Corona ilivyohangaisha makahaba dhuluma zikiongezeka

NA RICHARD MAOSI

MAKAHABA kutoka Magharibi mwa Kenya wamekuwa wakipitia hali ngumu ya kiuchumi tangu janga la corona kubisha humu nchini.

Wanasema wamekuwa wakipitia masaibu chungu nzima, baadhi yao wakibakwa, kuuawa na wengine kunyanyaswa kijinsia katika harakati ya kila kitu kutafuta riziki.

Muungano wa Makahaba wa Magharibi Western Sex Workers Association(Wekeswa) kupitia mratibu wao wa eneo la Magharibi J.O, wamekuwa windo rahisi kwa wateja wanaodai ngono cha nguvu na maafisa wa usalama.

Alieleza kuwa wamekuwa wakihangaishwa na wateja katika maeneo ambayo walidhani ni salama.

“Ni hali ambayo imekuwa ikileta unyanyapaa kwa kuhisi kubaguliwa katika sehemu ambazo awali tulikuwa tukiendesha biashara bila woga wa kupotea maisha,”J.O akasema.

Anasema kuwa mnamo 2020 waliamua kuchukua hatua isiyokuwa ya kawaida kujikinga.

Aidha alieleza kuwa Wekeswa ni muungano wa zaidi ya makundi 11 kutoka Kisumu, Migori, Homabay, Mumias, Siaya , Bungoma na kwingineko.

“Matatizo yalianza wakati ambapo wateja wengi walipoteza kazi serikali ikiwaomba kujikinga dhidi ya msambao wa covid-19, waliposhauriwa kuchukua tahadhari za kukaa nyumbani na kudumisha umbali wa mita moja,”akasema.

J.O aliongezea kuwa wengine wao walilazimika kurejea mashambani waliposhindwa kulipa hata kodi za nyumba.

“Walioshindwa kustahili shinikizo la kupata hela waligeukia ulevi, wakitumai kuwa wangefanikiwa kutuliza mawazo, ndio maana tuliamua kusaka msaada wa kitaaluma kuwasaidia wenzetu kujinasua kutoka kwa kwa matatizo kama haya,”

Aidha alisuta baadhi ya vyombo vya habari kwa kufanya mahojiano na wanachama wao bila kupata idhini kutoka kwa muungano wa Wekeswa, jambo ambalo limekuwa likiwaharibia jina kwa umma.

J.O alisema kuwa baadhi ya wanachama kutoka Magharibi na Nyanza wamekuwa wakitafuta tenda kutoka kwa serikali, ila hawana uwezo kutokaa na kipato cha chini.

Aidha vyumba vya burudani ambapo wamekuwa wakiendesha biashara yao vilifugwa makali ya Covid-19 yalipoendelea kusambaa nchini.

Aliongezea kuwa licha ya changamoto nyingi wamefanikiwa kusomesha ndugu zao mpaka kiwango cha Chuo Kikuu kutokana na hela za ukahaba.

“Nilipokuwa darasa la saba nilipoteza wazazi wangu wote, jamaa zangu walinyakua urithi ingawa nilifanikiwa kufika kidato cha nne, hivi sasa ninapigania haki za makahaba wenzangu katika eneo la Magharibi,”alisema.

J.O aliongezea kuwa katika mtaa wa Nyalenda kuna zaidi ya makahaba 300, wengi wao wakiwa ni wanafunzi walioingilia biashara hii wakati wa likizo ndefu ya 2020.

Wengi wamekuwa wakipata ujauzito, na kuanza kuwategemea marafiki zao wawasaidie kulisha watoto wao.

J.O analenga kuwasaidia wasichana kama hawa akiamini kuwa watarejea shuleni, na watafanikiwa kupata walezi ambao watawasaidia kulinda watoto.

“Kabla ya Covid-19 kuingia nchini tulikuwa na makahaba 5000 pekee mjini Kisumu lakini hivi sasa wamefikia 7000 na idadi yao inaendelea kuongezeka hususan sehemu za mijini,”

Hata hivyo kaunti ya Bungoma na Trans Nzoia zimekuwa na idadi ndogo ya wanawake ambao wanaendesha biashara ya ngono.

Msemaji wa Wekeswa P.O aliomba vyombo vya habari kukoma kuwaharibia jina makahaba kwani ni wafanyikazi kama mawakili, tabibu na walimu.

Vilevile alieleza kuwa wameweka mpangilia kabambe wa kustaafu hususan kwa wale ambao wamejiendeleza kimaisha kwa kuongeza kiwango cha elimu.

Alisema kuwa wa punde zaidi kuachana na kazi ya ukahaba meendea taaluma ya utabibu, wengine 30 walifaidika Sh 1000 za kila siku za Covid Relief Fund, huku wengine 40 wakipata nafasi katika mradi wa Kazi Mitaani.

Wanaume makahaba waongezeka Mombasa

Na WINNIE ATIENO

TAHARUKI imetanda Kaunti ya Mombasa baada ya vijana kati ya umri wa miaka 19 na 23 kujitokeza na kutangaza hadharani namna wanavyosajiliwa na wanawake matajiri kula uroda nao katika hoteli za kifahari na majumba ya ukwasi eneo la Nyali.

Idadi ya wavulana wadogo wanaowekwa kimada na wanawake wenye umri wa makamo au hata zaidi inaongezeka katika mji wa kitalii wa Mombasa, suala linaloendelea kuzua taharuki eneo hilo.

Hata hivyo, baadhi ya vijana hao waliambia Taifa Leo kuwa walisukumwa kwenye biashara ya ngono kutokana na ugumu wa maisha wakati shughuli za kawaida zilipoyumbishwa na janga la corona.

“Nilijitosa katika tabia ya ukahaba sababu ya ukosefu wa ajira. Wale wanawake wana pesa, anakutumia teksi uende mahali aliko ama mnakutana hotelini. Ni biashara iliyo na pesa,” akasema kijana wa umri wa miaka 22 anayekiri kujiingiza kwa hiyo tabia.

Mtaani Bamburi, Shawn alisema alisajiliwa kwenye biashara hiyo na rafiki yake kwenye kikundi cha makahaba wanaume.

“Rafiki yangu alinijuza kuhusu biashara hii ya ngono na nikalipishwa Sh500 kuwa mwanachama wake. Msajili wetu hututafutia wateja. Kila mteja ninayepata huwa nalipwa Sh4,000 ikiwa chache lakini kazi ikiwa nzuri huwa nalipwa Sh7,000 kwa kila mteja,” afichua Shawn kutoka Bamburi.

Wapo wanaohisi biashara hii inayokiuka maadili imenasua vijana kutokana na uhalifu na matumizi ya dawa za kulevya.

Hata hivyo, wapo waliojinasua kutoka mtego huo na kuanza kurekebisha tabia ya walionaswa na biashara hiyo.

“Wakati corona ilipoanza ndipo mambo yalipokuwa mabaya kwa sababu wazazi walikuwa wanang’ang’ana sana. Mzazi wangu alikuwa anafanya kwa hoteli lakini zilipofungwa akakosa ajira. Ikabidi aanze kwenda kuwaoshea watu nguo ili tupate riziki. Ikabidi nisake pesa ili nimsaidie mamangu,” alisema Jackson.

Wale waliohojiwa na Taifa Leo walisema kuna kundi la WhatsApp lenye vijana zaidi ya kumi, ambao wanashirikiana pamoja na mkubwa wao mwenye kuwahadaa na kuwaingiza kwenye biashara hiyo.

“Hpao ndipo wanatafutiwa wateja kupitia mitandao ya ngono au kuunganishiwa na jamaa huyo anayesemekana ni kiongozi wao. Hao wanawake huishi sehemu kama Nyali wanasema mabwana zao hawawezi shughli,” aliongeza kijana mwingine ambaye aliomba jina lake libanwe.

Baadhi ya vijana hao wamejinasua na kundi hilo na sasa ni wasanii wanaotoa nasaha kwa wenzao kuvuka sakafu

“Yaliyopita si ndwele tugange yajayo..mtu akinihukumu sababu ya maisha yangu ya hapo awali ni sawa. Lakini nimebadilika na wazazi wangu wamenikubali,” alisema Wandera.

Maryline Laini, Mkurugenzi wa Ikoko Iju Africa alisema wazazi wengi hawajui maisha ya watoto wao.

“Wazazi wengi hawajui watoto wao ni makahaba. Ni dharihiri kuwa idadi ya wanaume makabaha imeongezeka. Vijana wanasajiliwa kuingia kwenye biashara za ngono kati ya wanaume ambayo imekithiri katika fuo zetu,” akaeleza Laini.

Hata hivyo, vijana hao kwa sasa wanaendelea kupata ushauri na nasaha kutoka kwa shirika la Ikoko Iju Africa, ambalo lina lengo la kuwafikia vijana wengi zaidi na kuwatoa kwenye maisha hayo.

Makahaba walilia serikali iwalinde dhidi ya dhuluma za wazee wa mitaa

Na WINNIE ATIENO

MAKAHABA mjini Mombasa wanaitaka serikali iwalinde dhidi ya dhuluma na unyanyasaji wanaopitia mikononi mwa wazee wa mitaa.

Wanadai wazee hao huwatoza Sh200 kwa kila mteja, huku wakishirikiana na vijana kuwadhulimu wanapokuwa kazini, hasa katika eneo la Nyali.

“Tunapigwa kila mara. Usalama wetu uko hatarini. Hatuna pa kukimbilia. Tukienda vituo vya polisi tunafukuzwa. Wakati wa kura huwa tunabembelezwa lakini sasa hatuna maana,” alisema mmoja wao, walipokusanyika jana mtaani Bombolulu.

Aidha, waliwalaumu wenye nyumba za wageni kwa kuongeza kodi ya ukahaba.

“Kitambo tulikuwa tunalipishwa Sh500 tukienda kukodi nyumba. Siku hizi wenye vyumba wanataka mtu alipe ada ya mteja na kahaba. Ukahaba umekuwa ghali sana na wateja wenyewe hawataki kulipa pesa. Kafyu imetuathiri sana hata hatupati faida yoyote,” alisema mwanachama mwingine aliyejitambulisha kuwa Bi Jane.

Mwanamke huyo ambaye ni mama wa watoto watano alisema aliingilia sekta ya ukahaba kutokana na ukosefu wa kazi.

“Mume wangu aliniacha na watoto miaka 10 iliyopita. Ikabidi nisake riziki kwa njia yoyote. Lazima niwalishe, niwavishe na kuwaelimisha wanangu. Si kupenda kwangu kuwa kahaba,” akasema.

Mama huyo alisema huwa anatoza mteja Sh700.

“Wenzangu wametorokea miji mingine kama Diani na Mtwapa sababu ya unyanyasaji unaoendelea hapa Mombasa. Tunashangaa kwa nini mzee wa mtaa achukue pesa zetu. Nyakati zingine tunakosa hata wateja,” akalalama.

Kutokana na mamalishi yao, mwakilishi maalum wa wadi, Bi Fatma Kushe aliwasihi maafisa wa usalama kuwakamata wanaoendelea kuhangaisha makahaba hao.

“Si kupenda kwao, wanatafuta riziki. Kwa nini uwadhulumu? Wazee wa mtaa wanaojihusisha na tabia hii wanafaa kuchukuliwa hatua,” alisema Bi Kushe.

Aliwataka wanaume wasio katika ndoa watumie lugha nzuri wawatongoze na kuwaoa wanawake hao, badala ya kuwaacha kuendeleza biashara hiyo.

