa mabwanyenye katika kipindi cha muda mfupi, na ndiyo maana wanawekeza pesa bila kuelewa mbinu bora ya kufanya hivyo, na kuishia kupoteza kila kitu.Ripoti ya Citibank inaonyesha kuwa Kenya ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yanayomiliki idadi kubwa ya sarafu za dijitali.

Utafiti mwingine wa Paxful unafichua kuwa katika kipindi cha corona, Wakenya waliwekeza zaidi kwenye sarafu hizi, kima cha Sh5 bilioni.

Nilipomtembelea Bi Beatrice Wanjiru katika mkahawa wake mjini Nyeri ambao unakubalia malipo ya sarafu za dijitali kama Bitcoin, Bitcoin Cash na Dash, niling’amua kuwa vijana wa mijini hawaelewi maana ya sarafu za kidijitali.

Alikiri kuwa kwa wakati mmoja, pia yeye alipoteza Bitcoin za thamani ya Sh500,000 kwenye tukio la wizi mtandaoni, wakati ulingo huo ulipokuwa ungali mpya nchini.

Ni kutokana na wizi huu ambapo benki kuu za Kenya, Uganda, Tanzania, Malawi, Zimbabwe, Nigeria na Afrika Kusini zimewaonya raia wao dhidi ya kuwekeza katika sarafu hizi kwa kuwa “hakuna usalama wowote mitandaoni na majukwaa hayo hayajadhibitiwa na serikali”.

Nikimhoji afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Amerika, Paxful inayoeneza elimu ya sarafu hizi duniani, Bw Ray Youssef, alisema ni hatua nzuri kwa mataifa hayo kutahadharisha raia dhidi ya kuwekeza kwenye biashara wasiyoielewa.

Ni wazi kuwa wakati wafanyabiashara wa mitandaoni wanapoteza hela zao kutokana na udukuzi, serikali hupatwa na hofu.Hata hivyo, watu wengi wanaopoteza fedha zao ni wale wazembe wasiopenda kusoma wala kutafiti kuhusu jambo baada ya kulisikia.Wengi ni wale wa tabaka la kati na juu wenye hela za ziada, lakini kukosa juhudi za kujielimisha kumewaponza.

Jihadhari na matapeli wa sarafu za kidijitali, mwanzo ujue kuna zaidi ya sarafu 9,000 kote duniani. Kuna zile za hakika na nyingine hewa ambazo zitakuhadaa kuwa zina thamani kisha kuporomoka baada ya wiki chache.

Hufai kuisubiri serikali au kampuni yoyote ile ikuelimishe kuhusu masuala haya, unafaa kujielimisha mwenyewe kwani taarifa za kuaminika ziko mitandaoni bila malipo.Kukosa kufanya hivi kutakuletea balaa. Utaendelea kulaghaiwa hela ulizosaka kwa jasho jingi, na kujutia kwa nini hukuwekeza muda wako katika kuelewa mwanzo unachokifanya.

Usiwasikilize wenzio wakidai hela haziwezi kuibwa kwenye kipochi cha dijitali, chukua muda wako na kutafiti ni kwa nini watu wengi wamepoteza nywila za akaunti zao na kupoteza hata mabilioni ya pesa.

FAUSTINE NGILA: Tuwazime wafisadi iwapo tunataka teknolojia itufae

Na FAUSTINE NGILA

Inashangaza kuwa licha ya Kenya kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiteknolojia, karatasi bado zinatumika katika sekta mbalimbali humu nchini.

Sekta za bima, uanasheria, ardhi na afya zimelemewa kabisa kuongeza kasi ya huduma kwani bado zinategema karatasi ambazo huharibu wasaa na hata kupandisha gharama ya huduma.

Utapata kuwa mteja amekuwa akilipia bima ya afya, lakini anapohitaji hela hizo kutibiwa, hospitali na kampuni za bima zinachukua miezi mine kutoa zile hela za malipo.

Mchakato mzima hutumia zaidi ya stakabadhi nane za karatasi lakini kwa kutumia teknolojia, hatua zote za gharama ya matibabu zinaweza kuchukua siku moja tu.

Kwa sasa tunaelewa kuwa kuendelea kukwamilia mifumo ya kikale, hasa katika uanasheria, kumechelewesha kuamiliwa kwa maelfu ya kesi, na hivyo kuwanyima wananchi haki yao ya kikatiba.

Na ingawa Tume ya Ardhi Nchini (NLC) Jumatatu ilitangaza kuhamisha michakato yote kuhusu umiliki wa ardhi kwa mfumo wa kidijitali, pengo kubwa linalowapa mafisadi msukumo wa kubadilisha stakabadhi lafaa kuzimwa.

Hongera kwa NLC kwa kukubali kuwa umefika wakati wa vipande vya ardhi nchini kuuzwa au kumilikiwa kupitia stakabadhi za kidijitali, lakini inafaa kutambua kuwa wakora pia wana uwezo wa kutumia teknolojia hiyo kunyakua mashamba.

Si mara moja ambapo kumeripotiwa wizi wa fedha za umma katika mfumo wa serikali wa malipo maarufu kama Ifmis, ambao ulipozinduliwa ulisemekana kuwa ungemaliza ufisadi.Kilichofuata ni kinyume chake.

Maafisa wa serikali walikuwa wanatoa nywila zao kwa watu wasioruhusiwa kuingia kwa mfumo huo na kufanikisha malipo ya huduma hewa.Wengine walitengenezea watu wa familia zao akaunti kufanikisha utoaji wa hela kupitia kampuni zao wakidai zimepewa zabuni na serikali.

Hivyo, katika mradi wowote ule wa teknolojia unaohusu hela au mali ya thamani kama ardhi, hulka ya watu walioajiriwa kuusimamia inafaa kuchunguzwa kwa makini.

Watu wenye ushawishi mkubwa wa kifedha wanaweza kutumia wale maafisa wa chini kupata chochote watakacho mle ndani, na kujaribu kutoboa siri kama hizo ni kama kujiitia mauti.

Hali ni sawa katika sekta ya uanasheria ambapo visa vya faili muhimu za kesi kutoweka kwa njia isiyoeleweka si vigeni.Inapojaribu kuhamia mitandaoni, Tume ya Huduma za Mahakamani (JSC) yafaa kujua kuwa kufaulu kwake kutategemea jinsi majaji na mahakimu wanajitolea kukabili ufisadi.

Nimejionea kuwa licha ya uwepo wa teknolojia zinazoweza kuzima ufisadi kabisa kama blockchain, maafisa wa serikali bado hawako tayari kukumbatia ubunifu huo kutokomeza wizi wa mali ya umma.

Kwa yakini, teknolojia pekee haiwezi kuzima maovu yanayoendelea katika mashirika ya kiserikali, tunahitaji kukemea ufisadi, la sivyo, kuunda mifumo ya kidijitali kutakuwa ni kurahisisha ufisadi.

Tunafaa kuona adhabu kali zikitolewa dhidi ya maafisa wenye uroho wa kumumunya mamilioni ya walipa ushuru ili kuhakikisha mtindo huo haufikii mifumo ya kiteknolojia inayorahisisha huduma.

Biashara ya mitandaoni yawaletea Wakenya fursa mpya ya uwekezaji

Na MASHIRIKA

Kutokana na ongezeko la matumizi ya simu tamba na za kisasa pamoja na kuimarishwa kwa mitandao, imekuwa rahisi kwa idadi kubwa ya Waafrika kutumia intaneti katika maisha yao ya kila siku, kama vile kupata habari za aina mbalimbali, kujiburudisha, hata kuuza na kununua bidhaa mtandaoni.

Takwimu zinaonyesha kuwa, hivi sasa watumiaji wa mtandao nchini Kenya wamezidi milioni 43, na biashara ya mitandaoni imeibuka kuwa eneo la fursa mpya za ajira, na kuwavutia wawekezaji wa kigeni nchini Kenya. Kwa sasa majukwaa ya biashara ya mitandaoni yanayojulikana nchin Kenya ni pamoja na jumia , kilimall, jiji, na amambo.

Joseph Odhiambo, baba ya watoto wawili na mwendeshaji pikipiki za uchukuzi amefika kila pembe ya jiji la Nairobi. Kazi yake ya kuwafishia bidhaa walizoagiza mitandaoni imelazimu kifika kila pembe ya jiji hili na kumkutanisha na watu wa matabaka tofauti.

Kuwepo kwa simu za kisasa na huduma za intaneti kumemuwezesha Bwana Odhiambo na wenzake kujiunga na msururu huu mrefu wa biashara ya kisasa.

Kuwepo kwa fursa za biashara na uwezo wa kununua kumewavutia wawekezaji wa kigeni kuanzisha biashara ya mtandaoni jijini Nairobi na Kenya kwa jumla.

Angela Lei ametokea nchini China ambako biashara ya kuuza na kununua bidhaa mtandaoni imepiga hatua kubwa. Lei alianza biashara ya kuuza bidhaa hasa za elektroniki mtandaoni mwaka 2016.

“Biashara yamtandaoni ni tasnia inayoendelea kuongezeka, tangu janga la corona kubisha ulimwenguni, watu wengi zaidi wananunua bidhaa mitandaoni, biashara yetu imenoga, hivi sasa napata zaidi ya wateja 3,000 kwa siku,” anasema Bi. Angela Lei.

Ikilinganishwa na maduka ya kawaida, kuendesha biashara mtandaoni ni jambo rahisi sana. Mfanyabiashara hahitaji hela nyingi kuanzisha na kuendesha aina hii ya biashara.

Susan wangare, mwanafunzi wa chou Kikuu cha Kenyatta ni miongoni mwa Wakenya ambao wamekumbatia ununuzi wa bidhaa mitandaoni. Kupitia kwa simu yake ya mkononi, Susan anaagiza saa na chakula kutoka duka la Annov.

“Leo nimenunua saa na rinda, ni rahisi kununua bidhaa mitandaoni kuliko kusumbuka mjini ukitafuta maduka ya kuuza bidhaa.”

Biashara hii imeongeza nafasi za ajira nchini kufuatia ukuaji wake wa kasi. Ripoti ya halmashauri ya mawasiliano nchini Kenya CA inaeleza kuwa biashara hii hukua kwa kasi ya 40% kila mwaka. Joseph Odhiambo anakiri kuwa ni kutokana na biashara hii ndipo amefanikiwa kuwapeleka wanawe shule na kukidhi mahitaji yake ya kimsingi.

“Siwezi lalamika sasa, maisha yangu yamebadilika kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita kutokana na kazi hii. Ona watoto wangu wanaenda shule, siwezi lala njaa kama kitambo.”

Kenya, Nigeria na Afrika kusini zinaongoza kwa kufanya biashara ya mitandaoni barani Afrika huku bidhaa nyingi zikiagizwa kupitia kwa simu za mkononi. Nguo,saa, viatu na simu zikiwa baadhi ya bidhaa ambazo huagizwa kwa wingi hapa nchini kutoka maduka kama vile Amazon, Alibaba, AliExpress na Jumia.

CRI

FAUSTINE NGILA: Mitandao yabadili sura ya maandamano nchini

NA FAUSTINE NGILA

KWA wiki nzima, Wakenya wamepiga kambi katika mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook kuishinikiza Hazina ya Kimataifa ya Fedha (IMF) kukoma kuikopesha Kenya pesa.

Wakenya walifoka kila aina ya matamshi kuonyesha kero lao kwa mtindo wa serikali wa kukopa mabilioni kila mwaka, wakidai hela hizo huibwa na maafisa wa serikali na kuwaacha kwa umaskini zaidi.

Hii ni aina mpya katika uanaharakati, ambapo wananchi wanatumia uwezo mkubwa wa teknolojia kutoa malalamishi yao na kuwafikia walengwa kwa muda mfupi.

Ni unaharakati ambao uliilazimisha IMF kuchapisha taarifa ndefu katika tovuti yake ikiwaelezea Wakenya sababu ya kuikopesha serikali ya Rais Uhuru Kenyatta Sh257 bilioni.

Kando na unaharakati wa zamani ambao hutegemea maandamano barabarani watu wakiinua mabango yenye maandishi ya kupinga sera, uanaharakati wa mitandaoni unaonekana kubadilisha kabisa matumizi ya nguvu na makabiliano na polisi barabarani.

