LISHE: Ugali na dagaa

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 15

Muda wa mapishi: Dakika 30

Walaji: 4

Vinavyohitajika

 • dagaa wabichi
 • unga wa ugali kilo 1
 • nyanya ya kopo
 • vitunguu maji 2
 • limau ½
 • pilipili
 • chumvi
 • mafuta ya kupikia
 • pilipili mboga
 • kitunguu saumu
 • tangawizi
 • binzari ya curry

 

Maelekezo

Safisha dagaa kisha waoshe na uwakaushe na taulo ya jikoni na uwaweke pembeni. Kisha katakata vitunguu na pilipili mboga kisha weka pembeni.

Baada ya hapo weka sufuria mekoni na umimine mafuta ya kupikia kwenye sufuria. Yakishapata moto, tia dagaa na uwakaange mpaka wawe wa kahawia.

Sasa tia kitunguu saumu, curry powder na tangawizi. Kaanga kidogo kisha malizia kwa kutia vitunguu maji, pilipili mboga, pilipili kichaa, chumvi na ukamulie juisi ya limau.

Kaanga kwa muda wa dakika tano na hakikisha vitunguu na pilipili mboga kwa pamoja haviivi sana na hapo dagaa watakuwa tayari.

Kusonga ugali

Kwanza unatakiwa kuchemsha maji ya moto, kisha koroga pembeni unga kiasi katika maji ya baridi na utie kwenye maji yanayochemka.

Fanya kama unatengeneza uji, uji wa ugali ukishachemka, tia unga na uanze kuusonga mpaka ugali uive. Ukishaiva pakua na dagaa tayari kwa ajili ya kuliwa.

Himizo serikali na mashirika kuwapelekea msaada wakazi wa vijiji vya Boni wanaokabiliwa na baa la njaa

Na KALUME KAZUNGU

WAKAZI wapatao 3,000 wa vijiji vya msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu wanakabiliwa na njaa, hali ambayo imewasukuma wengi wao kujitafutia matunda na mizizi msituni kutumika kama chakula.

Vijiji vinavyokabiliwa na tatizo hilo ni pamoja na Milimani, Basuba, Mangai, Mararani, Pandanguo, Madina na Kiangwe.

Vijiji hivyo hukaliwa na jamii ya walio wachache ya Waboni.

Taifa Leo ilizuru vijiji hivyo juma hili na kubaini kuwa wakazi wengi wanalazimika kuingia msituni kuchuma matunda ya mwitu ili kulisha familia zao kutokana na uhaba wa chakula unaoshuhudiwa eneo hilo.

Wakazi walisema licha ya kujitahidi kulima mashamba yao mwaka huu, hakuna mavuno yoyote walipata kutokana na wadudu pamoja na wanyama pori waliovamia na kuharibu mimea yao.

“Hatuna chakula na maji hivyo tunalazimika kuingia msituni kuchuma matunda ili kulisha wake na watoto wetu na tusipofanya hivyo tutakufa njaa kwa sababu hakuna mavuno yoyote tulipata eneo hili,” akasema mkazi wa Milimani Bw Musa Abatika.

Naye Bi Fatma Barissa alisema watoto wao huenda wakaugua utapiamlo kutokana na kukosekana kwa lishe bora.

Ameiomba serikali na wahisani kujitolea na kupeleka misaada ya chakula vijijini mwao.

Kwa upande wake, Msemaji wa Jamii ya Waboni, Ali Sharuti ameielekezea serikali lawama kwa kukosa kutimiza ahadi ya kuwasambazia wakazi wanaoishi msitu wa Boni chakula katika kipindi chote ambacho operesheni inayoendelea – Operesheni Linda Boni – inayolenga kuangamiza na kusambaratisha wapiganaji wa al-Shabaab.

Operesheni hiyo ilizinduliwa Septemba 2015.

“Serikali ilituahidi kwamba tungepewa misaada ya chakula na mahitaji mengine ya kibinadamu kipindi chote cha operesheni. Jamii yetu kwa sasa haisaidiwi. Msitu pia wameukataza sisi kuingia kujitafutia matunda. Tungeomba wazingatie hilo na watusaidie,” akasema Bw Sharuti.

Wasagaji unga walia wanunuzi kupungua

Na BARBANAS BII

KAMPUNI kadhaa za kusaga unga Magharibi mwa Kenya, zinakabiliwa na hatari ya kufunga biashara zao baada ya wanunuzi wengi wa unga kuacha kununua bidhaa hiyo na kuamua kutumia unga unaosagwa katika vinu vya kawaida, wanaoamini kuwa salama.

Watu wengi wanahofia unga unaosagwa viwandani una sumu ya aflatoxin kutokana na kiwango ambacho serikali ya Kenya imetoa kizingatiwe.

Hii ina maana kuwa baadhi ya wafanyakazi katika kampuni hizi watapoteza ajira.

Kampuni 10 ndogo ndogo za usagaji tayari zimewatuma baadhi ya wafanyakazi wao katika likizo ya lazima kutokana na ukosefu wa soko kwa bidhaa zao.