“Kama umefika umri wa kuoa heri uchukue mmoja wa hawa akina mama ili uwasitiri. Baadhi yao huenda wakawa wanawake wazuri tu kwa tabia, lakini wamesukumwa huku na matatizo,” akasema.

Pia alimtaka mwakilishi wa wanawake kaunti ya Mombasa Asha Hussein kuwapa wanawake hao fedha za kufanya biashara.

FUNGUKA: Mimi ni kahaba mchana lakini mke wa mtu usiku

NA PAULINE ONGAJI

Kwa wengi, ukahaba mara nyingi hutokana na umaskini. Lakini sio kwake Bi Merita. Bibi huyu ameamua kufanya kazi hii licha ya kuwa ana taaluma ya kifahari na ameolewa na dume lililo na mfuko mzito na mama wa watoto wanne

Merita ni binti wa miaka 34 na amekuwa akifanya kazi hii kwa zaidi ya mwongo mmoja. Ni mkazi wa Pwani. Yeye ni msomi ambapo ana shahada ya uzamili katika masuala ya biashara na hata ana ajira nzuri tu.

Ni mkurugenzi msimamizi wa biashara katika shirika moja mjini Mombasa. Mumewe ni mfanyabiashara maarufu na anamiliki majumba na magari kadha wa kadha.

Kimapato, familia hii haina upungufu wa pesa na mumewe amekuwa akikidhi vilivyo mahitaji ya wanawe. Lakini hilo halijamzuia Merita kuendesha shughuli za ukahaba, kazi ambayo amekuwa akiifanya kwa usiri mkuu.

“Nimebobea katika masuala ya ukahaba ambapo wateja wangu wengi ni watalii wa kigeni.Mimi huwa nafahamiana na wateja wangu mitandaoni hata kabla ya wao kufunganya virago na kuzuru humu nchini.

Ni katika mazungumzo haya ambapo pia masuala ya malipo hushughulikiwa, kumaanisha kwamba baada ya shughuli kila mtu anaenda zake pasipo manung’uniko.Hii pia inasaidia kuzima shaka tunapokutana kwa mara ya kwanza.

Mara nyingi shughuli zetu huisha mchana, nyakati rasmi za kazi, ambapo ni vigumu sana kwa wanaonifahamu, na hasa mume wangu kufuatilia mienendo yangu.Kazi yangu nzuri imenifanya kusakwa sio tu na watalii wa kizungu, bali pia mabwenyenye kutoka humu nchini wanaozuru ufuoni wakiwa likizoni.

Wengi wao hunipigia simu kupanga jinsi watapokea huduma hizi pindi wanapofika mjini.Kuna wale wanaoniuliza kwa nini nafanya ukahaba ilhali pamoja na mume wangu tuna pesa? Ila mimi huwajibu kwa kuwauliza swali hili; je, ni wakati gani pesa zimewahi kutosha?

Pesa na zawadi

Kila wakati nikiishiwa na pesa, ninachohitaji ni kuwapigia wateja wangu simu tu, na muda si muda napokea senti katika akaunti yangu. Kumbuka kwamba katika haya yote, mume wangu pia ananishughulikia vilivyo kifedha kama mkewe.

Nimepokea pesa na zawadi za fedha na mali kutoka kwa wateja wangu, rasilimali ambazo mume wangu hafahamu kwamba namiliki.Kuna mmoja ambaye ameninulia jumba katika eneo la Lamu, mwingine ameninunulia gari la kifahari, na mwingine anaendelea kunijengea jumba la kukodesha katika mji fulani huku huku Pwani.

Mbali na pesa, kiu yangu inatokana ni ile raha tu ya kutumbuiza wageni. Mume wangu hajui nina ‘Side hustle’. Anachojua ni kwamba nikiondoka nyumbani huwa naelekea kazini nilikoajiriwa.

Kawaida mimi hurauka kwenda kazini alfajiri na mapema, hivyo hakuna anayeweza shuku nina shughuli ziada.Aidha huwa simpi mume wangu nafasi ya kunishuku kwani huhakikisha kwamba kila anapowasili nyumbani, anapata nishafika.

Nafanya majukumu yangu yote ikiwa ni pamoja na kumwandalia chakula, vilevile kumshibisha kimahaba”.

KURUNZI YA PWANI: Shirika lawataka wanaojiuza kimwili waanze kuuza sabuni

Na MISHI GONGO

SHIRIKA la kijamii la Nkoko Iju Africa linapanga kuwafaidi makahaba 4,000 mjini Mombasa kwa kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kujipatia mkate wao wa kila siku badala ya kujiuza kimwili.

Mradi huo unalenga kunufaisha asilimia 90 ya makahaba waliyopoteza ajira kufuatia kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19.

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa katika uzinduzi wa mradi huo Jumatano, mkurugenzi mtendaji katika shirika hilo Bi Maryland Laini alisema kufungwa kwa vilabu vya burudani na mikahawa ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona kumewaathiri makahaba pakubwa.

“Makahaba hupata wateja wao katika sehemu hizi, lakini tangu kuwekwa kwa marufuku ya kutembea baada ya saa moja usiku na kufungwa kwa sehemu hizo, uchumi wa kundi hilo umepata pigo kubwa,” akasema.

Mradi uliozinduliwa unalenga kuwapa makahaba hao ujuzi wa kutengeneza sabuni na maziwa kutokana na maharagwe ya soya; bidhaa ambazo watauza ili kujipatia riziki.

Bi Laini alisema mradi huo unawalenga makahaba na wanawake walioachiwa majukumu ya kulea watoto wao.

Aliongezea kuwa kuwekwa marufuku ya kuingia na kutoka katika baadhi ya kaunti pia kunawazuia makahaba kukutana na wateja wao.

Alisema kufuatia kudorora kwa biashara hiyo makahaba wamelazimika kutoza wateja wao Sh20 kuwapa huduma kinyume na hapo awali ambapo waliwatoza Sh50 hadi 10,000 kutegemea na umri, sehemu waliyokutana na mambo mengine.

Mkurugenzi mtendaji katika shirika la Nkoko Inju Africa (kushoto) Bi Maryland Laini akiwa na baadhi ya makahaba walionufaika. Picha/ Mishi Gongo

Mbali na kuwapa ujuzi huo, pia watawaelimisha kuhusu haki zao za kikatiba.

“Tumeona makahaba wakinyanyaswa na wateja na hata maafisa wa polisi bila ya wao kuripoti matukio haya kwa kuchelea kutiwa mbaroni, katika mradi huu tutawafunza kuhusiana na haki zao,” akasema.

Alisema katika eneo la Nyali pekee kuna makahaba 2,900 huku Kisauni ikiwa na makahaba takriban 2,000.

“Kufuatia kufungwa kwa shule, idadi ya makahaba inaongezeka. Watoto wanapopata mimba za mapema huingilia ukahaba ili kujimudu wao na watoto wao,” akasema.

Mmoja wa wanachama katika shirika hilo Bi Elizabeth Mbuli aliiomba serikali kuwajumuisha makahaba katika mradi wa chakula unaolenga familia zisizojiweza.

Aidha aliwahimiza wanawake kuunda vyama ili kujiendeleza kiuchumi.

Bi Mbodze Katana ambaye ni mmoja wa waliofaidika na mradi huo alisema tangu janga la Covid-19 makahaba wengi wanashindwa kumudu mahitaji yao.

Alisema kuna baadhi ambao wanahitaji dawa za kupunguza makali ya Ukimwi lakini kufuatia hali ngumu ya maisha, wanashindwa kununua dawa hizo.

“Tunahofia kufa na makali ya njaa. Tunaomba serikali kutupa msaada wa chakula,” akasema.

Awali makahaba hao waliomba serikali kuwaorodhesha katika kundi la watu wanaotoa huduma muhimu.

Karantini zageuzwa madanguro

Na WAANDISHI WETU

MAAFISA wa serikali Kaunti ya Nyamira wanasema baadhi ya watu wanaozuiliwa karantini kwa kushukiwa kuwa na virusi vya corona wamebadilisha vituo hivyo kuwa madanguro ya kufanyia mapenzi.

Kulingana na Kamishna wa hiyo, Bw Amos Mariba na Waziri wa Afya wa kaunti hiyo Douglas Bosire, baadhi ya watu walio karantini wamekuwa wakishiriki vitendo vya ngono katika vituo hivyo na kujiweka katika hatari zaidi ya kupata virusi hivyo kwa kukiuka agizo la kutokaribiana.

Maafisa wa serikali sasa wameapa kuchukua hatua ikizingatiwa kuwa tabia hiyo inaweza kusambaza virusi hivyo.

Watu 95 wamewekwa karantini ya lazima kwa kukiuka kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona kaunti ya Nyamira.

Miongoni mwa vituo wanamozuiliwa ni shule ya wavulana ya Nyambaria iliyoko kaunti ndogo ya Manga, shule ya upili ya Nyakongo iliyoko Masaba Kaskazini, shule ya upili ya Menyenya iliyoko Borabu, shule ya wasichana ya Kebabe iliyoko Nyamira Kaskazini na shule ya wasichana ya Sironga inayopatikana Nyamira Kusini.

Bw Mariba alisema serikali haitaweka vifaa vya kujikinga wakati wa kufanya mapenzi katika vituo vya karantini.

“Haya ni maeneo yaliyotengwa na hatutaruhusu yeyote kupeleka kondomu huko. Hatukubali tabia ya ukahaba katika jamii,” alisema.

“Wale wanaoingia karantini, wanafaa kuzingatia kanuni zilizowekwa na pia kutuarifu maovu yanayofanyika huko,” alisema Bw Bosire.

Bw Mariba alisema wale wanaokiuka kanuni za karantini watazuiliwa kwa muda mrefu katika vituo hivyo.

Kamishna huyo wa kaunti alikuwa akizungumza katika makao makuu ya kaunti ya Nyamira ambapo kamati ya eneo hilo ya kukabiliana na janga la corona ilipokea misaada kutoka kwa taasisi tofauti.

Katika kaunti ya Bomet, serikali imewaweka karantini watu wanne waliotoroka kutoka kaunti ya Nairobi. Watu hao walikamatwa umma ulipowaripoti kwa maafisa wa serikali. Kamishna wa kaunti hiyo Geoffrey Omoding alisema kwamba washukiwa hao wanatoka eneobunge la Chepalungu.

Watu hao watashtakiwa baada ya kukamilisha karantini.

Katika kaunti ya Kisumu, Gavana Anyang Nyong’o alisema watu 157 wamekaguliwa. Jumatatu, watu 87 waliopimwa korona hawakupatikana na virusi hivyo. Alisema serikali yake iliwapa mafunzo wahudumu wa afya na kuunda kamati vijijini vinavyoshirikisha machifu na wanachama wa nyumba kumi kukabiliana na corona.

Katika kaunti ya Migori, watu 25 wanaoshukiwa kutangamana na wagonjwa wawili wa corona, wamewekwa karantini. Miongoni mwa watu hao ni wanabodaboda na watu 23 wa familia moja kutoka eneo la Kuria Mashariki.

 

Ripoti za RUTH MBULA, RUSHDIE OUDIA, VITALIS KIMUTAI na IAN BYRON

Makahaba wataka wawekwe kwa orodha ya wanaotoa huduma muhimu!

Na Wachira Mwangi

HOFU ya kufa njaa imewakumba makahaba katika Kaunti ya Mombasa na sasa wanataka wajumuishwe miongoni mwa watu wanaotoa huduma muhimu, la sivyo, wapewe chakula cha msaada.

