Kaunti za Pwani kusaka ?watalii kama eneo moja

Na SIAGO CECE

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa itashirikiana na kaunti zingine za Pwani kuinua sekta ya utalii ambayo imepata pigo kubwa katika miaka ya hivi majuzi.

Kupitia mpango wa ‘Sister Cities’ ambao hulenga kutafuta ushirikiano wa miji ya kimataifa kuvutia utalii, kaunti hiyo ikiongozwa na Gavana Hassan Joho imeanza kutafuta umoja wa Pwani kitalii, ikianza na Kaunti ya Kwale.

Akizungumza katika Hoteli ya Neptune Beach iliyo Diani, Kaunti ya Kwale, Afisa Mkuu wa Vijana, Jinsia na Michezo katika Kaunti ya Mombasa, Bw Innocent Mugabe alisema mpango huo unakusudia kukuza utalii katika eneo lote la Pwani na kuvutia watalii zaidi wa kimataifa ambao idadi yao imepungua kwa sababu ya janga la corona.“Kaunti ya Kwale ni ya kipekee.

Hatuangalii tu Kaunti ya Mombasa, lakini pia kaunti nyingine jirani kwa sababu hatuwezi kuuza Pwani ya Kenya kupitia kwa kaunti moja tu,” Bw Mugabe alisema.

Alikuwa akizungumza alipoandamana na waandishi wa habari na maajenti wa utalii na usafiri kutoka Ukraine waliotembelea Kwale, ili kugundua vivutio ambavyo vinaweza kuwafuraisha watalii wa Kiukreni.

Kaunti ya Mombasa ilitia saini ushirika wa utalii na serikali ya Ukraine kufufua sekta ya utalii kupitia mpango maalumu wa ‘Sister Cities’.

Bw Mugabe aliongeza kuwa Kaunti za Taita Taveta na Kilifi pia zinalengwa kutokana na vivutio kama vile Mbuga ya Wanyama ya Tsavo ambayo inajulikana kwa wanyama pori na uhamiaji wa nyangumi huko Watamu, Kilifi, ambao kwa muda mrefu umevutia watalii kutoka kote ulimwenguni.

Balozi wa Ukraine nchini, Bw Oleksii Sierkov alisema kuwa tayari, ndege zaidi za kukodisha zimepangwa kuleta watalii kutoka nchi yake ambao watatua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi, Mombasa.Wiki hii, watalii zaidi ya 200 wanatarajiwa kuwasili Mombasa.

‘Tangu tuanze ushirikiano huu, zaidi ya watalii 1,000 kutoka Ukraine wamefika Kenya na tunatumaini pia kwamba Wakenya wengi watatembelea Ukraine,’ alisema balozi huyo katika mahojiano akiwa Kaunti ya Kwale.

Mkurugenzi wa mpango huo wa Sister City, Bi Salma Noor alisema angalau miji 22 ya kimataifa imekubali kushirikiana na Kenya kupitia mpango huo wakati miji kutoka Ukraine tayari imeahidi kuwa na ndege zao za kukodi kwenda Mombasa.

‘Miji mingine mingi sasa inavutiwa kujisajili nasi na hii itaongeza idadi ya watalii huko Mombasa ambao pia watatembelea kaunti nyingine,’ alisema, akisisitiza kuwa lengo ni kunufaisha kaunti zote katika eneo la Pwani.

Hivi sasa, utalii wa kimataifa umeanza kuimarika Pwani na hoteli nyingi zinarekodi idadi kubwa za watalii kutoka nchi za nje ikilinganishwa na mwaka jana.

Covid: Wadau wa utalii walalama kubaguliwa

Na WACHIRA MWANGI

WADAU katika sekta ya utalii wamelalamika kuwa sekta ya utalii inabaguliwa serikali inapoendelea kujaribu kurejesha hali ya kawaida ya kimaisha kipindi cha janga la corona.

Hii ni baada ya serikali kutangaza itaruhusu magari ya uchukuzi wa umma kubeba abiria kwa viti vyote kuanzia leo.

Wasimamizi wa hoteli maeneo ya Pwani wameitaka serikali ilegeze kamba kuhusu kanuni za kupambana na virusi vya corona ambazo zinaathiri sekta ya utalii.

Afisa mkuu katika Chama cha Wahudumu wa Hoteli, Dkt Sam Ikwaye alisema sekta hiyo imeathirika sana na sera za serikali zilizonuia kuepusha maambukizi ya virusi vya corona ikilinganishwa na sekta nyingine za kibiashara na kijamii.

“Tunataka mkutano na maafisa wa wizara za afya na utalii ili tupate mwelekeo kuhusu sekta hii. Mwaka mzima wa 2020 ulikuwa wa hasara, hivi sasa 2021 inakaribia kukamilika kwa hasara. Ifikapo 2022 itakuwa ni mwaka wa kisiasa, tutafufua vipi biashara zetu baada ya 2022?” akauliza.

Sekta ya utalii ni miongoni mwa zile zilizoshuhudia maelfu ya watu wakipoteza ajira hasa katika maeneo ya Pwani kwa sababu ya upungufu wa watalii.

Hali hiyo ilisababishwa na sera ambazo zilifanya iwe vigumu kwa watu kusafiri kitaifa na kimataifa, sera kuhusu idadi ndogo ya watu wanaotakikana kukubaliwa kukutana kwa wakati mmoja na wakati mwingine marufuku ya mikutano ya ana kwa ana, kufungwa kwa maeneo ya burudani yaliyokuwa vivutio vya utalii, na sheria kali za kudhibiti mikahawa na baa.