“Kwa kipindi cha majuma mawili yaliyopita hatujafanya kazi kikamilifu kwa sababu wanunuzi wanakataa unga gredi 1. Hali hii imetulazimisha kusitisha baadhi ya kanuni za serikali kuhusu kiwango cha aflatoxin kinachohitajika mahindi kuwa salama.

Wanasema mahindi mengi yanayozalishwa nchini yana kiwango cha aflatoxin kinachopelekea mazao hayo kutochukuliwa kuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Kulingana na wakurugenzi wa kampuni hizo, mahindi yanayozalishwa katika sehemu nyingi nchini yana kiwango cha aflatoxin ya punje 12 kwa kila punje bilioni ya mahindi. Wanataka viwango salama vya inflatoxin vilegezwe kwenda sambamba na viwango vinavyokubalika kimataifa.

Kupitia Muungano wa Wasagaji Nafaka (GBMA), kampuni hizo pia zimelalamikia uhaba wa mahindi kutokana na kupungua kwa uzalishaji msimu uliopita-kutoka magunia milioni 444 hadi magunia milioni 33. Aidha, wanataja kero la sumu ya aflatoxin kuwa changamoto kuu kwa shughuli zao.

“Wakati huu tumepunguza kiwango cha uzalishaji hadi asilimia 30 kutokana na uhaba wa mahindi, hali iliyosababishwa na changamoto ya uwepo wa kiwango cha juu cha aflatoxin,” akasema mwenyekiti wa GBMA Kipngetich Mutai.

Muungano huo ambao unaleta pamoja zaidi ya kampuni 35 za wasagaji wadogo, umeitaka serikali kulegeza kanuni kuhusu kiwango cha aflatoxin kinachochukuliwa kuwa salama kutoka 10 hadi 20 kwa bilioni moja ya punje za mahindi.

“Mexico ina viwango vya 20, China (40), Misri (30) na Korea Kusini (20). Viwango vyetu vikipunguzwa hadi 20, tutaweza kushindana vizuri katika soko huru,” akaongeza Bw Kipngetich.

Jinsi ya kusonga ugali

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 5

Mudda wa mapishi: Dakika 20

Walaji: 3

Vinanyohitajika

• maji vikombe 3

• unga wa ugali

• sufuria

• ubanio

• mwiko

• jiko la aina yoyote ama mkaa, umeme au gesi

Maelekezo

Injika sufuria yako mekoni ikiwa na maji yenye unga kidogo.

Hakikisha maji utayoweka yatakutosha. Pia hakikisha moto unakua sio mwingi bali ni wa wastani.

Pale maji yatakapochemka na kutokota, weka unga kiasi kwenye maji hayo huku ukianza kuusonga taratiiibu na ubanio.

Songa ni kama unauminya huku unauzungusha kwa mwiko. Utaona mabadiliko ule uji utakuwa mgumu kila unapoendelea kuusonga.

Ukishaona mabadiliko hayo, punguza moto na ufunike ugali wako kwa dakika 10.

Andaa sahani au hotpot kisha uepue ugali wako.

Pakua kuliwa na mboga yoyote ile uliyoiandaa; inaweza ikawa samaki, nyama au chochote ukipendacho.

Mboga sukumawiki ba mayai. Picha/ Margaret Maina

Kaunti yawapa chakula ombaomba kama njia ya kuwataka wasijazane mjini

Na WINNIE ATIENO

WAKATI huu wa janga la Covid-19 ni kipindi ambacho familia za kurandaranda na wale wa kuombaomba wanaendelea kumiminika Kaunti ya Mombasa kuomba chakula na pesa.

Hii ni kufuatia makali ya maisha yaliyoletwa na athari za virusi vya corona.

Kulingana na serikali zaidi ya watu laki 300,000 nchini wamepoteza ajira kufuatia athari za janga la corona huku biashara nyingi na hata hoteli zikifungwa.

Hata hivyo, serikali ya Kaunti ya Mombasa imeweka mikakati kuwaokoa wakazi hao kwa kuwapa vyakula ili warudi makwao.

“Tumebaini familia nyingi zinamiminika katikati mwa jiji la Mombasa kuomba vyakula na pesa kufuatia janga la corona ambalo limesababisha wengi kupoteza ajira,” alisema Bw Innocent Mugabe afisa wa kaunti anayesimamia lishe.

Kulingana na takwimu za kaunti, kuna takriban familia 1,809 za kurandaranda jiji hilo la kitalii.

Serikali ya kaunti hiyo ilishindwa kudhibiti na kukabiliana na idadi kubwa ya familia za kurandaranda na wale ombaomba hususan wakati huu wa janga la ugonjwa wa Covid-19.

Hata hivyo wadadisi wameonya kwamba wamo katika hatari ya maambukizi ya virusi vya corona wakisalia bila makao.

“Tunataka watu wa familia waache kujazana katikati mwa jiji kutokana kwa sababu wanajiweka katika hatari ya virusi vya corona. Tunawapa vyakula ili wasalie majumbani mwao ambako wako salama zaidi,” aliongeza Bw Mugabe.