Makahaba hao walisema kuwa kufungwa kwa baa, hoteli na maeneo mengine ambapo walikuwa wanapata kipato, na pia watalii kuzuiliwa kuingia nchini, sasa kumewakosesha kipato kabisa.

Walisema pia tangu marufuku ya kutotoka nje usiku iwekwe ili kudhibiti ueneaji wa virusi vya corona, maisha yamezidi kuwa magumu kwa kuwa hawana wateja.

Afisa wa sheria kutoka Changamwe, Bi Betty Kitili, alisema kuwa makahaba hawana muda wa kutosha kufanya kazi zao mchana na pia malipo ni duni.

“Bado tunahitajika kulipa kodi za nyumba, kununua vyakula na kufanya mambo mengi ambayo yanahitaji pesa. Ninaona hatutakufa kwa corona, ila njaa ndiyo itakayotumaliza,” akasema Bi Kitili.

Mwenyekiti wa shirika la High Voice Africa, Bi Maryline Laini, alisema wengine wanalipwa Sh20 pekee ili angalau wakanunue chakula.

“Asilimia 90 ya makahaba sasa hawana kazi. Majengo kama vile baa, hoteli na klabu yamefungwa. Hizo ni sehemu ambazo wengi wetu tulipata riziki,” akasema Bi Laini.

Kioja cha ukahaba kuvuma makanisani

Na SAMMY WAWERU

Uthiru, ni mojawapo ya mitaa inayounda kaunti ya Kiambu, na ambao ramani inaonyesha unapatikana katika eneobunge la Kabete.

Mtaa huo u kati ya Kikuyu na Kangemi, takriban kilomita 18.3 kutoka kitovu cha jiji la Nairobi.

Sawa na mitaa mingine Nairobi na Kiambu, wakazi na wenyeji wa Uthiru wanaendesha shughuli mbalimbali angalau kukithi mahitaji yao ya kimsingi na kujiendeleza kimaisha.

Katika mtaa huohuo, kinapatikana kitongoji cha Mariguini, ambacho sawa na jina lake lenye asili ya Agikuyu linalomaanisha ‘ndizi’ kimesheheni migomba inayozalisha matunda hayo.

Upande mmoja wa Mariguini umepakana na barabara kuu inayounganisha Nakuru, Naivasha na jiji la Nairobi.

Unapoabiri gari Nairobi kuelekea kitongoji hicho, kabla kutua utapitia ‘Uhuru Park’ ndogo, bustani ambayo wikendi huwa na shughuli kibao hasa za kuburudisha na kufurahisha watoto.

Barabara ya lami inayoelekea Mariguini kutoka barabara kuu ya Nairobi – Naivasha – Nakuru. Picha/ Sammy Waweru

Kando na kulakiwa na migomba, baadhi ya wenyeji hususan wenye ploti na mashamba wameingilia shughuli za kilimo, ingawa kwenye viunga na vivungulio – mahema.

Kuna wanaokuza karoti, spinachi, sukuma wiki, kabichi, na mboga zingine asilia, pamoja na mimea inayochukua muda mfupi kuzalisha na kuvuna.

Ipatayo miaka mitatu iliyopita, Wanjiru Kagotho alihamia Mariguini, baada ya kupata nafasi ya kazi katika mojawapo ya afisi za shirika la Price Water House Coopers, ndiyo PWC, Westlands, kama mpishi na mhudumu.

Hiyo ilikuwa baada ya kufanya vibarua vya hapa na pale eneo la Ruai, Nairobi, na alipopata fursa hiyo hakusita kuikumbatia.

Mtaa ulio karibu na uliomfurahisha kuishi ili kupunguza gharama ya usafiri ukawa Uthiru. Wanjiru anasema alielekezwa kutafuta nyumba ya kukodi ya bei nafuu katika kitongoji cha mabanda cha Mariguini.

Wanjiru Kagotho, anaishi eneo jirani na Mariguini. Alionywa dhidi ya kuishi humo kwa sababu ya utovu wa usalama. Picha/ Sammy Waweru

Hilo kwake lilikuwa pendekezo bora, akitumai ataweza kulea familia yake changa. Alitenga siku, akajituma kutafuta nyumba, na ni katika harakati hizo alikutana na mama mkongwe aliyemtahadharisha dhidi ya kuishi humo.

“Baada ya kunikagua kwa macho kwa muda, aliniambia hadhi yangu hainiruhusu kuishi katika nyumba za mabanda za Mariguini. Hakunieleza bayana sababu za kunionya,” Wanjiru ambaye ni mama wa watoto wanne anakumbuka.

Isemwavyo wazee waliokula chumvi wana maneno ya busara, hakuwa na budi ila kutii ushauri wa mama huyo, anayemtaja kama ‘muungwana na msamaria mwema’.

Alipata nyumba anayomudu kulipa kodi katika kitongoji jirani na Mariguini, hiyo ikiwa na maana kuwa akielekea kazini na kurejea hupitia pembezoni mwa alikoonywa kutoishi.

Mwezi wa kwanza, wa pili, wa tatu na miezi kadhaa ikayoyoma akiendelea kugubikwa na maswali “kwa nini huyo mama alinionya kuishi mabanda ya Mariguini, ilhali huskia yana nyumba za bei nafuu?”

Mwaka wa kwanza ulipokamilika, alianza kupevuka, akafumbuka macho na akili. Wanjiru anasema mwaka wa pili alikuwa na taswira kamili ya filamu ya Mariguini.

Mtaa wa mabanda aliotamani kwa sifa za kodi nafuu ya nyumba, una hulka za kipekee. “Mariguini ina zaidi ya makanisa 20 ambayo kila Jumapili mchana anga yake huhinikiza mahubiri na nyimbo za kumtukukuza, kumshukuru na kuabudu Mwenyezi Mungu.

“Kuanzia jioni, usiku kucha hadi asubuhi, mambo huwa tofauti kabisa na yanayofanyika mchana kutwa,” Wanjiru akaambia Taifa Leo Dijitali wakati wa mahojiano katika eneo hilo.

Wanjiru Kagotho, anaishi eneo jirani na Mariguini. Alionywa dhidi ya kuishi humo kwa sababu ya utovu wa usalama. Picha/ Sammy Waweru

Hadithi ya Sodoma na Gomora, huisoma kwenye Biblia na vitabu vya historia vya kidini, na kulingana na mkazi huyo sifa za Mariguini zinawiana na hadithi hiyo.

Licha ya eneo hilo kuwa na idadi kubwa ya makanisa, Wanjiru anasema ukahaba na uzinzi ndio ratiba ya kitongoji hicho kuanzia majira ya jioni, usiku hadi kunapokucha, kila siku.

“Kwa kuwa ninahudumu katika mkahawa, ninaporatibiwa kuhudumu usiku, ninapoelekea kazini jioni hujionea makuu ‘watu wakiingia kazini Mariguini na wakitoka asubuhi’ ninaporejea,” afafanua.

Isitoshe, ni katika mazingira yayo hayo yenye makanisa Wanjiru anasema mihadarati na dawa za kulevya hulanguliwa na kuuzwa.

Job Njuguna ambaye pia ni mkazi anafichua kwamba uuzaji wa pombe haramu Mariguini si jambo geni, na hufanyika mchana peupe.

“Pombe haramu kama vile chang’aa eneo hili la Uthiru hupatikana kwa urahisi hapa Mariguini,” Njuguna anaeleza.

Ni katika mazingira yayo hayo, tawi la kanisa la Nabii maarufu Dkt Edward David Awuor lipo.

Visa hivyo vikijumuishwa, kiwango cha usalama ni wazi kimedorora. “Changamoto kuu Mariguini ni utovu wa usalama, watu hulaghaiwa na kuibwa mali yao mchana. Usiku hakipitiki,” kauli ya pamoja iliyoradidiwa na wakazi tuliozungumza nao.

Kutia msumari moto kwenye kidonda kinachouguza majeraha, unapozuru Mariguini majira ya asubuhi hutakosa kutazama vijana na hata wazee wakitoka kwenye mabanda wakiwa walevi chakari.

Hatujali sura ya masponsa bora wawe na pesa nyingi – Wanafunzi

Na NASIBO KABALE

WANAFUNZI wa kike katika vyuo vikuu nchini wamefichua kwamba huwa hawajali jinsi sura ya mwanamume inavyokaa wanapotafuta ‘masponsa’, mradi tu mwanamume huyo awe na pesa zitakazowapa maisha ya kifahari.

Kulingana na utafifiti, wasichana hao hutarajia kupokea takriban Sh50,000 kila mwezi kutoka kwa ‘masponsa’.

Utafiti huo uliofanywa na shirika la Busara Center for Behavioural Economics, umeonyesha kwamba kati ya wanafunzi watano wa kike vyuoni, mmoja ana uhusiano wa kimapenzi na mwanamume wa umri wa juu ambaye jukumu lake kuu ni kufadhili mahitaji ya kifedha.

Shirika hilo liligundua kuwa wakati wanafunzi wanapopekua mitandao ya kijamii kutafuta wanaume, wao hutazama zaidi uwezo wake wa kifedha kuliko sura.

“Mapato yalitiliwa uzito kwa alama ambazo mwanamume alipewa ili awe ‘sponsa’. Aliye na mapato ya juu alipata alama zaidi. Walio na magari waliongezwa alama pia,” ikasema ripoti hiyo.

Kando na hayo, wasichana waliohojiwa walisema huwa hawajali kama mwanamume sponsa ana mke na familia. Hata hivyo, wangetilia maanani suala hilo kama mwanamume ni mpenzi wao wa kawaida.

Lakini wengi walifichua huwa wanaona aibu kufichulia watu kuhusu uhusiano wao wa kimapenzi na masponsa ambao kwa kawaida huwa ni wazee sana kuwaliko.

Utafiti huo ulisema uhusiano huo umebainika kuwapa wasichana nafasi ya kupata pesa, burudani na kufadhili maisha yao wanapokuwa chuoni ili waishi kwa starehe.

Yale wanayopata kutoka kwa wanaume hao ni usafiri katika maeneo ambayo kwa kawaida hawangefika wakiwa wanafunzi, burudani na nafasi ya kununua chochote watakacho ikiwemo kukodisha vyumba katika mitaa ya kifahari wakiwa wangali wanafunzi.

Utafiti huo ulishirikisha wanafunzi wa kike walio na umri kati ya miaka 18 na 24 kutoka vyuo vikuu mbalimbali jijini Nairobi.

Hata hivyo, kwa jumla ilibainika wanawake hutarajia kupewa pesa wanaposhiriki ngono na mwanamume, iwe ni mpenzi wao au sponsa.

Tofauti ya matarajio kutoka kwa wapenzi na masponsa ni kwamba masponsa hutarajiwa kutoa pesa nyingi zaidi na zawadi nono kuliko inavyotarajiwa kutoka kwa wapenzi wa kawaida.

Serikali kushtaki wazazi wa watoto katika ukahaba

Na MISHI GONGO

SERIKALI itawachukulia hatua wazazi wanaohimiza watoto wao kushiriki ngono na watalii kwa lengo la kujipatia pesa.

Mratibu wa Ukanda wa Pwani, Bw John Elungata, alisema hatua hii ni kuzuia visa vya wazazi kuwatumia watoto wadogo katika ukahaba ili kujipatia pesa kutoka kwa watalii wanaozuru Pwani.

Alisema baadhi ya wasichana hutoka kaunti zingine na kusafiri maeneo ya Pwani kwa lengo la kushiriki mapenzi na watalii.

“Tumekuwa tukishuhudia visa vya watalii kutumia watoto wadogo kimapenzi na tabia hii hatutaikubali.Tunataka wazazi wazingatie majukumu yao kikamilifu,”alisema.