Dkt Ikwaye alilalamika kuwa wafanyabiashara katika sekta hiyo sasa wamegeuka ombaomba wanapojaribu kuendeleza maisha yao.

Alisema wamiliki wengi wa hoteli waliwekeza pesa nyingi ili kuhakikishia wageni usalama wao dhidi ya Covid-19 lakini bado serikali haitaki waendeleze biashara kama ilivyokuwa kawaida ilhali sekta nyingine zinaruhusiwa.

Meneja Mkuu wa Hoteli za kenya Safari, Bw Joseph Ndunda, alisema sekta hiyo inabaguliwa kwani nyingine ambazo hata hazifuati kanuni ipasavyo zinaruhusiwa kuendeleza biashara kama kawaida.

Jumanne iliyopita, Waziri wa Utalii, Bw Najib Balala alitangaza mikakati mipya inayolenga kufufua utalii wakati huu wa janga la corona, lakini wawekezaji katika sekta hiyo wanalalamika kuwa serikali haijamakinika katika suala hilo.

Mojawapo ya mipango aliyotangaza ni kuwapa kipaumbele wahudumu wa hoteli kupokea chanjo ya kuwalinda dhidi ya Covid-19.

Utalii wapigwa jeki Lufthansa ikizindua safari

Na SIAGO CECE

SEKTA ya utalii nchini imepigwa jeki baada ya Kenya kupokea ndege ya watalii kutoka Frankfurt, Ujerumani katika uwanja wa ndege wa Moi mjini Mombasa.

Ndege hiyo ni ya kwanza aina ya Eurowings kutoka kampuni ya Lufthansa, iliyotoka Ulaya na ilikuwa imebeba watalii 150.

Akizungumza mjini Mombasa baada ya kukaribisha ndege hiyo Jumapili alfajiri, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii, Bi Safina Kwekwe alisema safari hiyo imeleta matumaini kwa sekta ya utalii iliyokuwa imedidimia tangu janga la virusi vya corona lilipoanza kutikisa dunia.

Ndege hiyo itakuwa ikitua Mombasa mara mbili kwa wiki, Jumapili na Alhamisi.

“Katika serikali, tunajitahidi kuhakikisha kuwa tuko tayari kukaribisha watalii wengi nchini Kenya,” Bi Kwekwe alisema.

Balozi wa Ujerumani humu nchini, Bi Annette Gunther ambaye alikuwa Mombasa kuilaki ndege hiyo alisema safari hiyo ya ndege inaashiria pia uhusiano mwema ulioko kati ya nchi ya Kenya na Ujerumani.

Watalii Wajerumani wamekuwa wakitembelea maeneo ya Kenya hasa Pwani kwa miaka mingi na baadhi yao wamefanya miji kama vile Malindi na Mtwapa kuwa makao yao.

“Kampuni nyingi ambazo zinakuja kufanya biashara Kenya huwa haziondoki, na tunajua pia ndege hii haitakuwa ya mara moja tu bali itaendelea kwa miaka ijayo,” Bi Gunther alieleza.

Itakapofika mwaka ujao, ndege hiyo itaanza kutua Mombasa mara nne kwa wiki.

Wadau katika sekta ya utalii nchini Kenya pia wamefurahia kuja kwa ndege hiyo wakisema kuwa wanatarajia ndege zaidi za kukodisha kutua Mombasa.

“Tumeona katika siku za hivi majuzi idadi ya watalii kutoka nchi za nje inaongezeka. Hii ina maana kuwa sekta hii yetu iliyokuwa imeathirika na janga la corona itaimarika,” alisema Bw Wasike Wasike, ambaye ni naibu mwenyekiti wa Chama cha Wahudumu wa Hoteli (KAHC).

Alisema hoteli nyingi zimejiratayarisha ipasavyo kuhakikisha kuwa afya ya wageni wao ni salama kwa kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Tangu mwaka 2020, maelfu ya wafanyikazi wa hoteli na mashirika mengine ya utaliii walipoteza kazi baada virusi vya Corona kuongeza na kusababisha nchi nyingi kukomesha usafiri wa nje.

Eneo la Pwani linategemea sana watalii wa kigeni, mara nyingi wakazi hufanya biashara na watalii hao na mwishowe kujiendeleza kimaisha.

Wamaasai wanavyovumisha utalii kupitia sherehe za Moran

Na GEORGE SAYAGIE

KAUNTI ya Narok inatarajiwa kuwa kivutio kikubwa cha utamaduni kwa miezi mitatu hadi minne ijayo, ukoo wa Purko miongoni mwa jamii ya Wamaasai unapojitayarisha kwa hafla ya kuwaingiza vijana wa Moran kwenye utu uzima.

Hafla hiyo huwa inafanyika mara moja kila baada ya miaka kumi, na huwa hatua muhimu kwa vijana hao.Kabla vijana kuvuka rika, huwa kuna shughuli kadhaa ambazo hufanywa kama njia ya kuwatayarisha.

Baadhi yazo ni kuwanyoa nywele, wavulana kufunzwa masuala na mienendo ya utu uzima na hafla nyingine, ambapo huwa wanakula nyama pamoja.

Ulaji nyama pamoja miongoni mwao huashiria mwisho wao kuwa wavulana na mwanzo wa maisha mapya kama watu wazima.Kufikia sasa, tarehe ambapo hafla yenyewe itafanyika bado haijatangazwa.Hafla hiyo huwavutia maelfu ya watalii kutoka humu nchini na nchi za nje kutokana na upekee wake wa kitamaduni.