Familia 200 za kurandaranda zinaendelea kunufaika na shughuli hiyo.

Kitoweo cha samaki chajileta Garsen lakini hakuna ugali

Na CHARLES LWANGA

BAADHI ya waathiriwa wa mafuriko katika kijiji cha Hewani eneobunge la Garsen wamelalama wakisema hawana ugali wa kuliwa pamoja na samaki wa matope waitwao ‘mtonzi’ ambao wameletwa na maji ya mafuriko ya Mto Tana.

Kijiji hicho ni kimojawapo cha vijiji 15 ambavyo Shirika la Msalaba Mwekundu (KRCS) limekitaja kwamba kimeathirika zaidi na mafuriko baada ya mto kuvunja kingo zake na maji kuzingira kijiji hicho.

Mkazi Bi Fibi Jilo anayejulikana kama ‘Mama Bahati’ amesema kuwa wakazi wanahangaika kwa kukosa chakula baada ya mashamba yao ya mahindi kuharibiwa na mafuriko.

“Sisi ni wakulima wa mpunga, lakini siku hizi tumeachana nao na kuanza kupanda mahindi ambayo nayo yameharibiwa na maji,” akasema.

Akihotubia mkutano ulioandaliwa na mbunge wa Garsen, Bw Ali Wario pamoja na uongozi wa serikali ya kitaifa kupeana vyakula vya msaada, Bi Jilo alisema licha ya kuvua samaki aina ya mtonzi, wakazi wangali hawana chakula cha kutosha.

“Ingawa tuna mtonzi ambao wameletwa na mafuriko, hatuna sima, mpunga wala chakula kingine ambacho tunaweza kutemremshia nacho samaki hao,” akasema na kuongeza “sisi sasa tumebakia kuwa watu wa kula samaki kila siku.”

Kwa upande wake, Bw Wario alisema tayari amejadiliana na mkurugenzi mkuu wa Tarda Irrigation scheme ambaye ameahidi kugawia wakazi vyakula vya msaada ambavyo vitawakimu kimaisha.

“Vilevile, serikali kuu pamoja na shirika la KRCS ambalo limezuru waathiriwa wako mbioni kutafuta na kugawa vyakula vya msaada,” alisema na kuongeza serikali imetenga Sh250 milioni katika bajeti ya mwaka ujao kukarabati miundomsingi kuzuia athari hasi za mafuriko.

Alisema anaelewa kuwa watu hula chakula aina tofauti tofauti kulingana na mila na tamaduni na kwamba atahakikisha wakazi wote walioathiriwa na mafuriko wamepata vyakula vya msaada.

Takriban watu 11,000 katika eneobunge hilo wameathiriwa na mafuriko ambayo tayari yamemeza vijiji vya Danisa, Galili na Bandi, huku yakiendelea kufunika kituo cha polisi cha Gamba na ofisi ya chifu wa Galili.

Baadhi ya wavuvi katika kijiji cha Hewani waliambia Taifa Leo kuwa wamechoshwa kula mtonzi bila chakula kingine kwa sababu hawawezi kuvuka mto uliojaa mamba bila dau kwenda Sokoni Garsen kuuza samaki hao.

“Imebidi tuvue wa kula mtonzi nyumbani pamoja na familia zetu; hawa samaki wamo tele humu ndani na mara nyingi sisi hugawia majirani,” alisema Bw Joshua Jilo.

Isitoshe, katika soko la Garsen, Taifa Leo ilipata baadhi wakazi wakiuza samaki hao ambao wanasema huwa wengi wakati wa mafuriko kwa bei nafuu kuanzia Sh50 hadi Sh300 kulingana na ukubwa na uzito katika mizani.

Raha tele gharama ya kuandaa ugali ikishuka Magharibi

Na BARNABAS BII

WALAJI ugali katika eneo la Magharibi wamepata afueni baada ya bei ya unga wa mahindi kushuka.

Bei zilishuka kufuatia ukosefu wa soko la mahindi kwani kuna bidhaa hiyo tele inayoingizwa nchini kwa bei nafuu kutoka Uganda, wakati ambapo mavuno ya humu nchini pia yamejaa.

Wasagaji mahindi katika eneo hilo jana walisema hawana pa kuuza unga wa mamilioni ya pesa kwa sababu hakuna wanunuzi.

Hii imewalazimu kuteremsha bei hadi Sh90 kwa mfuko wa kilo mbili, kutoka Sh130 miezi miwili iliyopita.

“Tunakumbwa na changamoto kubwa kuuza bidhaa zetu kwa vile wanunuzi ni wachache sokoni ilhali tulitumia fedha nyingi viwandani,” akasema Bw Kipngetich Ngetich kutoka kiwanda cha usagaji mahindi cha Ineet, mjini Eldoret.

Bei ya mahindi ilishuka kutoka Sh3,200 hadi Sh2,800 kwa kila gunia la kilo 90 katika maeneo mengi ya Magharibi baada ya bidhaa hiyo kuwasili kutoka Uganda kwa bei ya chini.