Aliwaomba wazazi kutumia muda huu kuwaelekeza watoto wao kuhusu masuala ya kidini miongoni mwa mengine yanayofaa.

Bw Elungata alisema kuna baadhi ya watoto wa kike ambao hushawishiwa na wenzao kushiriki biashara hiyo ili kujipatia pesa za haraka.

Pia alisema kuna baadhi ya wazazi ambao hutumia watoto wao kama vitega uchumi.

Afisa mkuu katika idara ya watoto kaunti ya Mombasa, Bw Philip Nzenge, alisema idara yake itashirikiana na maafisa wa polisi kuhakikisha wanachukua hatua dhidi ya watu wanaohusisha watoto kwa mambo yasiyofaa.

Alieleza kuwa wazazi watakaotembelea vilabu vya pombe wakiwa na watoto watachukuliwa hatua pamoja na wamiliki wa vilabu hivyo.

“Mzazi unafaa kumlinda mwanao wakati wote.Si vyemai kuona mtoto katika kilabu cha pombe usiku wa manane. Utovu wa nidhamu hutokea sehemu hizi na watoto huiga ndiposa kumekuwa na ongezeko la mimba za mapema,dhuluma za kimapenzi na watoto kutumia vileo katika kaunti hii,” alisema Bw Nzenge.

Aliongeza kuwa hoteli nyingi mjini Mombasa hazijaweka mikakati ya kulinda haki za watoto.

Ukahaba ni hatia kama uavyaji mimba – Serikali

Na GEOFFREY ONDIEKI

SERIKALI imeapa kumaliza shughuli za ukahaba mjini Nakuru ambazo zimekithiri mitaani.

Kamishna wa Kaunti ya Nakuru Bw Erastus Mbui aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa kuna mipango ya kumaliza uovu huo.

Makahaba wanajishughulisha na uovu huo wameripotiwa kuwalazimisha wanaume wanaotumia mitaa hiyo kuchangia kwa utovu wa salama.

Bw Mbui alitaja shughuli hizo za ukahaba zinazoendelea mitaani kuwa kinyume na sheria za Kenya. “Hakuna kibali cha ukahaba nchini Kenya. Ni hatia, kama vile ushoga na uavyaji mimba,” alisema.

Kamishna huyo aliongeza kuwa watashirikiana na serikali ya kaunti kuhakikisha uovu huo unaondolewa.

“Tumepata habari kuwa kundi hilo la mwanawake wana muungano na unaongozwa na kiongozi wao, tutabaini nani aliwasajili na kuwapa kibali,” alisema Bw Mbui.

Hata hivyo, alikiri kutopata malalamishi kutoka kwa polisi kuhusu madai ya wanaume kusumbuliwa wakitumia mitaa hiyo. “Naomba wale wanaume ambao wamesumbuliwa kivyovyote vile wapige ripoti kwa polisi ili watusaidie kuwakamata wahusika,” alisema.

Shughuli za ukahaba hufanyika katikati mwa mji wa Nakuru, Kanu street, Maeneo ya ThreeWays na mtaa wa Kiambuthia.

Wakati mwingine huwa vigumu kwa wapita njia hasa wanaume kutumia mitaa hiyo wakiwa na wake wao kwa sababu [makahaba] huwalazimisha wanaume kwenye mitaa hiyo.

Taifa Leo ilipotembea maeneo ya Kisii Road, Kanu Street na maeneo ya Threeways, ilithibitisha ukweli wa madai haya.

Mwendo wa saa nne asubuhi, kina dada wa umri tofauti wanaonekana wameegema kuta wakiwa wamevalia nusu uchi.

Mmoja wao ambaye aliomba jina lake lisitajwe alisema kuwa wanawake wengi hufanya biashara hii ya ukahaba kutokana na umaskini na changamoto za kimaisha.

“Inatubidi kufanya hii kazi kukidhi mahitaji ya familia zetu na sio eti tunapenda anasa kama wengi wanavyofikiri,” alisema.

Bi Jane [sio jina lake halisi] aliongeza kuwa wasichana wengi wa vyuo vikuu wanajiingiza kwenye biashara hii chafu kwa tamaa ya kupata pesa kirahisi na mwishowe wanakuwa waraibu.

Wafanyabiashara Thika walalama makahaba wamekuwa kero

Na LAWRENCE ONGARO

UKAHABA unazidi kuenea mjini Thika huku wafanyabiashara wakidai umekuwa ni kero kubwa kwa biashara zao.

Bw Shardrack Kitoo ambaye ni mfanyabiashara kwenye barabara ya Uhuru Street mjini Thika, anasema biashara ya ukahaba inaendeshwa hata mchana.

“Tabia hiyo ya ukahaba inaendeshwa hata mchana hadharani na ni aibu kubwa kwetu na kwa wananchi kwa jumla. Cha kushangaza ni kwamba hata wao hutoza wanaume kiwango cha Sh100 kushiriki ngono nao,” alisema Bw Kitoo mnamo Jumatano.

Alisema ifikapo usiku, hapo ndipo ngoma huanza kwa sababu hata tabia ya kupora wapitanjia hushuhudiwa mara nyingi.

“Iwapo utalalamika kwao nao watatoa vijisababu kuwa umekataa kuwalipa haki yao. Hayo ndiyo masaibu wanaume wengi hupitia bila kutarajia,” alisema Bw Kitoo.

Alisema jambo hilo limekuwa ni shida kubwa kwa polisi kwa sababu wanapopelekwa mahakamani polisi anaulizwa na hakimu athibitishe ni jambo lipi linaloonyesha kuwa “huyo aliye kizimbani ni kahaba.”

Bw Daniel Mwangi, ambaye pia ni mfanyabiashara katika mji wa Thika alisema makahaba hao wengi wao huonekana wakizunguka ovyo kando ya maduka za wenyewe huku wakijaribu kuwashawishi wanaume.

“Asubuhi unapopitia kwenye vichochoro vya maduka, utapata vifaa vya kondomu vimetupwa ovyo njiani. Hata watu wengine hujisadia haja kubwa katika maeneo hayo,” alisema Bw Mwangi.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika Bw Alfred Wanyoike alisema hawatakubali makahaba hao kuendelea kuwasumbua wenye biashara wakati wanaendesha shughuli zao.

“Sisi kama wafanyabiashara hatutakubali kuyumbishwa na makahaba hao huku tukipata hasara katika biashara zetu,” alisema Bw Wanyoike.

Pendekezo

Alipendekeza waulizie jinsi ya kupata mikopo ya Uwezo Fund ili waendeshe biashara halali badala ya kuuza miili yao kwa wanaume.

Afisa wa polisi mjini Thika Bw Benard Ayoo, alisema tayari wamepata malalamishi hayo na watafanya wawezalo kukabiliana nayo.

Lakini alisema makahaba hao wafikapo mahakamani hujitetea kwa kutaka thibitisho halisi kama kweli wao ni makahaba.

“Kwa hivyo, inafanya hakimu anawatoza faini pekee kwa sababu hakuna thibitisho kamili kuhusu makosa hayo. Kaunti ya Kiambu inastahili kutunga sheria maalumu kuhusu maswala hayo ya ukahaba,” alisema Bw Oyoo.

Mombasa yawataka wakazi kukoma kuwabagua makahaba na mashoga

Na WINNIE ATIENO

SERIKALI ya kaunti ya Mombasa imeanza kuwahudumia makahaba, wapenzi wa jinsia moja na huntha (watu wenye sehemu mbili za uzazi) kwa kuwapa huduma za afya ili kupunguza maambukizi ya Ukimwi.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Afya katika kaunti hiyo, Dkt Shem Patta, amewahimiza wakazi wa Mombasa wawakubali watu hao ambao wamekuwa wakichukuliwa kuwa na tabia zisioambatana na maadili.

“Ni dada na kaka zetu, tunaishi nao katika jamii zetu. Tusiwahukumu manake hili ni swala ambalo limo miongoni mwetu. Tukiwakubali wataanza kwenda katika vituo vya afya kupokea matibabu na hivyo basi tutapunguza maambukizi ya ukimwi,” alisema Dkt Patta.

Kwenye mkutano wa afya katika afisi ya shirika la Msalaba Mwekundu, Dkt Patta alisema wapenzi wa jinsia moja na makahaba yafaa wakubaliwe na jamii zote ili Wakenya washirikiane kupunguza kuenezwa kwa maambukizi mapya ya maradhi ya ukimwi.

Alionya kuwa takwimu zinaonyesha ukimwi miongoni mwa kundi hilo bado ni hatari na endapo juhudi hazitachukuliwa basi huenda maambukizi yakaenea.

Dkt Pata alisema awali, kaunti ya Mombasa, ina idadi kubwa ya watu wanaoishi na ukimwi kwa asilimia 11, zaidi ya ile ya kitaifa ambayo ni asilimia 7.5.

“Lakini mwaka wa 2018 idadi ikaanza kupungua hadi asilimia 4.1 kufuatia mikakati tuliyoweka tukishirikiana na makundi ya kijamii ikiwemo Reachout Trust Centre, Mewa, AIDS Healthcare Foundation (AHF) na shirika la msalaba mwekundu,” alisema Dkt Patta.

Dkt Patta alisema ruwaza ya Mombasa inapania kupunguza maambukizi mapya ya ugonjwa huo hatari kwa asilimia 75.

Aidha alionya wakazi dhidi ya unyanyapaa akisisitiza kuwa unachangia pakubwa kwa msongo wa mawazo miongoni mwa watu wanaoishi na ukimwi.

“Unyanyapaa ni swala nyeti, jamii inafaa kubadilika. Kama serikali ya kaunti tunapania kuwahamasisha ili kupunguza unyanyapaa kwa asilimia 50. Pia tunataka kupunguza vifo vya ukimwi kwa kuwahamasisha wakenya kwenda kupimwa, wale wanaopatikana na ukimwi wanapewa dawa ili wapate afya na kurefusha maisha yao,” alisema.

Dkt Patta alisema takwimu za idara ya afya zinaonyesha watu elfu 41,000 wanaishi na ukimwi kaunti ya Mombasa, huku ikipata maambukizi mapya 1700 kila mwaka.

Hata hivyo alisema dawa za ARV’s, zinasaidia wale wanaoishi na ukimwi kuishi maisha bora ya afya.

Kuna zaidi ya watu 8,000 ambao ni wapenzi wa jinsia moja huku wale wanaojidunga sindano za dawa za kulevya wakizidi 18,000 nchini, kaunti ya Mombasa ikiwa na idadi kuwa.

Ugonjwa wa HIV na Hepatitis C huenezwa na watu wanaoishi na maradhi hayo wanaotumia sindano moja kujidunga dawa za kulevya.

Mkurugenzi huyo wa afya alisema kuna vituo 18 za afya ambapo wapenzi wa jinsia moja na makahaba hupokea huduma za afya, dawa za ARV’s na kondomu.

“Tunashirikiana na makundi ya kijamii kuimarisha afya na kukabiliana na ukimwi, dawa za kulevya na unyanyapaa. Mara ya kwanza hata wahudumu wa afya walikuwa na matatizo lakini wamebadili mwenendo,” alisema.

Dkt Patta alisema endapo waraibu wa dawa za kulevya hawatotumia sindano moja kujidunga basi mamabukizi ya ukimwi itapungua.

Baadhi ya wapenzi wa jinsia moja waliohojiwa na Taifa Leo walisema wanaishi maisha ya upweke baada ya kutenwga na jamii.