Mnamo Jumapili jioni, mamia ya Wamorani kutoka vijiji vya Melili katika maeneo ya Narok Kusini na Kaskazini waliingia mjini Narok kwa kishindo.

Wamorani hao walikuwa wamebebwa kwa pikipiki na magari, huku wakipiga vuvuzela.Waliigeuza taswira ya mji huo kuwa nyekundu kutokana na rangi ambazo huwa wamepaka nywele zao.

Msafara huo ni sehemu ya misafara kadhaa kama hiyo ambayo imeshuhudiwa mjini humo kwa muda wa majuma mawili yaliyopita.Wamorani hao wamekuwa wakielekea katika eneo maalum katika kijiji cha Rotian, Narok Kaskazini, ambako shughuli maalum ya kuwanyoa nywele itafanyika katika muda wa miezi mitatu ijayo.

Hafla hiyo huitwa Eunoto kwa lugha ya Kimaasai.Wamorani wote watanyolewa baada ya nywele zao kumwagiliwa maziwa, wakiwa wamekalia kiti chenye miguu mitatu.

Baada ya hatua hiyo, watashirikishwa kwa hafla ya kuwatawaza kama watu wazima.Kiongozi wa Wamorani hao, Bw Amos Ole Tikani alisema bado wanatarajia kuwapokea wengine wengi zaidi.

“Kufikia sasa, tumepokea Wamorani kutoka makundi tisa ambako ukoo huo huwa unaishi. Wanatoka katika maeneo kama Nkaretta, eneo la Mau katika Narok Kaskazini, Naroosura katika Narok Kusini na Mosiro katika Narok Mashariki. Watakuwa miongoni mwa Wamorani 6,000 wanaojitayarisha kwa hafla hiyo. Wanatarajiwa kula mafahali 3,000 na mbuzi na kondoo 30,000,” akasema.

Bw Joseph Ole Yenko, ambaye ni chifu wa kitamaduni wa jamii hiyo na anayewaongoza Wamorani kutoka eneo la Melili, alisema hafla hiyo inachukuliwa kwa uzito sana na jamii ya Wamaasai. Aliitaja kuwa “nguzo kuu” kwa maisha ya kila mtu kutoka jamii hiyo.

“Hafla inajumuisha ujenzi wa Manyatta, uteuzi wa viongozi, uchezaji densi, unyoaji nywele, ulaji nyama na utoaji baraka kwa washiriki wote,” akasema Bw Yenko.Hafla hiyo huhusisha vijana kutoka jamii hiyo walio kati ya umri wa miaka 15 na 30.

Wadau walia utalii unaendelea kusambaratika nchini

Na WINNIE ATIENO

SEKTA ya Utalii eneo la Pwani inazidi kudorora huku janga la corona likiendelea kuathiri biashara nchini.

Wawekezaji wa utalii wanasema wanaendelea kukadiria hasara kubwa kufuatia janga hilo na kuzorota kwa uchumi.

Kufikia sasa hoteli za pwani zina asilimia 20 ya wageni huku msimu wa chini wa wageni ukiingia baada ya mwaka mgumu wa utalii wa 2020 kufuatia janga hilo ambalo lililemaza utalii na usafiri.

Wawekezaji hao waliokuwa wakitegemea watalii wa humu nchini baada ya wale wa kimataifa kususia kusafiri kufuatia janga hilo wamebakia bila wageni katika hoteli zao.

Juhudi za serikali kuokoa sekta hiyo pia inakadiriwa zinagonga mwamba baada ya wawekezaji wengi kususia mkopo wa Sh3 bilioni ili kujinasua. Wanadai kuwa serikali imeweka sheria kali za mkopo huo.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wawekezaji wa Utalii nchini Bw Mohamed Hersi, Afisa Mkuu wa Muungano wa Watalii Pwani Julius Owino na Afisa Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi wa Hoteli nchini tawi la Pwani, Dkt Sam Ikwaye, walisema wageni wa humu nchini ndio wamekuwa wakipiga jeki sekta hiyo.

“Tunaishi siku baada ya siku, hatujui siku zetu za usoni. Awali tulidhani chanjo ya corona ndio sulu

hisho lakini tunaendelea kushuhudia maafa hususan Uingereza ambapo mambo yanazidi kuwa magumu. Nchi nyingi ambazo ni soko letu la utalii zimefungwa tena sababu ya maambukizi ya corona,” alisema Bw Hersi.

Alisema hatima ya janga haijulikani suala linaloendelea kutishia utalii.

Hata hivyo, kutokuwa na uhakika kumewalazimisha wamiliki wa hoteli kuanza kubuni mbinu maalum ili kushawishi soko la ndani na vivutio vingine. Wamiliki hao wanapunguza ada za hoteli.

“Hoteli zinatoa viwango vya chini kabisa ambavyo havijawahi kufanyika katika historia kutokana na janga hili. Hata hivyo tangu Januari, vituo hivyo vimebaki tupu,” akasema Bw Owino.

Utalii ni uti wa mgongo wa uchumi wa ukanda wa Pwani unaoajiri wafanyakazi 12,800. Lakini kwa sasa nusu ya wafanyakazi hao wanafanya kazi kwa mshahara wa asilimia 50 kwa sababu ya kudorora kwa uchumi.

Mei mwaka jana, Rais Uhuru Kenyatta alizindua mkopo wa Sh3 bilioni ili wawekezaji wa utalii wajinasue kutoka kwa changamoto.

Hata hivyo, wawekezaji wengi bado hawajachukua mkopo huo.