Ni mtindo mpya ambapo wanaotetea haki zao hujificha chini ya majina feki kwenye Twitter na Facebook, hali inayowapa nguvu za kuandika kila aina ya maneno mazito na mabango ya kidijitali yenye jumbe kali.

Maandamano ya zamani yaliwatia hofu wanaharakati, hasa wale wenye biashara. Waliogopa kukomolewa na polisi, kushtakiwa baadaye au kupoteza wateja, kwa kuwa nyuso zao zingeonekana kwa runinga.

Ingawa IMF haikufuta uamuzi wake wa kuipatia Kenya mkopo, ilitambua shinikizo za kipekee ilipojaribu kuongoza mkutano wa mitandaoni Facebook ambapo Wakenya walifurika kuikumbusha Kenya ni taifa fisadi lisilojua kutumia vizuri hela za deni.

Kwenye tovuti mbadala, Wakenya walifikisha saini zaidi ya 200,000 kwenye jukwaa la ##SignThePetition wakitia presha IMF kusitisha mkopo ule.

Kwa kawaida, maandamano huongozwa na wanaharakati kama hamsini hivi lakini wiki iliyopita, kila Mkenya anayemiliki simu ya kisasa alichangia katika sauti ya pamoja ya kutangazia dunia kuwa Kenya inaongozwa na viongozi fisadi.

Kati ya Wakenya hao wote, ni mmoja tu, Mutemi Kiama, aliyekamatwa na polisi, ila yeye naye alichapisha bango la kidijitali la kijasiri zaidi ambalo serikali ilihisi lilikiuka sheria za maadili ya mitandaoni.

Ni picha ambayo ilichochea hisia miongoni mwa Wakenya, na kusambazwa katika kila kundi la WhatsApp, lakini hilo halikuzuia IMF kukatiza mchakato wa kuipa serikali mabilioni.

Kelele hizo zote ziligeuka kuwa za chura tu, zisizoweza kumzuia ng’ombe kunywa maji kwani Wakenya wengi hawakuchunguza kwa nini IMF ilikubali kutoa hela hizo.

Ni kweli kuwa asilimia kubwa ya pesa za mikopo huishia mifukoni ya maafisa wa ngazi za juu serikalini, lakini ingawa mitandao ya kijamii inawapa wananchi jukwaa la kukosoa serikali, wanafaa pia kufanya utafiti wa kina kuhusu sababu za maandamano yao.

Serikali ya Kenya haina uwezo wa kutoa hela kwa wananchi kukabili makali ya corona kama yalivyofanya mataifa yaliyoendelea, hivyo mkopo huo utatumika kuhakikisha hela zinasambaa katika uchumi, usije ukakosa huduma au bidhaa muhimu.

Hata hivyo, ni wito kwa maafisa wa serikali kukomesha wizi wa mabilioni ya pesa za wananchi. Lakini nao wananchi wasikome hapo, waanzishe hashtegi za kutimua wezi hao.

FAUSTINE NGILA: Heko AU kuunda teknolojia ya paspoti za kidijitali

NA FAUSTINE NGILA

Je, unafahamu kuwa safari zote za ndege sasa zinawalazimu wasafiri kuwa na paspoti ya corona kando na ile ya kawaida? Mataifa yaliyoendelea yalikuwa ya kwanza kuleta mfumo huu lakini sasa bara la  Afrika limekumbatia teknolojia mpya ya paspoti za kidijitali.

Ni mtindo ambao utandelea kutumika katika viwanja vya ndege kote duniani, hata iwapo maambuziki mapya ya corona yatapyngua.

Kwa hili, mataifa ya Afrika, licha ya kukosekana kabisa katika juhudi za kuunda chanjo ya corona, raundi hii yamekuwa miongoni mwa mataifa ya kwanza kuunda paspiti ya kidijitali kwa kutumia teknolojia yake yenyewe.

Kampuni za ndege za Afrika tayari zimeanza kukumbatia teknolojia hiyo iliyoundwa na Umoja wa Afrika (AU) kurahisisha usafiri, katika kipindi ambapo usafiri wa ndege umelemazwa na ukosefu wa vipimo na vyeti vya corona.

Kampuni za Kenya Airways na Ethiopian Airlines zimeungana na Shirikisho la Usafiri wa Angani Afrika Magharibi na Kati (ASKY) kutumia mfumo wa kidijitali wa PANABios unaoendeshwa na AU ikishirikiana na Vituo vya Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC).

Jukwaa hilo la kidijitali kwa jina Trusted Travel Pass litawezesha abiria kuthibitisha vipimo vyao na vyeti vya corona kwa haraka kabla ya kupanda ndege, ithibati kuwa Afrika sasa imekomaa kiteknolojia na inaweza kujitegemea.

Ingawa teknolojia za mabara mengine bado zipo, AU imeonekana kuwa mstari wa mbele kuhamasisha mataifa yote kutumia teknolojia hiyo kama njia moja ya kusaidia kampuni za ndege brani kuongoza mapato katika kipindi hiki kigumu cha biashara.

Wateja sasa wanafurahia safari za angani bila bughudha wakitumia paspoti za kidijitali, kwani zimewawezesha maafisa katika viwanja vya ndege kutambua iwapo abiria wamechanjwa na kama wametimiza masharti ya kudhibiti virusi vya corona.

Binafsi nimependezwa na juhudi za AU kwa kuhakikisha bara la Afrika lina mtandao wake wa kuthibitisha vipimo vya corona kupitia kwa maabara, hali ambayo inahakikisha biashara inaendelea kama kawaida miongoni mwa mataifa ya Afrika.

Kwa mara ya kwanza, Waafrika tumeungana kukataa teknolojia za majuu ambazo gharama yake iko juu, na kujikubali kwamba tuna ubunifu wa kutosha kuoambana na changamoto ztu wenyewe.

Hata hivyo, baadhi ya mataifa bado yanazembea kuchangamkia jukwaa hilo, hata wakati yanajua fika kuwa vyeti vya corona vya kidijitali vinahitajika iwapo taifa linafanya biashara ya uchukuzi wa angani.

Mataifa hayo yanapaswa kukoma kutilia shaka juhudi za AU, kwani teknolojia yake imeundwa kwa kiwango cha kimataifa kuwajali Waafrika wote bila ubaguzi na kutokomeza ufisadi katika sekta ya afya, huku ikipunguza gharama ya vipimo vya maabara.

Cha muhimu ni kuwa huu ni mfumo ambao utatusaidi kukusanya data yetu binafsi kutuwezesha kufanya maamuzi ya kibiashara haraka, kando na mazoea ya mabara mengine ya kukama data katika uchumi wa Afrika bila hata kulipia senti.

Iwapo mfumo huo wa PANABios  utatumiwa na mataifa yote, utaboresha usimamizi wa sera kote Afrika na kuinua biashara baina ya mataifa, kupiga jeki utalii, uwekezaji na utamaduni, na hatimaye kuhakikisha Afrika haiachwi nyuma na mabara mengine katika maendeleo.

 

Corona ilivyoyasukuma makanisa kuchangamkia teknolojia

Na MWANGI MUIRURI

Athari za ugonjwa hatari wa Covid-19 zimechangia kusukuma makanisa hadi kukumbatia Tenknolojia za kimawasiliano (IT) kuwafikia waumini wao wanaozidi kuzimwa kufika kanisani.

Huku awali wahubiri wengi wakitumia mitandao ya facebook, Twitter, WhatsApp na jumbe za moja kwa moja hadi kwa simu za mikononi mwa waumini, hali imebadilika baada ya kutambuliwa kwamba sio washirika wengi huwa na uwezo wa kununua simu mwafaka za kuingia katika intaneti na ikiwa wako nazo, uwezo wa kununua mbado za data au ufahamu wa kutegea mahubiri hayo ni finyu sana.

Ndipo wahubiri wanang’ang’ana sasa kusajili vituo vya radio na pia runinga ili kuwawezesha kuwafikia waumini katika manyumba yao.

Hapo ndipo sasa ushindani mkuu wa Kunasa washirika uko kwa kuwa kufungulia runinga au radio hakuna ule utiifu wa imani kwamba ikiwa Basi kanisa langu haliko angani kunihubiria basi sitawasikiliza wale wanaonifikia.

Tayari, kuna zaidi ya vituo 15 vya runinga ambavyo vimezinduliwa na makanisa huku pia kukiwa na zaidi ya vituo 10 vya radio vya kuwafikia washirika.

Wale ambao hawajaweza kuzindua runinga au radio wamenunua nafasi katika vyombo vya habari hapa nchini ya kuwawezesha Kutoa mahubiri yao.

Kanisa la Kipresibeteria hapa nchini (PCEA) tayari limeelekeza matawi yake yote yaliyo katika Kaunti za Nairobi, Kiambu, Kajiado, Nakuru na Machakos yazindue misa za kimitandao ambapo linawataka wachungaji wao wawe wabunifu katika kuwafikia washirika wao.

Hii ni baada ya Kutoa amri pia makanisa hayo yote ndani ya hizo Kaunti tano yasistishe ibada zao zote mara moja kwa mujibu wa amri ya rais Uhuru Kenyatta.

Alhamisi, rais aliorodhesha kaunti hizo tano kuwa zilizoambukiwa kwa kiwango kikuu maradhi ya Covid-19 yanaosababishwa na virusi vya Corona na kwa kutii ushauri wa wataalamu wa Kiafya, akaziwekea vikwazo vgya kutangamana.

Katika amri yake, rais alisitisha kuingia au kutoka kwa Kaunti hizo ambazo zote ziko katika mduara mmoja wa ujirani lakini akawakubalia wao wenyewe kutembeleana akisema kufanya hivyo ni kusaka mbinu ya kuzima uenezaji hadi mashinani ya kwingine nchini kupitia shughuli za uchukuzi.

Rais Kenyatta aliambatanisha amri hiyo na kuzima ibada zote za makanisa katika mduara huo wa Kaunti tano, sasa kanisa hili la PCEA likitii na kuwaelekeza wachungaji wake wazindue mikakati ya kuwafikia waumini wao kupitia njia za kiteknolojia.

Misa zote zitaathirika na amri hiyo ambapo hata wale watoto ambao hushiriki misa za ukombozi, utakaso na ubatizo wataahirisha harakati hizo hadi ushauri mwingine wa kufutilia mbali makataa hayo utolewe.

Katika barua iliyoandikwa na Kaimu Katibu Mkuu wa PCEA Askofu Paul Kariuki na kisha kutumwa kwa dayosesi zote za Kanisa hilo, ilisema kuwa pia ni lazima makanisa yote yake nchini yazingatie amri ya awali ya rais kuwa idadi ya watakaokuwa wakifika makanisani katika Kaunti zingine 42 ambazo hazikuathirika na makataa ya usafiri iwe ni asilimia 30 pekee.

Waumini wa kanisa hili ambao Taifa Leo iliongea nao waliunga mkono hatua hiyo wakisema watatii na waendelee kumuomba Mungu wakiwa katika makazi yao na pia walio na uwezo wakifuatilia misa katika mitambo ya kiteknolojia.

Nalo kanisa la Jesus Winner Ministries lake Askofu Edward Mwai likitangaza kuwa kuambatana na amri hiyo Rais Kenyatta, limeahirisha ibada makanisani katika Kaunti hizo tano.

“Ningewaomba washirika wetu wawe wakitegea mahubiri ya Askofu wetu kupitia runinga ya Mwangaza na pia kituo cha radio cha Mwangaza FM,” ikasoma taarifa kwa vyombo vya habari.

Ni amri ambayo inaonekana tayari kukumbatiwa na mengi ya maeneo ya ibada tayari tangazo sambamba na hilo likitoka kwa makanisa ya Kianglikana, AIPCA, ACC&S, Katoliki, Deliverance huku mengine yakitazamiwa Kutoa mwelekeo sawa na huo.

Kampuni za ndege Afrika zakumbatia teknolojia ya paspoti za kidijitali kuokoa biashara

NA RICHARD MAOSI

KAMPUNI za ndege za Afrika zimeanza kukumbatia teknolojia ya Umoja wa Afrika (AU) ya kuwapa abiria paspoti za kidijitali kurahisisha usafiri.