Vijana wanavyoponzwa na ulevi na ukahaba

Na MWANGI MUIRURI

VIJANA waliokuwa wameandaliwa kikao cha kutafuta mbinu za kufanya Mji wa Murang’a uafikie biashara ya masaa 24 wamesema kinachohitajika ni kukubaliwa kwa makahaba warembo wahudumu katika mitaa ya eneo hilo.

Kikao hicho katika ukumbi wa Manispaa ya Murang’a kiliandaliwa Jumamosi chini ya ufadhili wa serikali ya Kaunti pamoja na wawekezaji wa kibinafsi.

Ni kikao ambacho kilibakia kimeduwazwa na ujasiri wa vijana hao na pia kuzua mjadala mkali kuhusu msukumo wa kimaisha wa wengi wao.

Walishikilia kuwa biashara inayoweza ikafanikiwa ni ile ya uuzaji vileo na kisha kuwe na warembo mitaani.

Bw Eliud Kirika wa miaka 24 alipoamka kutoa mchango wake kwa niaba ya vijana alisema kuwa kwa sasa mji huo uko na makahaba wasio wa kupendeza macho hivyo basi kuwafanya wanaume wasusie mji huo.

“Pia, hatua ya serikali ya kuweka vikwazo uuzaji wa pombe kwa masaa 24 imewafanya wanaume wasiwe na la kufurahia katika mji huu. Kishawishi cha mwanamume kutumia pesa ni raha na wakati umeweka vikwazo katika raha, basi unafukuza wanaume mjini,” akasema.

Hatua ya mshirikishi wa mkutano huo, Bw James Njoroge ya kumtaka kijana huyo aketi kwa msingi kuwa mchango wake ulikuwa wa ucheshi ulikumbana na kelele za pingamizi kutoka kwa vijana waliokuwa katika ukumbi huo wa Murang’a.

“Anasema ukweli! Huo ndio mchango wetu wa kuafikiana na hakuna mahali amepotoka. Hivyo ndivyo tumekubaliana achangie nka ukimuamrisha akae chini hata sisi tutatoka nje,” akateta mmoja wa vijana huyo akijifahamisha kama Titus Njogu.

Bw Kirika aliendelea mbele na mchango wake akisema kuwa kwa sasa mji wa Murang’a uko na makahaba 16 pekee na ambao wamezoeana na wanaume kiasi kwamba kunahitajika wengine wakubaliwe kufanya biashara yao mjini bila vikwazo.

“Hawa makahaba 16 huwa wanawafukuza makahaba wapya. Hawataki ushindani kamwe. Lakini ukiwatazama, ni wale tu wamekuwa mjini humu kwa zaidi ya miaka 15 hivyo basi kuishiwa na ule uvutio kwa wanaume.

“Sura zao ni tosha kuwafanya wanaume walio na hela za kutumia waelekee katika miji mingine kusaka raha,” akasema.

Aliteta kuwa mji ambao haukubalii makahaba wawe na Uhuru wao na wawe tu ni wale warembo, kisha mji huo ukose kukubalia uuzaji wa pombe bila vikwazo na mtaani kukubaliwe uuzaji wa miraa, basin i sawa na kuua uchumi wa eneo hilo.

“Mimi naongea ukweli ulio uchi kabisa. Biashara ya usiku wa manane huwezi ukatarajia watu wakuje kununua unga au mavazi. Masaa ya usiku ni ya wasakao raha. Kuanzia saa moja asubuhi hadi saa tatu usiku, unaweza ukapigia debe biashara zile za kawaida. Lakini kuanzia saa nne usiku hadi asubuhi ya saa 12, biashara ni ulevi na mahaba,” akasema Kirika akishangiliwa na wenzake.

Alisema kuwa biashara za usiku hazitakuwa zikizingatia sana wanawake kwa kuwa kwa kawaida wao sio wa kuhatarisha maisha yao kwa giza ya usiku mjini.

Alipendekeza kuwa maafisa wa polisi wazimwe kuhangaisha wanaosaka raha usiku mjini humo, akitaka wawe tu wakisaka wezi pekee.

“Mji wetu unaishiwa na pesa usiku kwa kuwa wale wote wanaosaka raha zao masaa hayo huwa wanakumbana na hatari ya kukamatwa na maafisa wa polisi. Unashindwa kuelewa ni kwa nini mtu ambaye ameamua kutumia pesa zake usiku anahangaishwa huku wezi wakiwa tele kwa giza,” akasema.

Mwakilishi wa afisi ya gavana katika mkutano huo, James Gathuita alitaja kauli hizo kuwa za kipekee na ambazo zinaangazia hali halisi ya fikira za vijana wa taifa hili.

“Sitaki kuwalaumu au kuwaunga mkono kwa kuwa dunia iko hivyo. Lakini ni ishara tosha kuwa tuko na shida kubwa ya kimtazamo miongoni mwa vijana wetu,” akasema.

URODA KWA FOLENI: Je, ni rahisi kuacha ukahaba?

NA MWANDISHI WETU

SIO mara ya kwanza kwa mji wa Nakuru kugonga vichwa vya habari kutokana na biashara ya ukahaba inayoendeshwa na wasichana na wanawake.

Maeneo ambako utapata biashara hii ikifanywa waziwazi ni Gitwamba, Three Ways, Kanu Street, Baringo Lodge, Kiambuthia Lodge na Ndumu.

Katika barabara ya Kanu Street kwa mfano, utakuta foleni ya wanawake waliosimama na kuwaita baadhi wa wanaume wanaopita, wengine wakiwashika mkono na kuwavuta ili kuwauzia ‘huduma.’

Makahaba katika mitaa mingine mjini Nakuru hujiuza kimyakimya ndani ya giza, na wale wenye ujasiri hujianika hadharani mchana.

Makahaba katika eneo la Three Ways katikati ya mji wa Nakuru wakisaka ‘wateja’ gizani. Picha/ Richard Maosi

Wakiwa wamejipodoa, utawakuta wamepiga foleni ndefu mchana tena peupe ili kunasa windo kwa urahisi, huku wakivuta sigara.

Miaka ya nyuma, vidosho hawa wamekuwa wakikaangwa mtandaoni kwa kuchangia ndoa nyingi na mahusiano kusambaratika.

Biashara hii ya kuchuuza uroda imefanya jamii kuwatazama kwa jicho la dharau na kuwaona kama watu wazembe wasiopenda kupambana na maisha kupata riziki halali.

Je, hii ni kazi halisi?

Taifa Leo Dijitali ilipiga kambi katika ngome zao kung’amua ukweli wa mambo. Tulikutana na msemaji wao aliyekubali kuzungumza nasi, kwa masharti ya kubana jina lake.

Kulingana naye, ukahaba ni kazi kama nyinginezo muradi kuna kitu cha kutia mfukoni mwisho wa siku baada ya kuchuma gizani.

Alieleza kuwa bali na biashara yenyewe kunoga misimu fulani, kuna wakati kiwango cha mapato huenda chini na hata kudorora kabisa.

Mmoja wa makahaba akiwa amesimama karibu na Kiambuthia Lodge, Nakuru mchana. Picha/ Richard Maosi

Kwa upande mmoja, anachekesha anapowalaumu wanaume wanaojifanya mkono ngamu wakati wa wanaposaka huduma hizi, huku wengi wao wakiwa ni vijana. Pia anawalaani wanaume ambao hujifanya ‘wateja’ kisha kuwaibia hela zote walizopata usiku mzima.

Aliwasimanga baadhi yao waliozowea kutoroka pindi tu baada ya kurina asali bila kulipa pesa, na kutisha kuwaitia polisi.

Polisi wamekuwa wakiingilia kati na kutatiza ‘biashara’ yao kwa kuwakamata wateja wanaofika kuburudika katika barabara ya Gusii Road wakisingizia kushika doria.

“Wanaume wanaopatikana wamesimama karibu na gesti au baa, hasa wakati wa jioni wamekuwa wakinaswa na polisi bila hatia,” alisema.

Makahaba wamedhibiti vichochoro vya Threeways wakati wa mchana, na ifikapo husiku hujitokeza barabarani.

Sheria kali za manispaa ya kaunti kuwafurusha zimeonekana kugonga ukuta licha ya uhamasisho kuhusu kutafuta biashara mbadala. Polisi huwakamata baadhi yao na kuwaachilia huru siku chache baadaye.

Hivyo, hii si kazi ya kutegemea kwani huduma ni kati ya Sh100 na Sh300. “Kwa siku kila demu hapa hupata wateja wawili kwa wastani,” anafichua mmoja wao.

Wengi wa makahaba ni wa umri wa makamo, kama mwanamke huyu aliyejibanza katika barabara ya Kenyatta, Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Mbinu mpya

Kila wakati, makahaba wamekuwa wakibuni mbinu tofauti kuepuka mkono mrefu wa sheria na kuendeleza biashara yao haramu ndani ya vyumba vya kibinafsi wanavyokodisha mjini.

Wengi wao wameanika uchi wao na nambari zao za simu kwenye mitandao ya ngono kwenye intaneti, ili kuwanasa ‘wateja’ wasiopenda kwenda kuwatafuta vichochoroni kutokana na fedheha ya kuonekana wakiandamana na vimada.

Polisi wamekuwa wakishirikiana na wachuuzi kuwatimua, hasa pale wanapoanika sehemu za miili karibu na biashara zao, lakini bado wao hurejea barabarani ‘kusaka riziki.’

James Munywa ni mmoja wa wachuuzi hao na anafanya kazi ya kuuza viatu na nguo karibu na eneo la Three Ways. Anasema kwa miaka mitatu amekuwa akizozana na makahaba ambao huzuia wateja kununua bidhaa zake lakini siku hizi amewazoea.

Dada huyu katika barabara ya Gusii, Nakuru anajaribu kumuuzia mwanamume huduma. Picha/ Richard Maosi

Anaeleza jinsi siku za mbeleni wateja walikuwa wakitiliwa mchele ndani ya vinywaji na mashangingi hawa, na kuibiwa kila kitu.

“Hususan wakitambua wewe sio mwenyeji wa hapa watatumia kila mbinu kuhakikisha huondoki bila kuacha kitu kidogo,” James alisema.

Aidha tuligundua kuwa biashara hii huendeshwa na wanawake wenye umri wa makamo pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu.

Ushindani mkali kati ya makundi haya mawili umekuwa ukizua uhasama na kuleta zogo, na utawakuta wakirushiana cheche za matusi baada ya kunyang’anyana ‘mteja.’

Mbona wanajitosa kwa ukahaba?

Changudoa mwingine aliyekubali kuzungumza nasi ni Ann (sio jina lake kamili). Alitusimulia kwa kina jinsi alijikuta katika biashara ya ngono miaka mitatu iliyopita bila kupenda.

Akiwa mzaliwa wa Nyandarua, alikuja Nakuru kutafuta kibarua alipoahidiwa na mjomba wake kuwa angepata kazi.

“Wazazi wangu wanajua ninafanya kazi ya kuuza nguo mjini Nakuru. Kila mwezi huwa ninawatumia pesa za matumizi kwa sababu walinisukuma mjini kutafuta kibarua,” alifungukia Taifa Leo Dijitali.

Hapa swali ni: Mkunwa na mkunaji, muona raha ni nani? Picha/ Richard Maosi

Japo siku za mwanzoni ilikuwa vigumu kujikubali kwamba alikuwa anauza mwili wake, kufikia sasa ameridhia hali na anajaribu kupigana na unyanyapaa.

Alijifundisha kuvalia nguo fupi za kubana, kabla ya kubobea rasmi akaanza kutembea nusu uchi!