Wawekezaji hao wanaitaka serikali kupunguza kodi na gharama za ada ya umeme wakisema iko juu.

Eneo la Pwani lilipewa mgao mkubwa wa mkopo huo wa Sh1.8 bilioni kati ya Sh3 bilioni sababu uchumi wake unategemea utalii.

Wamiliki wa hoteli wanapewa mkopo huo kwa kiwango cha riba ya asilimia tano. Bw Owino alieleza wasiwasi wake kwamba endapo wamiliki wa hoteli hawatochukua mikopo hiyo huenda ikaregeshwa serikali kuu.

“Tunatoka katika kipindi kigumu lakini lazima tung’ang’ane. Tunaisihi serikali kupunguza ushuru ambao bado uko juu kutoka asilimia 16 hadi 14. Serikali inafaa kufutilia mbali kodi za mwaka 2020 sababu hakukuwa na biashara,” alisisitiza Bw Owino.

Hata hivyo wawekezaji hao wana matumaini kwamaba sekta hiyo itafufuka kwanzia likizo ya Agosti. Walisema asilimia 80 ya faida wanazopata kwenye biashara hizo huregea kwenye mahoteli ili kuendesha sekta hiyo.

Dkt Ikwaye alisema utalii wa ndani huendeshwa kulingana na kalenda ya elimu.

“Lakini badala ya wakenya kusafiri watu wanafikiria karo za shule, janga hili limeathiri soko letu. Serikali inaa ibuni sheria zitakazoongoza ufufuaji wa sekta hii. Lakini mfumo unaochukuliwa na serikali utalemaza utalii sababu ya kuinyima wizara fedha za kuuuza Kenya,” alisisitiza Dkt Ikwaye.

Kero mitandaoni Balala akiteua Mwingereza kupigia debe utalii

NA WANGU KANURI

Wakenya kupitia mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook wameeleza masikitiko yao kuhusiana na uamuzi wa Wizara ya Utalii wa kumteua mwanamitindo wa Uingereza Naomi Campbell kama balozi wa kimataifa wa Magical Kenya.

Akitoa tangazo hilo Januari 12, 2021, Waziri wa Utalii na Wanyamapori Najib Balala alisema kuwa Campbell alipewa jukumu la kustawisha Kenya kama utalii bomba na kusafiri duniani.

Katika ripoti, wizara hiyo ilisema kuwa kuteuliwa kwake kulifikiwa baada ya mkutano kati ya msanii huyo na Bw Balala.

“Tunawakaribisha katika habari za kufurahisha ambapo Naomi Campbell atatetea utalii na atasafiri barani kama balozi wa Magical Kenya,” Balala akasema katika taarifa kwa vyombo vya habari. Campbell kwa upande wake, alishukuru serikali ya Kenya kwa kuboresha usafiri Pwani, akiongeza kuwa kituo cha ndege cha Malindi kimefikia kiwango cha kimataifa.

“Nimevutiwa sana na ufasaha wa kiwango wa cheo cha dunia na muungano wa utaalamu wa gofu ulio katika Vipingo Ridge, muungano pekee uliopewa sifa Afrika nzima. Ninawakaribisha wataalamu wa gofu duniani kote kutembelea eneo hilo na kujifurahisha,” akasema.

Modeli huyo alikuwa Kenya katika likizo yake huku akiishi katika nyumba ya mapumziko ya bilionea mmoja ambaye inasemekana ilikuwa ya mchumba wake, mfanyibiashara wa Kiitaliano na aliyekuwa mkuu wa timua ya Formula One, Flavio Briatore.

Campbell, aliyekuwa katika safari yake ya tatu nchini Kenya, hata hivyo alidinda kuzungumza na vyombo vya habari na amekuwa akificha habari kuhusu safari yake huko Pwani kaskazini.

Wakati wa safari yake ya mwisho nchini Kenya, aliwafanya wengi kutoa maoni yao alipopiga picha akiwa uchi katika pahali pageni Malindi. Alitembea tena Malindi mwaka wa 2014 wakati wa likizo ya Krismasi lakini ili kuwasaidia watu.

Haya ni baadhi ya maoni ya Wakenya kuhusu kuteuliwa kwake, huku wengi wakisema kuwa jukumu hilo lingepewa Mkenya.

“Huo wadhifa wamepea Naomi Campbell sababu Lupita ni mzaha kwao?” akauliza @AdanZamuh.

“Taarifa kuhusu Naomi Campbell kuteuliwa kama balozi wa Magical Kenya ni upuzi. Vipi katika ardhi hii ya Mwenyezi Mungu, walimchagua Naomi badala ya Lupita Nyong’o? Mbona si Trevor Noah? Kivipi? Ama sababu Waziri anampenda? MAAJABU!” akakamilisha @DavidoOsiany.

“Wueh, ningependekeza Mulamwah badala ya mgeni Naomi Campbell na huyo mwanamke anayecheka peke yake,” akasema @MoseMungai.

“Inasikitisha sana kuona kuwa tunalipa wageni kama Naomi Campbell kustawisha Magic Kenya ulimwenguni ilhali tuna watu wenye umaarufu nchini Kenya kama Lupita Nyong’o wa Hollywood lakini punde tu Mkenya amestawi huko nje wanatuepuka kama Corona,” akateta @beatambutei.

Wengine, hali kadhalika walifikiri alikuwa chaguo bora.

“Naomi Campbell anastahili wadhifa huo wacheni ukabila,” akasema @IAm_Danniek.