Kampuni za Kenya Airways na Ethiopian Airlines zimeungana na Shirikisho la Usafiri wa Angani Afrika Magharibi na Kati (ASKY) kutumia mtandao wa PANABios unaoendeshwa na AU ikishirikiana na Vituo vya Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC).

Bw Justus Thairu, afisa wa mauzo wa Kenya Airways alisema jukwaa hilo la kidijitali kwa jina Trusted Travel Pass litawezesha abiria kuthibitisha vipimo vyao na vyeti vya corona kwa haraka kabla ya kupanda ndege.

“Tunafurahia kushirikiana na AU na Africa CDC katika jitihada zao za kuhakikishia abiria usalama wa kiafya huku pia maambukizi mipakani yakipunguzwa,” alisema.

Akihutubu alipozindua matumizi ya teknolojia hiyo, afisa wa mawasiliano katika kampuni ya Ethiopian Airlines alisema ubunifu huo utasaidia kampuni hiyo kuongoza mapato katika kipindi hiki kigumu cha biashara.

“Wateja wa Ethiopian Airlines sasa wataweza kufurahia safari za angani bila bughudha wakitumia paspoti za kidijitali. Zitawawezesha maafisa katika viwanja vya ndege kutambua iwapo abiria wamechanjwa na kama wametimiza masharti ya kudhibiti virusi vya corona,” alisema kwenye taarifa iliyoonekana na Taifa Leo ilisema.

ASKY ilisema imependezwa na juhudi za AU kwa kuhakikisha bara la Afrika lina mtandao wake wa kuthibitisha vipimo vya corona kupitia kwa maabara, hali ambayo inahakikisha biashara inaendelea kama kawaida miongoni mwa mataifa ya Afrika.

“Tukishirikiana na AU, tunaunda mfumo wa Kiafrika wa kiwango cha kimataifa unaowajali Waafrika wote bila ubaguzi na kutokomeza ufisadi katika sekta ya afya, huku ukipunguza gharama ya vipimo vya maabara. Pia utatusaidi kukusanya data yetu kutuwezesha kufanya maamuzi haraka,” ikasema ASKY kwenye taarifa.

Mfumo huo wa PANABios unatarajiwa kuboresha usimamizi wa sera kote Afrika na kuinua biashara baina ya mataifa, kupiga jeki utalii, uwekezaji na utamaduni, na hatimaye kuhakikisha Afrika haiachwi nyuma na mabara mengine katika maendeleo.

“ASKY inaona faraja kwa AU kutengeneza na kuzindua mradi huu kabla ya mabara mengine, na kuyapa mataifa ya Afrika Imani ya kufungua uchumi kwa kumshirikisha kila mwananchi,” akasema Bw Ahadu Simachew, afisa mkuu mtendaji wa ASKY.

Dkt John Nkengasong, mkurugenzi wa Africa CDC alisema ushirikiano na kampuni za ndege utakuwa nguzo muhimu katika kuokoa biashara zilizoangushwa na corona.

“Kiwango cha madhara yaliyoletwa na Covid-19 kinahitaji ushirikiano mkuu na ubunifu wa kiteknolojia. Kutumika kwa teknolojia yetu kutasaidia pakuwa kunyanyua maazimio yetu ya maendeleo kama bara,” alisema.

FAUSTINE NGILA: Tuzime video feki zisivuruge uchaguzi 2022

Na FAUSTINE NGILA

HUENDA hujaziona lakini katika kipindi cha miezi minne iliyopita nimekumbana na video nyingi feki za kisiasa kuwahusu Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, zikisambaa mitandaoni.

Ni hali inayotia wasiwasi, kwamba fikra za wapigakura zitatekwa na makusudi ya wanaounda video hizi.Hasa ikizingatiwa kuwa Wakenya wengi huamini chochote kinachochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.

Teknolojia inayounda video hizi ni ya kiwango cha juu mno, kwani inawezesha kutoa nakala ya maumbile ya mtu, sauti yake, sura yake, anavyotembea n ahata anavyotabasamu.

Ni video chache tu ambazo utatambua kuwa ni feki, lakini nyingi zimefanywa kwa ustadi mno, na kutia maneno ya uwongo kwa vinywa vya wanasiasa.

Utata zaidi unajitokeza ukitazama mtindo wa siasa humu nchini, ambapo wanasiasa husema mambo fulani lakini wanapokamatwa na serikali kwa kuchochea chuki, wanadai si wao waliyatamka.

Hivyo, bila kuchukua hatua za kiteknolojia kudhibiti video hizi pamoja na wanaoziunda, itakuwa rahisi mno kwa wanasiasa kufoka maneno machafu kisha kisingizia video hizi.

Uwezekano wao kujificha nyuma ya ukuta wa video feki ni tisho kuu kwa amani inayohitajika, hasa katika msimu huu ambapo kampeni za Uchaguzi Mkuu zimeshika kasi.

Tayari wanasiasa 10 wiki iliyopita waliitwa na Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kueleza sababu zao kutoa matamshi yaliyochochea ghasia kwenye chaguzi ndogo za Machi.

Hii ni ishara kuwa idadi hii huenda ikaongezeka mwaka unavyozidi kukomaa na kura ya 2022 ikijongea.Ingawa Idara Ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imekuwa ikifanya kazi nzuri ya kunasa watu wanaoeneza habari feki, itahitaji kuwekeza katika teknolojia za kiwango cha juu zaidi kuweza kutambua video bandia na watu wanaozitengeneza.

Hebu fikiria. Video feki inayomwonyesha Bw Odinga akisema “Ruto tosha” ikisambazwa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, ambao unakisiwa kutumiwa na Wakenya zaidi ya milioni 7 waliotimu kupiga kura!Au hata video feki inayodai kufichua maovu ambayo Dkt Ruto hufanya nyakati za usiku! Kanda moja tu pekee ya aina hii ikiwafikia Wakenya milioni moja kwenye Twitter au WhatsApp inatosha kubadilisha matokeo ya uchaguzi.

Ni kweli kuwa Wakenya wengi wanamiliki simu za kisasa na wamechangamkia mitandao ya kijamii kuliko mataifa mengine barani Afrika.Hata hivyo, zaidi ya asilimia 80 ya Wakenya hawa hawana ujuzi wa kidijitali kutambua ni ujumbe upi wa ukweli na upi ni feki.

Hata ninapoipa changamoto DCI kunoa makali yake kiteknolojia, wananchi wenyewe wanahitaji kujielimisha kuhusu masuala haya sio tu kutarajia serikali iwahamasishe.Itakulazimu kuweka programu ya kutambua video, picha na sauti feki kwa simu yako usije ukahadaiwa na wakora wa siasa; wanaotumia ujuzi wa kidijitali kuchapisha mambo feki mitandaoni.

Itabidi uwe makini zaidi kupuuza mawasialiano ya aina hii. La sivyo, utanaswa kwenye mtego wa kuamini chochote kinachosambazwa mitandaoni, na huenda hatimaye ukahusika kuchochea chuki na hata ghasia.

Aunda programu za kompyuta kuifaa mikahawa

Na MAGDALENE WANJA

Bw Dennis Omito alizaliwa na kulelewa mjini Nanyuki karibu na kambi za kijeshi ambapo aliweza kuona ndege za wanajeshi mara kwa mara.

Hii ilimfanta kuwa na hamu sana ya kutaka kuwa rubani, na punde tu alipomaliza masomo yake, aliweza kusomea urubani. Alipata ujuzi wa kue desha ndege aina ya Cessna C15.

Hata hivyo, Omito anasema kuwa alijifunza hayo yote ili kujifurahisha na kutimiza kama moja wapo ya malengo yake maishani.

Kando na hayo, alipenda sana ufundi wa kutengeneza programu za kompyuta na simu.

Alipofuzu na cheti cha stashahada katika mafunzo Sayansi ya Kompyuta mnamo mwaka 2004, alipata kazi katika kampuni ya CMC Motors Group Ltd ambako alifanya kazi kwa muda wa miaka miwili katika cheo cha Computer Programmer.

“Baada kufanya kazi hio kwa muda wa miaka miwili, nikiweza kupata nafasi nyingine katika kampuni ya Toyota East Africa Ltd.

Alipokuwa pale, aliweza kujifunza mengi kuhusu biashara, na baada ya miaka mitatu, alijiuzulu na kuendeleza masomo ya kirubani.

Masomo hayo yalimchukua muda wa mwaka mmoja kisha ajarejelea kazi yake ya kuunda programu.

Alifanya kazi hio kama mshauri wa kampuni kubwa nchini kama vile Verve KO Ltd, amebaki aliweza kutengeneza program ya1963 Matatu Cashless platform, ambayo ilizinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta.

“Mnamo mwaka 2016, nilizindua kampuni yangu kwa Jina e-ofisi Technology Limited ambayo niliendesha kwa ushirikiano na mke wangu Martha Omito,” aliongeza.

Kupitia kampuni hio, ameweza kuunda programu kadhaa ikiwemo ile ya hivi punde ya BizWiz POS na ERP System.

Hii ni programu ambayo inatumika na baadhi ya hotel na mikahawa mkubwa ili kuleta pamoja shughuli zote za kibiashara pamoja.

Omito mwenye umri wa miaka 37 anasema kuwa programu hii ni tofauti na zile za hapo awali amabazo baadhi ya hoteli na mikahawa huzitumia ambazo ni miigo ya zile za ulayani.

“Niliunda program hii mnamo mwezi Juni 2017 baada ya kupatana na mteja ambaye alitaka programu ambayo ni tofauti na zile za ulaya,” aliongeza Omito.

Aliongeza kuwa program hii huwezesha mmiliki wa biashara kueza kufuatilia rekodi zote kupitia kurasa hio kwa urahisi.

Baadhi ya mikahawa na hoteli ambazo zinatumia program hii ni pamoja na The Tunnel iliyoko eneo la Mombasa Road, The Curve By the Park iliyoko karibu na mbuga ya wanyama ya Nairobi, Ziwa Beach Resort iliyo eneo la Bamburi Mombasa, Dari Restaurant – Ngong Road na Brew Bistro Tap Room- Ngong Road.

Kupitia muundo huo, ameweza pia kuunda program nyingine ambayo inatumika kanisani.

“Wafuasi wanaweza kufuatilia matukio kanisani kama vile maombi,mahubiri na ata kutoa sadaka kupitia program hii,” alisema Omito.

Programu hii imekuwa na manufaa zaidi wakati wa mkurupuko wa maradhi ya Covid-19 mwaka mmoja uliopita.

 

FAUSTINE NGILA: Tujizoeshe maisha ya dijitali

Na FAUSTINE NGILA

NAWASHANGAA baadhi ya walimwengu kulia kuwa wamechoka kufanyia kazi nyumbani, wamechoka kutumia teknolojia; eti sasa wanaomba waruhusiwe kurudi kufanyia kazi ofisini.

Mataifa mengi bara Ulaya yalifungwa kuzuia maambukizi ya virusi hatari vya corona, na hivyo kuwafungia watu wajumbani mwao.

Inatamausha kwamba watu hao wanatamani kurudi kufanya kazi katika mazingira ya ofisi. Ni mwenendo ambao pia mimi nimeuona hapa Kenya.

Pindi tu baada ya serikali kulegeza masharti ya kuzuia maambukizi ya virusi hivyo, vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19, watu walirudi kujaa tena ofisini kama zamani.

Hii ni ithibati kuwa licha ya janga hili kufumbua ulimwengu macho kutambua kuwa ajira za usoni zitategemea teknolojia, Wakenya bado wamekwama katika fikra zilizopitwa na wakati.

Huwezi kuniambia miaka mitano ijayo bado utakuwa ukifanyia kazi ofisini, utakuwa ukisafiri hadi jijini kwa ajili ya ajira. Kufanya hivyo ni kuonyesha kuwa hakuna ulifunzalo kwa kila aina ya mapinduzi.

Ni mwaka mzima tangu corona itokee na kisha kutua hapa nchini. Unapaswa kuwa umejipanga kuunda ofisi yako nyumbani, ukazoea kuwahudumia wateja mitandaoni, kulipwa kwa majukwaa ya kidijitali na kupiga sala mitandaoni.