Bidhaa nyinginezo pia zimeanza kushuka bei, kama vile kabeji iliyoshuka hadi Sh1,300 kutoka Sh1,800 na sukuma wiki inayouzwa kwa Sh700 kutoka Sh1,300 kufuatia mavuno tele eneo la Kerio Valley.

“Bei za mahindi zinatarajiwa kushuka zaidi kwa sababu kuna mavuno ya bidhaa mbadala, kuwasili kwa mahindi kutoka Uganda, na mavuno yanayotarajiwa katika eneo hilo,” akasema Bw Moses Kiptoo, mfanyabiashara wa mahindi Eldoret.

Hali hii imetokea wakati ambapo mzozo unatarajiwa kati ya kaunti zilizo chini ya Jumuia ya Kiuchumi Kaskazini mwa Rift Valley (NOREB) na wamiliki wa viwanda vya kibinafsi kuhusu ununuzi wa mahindi kutoka kwa wakulima kupitia kwa madalali.

Kaunti hizo zinataka viwanda vinunue mahindi moja kwa moja kutoka kwa wakulima.

KEBS yapiga marufuku unga chapa kadha

Na MWANDISHI WETU

SHIRIKA la Ukadiriaji Ubora wa Bidhaa Nchini (KEBS) limepiga marufuku unga wa mahindi unaotumika kwa maandalizi ya sima wa Dola, 210, Kifaru, Starehe na Jembe kwa sababu una aflatoxin kiwango cha juu huku ikiagiza uondolewe sokoni mara moja.

Kampuni zinazosaga na kuuza unga ulioathirika ni Kitui Maize Millers, Kenblest Limited, Alpha Grain Limited, Pan African Grain Millers, na Kensalrise Limited mtawalia.

“Kwa muda mrefu maafisa wa KEBS waklichukua na kupima sampuli za unga chapa mbalimbali na matokeo yanaonyesha unga Dola, 210, Kifaru, Starehe na Jembe una viwango vilivyopitiliza vya sumu aina ya aflatoxin vinavyoufanya kuwa hatari kwa ajili ya kuliwa na binadamu,” inasema sehemu ya taarifa ya KEBS iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumamosi.

Shirika hilo limeomngeza kwamba kampuni za usagaji mahindi na uuzaji wa unga chapa zilizoathirika wanafaa kusitisha upakiaji wa bidhaa hizo na usambazaji kwa ajili ya kuwauzia wateja.

MBURU: Serikali isihadae kuhusu uchumi, Wakenya wanaumia

Na PETER MBURU

SERIKALI kudai kuwa uchumi wa taifa unazidi kukua wakati mamilioni ya Wakenya wanazidi kulia kutokana na ugumu wa maisha ni kinaya kikubwa na ishara ya jinsi tuko katika kile tunachoweza kusema ni ‘Kenya mbili’.

Hii ni kwa kuwa licha ya kudai kuwa mambo yako sawa kiuchumi, idadi ya watu ambao wamefutwa kazi baada ya waajiri wao kushindwa kuhimili ugumu wa kiuchumi inazidi kuongezeka kwa maelfu, huku kampuni zaidi zikiendelea kutangaza mipango ya kufuta wafanyakazi.

Mitaani na vijijini, Wakenya wanateseka kwa kukosa kazi, mapato madogo kwa walio na kazi na mfumkobei wa bidhaa muhimu, hasa vyakula.

Tafiti za kiuchumi miaka ya majuzi zimeonyesha jinsi Wakenya wamekuwa wakikopa bidhaa za kimsingi kama vyakula madukani ili kuendesha maisha, kando na wengine wengi ambao wanazidi kufilisika na kuuza mali, ama kufunganya virago na kurudi mashambani kutoka mijini, kutokana na kulemewa na gharama ya maisha.

Maelfu ya wanafunzi wanazidi kufuzu kutoka vyuo, lakini wanaishia kukaa manyumbani kutokana na ukosefu wa kazi, wakati nyingi za kazi zilizopo serikalini zinapewa wazee wakongwe.

Ndiposa, pamoja na Wakenya wengi, tunashindwa kuelewa ni uchumi gani ambao serikali inazungumzia inaposema kuwa Kenya inazidi kukua, kwani hatuhisi chochote.

Ni kinaya kikubwa ikiwa uchumi unaimarika machoni pa serikali, lakini kwa wananchi unazidi kuzorota.

Unapodurusu mitandaoni ama kuzungumza na watu, ishara zote ni wazi kuwa Wakenya, haswa vijana, wana hasira- wamekasirikia serikali na viongozi kwa kuwatelekeza na kuwafanya kuadhibiwa vikali na uchumi.

Kitu cha pekee ambacho serikali imekuwa na bidii ya kuwapa Wakenya, hata bila kuitishwa- ni ahadi, ahadi kuwa kilimo kitaimarishwa, afya na elimu kuboreshwa, vijana kupewa kazi na kila Mkenya kuhakikishiwa anapata chakula.