“Ninafikiri Naomi Campbell anastahili wadhifa huo kama balozi. Ukifahamu kuwa audience walikuwa watu kutoka bara. Pia anaelewa mandhari ya nchi na amejihusisha na Kenya mara kadhaa; kwa hivyo anastahili cheo hicho na atafanikiwa kwake,” akasema @walowe_mlolwa.

“Anastahili. Naomi Campbell amekuwa akija Malindi kwa likizo za Disemba, kila mwaka kwa miaka mingi,” akaandika @John Musembi.

Mombasa yaandaa burudani aali siku ya utalii duniani

Na MISHI GONGO

KAUNTI ya Mombasa imeandaa burudani ya kukata na shoka kuadhimisha Siku ya Utalii Duniani.

Sherehe hiyo ambayo inafanyika hii leo katika bustani ya kifahari ya Mama Ngina Waterfront itakuwa na burudani aali ambapo wasanii kutoka nchi za kigeni na wa humu nchini wanatumbuiza, huku vyakula vya kitamaduni, na tamasha zinginezo zikitarajiwa kutia fora.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Utalii na Maendeleo Vijijini’.

Aidha kutakuwa na mashindano ya baisikeli ambayo yatawaleta pamoja zaidi ya waedeshaji 300 kutoka sehemu mbalimbali za nchi.

Akizungumza Jumamosi katika maandalizi ya tamasha hizo, Waziri wa Utalii na biashara katika kaunti hiyo Bw Fauz Rashid alisema kuwa tamasha hizo zinapanga kufufua sekta ya utalii ambayo iliathiriwa pakubwa na janga la corona.

Alisema sekta ya utalii imekuwa mbele katika kuwaajiri watu wa vijijini.

“Washikadau katika sekta ya biashara na utalii wote wako hapa,madhumuni ya hafla hii ni kufufua sekta ya utalii ambayo kwa sasa iko katika hali mbaya, sekta ya biashara dunia nzima iliathirika pakubwa so tunatarajia hafla hii itasaidia kuboresha biashara,”akasema Bw Rashid.

Anaeshikilia kitengo cha afya ya umma Bw Pauline Oginga alisema kuwa wako tayari kwa hafla hiyo akisema kuwa wameweka mikakati ya kuhakikisha kuwa umati utakaofika sehemu hiyo utakuwa salama.

Alisema watahakikisha kuwa umati utakaohudhuria watafuatilia masharti yote yaliyowekwa na wizara ya afya.

“Tumehakikisha kuwa kuna maji ya kutosha kuhakikisha watu wanaosha mikoni na kutumia sabuni za kuuwa viini kabla ya kuingia eneo hilo. Aidha wote watakao hudhuria watalazimika kuvalia maski,” akasema.

Alisisitiza kuwa eneo hilo ni kubwa kustahamili umati mkubwa utafika eneo hilo akiongezea kuwa litawekwa alama kuhakikisha kuwa watu hawakaribiani.

Aidha alisema madaktari na wauguzi watakuwa katika eneo hilo kuhakikisha kuwa wanawasidia wote watakao hitaji huduma za maafisa hao.

Afisa mkuu wa afya katika kaunti hiyo Dkt Khadija Shikely alisema watakuwa na gari ya wagonjwa mahututi tatu ambazo zitahudumia wanaoendesha baskeli na pia watafanyia watu watakaotaka vipimo vya Covid 19 vya bure.

Afisa wa utalii katika kaunti ya Mombasa Bi Asha Abdi alisema sherehe hiyo itahusisha zoezi mbali mbali zikiwemo vyakula na ngoma.

Fort Jesus yafunguliwa kufufua utalii Pwani

Na DIANA MUTHEU

BAADA ya kufungwa kwa miezi sita sasa, hatimaye kivutio maarufu cha watalii eneo la Pwani, Fort Jesus, ilifunguliwa Jumatatu asubuhi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika majengo ya Fort Jesus, mtaalamu wa miundo misingi katika ngome hiyo, Bi Fatma Twahir alisema kuwa eneo hilo sasa limefunguliwa na wamejiandaa vizuri kuwapokea wageni.

Bi Twahir alisema kuwa sehemu za watu kunawa mikono ziko tayari, kwani mifereji na sabuni zimewekwa langoni.

Pia, mtindo wa kulipia tiketi umegeuzwa na malipo yanafanywa kwa njia ya kieletroniki, ambapo wageni wanakubaliwa kutumia M-pesa au kadi za benki pekee.

Zaidi, Bi Twahir alisema kuwa wameweka vidude vya kielektroniki vitakavyotoa viyeyuzi bila kubonyezwa, watu hawaruhusiwi kugusa vitu ovyo ovyo, njia zimewekewa alama ili kuhakikisha wanaotembelea jingo hilo wanasimama umbali wa mita moja unusu, hayo yote kuhakikisha kuwa wageni wako salama na wanalindwa dhidi ya maradhi ya covid-19.

Baadhi ya wageni wakisajiliwa nje ya majengo ya Fort Jesus. Ngome hiyo imefunguliwa leo baada ya kufungwa kwa miezi sita. PICHA/ DIANA MUTHEU

“Baada ya kufunga kwa miezi sita, hatimaye tumefungua na tayari leo tumewapokea wageni karibu 30,” akasema Bi Twahir. Wageni wetu wanapaswa kuvalia barakoa zao, pia tumehakikisha kuwa kuna njia moja itakayofuatwa na wageni wote ili kuhakikisha kuwa watu hawatembei kiholela. Pia, tumeweka ilani kuonyesha idadi ya watu watakaoingia katika vyumba vya maonyesho, ili kuzuia msongamano wa wageni mle ndani,” akasema Bi Twahir.