Iweje hadi sasa bado unaamini ajira itasalia ilivyo? Nakerwa na maelfu ya kampuni ambazo zimezembea kuwaelimisha wafanyakazi wake kuhusu mustakabali wa ajira dijitali.

Kampuni hizi hazijaweka mikakati ifaayo kuwezesha wafanyakazi kuendesha biashara nyumbani. Hawana vipakatalishi, hawana intaneti, wala kampuni hazijanunua programu za kisasa za kuratibu na kufuatilia utendakazi.

Kampuni zipo tu! Zinategemea mifumo ya zamani kama vile kufuatilia wafanyakazi kama wamefika kazini.

Hazina habari kuwa kwa kutumia programu hizo za kisasa unaweza kufuatilia kila mfanyakazi kwa urahisi zaidi na kujua anafanya kazi kiasi gani, amefikia malengo au la.

Watu wengi nikiwauliza masuala haya wanasema kuwa wamechoka kuona marafiki zao kwenye video za mawasiliano, wangetaka wakutane nao uso kwa macho.

Hilo linakubaliwa; lakini haifai kuwa ndio mtindo, iwe mara moja tu kwa miezi kadhaa. Dunia ya sasa inakwenda kwa kasi mno, yule anayetaka kufanya mambo kama mwaka uliopita atapitwa. Ni wakati wa kubadilisha fikra kabisa.

Usidhani kuwa baada ya watu kuchanjwa eti sasa teknolojia itarudi nyuma hadi hali ilivyokuwa kabla ya janga la corona. Ukweli ni kuwa utajionea teknolojia za uwezo mkuu hata zaidi kufikia mwisho wa mwaka huu.

Fikiria hivi. Je, iwapo janga lingine lingetokea duniani na kulazimisha kila mtu kufungiwa mahali bila kutangamana hata na familia, utaweza kuvumilia na kuponea kifo?

Ni wakati wa kufanya mambo ni kana kwamba kuna janga lingine njiani. Jifunze kutumia teknolojia zote kufanikisha maisha yako bila usaidizi wa mtu yeyote. Jiandae kwa maisha ya teknolojia tupu katika kila ulifanyalo.

Tumia mtandao kufanya utafiti ujue ni kifaa kipi kitakufaa zaidi kwa kazi yako, huduma gani itakupunguzia gharama. Haya yote yamejaa kwenye intaneti; anza kuitumia sasa.

Taharuki kuhusu teknolojia ya kutambulisha nyuso

NA MARY WANGARI

DELHI, India

TEKNOLOJIA ya vifaa vya kutambulisha nyuso katika shule kadhaa zinazofadhiliwa na serikali nchini India imezua hofu kuhusu ukiukaji wa haki za usiri wa data.

Wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu kidijitali wametaja teknolojia hiyo kama “ukiukaji uliovuka mipaka” kutoka kwa serikali na kuingilia faragha ya watoto.

Hatua hiyo ya kuanzisha teknolojia ya kutambulisha uso imefuatia uamuzi wa serikali ya jiji la Delhi 2019, wa kupachika kamera za CCTV katika shule zaidi ya 700 ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi.

“Mifumo hiyo ya kutambulisha sura inawekwa pasipo sheria za kudhibiti ukusanyaji na matumizi ya data, jambo ambalo ni la kuhofisha hasa kwa watoto,”

“CCTV tayari ni ukiukaji wa haki za watoto kuhusu faragha, hata ingawa baadhi ya wazazi walikuwa wameiunga mkono kwa usalama wa watoto wao…lakini matumizi ya teknolojia ya kutambulisha uso ni ukiukaji uliokithiri na si haki kamwe,” alifafanua Anushka Jain, wakili katika Wakfu wa Uhuru kuhusu Intaneti, kundi la wanaharakati lililofahamu kuhusu uzinduzi huo wiki iliyotangulia.

Jain alieleza vyombo vya habari kuwa matumizi ya teknolojia hiyo kwa watoto ina matatizo kwa sababu uhakiki wake ni wa kiwango cha chini mno, hivyo basi, endapo ni katika kisa cha uhalifu, watoto wanaweza kutambulishwa visivyo.

“Ingekuwa vigumu kwa wazazi kufahamu kuhusu hatari zinazohusiana na ukiukaji na matumizi mabaya ya sheria kuhusu uhifadhi wa data,” alisema.

Teknolojia ya kutambulisha sura inatumika pakubwa katika viwanja vya ndege, vituo vya treni na mikahawa kote nchini India.

Kuna mipango ya kuanzisha mfumo wa kitaifa wa kufanyia mageuzi ya kisasa kikosi cha polisi ikiwemo michakato yake ya kukusanya vitambulisho vya wahalifu.

Wachanganuzi hata hivyo, wanasema manufaa yake hayajabainishwa wazi, na kwamba itakiuka haki za watu kuhusu faragha.

Wamehoji kuwa itasababisha udadisi zaidi wenye vidhibiti vichache na ufafanuzi finyu kuhusu jinsi teknolojia hiyo inavyofanya kazi, jinsi data inavyohifadhiwa na ni nani anaweza kuipata.

FAUSTINE NGILA: DCI ijitahidi kung’amua mbinu za wizi mitandaoni

Na FAUSTINE NGILA

HAPO Jumatatu, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilichapisha kwenye Facebook kisa cha kustaajabisha kuhusu jinsi ‘mfu’ aliiba mamilioni ya ‘mfu’ mwenzake.

Katika maelezo yake, DCI ilisema kuwa wahuni wa mitandaoni walitumia simu ya mtu aliyefariki kuiba Sh2.8 milioni katika akaunti ya benki ya Mkenya mwingine aliyeaga dunia.

Kivipi? Walitumia simu ya mmoja wa wafu hao, ambayo ilikuwa imepotea, kupora pesa katika akaunti zake kwanza kabla ya kuitumia kuiba hela katika akaunti ya pili.

Wakenya wengi walidai kisa kama hicho kinatokana na ukosefu wa ajira kwa vijana walio na digrii, lakini sikubaliani nao kwani katika mtandao huo wa majambazi watano, niliona watu waliopitisha umri wa miaka 50.

Kuwa na ujuzi wa kiteknolojia kamwe haukupi uhuru wa kuutumia kunyanyasa Wakenya wenzako na hilo ni kosa linalopaswa kuadhibiwa vikali.Swali kuu ni kuhusu jinsi walifanikiwa kutoa kadiwia au kadi ya simu yenye nambari iliyosajiliwa na Safaricom, Airtel au Telkom na kupata nenosiri inayotumika katika sajili zote za benki.

DCI wanafaa kuchunguza ni vipi wakora hao waliweza kupata kuingia kwenye programu za simu za benki za NCBA, Co-operative, Equity na vipi walifaulu kuzituma hela hizo kwa akaunti nyingine na kuzitoa.

Mara nyingi nimezungumzia uwezo wa teknolojia ya ‘blockchain’ katika kuzima wizi huu, lakini Kenya inaonekana haijajitayarisha kuwekeza kwa teknolojia hii. Iwapo mtu amefariki, hela zake benki zinapaswa kutolewa tu na familia yake pekee, ambayo inafaa kujua nenosiri.

Awali nimeipongeza Safaricom kwa kujaribu kuleta ubunifu wa kutumia uso wa mwenye kadi ya simu kama neno siri, lakini kwa simu za bei ya chini zisizowezesha teknolojia hiyo, wezi hutoa kadi na kuibadilisha kwa kufuta nenosiri ya kwanza.Lakini ndipo ubadilishe nywila hii, lazima utambue nywila ya awali.

Na ndipo uibe mamilioni, lazima ung’amue nenosiri ya akaunti ya benki ya pili ambapo unatuma hela hizo ili ukazitoe.Je, wahuni hawa ni wafanyakazi wa zamani wa benki hizi au kampuni hizi za mawasiliano?

Walijuaje watu hao wana hela nyingi kwa akaunti, na kuwa wamefariki? Safaricom, kwa mfano, mwaka uliopita ilitoboa tundu katika mtandao wa M-Pesa ilipoambia watumizi kuwa wanaweza kuteua mtu wa familia na kumpa nenosiri ili wakati wanapofariki, mtu huyo anaweza kutoa zile hela kwa manufaa ya familia.

Iwapo DCI, itachukua muda wake kupeleleza kwa makini, itapata kuwa kuna mtandao wa watu wa familia, wafanyakazi wa benki na wa kampuni za mawasiliano ambao wamekuwa wakishirikiana kuiba mamilioni ya pesa zinazoachwa na Wakenya waliokufa.

Naipongeza DCI kwa kazi kuntu inayofanya, na pia kampuni za benki na mawasilino kwa kukubali kushirikiana na wapelelezi kutoa taarifa zinazosaidia kukamatwa kwa wakora wa mitandaoni.L

akini kuelewa kwa kina jinsi ujambazi huu unaendeshwa kutasaidia kuzima ndoto za mamia ya vijana ambao wanategemea kupora matunda ya jasho la watu wanapokufa.

fmailu@ke.nationmedia.com

Wanawake Kenya hulipa maradufu kupata huduma za M-Pesa ikilinganishwa na wanaume – Utafiti

NA FAUSTINE NGILA

Wanawake wa Kenya wanalipa mara dufu kuliko wanaume kupata huduma za pesa kwa njia ya simu, hii ni kulingana na data zilizotolewa majuzi na Shirika la Utafiti wa Malipo Kidijitali la Uingereza, Caribou Data.

Taarifa ya Shirika hilo, Payments System Design and the Financial Inclusion Gender Gap, inaeleza kwamba utafiti uliofanywa katika miji mikuu nchini Kenya umefichua jinsi wanawake wanatumia huduma za Kampuni tajika ya Mawasiliano Nchini – Safaricom kama vile M-Pesa, M-Shwari na Fuliza.

Aidha, utafiti huo umeonyesha kuna ‘ubaguzi’ wa kijinsia katika ada zinazotozwa, ikibainika wanawake wanalipa karibu Sh11 kusambaza au kupokea pesa, nao wanaume wakigharamika Sh7, kiwastani (Takwimu zilizojiri baada ya kukokotoa hesabu kwa mujibu wa data walizokusanya, wanawake na wanaume walivyokumbatia matumizi ya kidijitali kutuma na kutoa pesa).

“Kimsingi, inafikia kadri jumla ya Sh30 kila mwezi kwa wanawake, nao wanaume Sh16,” inaeleza data ya utafiti huo uliofadhiliwa na wakfu wa Bill na Melinda Gates.

Utafiti huo unaashiria kwamba wanawake hawajapigwa jeki kifedha, wakilazimika kutoa kiwango cha chini cha pesa, kikikadiriwa kuwa wastani wa Sh800.

Hilo linaashiria kwamba wanatozwa gharama ya juu ya ada, wakilinganishwa na wanaume na ambao hutuma au kupokea kiwango cha juu cha pesa, kupitia huduma za M-Pesa.

Kwa mfano, kwa sasa kutuma Sh800 ada ya Sh12 inatozwa sawa na asilimia 1.5, ikilinganishwa na kutuma Sh15, 000 ada inayotozwa ikiwa Sh97 (sawa na asilimia 0.64 ya kiwango hicho).

Kampuni ya Safaricom imekuwa ikitoza kuanzia ada ya Sh10 kutuma kati ya Sh101 – 500, kiwango cha ada ambacho kinabashiriwa kuwa ghali.

Wakati huohuo, watumizi wa huduma za Safaricom kusambaza pesa, hulipa ada ya kadri ya takriban asilimia 1.5 ya kiwango jumla cha pesa, wanawake wakionekana kugharamika zaidi wakilinganishwa na wanaume.

Mabaliko yalishuhudiwa Safaricom ilipotathmini kiwango cha ada inayotozwa kati ya Sh100 – 1, 000, Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa janga la Covid-19, ambapo serikali ilihimiza wananchi kukumbatia usambazaji na upokeaji pesa kwa njia ya M-Pesa.

Miezi kadhaa mwaka uliopita, 2020, Safaricom ilifutilia kwa muda ada inayotozwa kutuma kiwango cha Sh1, 000 kurudi chini, japo kampuni hiyo ilikuwa ikitoza shughuli za kutoa.