Lakini kwa bahati mbaya, nyingi za ahadi hizi zimesalia kuwa hivyo tu, nyoyo na mawazo ya Wakenya yakishibishwa matarajio, lakini uhalisia wa maisha ukiwa kinyume kabisa.

Serikali yenyewe huongoza juhudi za kuwapelekea Wakenya wanaoishi kaskazini mwa nchi na maeneo mengine yanayokumbwa na mafuriko ama kiangazi misaada ya vyakula na vitu vingine vya kimsingi, ishara wazi kuwa bado kuna tatizo.

Ripoti za uchumi kukua haziwezi kuwa na maana yoyote kwa Wakenya ambao hali ya maisha inazidi kuharibika.

MAPISHI: Ugali na sukumawiki

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

UGALI

Muda wa kusonga sima: dakika 15

Walaji: 2

Vinavyohitajika

–          Unga wa mahindi nusu kilo

–          Maji lita 1

Maelekezo

Mimina maji kwenye sufuria kisha bandika kwenye meko ili yachemke.

Tengeneza mchanganyiko kwa kuongeza unga kiasi kwenye maji yanayochemka huku ukikoroga.

Ongeza unga ukikoroga kwa mwiko hadi uwe mgumu.

Endelea kukoroga ukihakikisha hakuna mabonge ya unga hadi ugali uwe laini.

Punguza moto kisha funika ugali kwa dakika 10.

Epua na upakue.

 

Sukumawiki

 Muda wa kupika: Dakika 5

Walaji: 2

Vinavyohitajika

–          Sukumawiki

–          Pilipili kijiko 1

–          Chumvi kijiko 1

–          Maziwa vijiko 4

–          Kitunguu

–          Pilipili mboga

–          Mafuta ya kupikia

–          Kitunguu saumu kijiko 1

Sukumawiki zikiwa zimepikwa. Picha/ Margaret Maina

Maelekezo

Andaa kitunguu na pilipili mboga kwa kukata vipande vidogovidogo.

Andaa sukumawiki.

Bandika sufuria mekoni hadi ipate moto. Weka mafuta kisha weka sukumawiki. Koroga vizuri kisha funika na uache kwa dakika moja kisha koroga na uepue.

Kwenye sufuria nyingine, weka mafuta kisha kitunguu maji. Koroga, weka kitunguu saumu, pilipili na chumvi. Endelea kupinduapindua.

Weka pilipili mboga, koroga na uache kwa dakika mbili vichemke pamoja.

Weka sukumawiki, koroga vizuri kisha weka maziwa na uache ichemke kwa dakika 3 kisha epua.

Pakua na ugali na ufurahie.

Aua mkewe kwa kukataa kumpikia ugali

Na BENSON AMADALA

MWANAUME aliyemuua mkewe kwa kukataa kumpikia ugali, amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi cha Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kakamega baada ya kunywa sumu.

Mauaji hayo yalitokea kijijini Emukaba, Butsotso, Kaunti ya Kakamega na majirani walida yalitokana na mzozo ulioibuka baada ya mwendazake kukataa kumpikia ugali mshukiwa.

Mshukiwa mwenye umri wa miaka 45, anadaiwa kukasirishwa na hatua hiyo ya mwendazake hivyo akamshambulia kwa kisu na kumdunga mara kadhaa.

Baada ya kumuua, mshukiwa anadaiwa kufunika maiti kwa blanketi ili kuficha ushahidi. Baadaye alienda kutazama mashindano ya kupigana kwa fahali kijijini hapo.

Aliporejea nyumbani muda mfupi baadaye, majirani kwake walipata mwili wa mwendazake umefichwa ndani ya blanketi na mshukiwa amezimia baada ya kumeza sumu.

Majirani baadaye waliwaita polisi ambao tayari wameanzisha uchunguzi kuhusiana na kisa hicho.

“Mshukiwa alijaribu kujiua kwa kunywa sumu na alikimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu,” akasema Afisa Mkuu wa Polisi (OCPD) wa Kakamega Joseph Chebii.

Be Chebii alisema mshukiwa atafikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya mauaji atakapopata nafuu.

Mshauri wa Masuala ya Kijinsia na Mipango Maalumu wa Kaunti ya Kakamega, Peninah Mukabane alielezea masikitiko yake kuhusiana na ongezeko la mizozo ya kinyumbani katika eneo hilo.

“Kumekuwa na ongezeko la mizozo ya kinyumbani kutokana na matumizi ya dawa za kulevya,” akasema Bi Mukabane.

Alisema kuwa idara yake imeanzisha mikakati ya kushughulikia mizozo ya kinyumbani miongoni mwa wakazi wa kaunti hiyo.

Katika eneo la Shiyunzu, mwanaume mwingine wa umri wa miaka 30 aliaga dunia alipokunywa sumu mara baada ya kutembelea wakwe zake kutatua mzozo baina yake na mkewe.