Pia, mkahawa ulio ndani ya majengo ya Fort Jesus umeagizwa ufuate masharti yaliyowekwa na serikali.

“Tumewaelekeza wafuate mikakati yote iliyopendekezwa na wizara ya Afya, ili kulinda afya yao na ya wateja wao,” akasema Bi Twahir.

Ngome ya Fort Jesus ilifungwa mnamo Machi baada ya kisa cha kwanza cha mgonjwa wa virusi vya corona kutangazwa nchini, pale ambapo makavazi yote nchini yaliamrishwa kusitisha shughuli zao.

Bi Twahir aliiambia Taifa Leo Dijitali kuwa kufungwa kwa makavazi hiyo imekuwa hasara kubwa ikizingatiwa kuwa mapato makubwa hupatikana miezi ya Aprili na Agosti.

Wageni wakitalii ndani ya Fort Jesus, baada ya kivutio hicho cha watalii kufunguliwa. PICHA/ DIANA MUTHEU

“Mwaka jana mnamo Aprili tulipokea wageni 23,000 na mapato ya Sh5 milioni, na mnamo Agosti watalii walikuwa 52,000 huku mapato yakiwa Sh10 milioni. Pia, miezi hiyo ingine tulikuwa tunapata wageni japokuwa hawakuwa wengi,” akasema Bi twahir akiongeza kuwa katika mwezi wa Aprili, shule nyingi zilikuwa zinatembelea makavazi hayo na mwezi wa agosti, wanafunzi watalii wa humu nchini na kutoka nchi za nje walifurika Fort Jesus.

Hata kama mwezi wa Septemba idadi ya wageni wanaotembelea eneo hilo jhuwa wamepungua, Bi Twahir alisema kuwa majengo ya Fort Jesus yako salama na wana matumaini kuwa watapokea watalii wengi.

“Tuna matumaini kuwa wageni wataanza kutembelea eneo hili. Tuko tayari kuwapokea,” akasema afisa huyo.

Bi Twahir alisema kuwa eneo hilo lilikaguliwa na idara ya afya ya umma ya Kaunti ya Mombasa wiki tatu zilizopita, wafanyikazi wote wakapimwa virusi hivyo, na hakuna mmoja aliyeambukizwa maradhi ya Covid-19.

Zaidi alisema kuwa walichukua muda mrefu kujiandaa kupokea wageni, ili kuhakikisha kuwa wamezingatia sheria zote zilizopendekezwa na Wizara ya Afya, na pia kuwafanya wateja wao wawe na Imani na jinsi wanavyotoa huduma zao.

“Rais alipotangaza ufunguzi wa polepole wa uchumi mnamo Juni 2, wafanyikazi wetu walianza kazi za kukarabati na kusafisha eneo lote kwa matayarisho ya kuwapokea wageni. Walifanya kazi kwa kupishana,” akasema.

Watalii wakipigwa picha ndani ya majengo ya Fort Jesus, ilipofunguliwa leo asubuhi. PICHA/ DIANA MUTHEU

Mtalii mmoja kutoka Nairobi, Bw Jacob Simwero alisema kuwa amefurahishwa jinsi mikakati ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona imefuatiliwa katika ngome hiyo.

“Kabla ya kuingia ndani ya Fort Jesus, tuliandikishwa majina, nambari ya simu, tukapimwa joto na ikarekodiwa. Sijawahi kuona sehemu nyingine ambapo kiwango cha joto cha wateja kinanukuliwa. Pia, vidude wanavyotumia kuwekea viyeyuzi inatumia teknolojia ya hali ya juu ambapo hatuhitajiki kugusa pahali popote,” akasema huku akiongeza kuwa anajihisi salama katika mazingira yale na angewaomba Wakenya watembelee makavazi hiyo.

“Nilikuwa nimesoma na kusikia mengi kuhusu Fort Jesus, na mwishowe nimeiona mimi mwenyewe. Sikujua kuwa itafunguliwa leo, nilikuwa katika likizo na nikaamua kupitia eneo hili kuangalia hata angalau jengo lenyewe kwa nje, lakini nashukuru nimeweza kuiona sehemu ya ndani ya ngome hiyo,” akasema Bw Simwero.

Mtembezi wa watalii eneo la Fort Jesus na Old Town, Bw Esgar Gulambasi alisema kuwa janga la corona liliathiri kazi zao, lakini wana matumaini ya kupokea wageni wengi.

Mtaalam wa miundo misingi katika ngome ya Fort Jesus, Fatma Twahir akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutangaza kuwa eneo hilo limefunguliwa tena. PICHA/ DIANA MUTHEU

“Maisha yalikuwa magumu. Tulilazimika kufanya kazi mbadala ili kupata fedha za kulisha familia zetu. Tunamwomba Mungu atuondolee janga hili, na atuongezee idadi ya wageni,” akasema Bw Gulabasi huku akiongeza kuwa watu wote wanapaswa kuzingatia sheria zilizowekwa na wizara ya afya, ili kazi ziendelee bila ya maabukizi yeyote ya corona.

Makavazi ya Fort Jesus, fuo za bahari za umma kama vile Jomo Kenyatta maarufu ‘Pirates’ na bustani za kujivinjari kama vile Mama Ngina ni baadhi ya maeneo yaliyofungwa punde tu kisa cha kwanza cha mgonjwa wa maradhi ya covid-19 kutangazwa.