“Wateja wangu wengi ni wanaume walio kwenye ndoa,wanatumia fursa hii kujituliza moyo labda kutokana na usumbufu wa wake zao nyumbani,” aliongezea.

Aidha ananyooshea polisi kidole cha lawama, akisema ndio kikwazo kikubwa katika ‘kazi’ yake.

Anasema yeye hulazimika kugawana anachopata na maafisa hawa ili biashara iendelee, la sivyo waingie kizuizini siku kadha.

“Biashara hunoga msimu ambapo wakulima huwa wamevuna mahindi na ngano, au mwisho wa mwaka katika shamrashamra za kukaribisha Mwaka Mpya lakini sasa hali ni ngumu,” alisema.

Akiwa na watoto wawili katika shule ya upili na mmoja kwenye shule ya msingi, anategemea ukahaba kuliwalipia karo na kununua chakula.

Waendeshaji malori ya masafa marefu eneo la Pipeline, Nakuru wanaaminika kuwa wateja kwa huduma za makahaba. Picha/ Richard Maosi

Je, ni rahisi kuacha ‘kazi’ hii?

Jane (sio jina lake halisi) anatueleza jinsi alijaribu kuacha ukahaba lakini akashindwa. “Nilikuwa nimeamua kuacha kazi hii baada ya kupata kazi ya kuuza vyakula mjini. Lakini ule uchu wa kufanya ngono ulinirudisha tena kwa ukahaba. Kila mwanamume niliyemuuzia chakula nilitamani kulala naye. Wengi waliniitisha nambari ya simu, na baadaye nililala nao na kunilipa. Bosi wangu alipogundua alinitimua nami nikarudi vichochoroni,” anafichua.

Hata hivyo, Cate (sio jina lake) anatueleza jinsi yeye wakati ulitimia akaamu kujiondoa vichochoroni. “Ilikuwa baada ya kuhudhuria maombi ya kanisa ambapo niliungama dhambi zangu na kutubu. Niliahidi nafsi yangu kutofanya ukahaba tena,” anasema huku akiongeza kuwa baada ya maombi hayo alipata kazi ya kudumu inayolipa kuliko ukahaba.

“Kwa sasa nimeolewa kwa harusi na ndoa yangu ni ya raha. Siwezi kuchepuka hata kidogo nikikumbuka aliponitoa Mola,” anasema.

Kiongozi wa kidini akiwahutubu wakati katika hafla iliyowakutanisha na serikali ya kaunti kujadili namna ya kuzima ukahaba mjini Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Wakati mwingine makahaba hulazimika kusafiri hadi kaunti jirani za Uasin Gishu, Nairobi na Mombasa wateja wanapopungua.

Ni wazi hawara wengi hapa ni wake za watu, labda waliotengana, wajane au wanaoishi mbali na wapenzi wao kulingana na mahojiano yetu.

Kinyume na inavyotarajiwa, wateja wao wengi sio walevi wala watu hivihivi. Ufichuzi wetu uligundua pia wachungaji na mapasta wa kanisa ni wanunuzi wa huduma za ngono.

Serikali ya kaunti ya Nakuru imeweka mikakati kupunguza idadi ya vilabu na baa katika maeneo ya Kenlands na Section 58 ambapo vilabu ni vingi kuliko makanisa.

Naibu Kaunti Kamishna wa Nakuru Mashariki, Bw Herman Shambi alithibitisha haya mapema mwaka huu katika hafla iliyowakutanisha na viongozi wa kidini kujadili hali hii.

Na si ukahaba pekee, ufichuzi wetu ulibaini kuwa wanadada hawa pia hutumika kufanikisha biashara haramu ya bangi na mihadarati kwa kushirikiana na wanabodaboda.

Makahaba waililia serikali iwasaidie kuwekeza wakomeshe biashara ya uzinzi

ERICK MATARA NA RICHARD MAOSI

MAKAHABA 14 mjini Nakuru wameiomba serikali ya kaunti na wahisani kujitokeza ili wawasaidie kuachana na biashara ya kuuza miili yao.

Wakizungumza na Taifa Leo Dijitali, walihakikishia umma kwamba walikuwa tayari kuachana na ukahaba na kutafuta njia mbadala ya kujipatia mapato iwapo watapewa msaada kuwekeza kwa biashara.

Kwa mujibu wa msemaji wao Martha (sio jina lake halisi),  wameanzisha mfumo wa mageuzi wakitarajia kubadilisha mienendo siku za hivi karibuni.

“Tunakusudia kunyoosha mienendo na kuachana na ukahaba, isipokuwa changamoto inayotukabili ni ukosefu wa mtaji wa kuanzisha biashara,” alisema.

Baadhi yao waliungama kuwa alijiingiza kwenye biashara ya ngono kwa sababu ya ukosefu wa ajira, kukidhi maslahi ya watoto wake tano.

Walipokosa namna ya kukidhi mahitaji ya familia, hawakuwa na budi kujitosa ndani ya ukahaba.

“Sio nia yetu kuhangaika barabarani kila siku, kusema kweli tumekubali kwa sauti moja kuachana na ukahaba mradi tu wasamaria wema wajitokeze kutusaidia,” walisema.

Makahaba katika eneo la Three Ways katikati ya mji wa Nakuru wakisaka wateja kwa bidii gizani. Picha/ Richard Maosi

Mwaka 2018, mwenyekiti wa Muungano wa Wafanyibiashara Nakuru, Muchemi Mwangi alilalamika aliposema changudoa walikuwa wakitatiza shughuli za kibiashara na kuwatorosha wawekezaji .

Aidha wateja walianza kununua bidhaa kwingine, pale makahaba walipoanza kujazana mbele ya maduka ya kuuzia.

Ikizingatiwa kuwa kaunti ya Nakuru inatarajiwa kufikia hadhi ya kuwa jiji karibuni, makahaba wameanza kumiminika mjini na kutatiza shughuli za kibiashara.

Wakati mwingine wasichana wenye umri mdogo hupiga foleni ndefu mbele ya maduka na kwahangaisha wauzaji wanaowahudumia wateja.

Maeneo yaliyoathirika zaidi ni pamoja na barabara ya Gusii, Pandit Nehru na Kenyatta ambapo idadi ya makahaba ni baina ya 80-100 kila usiku kwa wastani. Wakati mwingine, wao huendelea kumiminika hadi wakafikia 300 au zaidi.

Pia makahaba wamedhibiti barabara ya Kanu Street viungani mwa mji wa Nakuru, bila kusahau eneo la Pipeline, Kikopey na Salgaa kwenye barabara ya Nakuru-Eldoret.

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Chumo haramu ni miongoni mwa dhambi za kutupeleka jehanamu

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mungu Azzawajalla, swala na salamu zimwendee Mtume Mtukufu Swallallahu A’alayhi Wasallam.

Amesema Allah Subhanahu wataala “Hakika mali zenu na watoto wenu ni fitna” (Taghaabun 15).

Mali ni fitna kwani ni kama upanga wenye ncha mbili, ambao ima itamnufaisha mtu au kumuangamiza; ima aichume katika njia za halali imnufaishe duniani na akhera, au aichume kwa njia haramu imnufaishe duniani na kumuangamiza akhera, Mtume rehema na amani ziwe juu yake ametuambia kuwa kila mtu ataulizwa mambo manne siku ya kiama na akataja kuwa moja ni mali; vipi kaichuma na vipi kaitumia, hivyo mali itakuwa na maswali mawili tofauti na mambo mengine yenye swali moja kwa kila jambo.

Uislamu haukatazi mtu kuwa na mali nyingi almuradi kachuma katika njia za halali na anazitumia zinavyostahiki, kwani historia imewataja baadhi ya waja wema waliokuwa matajiri na namna gani walivyozitumia mali zao katika kumridhisha Mola wao; tukianzia maswahaba akina Sayyidina Uthmaan, Abdul-Rahmaan bin Auf na maswahaba wengineo na wema waliokuja baada ya hapo radhiallahu anhum ajmain.

Amesema Mtume rehma na amani ziwe juu yake: “Ni mali bora iliyoje iliyokuwa nzuri inayomilikiwa na mtu mzuri” inaonesha kuwa mtu mwema anapomiliki mali basi hata mali yake huwa nzuri kwani hutolewa na kutumiwa katika njia anazozipenda Allah subhaanah.

Lakini pia Uislamu umekataza kuchuma mali kwa njia za haramu. Umekataza kuchuma mali kwa mambo aliyoyaharamisha Allah subhaanahu wataala: Tunaona tamaa za watu za kutaka kutajirika kwa haraka, wanatumia njia ambazo Allah ameharamisha, toka asili ya kile kitu seuze biashara yake. Na tutazame mifano michache:

Mifano

Allah subhanahu wataala amekataza ULEVI, hivyo hata biashara yake haifai. Tunaona katika hadithi ya Mtume Rehma na amani ziwe juu yake watu kumi wanaohusu ulevi wamelaaniwa. Toka muuzaji mpaka mkokoteni uliobeba pombe pia umelaaniwa. Ni vijana wangapi tunaoishi nao washalaaniwa? Vijana wangapi walojazana katika mahoteli kunakouzwa pombe na wao kushiriki katika biashara hiyo?
Vile vile, Allah subhanahu wataala amekataza RIBA, lakini tunaona inavyochotwa katika benki na kwingineko mpaka kupambiwa majina ili ionekane kuwa ni halali. Tumeona kuwa kilichoharamishwa na sheria ni haramu na riba ni haramu. Katika kitabu na Sunnah, amesema Allah “Na Allah amehalalisha biashara na kuharamisha riba” Baqarah 275, na kuna hadithi nyingi zinazoonesha ukubwa wa dhambi ya riba ikiwemo riba kuwa miongoni mwa madhambi saba yenye kuangamiza na ile hadithi ya Mtume kuwa riba ina milango 70; wa chini yao ni mfano wa mtu kuzini na mamake.

Aidha, tumekatazwa kula RUSHWA. Tunaona suala la rushwa liko kila kona, si wanasiasa tu wanaokemea rushwa, Uislamu umetangulia kuikemea rushwa na kuonesha kuwa Mtoaji, mpokeaji na anaeshuhudia wote wamelaaniwa. Imekuwa haki yako huipati mpaka utoe rushwa yaani laana za Allah zimejaa kila kona kiasi cha kutukosesha barka katika miji yetu.

Pia Allah subhanahu wataala amekataza kula MALI YA YATIMA. Hata hivyo ni wangapi wanafikia hata kiasi cha kupora haswaa mali za mayatima, wakisahau maneno ya Allah aliposema: “Hakika ya wale wanaokula mali ya mayatima kwa dhulma hakika wanakula moto katika matumbo yao…” (Nisai 10). Tayari washatia moto katika matumbo yao toka duniani kabla ya kufika Akhera. (Allah atuhifadhi).

Allah subhanahu wataala pia amekataza MUZIKI, hivyo biashara yake pia ni haramu kama alivyosema Mtume rehema na amani ziwe juu yake; kuwa biashara yake haina faida, wala thamani, lakini ni vijana wangapi wanashiriki kutoa, kuuza na kusambaza CD na mengineyo yanayohusu muziki?

Allah subhanahu wataala vilevile amekataza UZINIFU; hivyo kila kinachohusu na kuchangia uzinifu ni haramu, kwani tumekatazwa hata kuikaribia zinaa. Lakini ni watu wangapi wanafanya kazi kwenye sehemu zenye kuchochea zinaa au kushiriki katika uuzaji wa vitu vyenye kuchochea uzinifu? Haya yote ni haramu na mwenye kusaidia kufanya jambo baya basi na yeye atapata malipo sawa na mfanyaji pasi na kupunguziwa chochote.