Afueni hiyo hata hivyo iliondolewa Janauri 2021.

Licha ya mikopo inayotolewa na Safaricom kupitia apu ya Fuliza kuvutia wanaume kuliko wanawake, wanawake wameonekana kuikumbatia kwa kasi.

Fuliza ilizinduliwa Novemba 2018, takwimu za Safaricom zilizotolewa Novemba 2020 zikionyesha kima cha Sh830 milioni hukopwa kila siku.

Aidha, apu hiyo inaendelea kukumbatiwa, asilimia 21 ya wanawake na 26 wanaume wakiitumia, kulingana na takwimu za utafiti wa Caribou Data.

“Kwa mujibu wa utafiti tuliofanya, licha ya idadi ya chini ya wanawake waliokopa Fuliza, idadi ya wanaoikumbatia mara kwa mara ni ya juu ikilinganishwa na ya wanaume. Wanawake walifanya wastani wa huduma mara 4, kila moja ya Sh140, ikilinganishwa na wastani wa 1.6 wanaume, Sh80 kila moja,” inaeleza ripoti ya utafiti huo uliojumuisha zaidi ya wanaume na wanawake 1, 000.

Dhihirisho wanawake kukumbatia matumizi ya Fuliza, inaashiria uzinduzi wa huduma zingine za pesa kwa njia ya simu unaweza kuwasaidia kutatua ukosefu wa fedha wanaopitia.

Kulingana na Bi Roselyne Wanjiru, Mtafiti wa Masuala ya Fedha kutoka Shirika la Kesholabs, Nairobi, anahoji wanawake wengi wana majukumu ya malezi hivyo basi kiwango cha kutuma na kupokea pesa miongoni mwao ni cha chini kutokana na gharama inayowakodolea macho nyumbani.

“Wanaume hutumia kiwango cha juu cha pesa kwa familia zao na pia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwekeza. Isitoshe, wana nafasi bora kupata madaraka kazini na nafasi zingine kujiimarisha kifedha wakilinganishwa na wanawake,” mdau huyo anaiambia Taifa Leo Dijitali.

Anaendelea kueleza kwamba ni siku za hivi karibuni tu mwamko umeanza kushuhudiwa miongoni mwa wanawake, ambapo wamepata nafasi za hadhi ya juu serikalini na pia katika mashirika, nafasi ambazo zinawawezesha kupata donge nono.

“Kenya inapaswa kukumbatia usawa wa kijinsia katika utendakazi, wanaume na wanawake wapate mshahara au mapato yanayotoshana, ili wanawake waamke,” anafafanua.

Kulingana na Data ya Caribou, wanawake na wanaume wamehimizwa kutuma pesa zenye thamani chini ya Sh100 na ambayo haitozwi ada yoyote.

Asilimia 25 ya watumizi milioni 29 wa huduma za M-Pesa wametajwa kukwepa kutuma kiwango cha pesa kinachozidi Sh100.

Kampuni ya Safaricom, pia ina apu ya M-Shwari, inayosaidia wateja wake kuweka akiba kwa njia ya kidijitali na asilimia 19 ya wanaume wameikumbatia, kiwango chao kikiwa juu ya wanawake ambao wamewakilishwa na asilimia 14.

Alice Anangi, Mwanzilishi na Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Zeden Technologies, lililoko jijini Nairobi, anasema hali ngumu kiuchumi inayoshuhudiwa kwa sasa, imechangia wanawake kuwa katika hatari ya kukumbwa na umaskini wakilinganishwa na wanaume, hasa kutokana na dhana potovu ya umiliki wa raslimali na maamuzi katika ugavi.

“Tunashuhudia ubaguzi katika shughuli ya kusajili wanafunzi vyuoni, ndoa za mapema miongoni mwa wanawake na ukosefu wa hamasisho kuwajumuisha kwenye huduma za fedha kwa njia ya kidijitali. Hali kadhalika, utamaduni wa wanawake wafanye kozi zisizohitaji nguvu kama vile za kiteknolojia unawanyima fursa kupata kazi zenye mapato ya juu,” Bi Anangi anafafanua.

Utafiti huo pia umeonyesha, wanawake wanatumia simu za hadhi ya chini, chocheo ambalo ni kikwazo kupata huduma bora za fedha kwa njia ya simu.

Simu ya hadhi ya chini haina uwezo wala nafasi ya kutosha kuhifadhi apu muhimu, hususan zinazotoa huduma za mikopo.

“Idadi ya wanawake wanaomiliki simu zinazogharimu chini ya Sh20, 000 ni ya juu mno, huku zenye thamani zaidi ya kiwango hicho cha fedha zikimilikiwa na wanaume,” utafiti wa Caribou Data unaeleza.

Taswira hiyo kulingana na Bi Wanjiru inachangiwa na ukosefu wa hamasisho wanawake wainuliwe kifedha na kimaendeleo katika jamii.

Idadi kubwa ya wanawake waliohojiwa wanamiliki simu zenye thamani ya chini ya Sh10, 000 (sawa na asilimia 54), tafiti hizo zikiashiria asilimia 92 ya wanawake nchini wanamiliki simu za thamani ya chini ya Sh20, 000.

Ilibainika wanawake wenye simu ghali wamekumbatia huduma za utoaji na utumaji wa pesa mara kwa mara, kimsingi huduma za kifedha kidijitali.

“Tuligundua wanaomiliki simu za thamani ya juu (Sh20, 000) wanatekeleza huduma zenye thamani ya wastani jumla wa Sh1, 647 kwa mwezi, wakilinganishwa na wenye simu za hadhi ya chini, ambao kiwango chao kimesimaia Sh878 kwa mwezi,” utafiti huo unaelezea.

Kiwango cha utoaji na utumaji wa pesa, wanawake wenye simu ghali pia kimetajwa kuwa zaidi ya mara saba kwa mwezi, huku wanaomiliki za bei ya chini kikiwa mara nne pekee.

TAFSIRI: SAMMY WAWERU

FAUSTINE NGILA: Vita vya Iran, Israel visizuie ukuaji wa teknolojia nchini

Balozi wa Iran nchini Jafar Barmaki Iran (kushoto), makamu wa rais wa nchi hiyo Sorena Sattari (kati) na waziri wa Habari na Teknolojia nchini Joe Mucheru, wakikata utepe wakati wa uzinduzi wa kituo cha uvumbuzi na teknolojia (Iran House of Innovation and Technology-IHIT) katika eneo la Kilimani, Nairobi wiki iliyopita. Picha/Evans Habil

Na FAUSTINE NGILA

Juhudi za hivi majuzi za taifa la Iran za kuinua viwango vya ubunifu, teknolojia na biashara baina yake na Kenya zimeonekana kuikera Israeli, mataifa hayo mawili yakiwa na uhasama mkuu katika eneo la Mashariki ya Kati.

Iran wiki hii, inazindua kituo cha uvumbuzi na teknolojia kwa jina The Iran House of Innovation and Technology (IHIT), ambacho kinalenga kutoa nafasi ya biashara na intaneti bila malipo kwa kampuni za Kenya na Iran.

Akitaja mpango huo kama mkubwa zaidi duniani ulioanzishwa na Terhan, balozi wa Iran humu nchini Jafar Barmaki alisema kampuni 40 kutoka taifa lake zitahudhuria kuzinduliwa kwa kituo hicho.

Licha ya kuwa Kenya ni taifa linalohitaji usaidizi wa kiteknolojia katika kila pembe, Israeli imetaja mpango huo kama suala la kiusalama, hasa ikizingatiwa mataifa hayo mawili yamekuwa yakikomoana kiteknolojia huku kila moja likijaribu kudukua mitandao ya mwenzake kwa uhabirifu mkubwa.

“Iran inaendelea kuzua misukosuko ya kiusalama eneo la Mashariki ya Kati na Afrika kwa kufadhili mitandao ya kigaidi na kusambaza teknolojia na silaha kwa mataifa mbalimbali,” Israeli ilisema kwenye Facebook ilipogundua mpango wa Iran nchini Kenya.

Ingawa mataifa yote yanapendezwa na hali ya teknolojia nchini, huenda uhasama baina yao ukaathiri mipango ya kusaidia nchi hii kupiga hatua kiteknolojia, na kusambaratisha diplomasia ambayo umekuwepo baina ya Israeli Kenya.

Kituo hicho kitakuwa eneo la Milimani, Nairobi, ambapo ni karibu na makao ya ubalozi wa Israeli nchini, na kuna hatari ya mataifa haya kutumia Kenya kama uwanja wa vita vya kiteknolojia, ambapo Wakenya ndio wataumia zaidi.

Kimsingi, Kenya iko mbali mno kufikia upeo wa teknolojia wa Israeli na Iran, na serikali yetu isipoingilia kati na kutuliza joto hili la kidiplomasia, huenda raia wakaumia sana mataifa haya yakianza vita vya ubabe wa kiteknolojia nchini.

Serikali, kupitia wizara za Teknohama na Mambo ya Kigeni, inafaa kuwa mbioni kuchunguza madai ya Israeli, na kuwaambia Wakenya kwa nini Yerusalemu inahisi kuwa kutakuwa na utovu wa usalama mitandaoni Iran ikiruhusiwa kuzindua kituo cha teknolojia Nairobi.

Ni wazi kuwa Israeli imekuwa na maadui wengi katika Mashariki ya Kati, kama vile Iran, Iraq, Lebanon, Oman, Qatar, Kuwait na Syria na hata Afrika (Somalia, Libya, Algeria, Tunisia, Mali, Niger, Djibouti na Mauritania), lakini ilikuwa taifa la kwanza nchini Kenya kujenga ofisi za ubalozi, kabla ya kujinyakulia uhuru.

Ili kulinda wananchi dhidi ya athari ya vita hivi, si busara kwa serikali kuendelea kutekeleza mpango wa Iran bila kuzingatia masuala yaliyoibuliwa na Israeli, kwani farakano litokeapo, sisi nyasi ndio tutaumia – mitandao yetu itadukuliwa, bila kusahau mtandao mzima wa umeme nchini.

Serikali ichukulie suala hili kwa uzito. Hakuna haja ya taifa lenye uwezo mkubwa wa teknolojia kama Kenya kuzimiwa ndoto yake na mataifa yaliyopiga hatua kubwa tayari kwenye ulingo huo wa teknohama.

Kenya yasifiwa kutumia teknolojia kuzuia kuenea kwa corona JKIA

NA LEONARD ONYANGO

UMOJA wa Afrika (AU) kupitia asasi yake ya kiafya ya Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) umeipongeza Kenya kwa kuwa miongoni mwa mataifa ya kwanza barani kuanza kutumia teknolojia yake ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Uvumbuzi huo ambao unarahisisha mchakato wa kuthibitisha matokeo ya vipimo vya corona na uhalisia wa chanjo za virusi hivyo, tayari umeanza kutumiwa na Wizara ya Afya humu nchini.

“Wizara yetu imeshirikiana na AU na Africa CDC, kwa usaidizi wa kiteknolojia kutoka PanaBIOS kutekeleza mfumo wa mitandaoni wa kuthibitisha vyeti vya vipimo vya corona kwenye maabara,” Bw Mutahi Kagwe, Waziri wa Afya amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC Dkt John Nkengasong ameimiminia sifa Kenya kwa hatua hiyo ambayo Umoja wa Afrika unaamini utahakikisha usalama wa kiafya katika viwanja vya ndege, na hivyo kuwapa abiria imani ya kusafiri katika mataifa mbalimbali ya Afrika.

“Kenya imekuwa mstari wa mbele katika masuala ya kiteknolojia hapa barani, lakini ni juhudi zake katika mchakato mzima wa kuunganisha Afrika ambazo zinafanya ushirikiano wetu katika teknolojia za suluhu za kiafya kuwa ubunifu wa kutegemewa,” aliambia Taifa Leo.

Hapo Oktoba mwaka uliopita, AU ilizindua jukwaa la mtandaoni kwa jina Trusted Travel kama mojawapo ya suluhu za kuhakikisha biashara imeendelea Afrika, katika kongamano la mawaziri wa afya, uchukuzi na mawasiliano wa mataifa ya Afrika.