Fort Jesus ndilo jengo zee zaidi katika eneo la Pwani, kulingana na historia. Jengo hilo linaaminiwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 400.

Ni mojawapo ya vivutio vya utalii ambacho huvutia wageni wengi zaidi katika ukanda wa Pwani na jumuiya ya Afrika Mashariki, na siku hizi ni makavazi ya kuhifadhi vyombo vya kale, michoro na miundo mbalimbali ya zana za kivita.

Serikali yahakikishia wawekezaji sekta ya utalii kwamba inawapima wageni wote wanaoingia nchini kwa ndege

Na WINNIE ATIENO

SERIKALI kuu imewahakikishia wawekezaji katika sekta ya utalii kwamba inaweka juhudi kukabiliana na virusi vya corona ili kuzuia maambukizi kutoka nchi za kigeni baada ya kufunguliwa kwa viwanja vya kimataifa vya ndege.

Mkuu wa idara ya afya ya umma katika Wizara ya Utalii, Bi Susan Mutua, alisema serikali inajizatiti kukabiliana na tishio la maambukizi ya kigeni kutoka kwa wageni wanaoingia humu nchini kupitia viwanja vya kimataifa vya ndege na madereva mipakani.

Mnamo Agosti 1, 2020, serikali ilifungua rasmi viwanja vya kimataifa vya ndege, huku wawekezaji katika sekta ya utalii wakijizatiti kutafuta watalii baada ya soko hilo kudorora kwa sababu ya janga la corona.

Nchi nyingi bado hazijawaruhusu raia wake kusafiri nje kufuatia janga la corona.

Hata hivyo, Bi Mutua alisema serikali ya Kenya sasa inakabiliana na maambukizi ya virusi vya corona miongoni mwa wanajamii – community infection – na kwamba maambukizi kutoka raia wa kigeni ni machache.

“Tunapima wale wote wanaoingia humu nchini kupitia mipaka yetu na hata wale wanaotumia wnja zetu za kimataifa, ili kuzuia usambaa wa virusi kutoka nchi za kigeni. Ni sharti wageni wote wapimwe hususan madereva wa bodaboda wanaoigia humu nchini kupitia mikapa yetu ili kuzuia virusi kutoka nchi za kigeni,” alisisitiza.

Haya yanajiri huku wawekezaji wa sekta ya utalii wakiwa na matumaini kwamba utalii utaimarika endapo virusi hivyo vitapungua. Hata hivyo waliwaisihi serikali kuuza soko la Kenya ughaibuni ili kupata watalii wengi kuzuru eneo hilo.

Kwa sasa wadau wa sketa ya utalii wanategemea utalii wa humu nchini.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Utalii nchini, Bw Mohammed Hersi na mwenzake wa muungano wa pwani wa wakezaji wa utalii Bw Victor Shitakha walisema kufunguliwa kwa viwanja vya ndege za kimataifa kutaimarisha utalii.

“Tangu kufunguliwa kwa viwanja vya kimataifa wa ndege, sekta ya utalii imeanza kuimarika huku tukipata wageni wachache eneo la pwani. Lakini bado tuko asilimia 20 kwa idadi ya vitanda; wakati wa wikendi huwa tunapata wageni asilimia 50-60 kwa hoteli zingine kupitia utalii wa humu nchini,” alisema Bw Shitakha.

Bw Hersi naye alisema kufunguliwa kwa viwanja hivyo fufuo la tumaini kwa utalii.

“Gazeti la Forbes lilitaja Kenya kuwa miongoni mwa nchi tisa ambazo ziko tayari kupokea wageni. Hii ni habari njema kwa sekta yetu. Janga la corona limeathiri dunia nzima lakini tunafaa kuweka mikakati kufufua sekta yetu,” alisisitiza Bw Hersi.

Utalii kudorora kufuatia mzozo kati ya Kenya na Tanzania

Na WINNIE ATIENO

WAWEKEZAJI katika sekta ya utalii wamemsihi Rais Uhuru Kenyatta angilie kati na kusuluhisha utata wa usafiri wa ndege kati ya Kenya na nchi jirani ya Tanzania.

Wawekezaji hao wanashtumu serikali ya Kenya kwa kuwalazimisha raia wa nchi jirani ya Tanzania kuwekwa karantini ya lazima kila wanapoingia nchini kufuatia janga la corona.

Kupitia muungano wa wadau wa utalii nchini yaani Shirikisho la Utalii la Kenya – Kenya Tourism Federation – wawekezaji hao walisema Kenya haifai kuwahukumu Watanzania kutokana na hatua yao ya namna wanavyokabiliana na janga la Covid-19.

“Tumewakosea wenzetu Watanzania na tunafaa kutafuta suluhu kwa sababu tukiendelea kuwatenga na kuwatema nje ya orodha ya raia wa nchi kadhaa ambao wanakubaliwa kuingia humu nchini Kenya bila vikwazo kama vile karantini, basi mzozo huu utaendelea na huenda hata wakafunga mipaka yao,” alisema mwenyekiti wa muungano huo Bw Mohammed Hersi.

Bw Hersi alionya kuwa huenda mzozo huo ukatokota zaidi baada ya Tanzania kupiga marufuku kampuni tatu za ndege za humu nchini.

“Hatua ya kuwatenga watanzania kwenye orodha ya raia wanaoruhusiwa nchini bila vikwazo ndio imetuletea balaa hii, hatuwezi kwenda kwa jirani zetu tunavyotaka ilhali hatutaki waje kwetu. Kainaya ni kwamba malori na mabasi yanapita mipakani bila vikwazo vyovyote,” aliongeza.