Bw Chebii alisema mwanaume huyo alizimia na kufariki papo hapo. Maiti yake imehifadhiwa katika mochari ya hospitali ya Kaunti ya Kakamega na polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na kisa hicho.

MAHINDI TELE, UGALI GHALI

Mwangi Muiruri na Cecil Odongo

HOFU ya kushtakiwa kwa maafisa wanaoshukiwa kuhusika katika sakata ya mahindi ndicho kiini kikuu cha uhaba wa mahindi, ambao Jumatatu ulifanya wasagaji kutangaza wataongeza bei ya unga hadi Sh100 na zaidi.

Pia hatua ya wakuzaji mahindi eneo la North Rift kupinga makubaliano ya kuuza mahindi kwa bei nafuu imechangia uhaba huo.

Duru za kuaminika ndani ya Serikali zilieleza Taifa Leo kuwa kuna mashauriano yanayoendelea ya kutafuta uwezekano wa washukiwa kurudisha mahindi waliyonunua kwa njia zisizo halali kwa wafanyibiashara waliyouzia NCPB, ili nao wairudishie pesa ambazo walilipwa.

Hii ni kutokana na shinikizo ambazo Rais Uhuru Kenyatta amewekea Wizara ya Kilimo akiitaka kuhakikisha wakulima wamelipwa pesa zao haraka iwezekanavyo.

Ni kutokana na hali hii ambapo NCPB imesita kuuzia wasagaji mahindi kwa bei ya Sh1,600 kwa gunia la kilo 90 kama Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri alivyoahidi mwezi uliopita ili kuwawezesha wasagaji nao kuteremsha bei hadi Sh75.

Duru zilidokeza kuwa bodi hiyo inahisi kuwa iwapo itauza mahindi kwa Sh1,600 kama Bw Kiunjuri alivyokubaliana na wasagaji, kisha maafikiano ya kurudisha mahindi na pesa yafaulu, watapata hasara ikizingatiwa waliyanunua kwa Sh3,200 kutoka kwa wafanyibiashara waliyoyaagiza kutoka nje ya nchi na hivyo kupungukiwa na pesa wanazofaa kurudisha.

Sakata hiyo ilizuka mwishoni mwa mwaka jana NCPB iliponunua mahindi yaliyoagizwa kutoka nje ya nchi kwa pesa zilizokusudiwa kuwalipa wakulima wa humu nchini. Hatua hiyo imefanya bodi hiyo kupungukiwa na pesa za kulipa wakulima.

Hapo jana, Bw Kiunjuri aliambia Taifa Leo kuwa ahadi ya Serikali kuuza mahindi kwa wasagaji kwa Sh1,600 ingalipo akiongeza kuwa hifadhi ya mahindi nchini tayari ina mahindi ya kutosha.

Kwenye maafikiano na wasagaji unga kuhusu kupunguzwa kwa bei hadi Sh75 mwezi jana, Serikali iliahidi kuhakikisha imewauzia wasagaji mahindi yaliyo NCPB kwa bei nafuu ya Sh1,600 ili kuwawezesha nao kuteremsha bei ya unga.

Lakini ahadi hiyo imegeuka kuwa hewa baada ya wasagaji kusema wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa mahindi sokoni. Hii inamaanisha kuwa Serikali haikuheshimu ahadi yake ya kuuza mahindi kwa bei nafuu ili kuwezesha wasagaji kuteremsha bei zao

Mwenyekiti wa muungano wa wasagaji, Bw Peter Kuguru, alisema hawana mahindi yoyote katika hifadhi zao.

“Bei ya unga itapanda hadi Sh100 na zaidi katika maeneo mbalimbali kuanzia mwishoni mwa wiki kwa sababu hatuna mahindi ya kusaga. Serikali inaonekana haina nia ya kupunguza uhaba huo kwa kutoa mahindi yanayohifadhiwa na NCPB,” akasema Bw Kuguru.

Alisema kuwa maagizo ya Bw Kiunjuri kuwa unga wa pakiti ya kilo mbili uuzwe kwa Sh75 hayawezi kutekelezeka ikiwa bei ya mahindi itaendelea kuwa ya juu.

“Inasikitisha kwamba tunapitia hali ngumu wakati ambapo mahindi yamejaa katika mabohari ya serikali. Pia hatuwezi kununua kutoka kwa wakulima kwa sababu wanauza kwa bei ya juu,” akaeleza Bw Kuguru.

Mkurugenzi wa Muungano wa Wakulima nchini Kipkorir Menjo alisema hatua ya kupendekeza mahindi kuuzwa kwa Sh1,600 kwa gunia haikujali maslahi ya wakulima.

“Hakuna mkulima anayeweza kukubali kuiuzia NCPB au kampuni za kusaga mahindi kwa sh1600 jinsi walivyokubalina kwa sababu hiyo ni hasara kubwa sana kwetu. Makubaliano hayo hayakuhusisha mkulima wala kuyazingatia maslahi yake,” akasema Bw Menjo.

Ugali ghali wabisha

Na BERNARDINE MUTANU

HUENDA gharama ya unga wa ugali ikaongezeka ikiwa mswada uliowasilishwa Bungeni utapitishwa na kuidhinishwa na rais.