Allah subhanahu wataala aidha amekataza SHIRKI. Ni vijana wangapi wanatafuta utajiri kwa njia za kishirikina na kufikia sasa wanawaua wenzao kwa sababu ya mali? Ni haramu juu ya haramu. Tutaenda kumjibu nini Allah subhanahu wataala atakapotuuliza kuhusu mali; namna tulivyoichuma na kuitumia? Mifano ya njia za haramu iko mingi ambayo imeenea katika jamii.
Tunaona migogoro ya ardhi na watu kupora ardhi si zao, na baadaye kudai ni zao ili waziuze wanufaike! Ni makosa mtu kuzidisha shubiri moja tu ya ardhi isiyo yake seuze kupora ardhi.

Ndugu zangu wa Kiislamu, Mtume ametuonya pale aliposema katika hadithi ya Abdullah bin Mas-uud na kupokewa na Bukhari na Imam Ahmad rahimahumallah “Hatochuma mja mali ya haramu kisha akaitoa (kwa kuitumia) Allah akambarikia, wala hatoitolea sadaka Allah akamkubalia, wala hatoiwacha nyuma yake (baada ya kufa) isipokuwa itakuwa ni akiba yake ya kumpeleka motoni. Subhnallah!

Mali ya haramu haina manufaa yoyote si katika kuitumia kulisha familia au kujilisha mtu mwenyewe, wala si katika kuitolea sadaka, na ukiiacha pia ni mashaka. Allah atuhifadhi.

Makahaba watua Kiambu kunyonya Sh1.6 bilioni za fidia kwa wakazi

Na MWANGI MUIRURI

MAKAHABA wamevamia eneo la Gatundu Kaskazini, Kaunti ya Kiambu kwa nia ya kuvuna sehemu ya Sh1.6 bilioni zinazotarajiwa kulipwa wakazi kuanzia Jumatano.

Fidia hiyo ni kwa wakazi watakohamishwa kwenye mashamba yao kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Kariminu.

Kulingana na mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mikahawa katika Kaunti ya Kiambu, Philemon Mwaniki, vyumba vya malazi katika eneo hilo vimeshuhudia ongezeko la wateja wapatao 1,200 tangu wikendi.

“Biashara ya lojing’i imeimarika katika vituo vya biashara vya Gituamba, Githobokoni, Chania na Mang’u. Wengi wa wateja ni wanawake tunaoshuku ni makahaba,” akasema.

Kwa mujibu wa Mbunge wa Gatundu Kaskazini, Bi Wanjiku Kibe, makahaba hao walianza kuingia eneo hilo baada ya kupata habari kuwa kuanzia kesho wakazi wataanza kulipwa fidia ili waondoke katika mashamba yao.

“Wengi watalipwa kati ya Sh5 milioni na Sh40 milioni. Familia hizo zisipopanga vizuri jinsi ya kutumia pesa hizo, fidia hiyo inaweza kugeuka kuwa janga. Ombi langu ni kwa wakazi hasa wazee kutumia pesa hizo kwa makini kwa manufaa ya familia zao,” akaeleza Bi Kibe.

Alipotangaza kuhusu kuanza kulipwa kwa fidia hiyo, Waziri wa Maji, Bw Simon Chelugui aligusia suala hilo:

“Masikitiko yangu ni kuwa nimeona miradi kama hii ikigeuka kuwa balaa kwa familia nyingi. Nimeona familia zikilipwa fidia naye shetani anaingia ndani ya bongo za baadhi ya wazee ambao wanatoweka nyumbani na kufuja pesa hizo zote mitaani.

“Ninajua kuwa kunao wataanza kutafuta mabibi zaidi wa kuoa na wengine wa kula raha nao. Ombi langu ni kuwa pesa hizi ziwasaidie kujijenga lakini zisibomoe familia zenu.

“Ningeomba viongozi wa hapa Gatundu wawasaidie wakulima hawa kwa kuwatafutia wataalamu wa kuwapa mawaidha ya kutumia pesa hizo. Wengine watakimbia kununua magari ya kifahari huku wengine wakiingia mitaani kula raha,” akasema Bw Chelugui.

Alisema kuwa familia nyingi zilikataa kutafutiwa makao mbadala na kujengewa nyumba na badala yake zikaamua kupokea pesa taslimu.

Kamanda wa polisi wa Kiambu, Adiel Nyange alisema kuwa maafisa wake wako tayari kuwaandama wote watakaonaswa mitaani wakishiriki ukahaba ama kuwaibia wakazi kwa kuwawekea dawa za usingizi kwenye vinywaji.

“Hata ikiwa kazi ya polisi sio ya kuchunga watu wazima, tutajimudu kuokoa hali kadiri ya uwezo wetu. Wahudumu wa baa pia sharti wawe makini kuhakikisha usalama wa wateja wao,” akasema Bw Nyange.

Makahaba wapiga kambi Murang’a kumumunya mabilioni ya majani chai

Na KNA

WAKAZI katika Kaunti ya Murang’a wameeleza hofu yao kuhusu ongezeko la makahaba eneo hilo wanaopanga kunyemelea wakulima ambao wanatarajiwa kulipwa bonasi ya majani chai.

Baadhi ya wafanyabiashara wanasema kuwa vyumba vya kulala na lojing’i mjini Murang’a vimejaa huku makahaba kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kama vile Mombasa, Bomet, Nairobi na Eldoret wakilenga kuwapora wakulima wa chai baada ya kulipwa.

Diwani wa wadi ya Kangari, Bw Charles Kahoro amewaonya wakulima wa eneo hilo dhidi ya kuanguka kwenye mtego wa makahaba hao wanaojifanya kuwa madaktari au wahubiri wanapokodisha vyumba.

Bw Kahoro alidai kuwa wasichana hao awali waliripotiwa kuwapora wakulima wa chai na kuwaacha bila chochote cha kugharamia mahitaji ya familia zao.

Alisema makahaba hulenga wakulima wanaume ambapo huwawekea dawa za kuwalemaza ndani ya vileo vyao kabla ya kuwaibia.

Baadhi ya miji ambako makahaba hao wameripotiwa kuonekana kwa wingi ni Kangari, Kahuro, Kigumo na Kangema ambako wakulima wanatarajia kulipwa bonasi mwezi huu.

Katika soko la Kangari viwanda vinne vya majani chai vya Nduti, Makomboki, Ikumbi na Gacharage vinatarajia malipo ya mabilioni ya fedha.

Alisema kuwa wakulima wa majani chai wanafaa kukumbuka kuwa wamefanya kazi ngumu kwa muda wa mwaka mmoja, hivyo pesa watakazopata wanafaa kuzitumia kuimarisha hali ya maisha ya familia zao.

Mwakilishi huyo aliomba maafisa wa polisi kuwa makini kwa lengo la kutambulisha makahaba ambao kazi yao ni kupora wakulima na kuvunja familia zao.

Afisa Mkuu Msimamizi wa Kilimo katika Kaunti ya Murang’a, Bw Peter Njangi aliwashauri wakulima kutumia pesa zao kwa njia inayofaa.

“Baadhi ya wanaume huacha familia zao na kurudi pesa zinapoisha. Hilo ni jambo la kuhuzunisha sana,” alisema Bw Njangi.

Hali sawa na hiyo inatarajiwa katika kaunti zingine kunakokuzwa majani chai kwa wingi kama vile Nyeri, Kirinyaga, Meru, Kericho, Kisii, Nandi na Bomet.

Wachina 15 wafurushwa kwa kushiriki ukahaba South C

Na VALENTINE OBARA

RAIA 15 wa Uchina wakiwemo wanawake 13 na wanaume wawili, Jumatano walikamatwa kwa madai ya kushiriki ukahaba jijini Nairobi huku serikali ikizidisha msako dhidi ya raia wa kigeni wanaoishi nchini kiharamu.

Idara ya Uhamiaji ilisema maafisa wake wakishirikiana na wale wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) waliwakamata Wachina hao katika mtaa wa South C asubuhi kwenye nyumba mbili zinazoaminika kuwa madanguro, wakafurushwa nchini.

Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji, Bw Alexander Muteshi, alisema mmoja wao alikuwa amefurushwa nchini Mei 2017 kwa kuhusishwa na ukahaba na michezo haramu ya bahati nasibu lakini akarejea kwa kutumia paspoti tofauti.

“Tunashukuru mchango wa wawekezaji wa kigeni katika uchumi wa nchi hii lakini tunasisitiza kuwa wanaweza kufaidika tu kwa kufanya biashara halali nchini humu,” akasema.

Wakati huo huo, alisema idara yake ilizuilia Waganda 10 ambao walikuwa wanapelekwa Mashariki ya Kati na Mkenya ambaye anashukiwa kuwa mlanguzi wa binadamu katika mtaa wa Uhuru, Nairobi.Hivi majuzi, polisi walivamia makao makuu ya shirika la habari la China Global Television Network na kukamata wanahabari kadhaa wakiwemo Wachina 13 ambao walidhaniwa kuwa nchini bila idhini.

Baadhi ya Wachina waliokamatwa kwa danguro mtaani South C, Nairobi Septemba 19, 2018. Picha/ Hisani

Hata hivyo, waliachiliwa huru baada ya serikali kutambua kuwa habari zilizotolewa kuwahusu hazikuwa za kweli na Wachina hao walikuwa na vibali vinavyowaruhusu kufanya kazi Kenya kisheria.

Wakati huo, Ubalozi wa Uchina nchini ulisema taifa hilo linaheshimu sheria za Kenya lakini ikataka raia wake walio nchini kihalali wasidhulumiwe.

Raia mwingine wa Uchina, Bw Liu Jiaqi, alifurushwa nchini mapema mwezi huu baada ya video kufichuka ikimwonyesha akitoa matamshi ya kibaguzi dhidi ya Wakenya akiwemo Rais Uhuru Kenyatta.

“Ubalozi wa Uchina nchini Kenya huhitaji kampuni zote za Uchina na watu binafsi wafuate sheria za nchi, waishi na kufanya kazi Kenya kwa msingi wa sheria,” taarifa ya ubalozi huo ikasema.

Ingawa serikali ilizidisha juhudi zake za kusaka na kufurusha raia wa kigeni walio nchini kiharamu mwaka huu, raia wengi wa Uchina wamewahi kukamatwa na kufurushwa kwa msingi huu kwa miaka kadhaa sasa, hasa baada ya ushirikiano kati ya Kenya na Uchina kushika kasi katika kipindi cha miaka michache iliyopita na kufanya raia wengi wa nchi hiyo kuja nchini sana sana kufanya kazi kwa ujenzi wa miradi mikubwa kama vile barabara na reli ya kisasa.

Ripoti zinaonyesha kuna raia wa kigeni ambao huja nchini kama watalii kisha kutafuta njia za kilaghai ili waanze kufanya kazi zisizoruhusiwa na sheria za Kenya.

Serikali ilikuwa imetoa nafasi kwa raia wa kigeni kuhakikisha wana stakabadhi zifaazo kuwa nchini na kipindi hicho kilikamilika karibu miezi miwili iliyopita.

Makahaba walia kwa kutozwa ada na vijana wa magenge hatari

Na WINNIE ATIENO

MAKAHABA katika Kaunti ya Mombasa wanalazimika kulipa ada kwa magenge hatari ili kujihakikisha usalama wao.

Magenge hayo huwadhulumu makahaba kwa kuwapokonya pesa wanazolipwa na wateja wao wakidai wanahudumu katika himaya yao.