Suluhu hiyo iliyotengenezwa na shirika la PanaBIOS na kampuni tajika ya Zimbabwe Econet kwa sasa inatumika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kuwapima na kuwapa vyeti vya usafiri abiria wanaoingia humu nchini na wale wanaoondoka.

Antonia Filmer, raia wa Uingereza aliyesafiri Kenya majuzi ameelezea jinsi suluhu hiyo inawachangamsha Wakenya wakati ambapo raia katika mataifa ya bara Ulaya wanaonekana kugubikwa na huzuni.

“Nilipotua JKIA kabla ya kuingia kwa ofisi za uhamiaji, tulipigwa skeni na kupewa vyeti vya corona vya kuruhusiwa kuwa Kenya huku pia tukipimwa joto mwilini iliyounganishwa na kamera. Mchakato mzima ulichukua dakika 15 pekee,” alisema.

Abiria huonyeshwa vipimo vyao vya joto kwenye skrini, na wanapofika kwenye meza ya uhamiaji, wanachoonyesha ni visa na paspoti pekee.

“Wakati huu ambapo uchumi, shule na mipaka imefunguliwa, Afrika inahitaji mbinu madhubuti ya kupunguza hatari ya maambukizi ya corona. Ndio maana tumezindua teknolojia hii kupunguza kuenea kwa virusi hivi mipakani,” akasema Amira Mohammed, Kamishna wa Masuala ya Kijamii katika Tume ya AU.

FAUSTINE NGILA: Madikteta wasiruhusiwe kutumia mitandao wanavyotaka

VIONGOZI madikteta hawapendi ukweli, hasa ikiwa ukweli huo unaenezwa kupitia mitandao ya kijamii ambapo watu wengi hukita kambi katika muda wao wa ziada.

Mwezi huu tumejionea rais anayeondoka wa Amerika Donald Trump akizimiwa akaunti zake zote katika Twitter, Facebook na YouTube kwa kila kampuni hizo zilitaja kama matumizi ovyo ya majukwaa hayo kuwapotosha wananchi.

Akiendelea kusisitiza kuwa kulikuwa na wizi wa kura uchaguzini hata baada ya kuzimwa mitandaoni, rabsha ambazo zilitokea baada ya Bw Trump kuwaagiza wafuasi wake kuvamia bunge zilisababisha vifo vya watu watano.

Juzi, katika nchi jirani ya Uganda, ambapo Rais Yoweri Museveni alifanya Uganda taifa la kwanza duniani kulipa ushuru wa mitandao ya kijamii, Twitter na Facebook zilipigwa marufuku katika muda wote wa kabla, wakati na hata baada ya uchaguzi.

Mataifa haya mawili, ambayo yana misingi tofauti ya kisiasa na kiuchumi, lakini yanayotawaliwa na madikteta yameonyesha jinsi haki za wananchi zinaweza kukandamizwa kwa mbinu tofauti.

Kwa kuwa mitandao hiyo ya kijamii inamilikiwa na kampuni za Amerika, Bw Trump aliyahitaji majukwaa hayo zaidi ili kufikia wafuasi wake zaidi ya milioni 87.

Lakini akazimwa kutokana na ukomavu wa demokrasia nchini humo.Kinaya nchini Uganda ni kuwa, kwa kuona maandamano ya wafuasi wa chama cha Republican nchini Amerika, tume inayosimamia mawasiliano iliagiza intaneti izimwe wakati wa kura “ili tusishuhudie mauaji kama yale ya Amerika kutokana na maandamano.”

Kwa kuweka giza la mitandaoni, wananchi hawakuweza kutoa taarifa za moja kwa moja kuhusu visa vya udanganyifu au kulazimishwa na jeshi kupiga kura kama alivyodai mwaniaji urais Bobi Wine.L

akini Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alivyojaribu kumpongeza Bw Museveni kwa ushindi wake kupitia Facebook, ujumbe huo ulifutwa kutokana na kile kampuni hiyo iliona uchaguzi haukuwa huru kwani Bw Museveni aliagiza intaneti izimwe.

Wiki chache tu kabla ya intaneti kuzimwa Uganda, serikali iliitaka kampuni ya Google kuondoa akaunti zote za YouTube ambazo zilikuwa zinaeneza jumbe za kukashifu serikali.

Google ilidinda kufuata agizo hilo.?Facebook, kwa upande wake, iliondoa video nyingi tu zilizopigia debe kampeni za Bw Museveni ikisema ni “mwenendo usiofaa”.

Ukaidi huo ulioneka kumkera sana Rais huyo ambaye sasa ataongoza Uganda kwa miaka 40, na akaamua kuondoa mawimbi ya intaneti.? Hii inaonyesha uwezo mkubwa wa mitandao uliochangiwa na teknolojia ambapo watu wengi walio na simu za kisasa wanapenda kutoa maoni yao ya kukosoa serikali au kutetea mwaniaji wao.

Lakini viongozi walio mamlakani baada ya kugundua hilo, sasa wanatumia mitandao hiyo kwa manufaa yao wenyewe, hasa wakati wa uchaguzi ambapo mihemko ya kisiasa hushuhudiwa.

Kwa demokrasia iliyokomaa, matumizi ya mitandao kwa wanasiasa yanafaa kuwa na uwajibikaji, na wananchi wanapotoa hisia zao wanafaa kusikizwa na wala si kufungiwa nje.

Hata hivyo, kwa wanasiasa wanaopenda kutumia mitandao hiyo kupotosha wananchi kwa kueneza chuki na uongo, wazimwe.

FAUSTINE NGILA: Kukwamilia WhatsApp ni ithibati Afrika haitambui usiri wa data

Na FAUSTINE NGILA

JE, umehama kutoka mtandao wa kijamii wa WhatsApp? Iwapo ungali kwenye jukwaa hilo linalomilikiwa na Facebook, basi wewe ni mmoja miongoni mwa mamilioni ya Waafrika ambao wanapenda kuanika usiri wao.

Wiki iliyopita, WhatsApp ilitangazia watumizi wake kwamba itakuwa ikitumia data zao za siri kuporomosha matangazo katika mitandao ya Facebook na Instagram.

Ilionya kwamba wale ambao hawatakubali sera hiyo mpya basi hawatapata huduma walizozoea.Waafrika wengi wanaipenda WhatsApp sababu ya urahisi wa matumizi, unaowawezesha kuunda vikundi vya siri vya kupiga soga au hata kufanya mazungumzo ya kikazi.

Hata hivyo, mtandao huo hauwezi kuaminika tena kulinda data ya watumizi wake zaidi ya bilioni mbili. Alipoona kuwa Facebook inawanyanyasa wateja kwa kurina data bila ruhusa yao, na kisha kuitumia kibiashara kuunda matrilioni ya hela kupitia matangazo ya mitandaoni, Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya magari ya kielektroniki ya Tesla, Bw Elon Musk, aliwaomba walimwengu kugura WhatsApp mara moja na kujiunga na mtandao wenye huduma sawa wa Signal.

Kufikia leo, mamilioni ya watu bara Amerika, Ulaya, Asia na Australia wamejiondoa kutoka WhatsApp na kujisajili katika Signal – ambayo imeweka sera thabiti za kulinda data ya watumizi dhidi ya wizi au matumizi yasiyoruhusiwa.

Ninapotazama kwenye programu yangu ya Signal, wengi wa watumizi wanatoka mabara hayo, licha ya kuwa na nambari za simu za watu kutoka Afrika zipatazo 3800 huku 400 pekee wakiwa wa ughaibuni. Kwa simu yangu, Waafrika ambao wamechangamkia Signal ni 83 pekee, Wazungu ni 289.

Hii ndiyo taswira kamili ya jinsi Afrika ilivyo. Watu wasiojitambua kama wa maana, watu wasiojali data yao ikitumiwa visivyo, watu wanaotegemea mno uvumbuzi wa ughaibuni, watu wanaopenda kuelekezwa kuhusu wanachopasa kufanya, watu wasiojielewa.

Ni wakati wa kung’amua kuwa masoko ya dijitali katika mataifa yaliyoendelea tayari yamefurika.Hivyo, unapoona Facebook ikishurutisha watumizi kukubali sera hasi za kuwakandamiza, basi inalenga Afrika ambako soko bado li wazi kwa uwekezaji wa mabilioni ya dola.

Afrika bado ndilo bara lililosalia na changamoto nyingi, na kuondoa visiki hivi kunahitaji data na taarifa za mambo wanayofanya wananchi wake kuwekwa siri.

Kupata data hii hakufai kuwa jambo la utani bali ichukuliwe kama bidhaa ya kibiashara, ambapo Facebook lazima iwalipe watumizi wake kwa kuchanganua data kuhusu maisha yao.

Utajihisi vipi ukipata mnaso wa simu (screenshot) wa arafa zote ambazo umetuma na kupokea kwenye WhatsApp, ukisambaa mitandaoni? Wasichojua Waafrika wengi ni kuwa, kando na arafa, programu za Facebook husikiliza maongezi ya simu.

Kumaanisha hata wakati hautumii simu, bado inafuatiliwa kana kwamba wewe ni mhuni uliyefanya makosa ya jinai.

Ni wakati wa kugutuka na kufahamu kwamba kukwamilia katika WhatsApp kunaipa Facebook fursa ya kuendelea kukandamiza haki zetu za kimsingi, ambazo zimelindwa katika Sheria ya Ulinzi wa Data ya 2019.

FAUSTINE NGILA: Teknolojia itatusaidia pakubwa mwaka wa 2021

Na FAUSTINE NGILA

Leo ni siku ya mwisho ya mwaka huu wa masaibu. Nikitazama kuanzia Januari hadi Desemba, kwa kweli dunia imekumbwa na changamoto si haba.

Lakini nikisoma makala niliyoandika mwishoni mwa mwaka huo nikibashiri jinsi teknolojia itakavyoboresha maisha ya mwongo huu, nafsi yangu inapata faraja mno kwani yote niliyoyasema yametimia katika muda wa chini ya mwaka mmoja.

Huku ulimwengu ukilaani janga la corona, katika uchumi wa kidijitali, gonjwa hili limechangia pakubwa katika makuzi ya teknolojia, na kuongeza kasi ya uelewa wa teknolojia za kisasa miongoni mwa serikali mbalimbali na wananchi wake.

Kwa mfano, hapa barani Afrika, huu ndio mwaka ambao serikali nyingi ziliona haja ya kupunguza ada ya intaneti na ile ya kutuma na kutoa hela kwa simu.

Katika sekta ya kibinafsi, kuanzia Machi ambapo janga hilo lilianza kuhangaisha Waafrika, tumejionea ubunifu wa kipekee, mwanzo ukiongozwa na Umoja wa Afrika (AU) na kupokelewa vyema na wananchi hadi mashinani.

Fikiria kwa mfano, baada ya serikali nyingi kuweka masharti ya kudhibiti virusi hivyo, ambapo kampuni ziliwaagiza wafanyakazi kufanyia kazi nyumbani, maisha yangekuwakeje bila programu za kompyuta za kufanikisha ajira?

Wagonjwa waliougua magonjwa mengine wangehudumiwa vipi bila programu za simu za matibabu ambapo daktari wa jijini anaweza kumwona mgonjwa kupitia video ya mbashara na kumpima kisha kumshauri kuhusu dawa za kunywa au matibabu maalum?

Ni katika kipindi hicho cha miezi tisa ambapo mamilioni ya wanafunzi na walimu kote duniani waligundua kuwa si lazima masomo yafanyiwe darasani. Unaweza tu ukafundishwa na kutahiniwa kupitia mitandao.

Na hali imesalia sawa kwa mikutano yote ya ofisini au makongamano. Watu wamebaini kuwa kando na kuwa mbinu bora inayozuia utangamano wa watu, pia haina gharama ya juu na inaokoa wasaa.

Wakati wa janga la nzige lililoharibu mimea mingi Mashariki ya Afrika, watafiti waligeukia teknolojia kujaribu kuelewa wadudu hao na jinsi ya kuwadhibiti.

Matumizi ya droni kusharizia dawa wadudu hao angani yalisaidia kupunguza idadi yake.Na ni kupitia teknolojia ya uchanganuzi wa data ambapo dunia imepata chanjo ya corona.