Mswada huo ulifikishwa Bungeni miezi kadhaa iliyopita. Mswada huo wa Marekebisho ya Ushuru 2018 unalenga kubadilisha hadhi ya mahindi, ngano na mhogo, ambazo hazitozwi ushuru.

Kulingana na watengenezaji wa unga, kiwango cha ushuru kikibadilishwa kitapandisha bei ya unga, gharama itakayolimbikiziwa wateja wa unga.

“Hii ni kumaanisha kuwa watengenezaji wa unga hawawezi kujilipa ushuru unaotozwa bidhaa (VAT) kwa malighafi wanayotumia kutengeneza unga, kumaanisha kuwa gharama hiyo itapitishwa kwa wateja,” kilisema chama cha watengenezaji unga.

Bili hiyo inalenga mapato yanayotokana na unga wa mahindi, mkate na unga wa mhogo.

Mswada wa Ushuru kupandisha bei ya bidhaa muhimu

Na CHARLES WASONGA

BEI ya unga wa ugali, mikate na mihogo inatarajiwa kupanda ikiwa mswada uliowasilishwa bungeni mwezi Aprili utapitishwa kuwa sheria.

Mswada huo wa marekebisho ya Sheria za Utozaji Ushuru, 2018 unalenga kuwanyima wasagaji uwezo wa kukomboa ushuru wa thamani ya ziada kutoka kwa mahindi, ngano na muhogo.

“Athari ya hatua hii  ni kwamba wasagaji hawawezi kukomboa ushuru wa VAT kutoka kwa malighafi na hivyo kupelekea kupanda kwa bei ya unga, gharama ambayo itapitishwa kwa watumiaji bidhaa,” ikasema Chama cha Wasagaji.

Mswada huo unalenga kuanzisha ushuru unaolenga kuongeza ushuru unaotozwa unga wa mahindi, mkate na unga wa muhogo kwa zaidi ya asilimia 10.

Kampuni ya uhasibu PricewaterhouseCoopers (PwC) iliongeza kuwa hatua hiyo ya serikali kutoza ushuru huo utapelekea kupanda kwa bei ya bidhaa za kimsingi.

“Ingawa mswada huu utaiondolea serikali mzigo wa kulipa malimbikizi ya ushuru wa VAT, mabadiliko hayo yatachangia ungezeko la bei ya bidhaa nyinginezo,” ikasema PwC.

“Ukweli ni kwamba ikiwa mswada huo utatiwa saini kuwa sheria, maana yake itakuwa kuongezeka kwa bei ya bidhaa za kimsingi kama vile unga, maziwa, mkate….,” ikaongeza kampuni hiyo.

Bei ya mkate imesalia katika Sh50 kwa muda mrefu zaidi na mswada huo, ukipitisha, utapelekea ongezeko la bei yake.

“Serikali inafaa kutafakari upya kuhusu mswada huo wa marekebisho ya sheria za utozaji ushuru. Yatawaathiri Wakenya wengi ambao hutegemea bidhaa hizi za kimsingi ambazo wao hutegemea kila siku,” chama cha wasagaji kilisema kwenye taarifa.

OBARA: Serikali isibadili sembe bila ruhusa ya raia wake

Na VALENTINE OBARA

WIKI iliyopita nilipigwa na butwaa nilopofahamishwa kwamba serikali imenuia kuunda sera ambayo itawalazimu wasagaji mahindi kuchanganya unga huo na ule wa nafaka nyinginezo kama vile mtama, wimbi na mihogo.

Pendekezo hilo lililotangazwa na Katibu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia masuala ya mimea na sera, Bw Richard Lesiyampe, linalenga kupunguza jinsi wananchi hula kiwango kikubwa cha mahindi kila mwaka kuliko kile tunachozalisha.

Hakuna ubaya kuchanganya unga wa nafaka hizi kwani hiyo hufanywa na wanaotaka kwa hiari, lakini tatizo lililopo ni kwamba sera hiyo ilivyopendekezwa itaingilia biashara za watu binafsi isivyofaa.

Ulimwenguni kote jukumu la serikali huwa ni kubuni sera ambazo, mbali na kulenga kuboresha maisha ya wananchi wake, hutoa mazingira bora kwa wawekezaji kuendesha biashara zao bila kutatizwa isivyostahili.

Humu nchini inafahamika wazi kwamba unga wa mahindi ni bidhaa muhimu jikoni ndiposa kunapokuwa na uhaba wake, huwa taifa linaingia hofu kwani wengi huhisi kuna janga kuu la ukosefu wa chakula.

Hali huwa hivi hata kama kuna vyakula vingine sokoni kama vile mchele na viazi ambavyo virutubishi vyao vinaweza kuchukua mahala pa mahindi.

Hakika, wawekezaji katika biashara ya kilimo cha mahindi kwenye mashamba makubwa, uagizaji mahindi kutoka mataifa ya nje na utengenezaji wa unga wa mahindi wanafahamu fika jinsi Wakenya wanavyoenzi ugali wa mahindi na hivyo basi faida iliyo katika biashara hii.