“Wanatuambia tulipe kodi kwa kusimama kwenye mahala tunapotafuta wateja. Ukiingia kwa hoteli na mteja wako wanasubiri umalize shughuli zako halafu baada ya mteja kuondoka, wanakufuata na kuitisha nusu ya pesa ulizo nazo,” alisema mmoja wa makahaba hao.

Katika eneo la Kisauni, zaidi ya makahaba 180 wamelalamika kwamba wanapata hasara kwa kupokonywa fedha na magenge hayo maarufu kama “sungu sungu” na wanachapwa wakikataa kuwapa pesa.

“Siku hizi tumekuwa wajanja na inatubidi tuwabembeleze wateja wetu watutumie pesa kwa Mpesa, alafu tunaweka Sh100 kwa mfuko. Wanapotafuta fedha mifukoni mwetu wanapata Sh100 ambayo tunagawana nusu kwa nusu,” akasema kahaba mmoja.

Mmoja wao alisema alipigwa vibaya alipokataa kuwapa nusu ya pesa alizolipwa na mteja na akapata majeraha kichwani na mgongoni.

“Nilikuwa nimeenda kununua uji na mayai eneo la Ziwa la Ng’ombe, ghafla vijana hao wakajitokeza wakiwa na silaha butu wakisema nilikataa kuwalipa kwa kutumia uwanja wao kufanyia ukahaba. Hapa ni pahala tunaposimama tukisubiri wateja na wanadai ni pao,” alisema mmoja aliyejitambulisha kama Kananu.

“Walikuwa wananiuliza kwa nini nilikataa kulipa ilhali wenzangu wanalipa. Wakasema mimi ni mjeuri na tukiwa na wenzangu tulitandikwa. Nilitoroka na ambapo niliokolewa na kupelekwa hospitalini,” alisema.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 27 alisema alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Bamburi na hata kuwaambia polisi hao kuwa anaweza kuwatambua wahalifu hao lakini hajapata usaidizi.

Mama huyo wa mtoto mmoja alisema rafiki zake waliamua kuwa wakilipa Sh200 kwa siku kuepuka ghadhabu za vijana hao.

Afisa wa shirika la kutetea haki za binadamu Francis Auma alisema kesi za dhuluma za kimapenzi zimeongezeka Mombasa.

Naibu kamishna wa Kisauni Kipchumba Rutto alisema ataanzisha uchunguzi kuhusu madai hayo.

Makahaba kutoka UG na TZ wamiminika Narok kuvuna hela za ngano

Na GEORGE SAYAGIE

MAMIA ya makahaba wakiwemo wa kutoka nchi jirani wameingia Kaunti ya Narok kuvuna mapato kutoka kwa wakulima wa ngano ambao wameanza kulipwa.

Makahaba hao pia wanaotea watalii walioanza kwenda katika mbuga ya wanyamapori ya Maasai Mara kushuhudia uhamiaji wa kongoni.

Baadhi yao wametoka nchi jirani za Uganda na Tanzania huku wengine wakitoka maeneo ya Nakuru, Eldoret, Kericho, Nairobi, eneo la Kati na Mombasa.

Kwa kawaida wao hujaa Narok msimu huu ambapo wakulima wa ngano wanauza mazao yao kwa wingi.

Wafanyabiashara waliohojiwa na Taifa Leo walisema hali hii husaidia pia biashara zingine kufaidika ingawa walitaka wakulima wajihadhari.

“Kila mwaka msimu huu huwa ni wa faida kwa sababu ya utalii katika Maasai Mara na uvunaji wa ngano katika kaunti, lakini watu wengi wanaokuja huwa wana nia mbaya,” akasema Bw Joseph Kamau, mfanyabiashara wa ngano.

“Kuna makahaba ambao huja katika msimu wa kuvuna pekee. Wao huenda Kericho wakati wakulima wa chai wanapolipwa bonasi Novemba kisha hujazana hapa Julai na Agosti. Ikifika Septemba wataenda kwingine,” akaeleza.

Mkuu wa polisi wa Narok, Bw Joseph Kisombe, alisema polisi wameimarisha upigaji doria katika maeneo mbalimbali msimu huu ikiwemo Narok mjini, Suswa, Ntulele, Melili na Ololulung’a ili kuzuia ongezeko la uhalifu msimu huu.

Bw Kisombe alisema wamewahi kupokea malalamishi kadhaa kutoka kwa wakulima wa ngano na wateja wengine ambao waliibiwa pesa na mali nyingine baada ya kutiliwa dawa za kulevya na makahaba hao.

“Polisi watakuwa macho kuzuia uhalifu wowote ikiwemo jinsi wakulima wa ngano wanvyotiliwa dawa za kulevya,” akasema.

Visa vya watu kutiliwa dawa za kulevya katika msimu huu huongezeka katika eneo hilo ingawa vingi huwa haviripotiwi, pengine kutokana na jinsi wanaume husika wanavyotaka wasijulikane walihadaiwa na makahaba.

KURUNZI YA PWANI: Wautaja utalii ‘laana’ watoto wao wakigeuzwa makahaba

Na WINNIE ATIENO

JAPO utalii unachangia pakubwa pato la uchumi wa taifa, umegueuka kuwa ‘laana’ kwa jamii zinazoishi Pwani baada ya baadhi ya watalii kugeuza wasichana wa shule kuwa makahaba na kuwadhulumu wengine kimapenzi.

Visa vya watalii kudhulumu watoto wa kati ya umri wa miaka 12 hadi 17 vimeongezeka katika kaunti za Mombasa, Kilifi na Kwale.

Katika hoteli za kifahari maandishi “Haturuhusu ngono za watoto” zimechapishwa kama njia moja ya kufanya kampeni ya kuangamiza dhuluma hii.

Lakini watalii hao wamevumbua njia mbadala, huwachukua watoto hao na kuwadhulumu kingono kwenye villa au vyumba maalum vya kukodi (apartment).

Mwezi wa Mei mwaka huu, mtalii raia wa Uingereza Keith Morris alipatikana na hatia ya kuwadhulumu kingono watoto wa humu nchini.

Kesi ya mzee huyo mwenye umri wa miaka 72, ilisikizwa katika mahakama ya Uingereza baada ya upelelezi baina ya ofisi ya uchunguzi wa Uingereza ikishirikiana na ile ya humu nchini kupata ushahidi dhidi ya shutuma zilizokuwa zinamkabili.

Alipatikana na makosa tisa ya dhuluma za watoto huko Kilifi kwenye kesi.

Katika kijiji cha Maweni eneo la Kikambala kaunti ya Kilifi, mzungu huyo aliwalawiti watoto wengi.

“Alimlawiti mwanangu, tunashukuru haki imepatikana. Tulimjua kama mtu mzuri ambaye alikuwa anazuru eneo hili akifurahisha watoto wetu kumbe alikuwa na ila mbaya! Hatukumshuku,” akasema mzazi wa mtoto ambaye alilawitiwa na mzungu huyo.

Lakini mwaka jana, watu kutoka Nairobi walikuja kumhoji mwanangu.

Mtoto huyo alifichua kuwa mzungu huyo alikuwa anawapeleka matembezi eneo la Mombasa, baadaye kuwapeleka kuona sinema huko Nyali kisha anawapeleka katika chumba chake na kuwanajisi huko Bamburi.

Mtoto huyo alisema kila alipomkataza mzungu huyo dhidi ya uchafu huo alimsihi anyamaze wala asimwambie mtu yoyote.

Kisa hicho kilifanyika mwaka wa 2016.

“Kila siku alikuwa anatunajisi. Siwezi kukumbuka alininajisi mara ngapi. Alikuwa hatumii mpira. Ninashukuru haki imepatikana,” msichana huyo mwenye umri wa miaka 16 akafichua.

Msichana huyo ni miongoni mwa mamia ya watoto waliopitia madhila miongoni mwa watalii wakongwe.

Lakini sasa bodi ya filamu nchini (KFCB) imeanza mikakati ya kukabiliana na dhuluma hiyo.

Meneja wa KFCB tawi la Pwani Boniventure Kioko alisema hulka hiyo inaendelea kushuhudiwa maeneo ya kitalii huku akiwataka wazazi kushirikiana katika kukomesha uchafu huo.

Kando na kudhulumiwa kingono, Bw Kioko alisema watoto hao hutumiwa kutengeneza filamu za ngono.

Naye afisa wa huduma za umma za vijana na jinsia (Public service, Youth and Gender Affairs CAS) Rachel Shebesh aliwataka kina mama kutunza watoto wao waendeleze masomo yao.

Washukiwa wa ukahaba jijini walala fofofo kortini

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE (pichani) aliyekuwa miongoni mwa wachuuzi zaidi ya 200 waliokamatwa wakikaidi sheria za kaunti ya Nairobi alilala fofofo kortini akisubiri kesi inayombakili itajwe.

Sio mwanamke huyu aliyelala kortini peke yake bali ni wengi.

Washtakiwa walikoroma kwa kuzidiwa ni usingizi  hakimu alipochelewa kufika kuendelea na kesi zilizowakabili.

Hakimu alipoingia mahakamani, meza iligongwa kisha washukiwa wote wakasimama huku waliokuwa wamezama katika lindi la usingzi wakifuta matongo machoni.

Walitozwa faini ya kati ya Sh500 hadi Sh3000 kwa makosa ya kuendeleza ukahaba, kutupa chafu kwenye barabara na pia kuuza bidhaa mahala wasiporuhusiwa.

Mashoga 6,000 hatarini kuambukizwa HIV kuliko makahaba

Na CHARLES LWANGA

KARIBU watu 6,000 wanofanya ushoga mjini Malindi wako katika hatari ya kuambukizwa na virusi vya Ukimwi kutokana na ongezeko la vijana wanaofanya biashara ya ushoga katika mji huo wa kitalii.

Mtaalamu wa maswala ya Ugonjwa wa Ukimwi katika hospitali ya Malindi, Dkt Godfrey Njoroge, alisema idadi hiyo imeongezeka kutokana na ukosefu wa ajira.

“Kulingana na utafiti, karibu watu 6,000 wanakisiwa kufanya mapenzi na wanaume wenzao na nambari hiyo huenda ikawa kubwa ikilinganishwa na idadi ya wanawake wanaofanya ukahaba mjini humu,” alisema.

Akizungumza na wanahabari mjini Malindi, aliitaka serikali kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali wagawe mipira za kondomu na mafuta kwa mashoga hao ili ipunguze usambazaji ukimwi mjini humo.

“Kama unavyofahamu, sehemu inayotumiwa haikuumbwa kwa ajili ya kufanyia mapenzi na kwa hivyo ni mahali ambapo virusi vya ukimwi vinaweza kuigilia kwa urahisi wakati wa mapenzi,” alisema.

Dkt Njoroge alisema wateja wao ni watu matajiri mjini Malindi na watalii wanaozuru mji huo kwa likizo.

Bi Evans Onyango, ambaye pia ni mtaalamu wa janga la Ukimwi hospitalini humo aliwasihi watu wanaofanya ushoga watembelee vituo vya afya ili wapime hali yao ya virusi vya HIV wapate madawa.

“Baadhi yao hawapendi kwenda hospitali kupimwa na ingekuwa vyema waje hospitali ili tuweze kuwasaidia,” aliongeza.

Kulingana na Shirika la kupambana na janga la Ukimwi nchini, uambukizaji wa Ukimwi katika Kaunti ya Kilifi iko katika asilimia 4.2, kumaanisha kuwa katika kila watu 100 wanne wao wanabeba virusi vya Ukimwi.