Mifumo mingi ya kutatua changamoto mbalimbali iliasisiwa wakati wa janga hilo, na kufanya corona mwanzo wa kuenea zaidi kwa teknolojia zenye uwezo mkubwa mwaka ujao.

Mengi tu ya mambo ambayo tumezoea wakati wa corona yatasalia vivyo hivyo. Kwa mfano, waumini waliozoea kutazama mahubiri kupitia njia ya mtandao na kutoa sadaka kidijitali wataendelea na mtindo huo.

Watu wengi zaidi watafanyia kazi nyumbani 2021 kwa kuwa kampuni zimegundua zimekuwa zikipoteza mamilioni ya pesa kwa malipo ya kodi ya jumba la bishara na gharama za usimamizi.

Usishangae utakapoona suluhu za kidijitali kwa changamoto zilizolemea sekta mbalimbali zikipatikana. Kwa mfano, 2021 ndio mwaka ambao tatizo la msongamano wa matatu mijini utakomeshwa na teknolojia.

Teknolojia nyingi zaidi kutoka humu barani zitabuniwa mwaka ujao, na kupunguza kiwango cha ushawishi wa kampuni za teknolojia za mabara mengine katika masuala ya Afrika.

fmailu@ke.nationmedia.com

FAUSTINE NGILA: Shirika la Utafiti wa Angani limezembea mno, ligutuke

Na FAUSTINE NGILA

Katika ukurasa wake wa Facebook, Shirika la Utafiti wa Angani la Kenya (KSA) lilichapisha habari hapo Desemba 8. Kwenye Twitter, liliweka posti Desemba 14.

Katika ulimwengu ambao mataifa yanayoendelea yanawapasha wananchi wake habari za angani kila uchao, inashangaza kwwamba Kenya – inayojizatiti kufuata nyayo za Afrika Kusini katika ulingo huu wa utafiti kuhusu anga ya dunia na sayari zingine – inatoa habari baada ya wiki kadha, tena kama vidokezo.

Nikivinjari kwenye Twitter, Shirika la Usimamizi na Utafiti wa Angani la Amerika (NASA) huchapisha habari mpya mara nne kila siku, jambo ambalo limevutia wafuasi milioni 46 na wengine milioni 25 katika ukurasa wake wa Facebook.

Licha ya kutengewa mamilioni ya pesa katika bajeti, KSA inaonekana kulemewa na jukumu ililotwikwa na Wakenya. Kutokana na mtindo wake wa kuwanyima wananchi habari mitandaoni, shirika hilo lina wafuasi wachache mno – 600 Twitter na 64 Fabebook!

Hii inamaanisha kuwa halifanyi kazi yake inavyostahili; halichapishi ripoti za tafiti mbalimbali ulimwenguni kwa manufaa ya wananchi kung’amua maendeleo ya sasa; halilinganishi teknolojia za wavumbuzi mbalimbali; na huenda ndio maana halina chochote cha kuwaambia wananchi.Wakenya wangependa kuarifiwa kuhusu jitihada za taifa lao katika mpango mzima wa kutafiti kuhusu anga ya sayari.

Hususan ni lini itaweza kutuma chombo angani kukusanya data kama mataifa yanayoendelea.Ingawa mwaka huu KSA ilitoa Sh5 milioni kufadhili utafiti wa hali ya hewa kwa vyuo vikuu vya Eldoret, Dedan Kimathi na Taifa Taveta; kama taifa ambalo limejaliwa vipaji vya teknolojia, vizingiti katika kutoa habari za utafiti havifai kushuhudiwa.

Kenya, inayojipiga kifua kama mbabe wa utafiti wa kiteknolojia barani Afrika, inafaa kuchangia pakubwa katika utoaji wa habari muhimu kuhusu anga ya bara hili.

Utafiti unaonyesha kuwa kutokana na ukosefu wa data kuhusu mawimbi katika sehemu mbalimbali za njia za ndege angani, kampuni za ndege hupoteza Sh5 trillioni kila mwaka kwa sababu ya kucheleweshwa kwa safari za ndege, ambazo huishia kuelekezwa katika njia mbadala.

Sekta ya utalii inategemea mno utafiti huu kwani husaidia watalii kuamua iwapo watasafiri mataifa fulani. Kuvurugwa kwa mawimbi yanayotumika kufanikisha mawasiliano ya rubani anayeendesha ndege na viwanja vya ndege, husababisha kuchelewa kwa abiria.

Zaidi, kujua ni wapi mawimbi hayo yatasababisha mtingiko wa ndege angani, ndizo habari muhimu sana katika sekta ya usafiri wa ndege.

Inachofanya Kenya ni kutegemea watafiti wa mataifa ya ng’ambo kama Amerika, China na Urusi, bila kujali kuwa anga zote ni tofauti kutokana na mvuto wa jua kwa dunia.

Tunaishi katika dunia inayobadilika kwa kasi, ukizingatia kuwa Amerika sasa ishaanza mpango wa kupeleka watalii angani ili wakaishi katika sayari nyinginezo, kutokana na machafuko ya hewa na mabadiliko ya tabia nchi kila mwaka.

Hayo tumeyajua kutokana na habari zinazochapishwa na NASA. Je, KSA isipotuarifu mitandaoni kuhusu mipango yake tutaijuaje?

fauzagila@gmail.com

AfCFTA yazindua programu ya simu kupanua biashara barani Afrika

NA RICHARD MAOSI

BARA la Afrika limepiga hatua muhimu katika ndoto yake ya kuanzisha soko la pamoja la kidijitali baada ya kuzindua programu ya simu hapo Jumanne itakayounganisha wafanyabiashara katika mataifa yote 54.

Hatua hiyo sasa imezidisha juhudi za kuwa na usemi katika soko la kidijitali duniani, huku wajasiriamali barani wakifunguliwa mfumo wa mtandaoni chini ya mpango wa Soko Huru la Africa (AfCFTA), ambao unalenga kuondoa visiki vya biashara mipakani.

Usimamizi wa AfCFTA uliambia Taifa Leo kuwa mradi huo wa kidijtali utawasaidia wafanyabiashara kupata ufadhili wa kifedha kabla na baada ya uzinduzi wa soko hilo hapo Januari Mosi, 2021.

“Kuzinduliwa kwa program hii pamoja na mashindano ya Vision Challenge ili kuwapiga jeki wavumbuzi wetu kufanya bishara barani ni idhibati kuwa kuna uwezo mkubwa na moyo wa kujituma kukuza biashara,” alisema Bw Francis Mangeni, mkurugenzi wa mipango na matangazo katika AfCFTA.

Apu hiyo pia inanuia kumaliza changamoto ya utambulisho wa mitandaoni kwa baadhi ya kampuni na biashara zinapohitajika kufanya hivyo na benki.

Programu hiyo ya simu inaweza kupakuliwa kutoka mtandao wa AfCFTA na itatumika kutoa taarifa muhimu za uwekezaji kwa wafanyabiashara.

Hili linajiri siku chache kabla ya kuandaliwa kwa kongamano la marais wa mataifa ya Afrika hapo Desemba 5, 2020 ambapo masuala muhimu kuhusu mpango mzima wa mradi huo yatajadiliwa.

Mradi huo sasa huenda ukawa fursa kubwa zaidi ya Afrika kujiletea mageuzi ya kimaendeleo, ikizingatiwa unaunda soko kubwa zaidi duniani lenye watu bilioni 1.3, Alitakalokuwa na uwezo wa kutoa ushindani kwa China, India, Ulaya na Amerika.

“Ni kweli kuwa Afrika tayari ina mikataba kadhaa ya kibiashara katika ngazi ya maeneo, lakini AfCFTA ni tofauti kwani imeundwa kufikia ndoto za waliounda wazo la Umoja wa Afrika. Litakuwa soko la hakika lenye uwezo mkubwa wa kushindana na mibabe ya biashara duniani,” aliongeza Bw Mangeni.

Benki kadhaa zikiwamo TDB, Africa50, AfDB, AFC, Equity Bank, Ecobank na Afreximbank zitasaidia katika ufadhili wa AfCFTA Vision Challenge ambapo wajasiriamali mbalimbali barani watajitokeza kuwania tuzo.

Mradi huo ukitekelzwa ipasavyo utapanua biashara baina ya mataifa ya Afrika huku uichangia pakubwa kukuza uchumi wa bara katika sekta mbalimbali.

FAUSTINE NGILA: Heko Twitter na Facebook kuzima tetesi za Trump

NA FAUSTINE NGILA

Katika uandishi wangu, nimekuwa nikiikemea mitandao ya kijamii kwa kuchangia pakubwa kwa kuenea kwa habari za kupotosha kutoka kwa watu maarufu na wenye ufuasi mkubwa.

Lakini raundi hii nataka kuipongeza mitandao hiyo, hususan Twitter na Facebook, kwa kujitokeza na kuwa ange kukabiliana na Rais wa Amerika anayeondoka Donald Trump ambaye amezoea kuchapisha cheche za maneno makali na jumbe za kupotosha zinazosomwa na mabilioni ya watumizi wa mitandao hiyo katika uchaguzi mkuu uliotamatika.

Bw Trump ana wafuasi wapatao milioni 88 kwenye mtandao wa Twitter na wengine milioni 32 katika ukurasa wake wa Facebook.

Pindi tu Amerika ilipoanza kuhesabu kura, Bw Trump alikuwa mwingi wa bidii kwenye mitandao hiyo akichapisha kila aina ya madai. Alisema kuna wizi wa kura, huku akijitangaza kama mshindi mtarajiwa katika kinyang’anyiro hicho cha urais.

Lakini baada ya kugundua njama zake, Twitter na Facebook hazikuchelewa. Zilimzima papo hapo kwa kueleza watumizi wa mitandao kuwa ‘habari hii haijathibitishwa na inapotosha.’

Hapo Jumanne bado Bw Trump alionyesha matumaini ya kutangazwa mshindi kwa kuchapisha kwenye akaunti zake za mitandao kuwa “tutashinda uchaguzi huu” na “kuna watu wanatumia vibaya fursa ya kuhesabu kura”, licha ya mpinzani wake Joe Biden kumiminiwa sifa na marais wengi dunia kwa kumbwaga.

Facebook iliwaeleza watumizi kuwa “Joe Biden ndiye Rais mtarajiwa baada ya uchaguzi kufanyika”, ujumbe ulioambatana na kila chapisho la Trump. Twitter nayo iliwashauri watumizi wake kuwa “madai haya ya wizi wa kura ni potovu”.

Kwa mara ya kwanza, nilifurahia hatua ya mitandao ya kijamii kuungana kupunguza kusambaa kwa habari feki, hasa katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa taifa lenye uwezo mkubwa duniani, ambao ulifuatiliwa na kila nchi.

Hapo awali mitandao hii ambayo inategemewa sana duniani kwa habari za kuaminika imejipata pabaya kwa kusaidia kupotosha mamilioni ya watu. Facebook, kwa mfano, ilikuwa taabani hapo Julai baada ya kubainika kuwa ilishindwa kuzima habari feki kuhusu virusi vya corona, habari hizo zikifikia watu bilioni 3.8.

Lakini kilichofanya mitandao hii kuchukua uchaguzi huo kama jambo la kiusalama ni agizo kutoka kwa Bunge la Amerika, kuwa wiki mbili baada ya uchaguzi, kampuni hizo zitafika mbele yake kuelezea jinsi zililinda haki na demokrasia mitandaoni.

Ninaamini hatua hii italeta mwamko mpya katika uchaguzi wa taifa lolote lile, ikizingatiwa kuwa ni wakati wa kampeni na kupiga kura ambapo wanasiasa wana mazoea ya kutuma jumbe za kubadilisha maamuzi ya wapigakura.

Sasa ninasubiri kuona kampuni hizi mbili zikichukulia uchaguzi katika mataifa yanayoendelea kwa uzito zilizoonyesha, hasa hapa Kenya ambapo tayari kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022 zimeanza.

Katika dunia ya sasa, demokrasia hufa katika giza la kidijitali, na ni wajibu wa wamiliki wa mitandao kulinda hali na ukweli, wapigakura wasije wakachagua viongozi wasiofaa.