Faida ni lengo kuu la biashara yoyote ile, na ni kutokana na faida hii ambapo serikali hupata ushuru wa kutosha kuendeleza majukumu mengine ya kujenga nchi.

Kwa hivyo sera yoyote inayopendekezwa na kupitishwa haifai kudhuru uwezo wa mfanyabiashara kupata faida zake.

Hatari iliyopo kuhusu pendekezo la Bw Lesiyampe ni kwamba linaweza likasababisha hasara kwa waekezaji na athari zake hazitapendeza.

Ingekuwa vyema kama tungeelezwa pendekezo hili lina msingi wake kwa utafiti upi ambao ulipata kuwa Wakenya watajitolea kununua unga wa ugali wenye mchanganyiko wa nafaka.

Kwa mtazamo wangu, hili ni suala ambalo kwanza litahitaji mchango wa wananchi kwani masuala ya unga si ya kufanyiwa mzaha katika nchi hii.

Ni bora serikali iweke mawazo yake na rasilimali kwa juhudi ambazo zinaendelezwa kuongeza kiwango cha mahindi kinachozalishwa kama vile kilimo cha unyunyizaji maji mashambani badala ya kuleta mapendekezo ambayo hayana msingi.

Ilivyo kwa sasa, takwimu zinaonyesha kuwa Kenya huzalisha karibu magunia milioni 40 ya mahindi na kutumia magunia milioni 30 kila mwaka, lakini kuna lengo la kupunguza matumizi hadi milioni 20 ili kusiwe na hatari endapo kutakuwa na mahitaji ya dharura.

Kile ambacho serikali pengine inaweza kufanya kama ina lazima kupunguza matumizi, ni kuweka ushuru kwa unga wa mahindi matupu, na kuondoa ushuru kwa bidhaa nyingine zinazoweza kuchukua mahala pa unga wa mahindi ikiwemo unga huo wa mchanganyiko ambao unaweza kuleta hasara kwa biashara.

 

Kicheko mahabusu kumlilia hakimu aongezwe ugali rumande

TITUS OMINDE na BRIAN OCHARO

MAHABUSU aliye katika rumande ya Gereza Kuu la Elodret alisababisha kicheko mahakamani Jumatano alipodai kuwa maisha yake yamo hatarini kutokana na kipimo kidogo cha ugali ambacho anapewa kizuizini.

David Shikoli ambaye anakabiliwa na mashtaka ya kubaka mwanamke, alimwambia Hakimu Mkuu, Bw Harrison Barasa kuwa mwili wake unaendelea kudhoohofika kutokana na ugali mdogo anaopewa huko.

“Mheshimiwa huu mwili wangu haukuwa hivi. Nimepungua kutokana na chakula kidogo ambacho napewa kule jela. Sikuzoea maisha ya kula ugali kidogo. Tafadhali nitetee,” akasema Shikoli.

Aliiambia mahakama kuwa juhudi zake za kutaka kusikizwa na wasimamizi wa gereza hilo zimegonga mwamba, kwani maafisa husika wamekuwa wakimwambia kuwa jela si nyumba ya mama yake.

Hata hivyo, hakimu alimshauri awasilishe malalamishi yake kwa maafisa wa maslahi kutoka katika idara ya mahakama, ambao watazuru gereza hilo mwishoni mwa juma hili.

Shikoli alishtakiwa pamoja na wenzake ambao hawako mahakamani kwa kubaka mwanamke mmoja mnamo Desemba 23, 2017 katika kijiji cha Kambi Miwa kwenye kaunti ya Uasin Gishu.

Kesi yake itasikizwa Mei 7.

Katika mahakama ya Mombasa, mwanamume aliwaacha watu vinywa wazi, alipokiri kuiba vijiko 108 vya thamani ya sh3,780 kutoka duka kuu la Uchumi.

Theophilus Mutunkei Sakaya hata hivyo hakufafanua sababu za kitendo hicho.

Alishtakiwa kuiba vijiko hivyo kutoka kwa duka hilo kwenye barabara ya Moi mnamo Aprili 21 mwaka huu.

Hata hivyo, Sakaya aliachiliwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Edgar Kagoni baada ya kusema kuwa alitaka kwenda kwa mazishi ya mama yake ambaye alikufa wiki moja iliyopita.

“Nimesikia malilio ya mshukiwa na kuzingatia kwamba vijiko vyote vimepatikana, nitamuachilia huru chini ya kifungu cha 35 cha Kanuni ya Adhabu ya Jinai,” alisema Bw Kagoni.

Inasemekana kwamba siku hiyo, Sakaya aliingia katika duka hilo saa tatu na nusu asubuhi akijifanya kuwa mteja.

Ripoti za polisi zasema alielekea moja kwa moja kwenye rafu ambapo vijiko vilikuwa na kuchukua rundo tisa za vijiko na kuziweka katika mfuko wake wa mbele.