Ielewe teknolojia ya kisasa ya kuotesha mbegu

Na SAMMY WAWERU

Mafanikio katika shughuli za kilimo-biashara yanaegemea mambo kadha wa kadha, ambayo mkulima anapaswa kutilia maanani ili kuyaafikia.

Kando na kujihami na utafiti wa kutosha kujua anachofaa kukuza na ni eneo lipi bora, ikiwa ni pamoja na kuwa na soko tayari la mazao, uhalisia wa pembejeo yaani mbegu, mbolea na dawa, unatajwa kama mojawapo ya nguzo kuu kufanikisha kilimo.

Pembejeo bandia na ambazo hazijaafikia ubora wa bidhaa, ni miongoni mwa changamoto zinazozingira wakulima, na zimechangia kwa kiwango kikubwa kulemaza azma yao.

Katika eneo tulivu la Kennol, Kaunti ya Murang’a, wanandoa wawili wachanga wamejituma kuangazia baadhi ya masaibu yanayofika wakulima.

Lamech Kabuti, 25, na mchumba wake Loise Ndung’u, 21, wanafanya kilimo cha kuotesha mbegu kupata miche ya mimea mbalimbali.

Unapozuru eneo hilo, utalakiwa na rangi ya kijani cha matunda kama vile maembe, maparachichi, mapapai, karakara na ndizi. Pia kuna wanaokuza mahindi na maharagwe.

Katika shamba la familia ya wanandoa hao lenye ukubwa wa ekari nne, ingawa taswira inawiana na ya mazingira jirani, kuna suala moja tu linalowafanya kuwa wa kipekee. Kwenye mgunda huo, wana kivungulio ambacho kwa upeo wa macho utadhani kinatumika kuzalisha nyanya, pilipili mboga au mazao mengine yanayolimwa kwenye mahema.

Loise Ndung’u, meneja wa Victorious Green Farms akieleza kuhusu uoteshaji wa mbegu na miche kupitia mfumo wa kisasa wa trei. PICHA/ SAMMY WAWERU

Kikiwa na ukubwa wa mita 8, upana na urefu wa mita 40, kina shughuli maalum; ni kiunga cha kuotesha mbegu na miche.

Chini ya utambulisho Victorious Green Farms, kivungulio hicho kinaotesha miche ya nyanya, pilipili mboga za rangi mbalimbali wengi wanazitambua kama hoho, sukuma wiki, kabichi, broccoli na kolifulawa.

Aidha, kiunga hicho pia kinaotesha miche ya kupandikiza ya matunda mbalimbali kama vile maparachichi, maembe, machungwa na mapapai.

Lamech Kabuti, afisa mkuu mtendaji na mmwasisi wacho anasema huotesha mbegu za kabichi zenye asili ya Kichina. Kinyume na wanaootesha mbegu kwenye kitalu cha udongo, Victorious GreenFarms imekumbatia mfumo wa kisasa katika uzalishaji wa miche.

Kwenye kiunga cha wanandoa hao, wanatumia trei maalum zenye mashimo. “Aghalabu trei tunazotumia moja ina mashimo 200, japo kuna za hadi mashimo 400,” Lamech na ambaye anajulikana kwa jina la lakabu kama Mkulima Mdogo adokeza.

Ukilinganisha na kitalu, mfumo huo unasifiwa kwa kinachotajwa kama “kufanikisha uoteshaji na uchipukaji wa mbegu kwa takriban asilimia 100”.

Pili, miche inaepushwa dhidi ya changamoto za wadudu na magonjwa. “Miche inapooteshwa kwenye kitalu cha udongo eneo tambarare, huendelea kusambaza magonjwa na wadudu inapohamishiwa shambani. Mfumo tuliokumbatia unapunguza kwa kiasi kikubwa athari hizo,” anaelezea Loise Ndung’u, meneja Victorious Green Farms.

Trei maalum kuotesha mbegu. Mfumo wa trei ni nafuu pamoja kuwa salama kwa mbegu na miche. Picha/ SAMMY WAWERU.

Isitoshe, kwa kutumia trei na kwenye kivungulio, Loise anasema miche inaondolewa ‘msongo wa mawazo’ unaosababishwa na miale kali ya jua. “Chini ya mfumo wa kisasa, miche inakuwa salama jambo linalochangia kuongezeka kwa kiwango cha mazao,” asisitiza.

Fauka ya tija hizo, miche inachukua muda mfupi kuwa tayari kwa upanzi.

Lamech anasema miche inayochukua kati ya wiki 5 – 7, kwa kutumia trei muda huo unapungua hadi wiki 4 au 5. Akitoa mfano wa Uholanzi, anasema kinachofanya nchi hiyo kuimarika katika sekta ya kilimo ni anachotaja kama kukumbatia mfumo huo wa kisasa katika kuotesha mbegu.

Kivungulioni, trei wamezitengenezea meza maalum zilizoinuliwa futi kadhaa juu, wakizitambua kama ‘beds’.

Kimsingi, wataalamu wanasifia matumizi ya trei kuotesha mbegu wakihoji zinapunguza gharama. “Kwa kutumia trei, una uhakika mbegu zitaota kwa karibu asilimia 100 kwa 100. Ni mfumo ambao unapunguza gharama, ikikumbukwa kwamba athari za wadudu na magonjwa zinaepukwa,” anafafanua Lawrence Ngugi, mtaalamu wa kilimo kutoka Hygrotech, kampuni ya uzalishaji na uoteshaji mbegu iliyoko Naivasha.

Victorious Green Farms inazingatia uzalishaji wa miche kwa njia asilia. Lamech akidokeza kwamba hawatumii fatalaiza wala kemikali yoyote.

“Badala ya udongo, tunatumia maganda ya nazi iliyokunwa, yakasagwa kisha yanatibiwa kwa dawahai. Watafiti wa masuala ya kilimo na asasi husika wamethibitisha kuwa maganda hayo ni salama,” akasema wakati wa mahojiano.

Muhimu zaidi katika kuotesha miche kupitia mfumo huo, ni kuzingatia kiwango cha usafi, kiwe cha hadhi ya juu.

Wanaoingia kwenye kivungulio wanadhibitiwa, ambapo anayeruhusiwa sharti makanyagio yake ya viatu yatumbukizwe kwenye maji yaliyotibiwa kwa dawa na yaliyoko mlangoni.

Maji yanayotumika kunyunyizia miche, Lamech anasema lazima yawe safi na wana bwawa ndogo linalowasambazia kiungo hicho. PICHA/ SAMMY WAWERU

Safari ya Victorious Green Farms ilianza 2016, Lamech akifichua kwamba hiyo ni baada ya kuhusika katika ajali mbaya na ambapo alilazwa hospitalini muda wa mwaka mmoja mfululizo.

“Hospitalini, matunda niliyopendekezewa nile kama vile karakara, matundadamu na mapapai yalikuwa nadra kupatikana,” anaeleza.

Kulingana na maelezo yake, alipopata nafuu, changamoto alizopitia – ukosefu wa matunda, zilimchochea kuingilia shughuli za uoteshaji mbegu na miche ya miti ya matunda.

Anafichua kwamba alianza kwa mtaji wa Sh10, 000 pekee na ni kupitia oda za wateja wake alipata wazo la kuotesha miche ya nyanya, pilipili mboga za rangi tofauti, sukuma wiki, kabichi, broccoli na kolifulawa.

Anasema uwekezaji katika kivungulio, ulimgharimu kima cha Sh140, 000.

Akikadiria gharama ya kuotesha mche mmoja kuwa kati ya Sh1 – 2, anasema Victorious Green Farms kwa mwezi hufanya mauzo ya miche isiyopungua 40, 000.

Huuza mche mmoja kati ya Sh2 – 15, huku akitumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook na WhatsApp kutafuta soko.

NGILA: Huduma Namba itumie ‘Blockchain’ kufanikiwa

NA FAUSTINE NGILA

Jina langu kwenye kitambulisho ni Faustine, lakini ajenti wa M-Pesa aliyenisajili kwenye huduma hiyo ya kutuma na kupokea pesa alikosea herufi ya kwanza la jina langu na kunisajili kama Eustine.

Licha ya juhudi zangu za kujaribu kurekebisha tegu hilo kwenye jina langu, limesalia vile vile kila ninapotumia huduma hiyo. Hii inamaanisha ukishasajiliwa kwenye mtandao huo, ni vigumu kubadilisha, na kosa hilo litasalia milele.

Hapo ndipo kuna tatizo kuu. Iwapo mtu atasajiliwa kwa jina lisilofanana herufi kwa herufi na lile lililo kwa kitambulisho chake, basi mtu huyo anaweza kukwepa vipengee kadhaa vya kisheria na kuwatesa wenzake kimakusudi.

Tuseme, kwa mfano, ametumiwa Sh250,000 kwa M-Pesa kimakosa kisha akatae kumrudidishia aliyetuma, je, aliyetuma atamshtaki nani? Aliyepokea atakuwa na ujasiri wa kusema si yeye alitumiwa hela hizo kwa kuwa jina lake la M-Pesa halifanani na lile la kitambulisho, na hivyo korti itatupa kesi hiyo.

Hii ndiyo taswira kamili ya changamoto za utambulisho wa kijumla hapa barani Afrika. Utampata raia wa Burundi humu nchini amejisali kwa huduma za maongezi, M-Pesa na hata benki akitumia kitambulisho cha Mkenya.

Ni dhahiri kuwa maelfu ya wanafunzi wamejisajili kwenye huduma hizi wakitumia vitambulisho vya wazazi wao na hata babu zao.

Juzi nilipigwa na butwaa kuona ujumbe mmoja pale Twitter mtumizi mmoja akijipiga kifua jinsi Safaricom hawawezi kumnasa kirahisi kwa maovu anayofanya kwa kuwa alijisali akitumia kitambulisho cha nyanya yake aliyefariki zamani!

Kutokana na hili, serikali ya Kenya hivi majuzi imekuwa mbioni kuvumisha mradi wa Huduma Namba, Wakenya 12 tayari wakimiliki kadi zao.

Ingawa ni hatua nzuri inayolenga kuondoa kasoro katika utambulisho wa wananchi kidijitali, sina imani na jinsi mradi huo unaendeshwa. Huenda usitoe suluhu za maana kwa visiki hivi.

Ikiwa serikali inanuia kumaliza uhuni wa mitandaoni na kusawazisha data ya wananchi wote, basi mbona isitumie mfumo wa teknolojia ya blockchain? Kinachohitajika tu ni kukusanya data yote ya Wakenya kwenye seva za serikali na kuipakia kwa mfumo wa kidijitali, kisha kuwasajili kwenye mfumo huo kwa kutumia majina yao halisi na nambari za vitambulisho.

Data yote kuhusu kila mtu kama nambari ya simu, nambari ya Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA), nambari ya Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF), nambari ya Hazina ya Bima ya Afya nchini (NHIF), picha ya uso, aina ya damu, alama za vidole, historia ya elimu, cheti cha kuzaliwa, cheti cha ndoa, nambari za kaunti za benki, mashirika na hata vitambulisho vya kitaaluma yafaa kuunganishwa kwenye mfumo huo.

Mtu anapofariki basi data katika mtandao huo yafaa kuonyesha hayupo tena na taarifa zake haziwezi kutumika tena.

Hii ndiyo suluhu tosha kuzima wizi wa mitandaoni, uuzaji wa bidhaa ghushi na ulanguzi wa binadamu.

Ninaishangaa serikali kwa kuwa licha ya kuunda Jopokazi la Blockchain linaloshughulikia matumizi ya teknolojia hii humu nchini, haina nia ya kutumia mapendekezo yaliyotolewa kuhusu kuondoa vizingiti vya utambulisho wa wananchi.

Kwa kutekeleza mradi wa Huduma Namba tukitumia blockchain, basi matatizo mengi ya utambulisho ambayo tumeshuhudia kortini na hata kwenye uchaguzi yatatoweka yenyewe.

Lakini iwapo serikali itatekeleza mradi huo bila teknolojia hii, basi ni hadaa tupu kwamba inalenga kuwasaidia Wakenya, ni kisa tu kingine cha matumizi mabaya ya ushuru tunaolipa kila siku.