Bw Hersi alisema sekta za utalii, biashara na usafiri wa ndege zitabeba msalaba wa mzozo huo.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Waziri wa Utalii na Wanyamapori, Najib Balala kusisitiza kuwa raia wa nchi ambazo ziko katika hatari ya maambukizi ya corona ikiwemo Tanzania watawekwa karantini ya lazima wanapowasili humu nchini.

Bw Balala alisema raia hao watawekwa karantini ya lazima ya siku 14 kulingana na mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Waziri huyo alisema Kenya itaendelea kudumisha usalama wa watalii katika juhudi za kuimarisha sekta ya utalii.

Nchi hizo zimekuwa kwenye mzozo kuhusiana na swala la virusi vya corona huku Tanzania ikisisitiza imekabiliana na janga hilo.

Bw Balala alisema mipaka ya Kenya ingali imefungwa lakini watalii wanaoingia humu nchini kupitia viwanja vya kimataifa vya ndege ni sharti wafuate kanuni za afya ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

“Mipaka yetu ya barabara bado imefungwa lakini viwanja vyetu vya ndege viko wazi kwa watalii wa humu nchini na wale wa kimataifa kuzuru. Lakini tuna aina mbali mbali ya wageni; kuna wale wanaotoka nchi hatari zaidi, za maambukizi ya wastani na wale ambao wanatoka sehemu ambazo ziko shwari. Wale wanaotoka nchi ambazo zimetajwa hatari na WHO watawekwa karantini ya lazima kwa siku 14, ” alisisitiza Bw Balala ambaye alikuwa akijibu maswali kutoka kwa wawekezaji wa sekta hiyo kupitia mawasiliano ya mtandaoni.?

Sekta ya utalii kote duniani imepoteza zaidi ya Sh35 trilioni

GENEVA, Uswisi

SEKTA ya utalii duniani imeathirika pakubwa kutokana na janga la virusi vya corona huku ikipoteza mabilioni ya hela kulingana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres.

Katibu huyo ameeleza kuwa sekta hiyo imepoteza zaidi ya Sh35 trilioni kutokana na bidhaa zinazouzwa katika mataifa ya kigeni huku ajira kwa watu zaidi ya 120 milioni ikiwa hatarini.

Kupitia kwenye hotuba kwa njia ya video, Guterres alisema idadi ya watalii ilipungua kwa zaidi ya nusu kwa sababu ya janga hilo la kiafya, ambalo limelemaza mifumo ya kiuchumi duniani.

“Utalii ndio sekta ya tatu kuu zaidi ulimwenguni baada ya mafuta na kemikali, huku ikitoa ajira kwa mtu mmoja miongoni mwa kila kundi la watu 10 kote duniani na asilimia 7 ya biashara ulimwenguni.”

“Ndiposa limekuwa jambo la kutamausha mno kuona jinsi utalii umesambaratishwa na janga la Covid-19,” alisema mkuu wa UN.

Janga la virusi vya corona limesababisha vifo vya watu zaidi ya 813,000 ulimwenguni kote huku kukiwa na visa zaidi ya 23.6 milioni, kulingana na data iliyokusanywa na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.

Watu wapatao 15.3 milioni wamepata nafuu kufikia sasa.

Katika jaribio la kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo, mataifa kote duniani yamebuni mikakati thabiti ikiwemo kufunga shughuli nchini, kufunga viwanja vya ndege, kutangaza marufuku dhidi ya usafiri na kufunga mipaka yao kabisa.

Guterres alisema janga hilo limekuwa “tisho kuu” kwa mataifa tajiri yaliyoendelea lakini kwa “mataifa yanayoendelea, ni jambo la dharura, hasa kwa maeneo mengi ya visiwa na nchi za Kiafrika.”

Utalii kwa baaadhi ya mataifa unawakilisha zaidi ya asilimia 20 ya Kiwango cha Jumla cha Uzalishaji (GDP), kulingana na UN.

Mkuu wa Udadisi kuhusu soko na ushindani katika Shirika la Utalii Duniani, katika UN, Sandra Carvao, alisema Sh35 trilioni zilizopotezwa Januari hadi Mei, ni mara tatu zaidi ya kiasi kilichopotezwa mnamo 2009 katika kilele cha hali mbaya ya kifedha duniani.

Kulingana na taarifa za kisera, “mapato kutokana na utalii wa kuuza bidhaa katika mataifa ya kigeni huenda yakashuka kwa asilimia 1.5 hadi asilimia 2.8 ya GDP.”

Wito serikali ibuni sera ya kuruhusu ndege kupaa na kutua uwanja wa Moi bila vikwazo

Na WINNIE ATIENO

WAWEKEZAJI katika sekta ya utalii wametoa wito kwa serikali ikubali sera inayoruhusu ndege kutua na kupaa katika uwanja wa ndege wa Moi moja kwa moja bila vikwazo.

Wawekezaji hao walisema sera hizo zitasaidia kufufua sekta ya utalii ambayo inaendelea kuzorota kufuatia janga la corona.

Hata hivyo walisisitiza kuwa ndege za moja kwa moja uwanja huo zitasaidia kukuza sekta nyingi ikiwemo ile ya utalii, biashara na uchukuzi hivyo basi kufungua ajira miongoni mwa wakenya.

“Watu wengi hupenda usafiri bila changamoto, serikali inafaa kukubali sera inayoruhusu ndege kutua na kupaa katika uwanja wa ndege wa Moi moja kwa moja bila vikwazo” alisema Bw Husnain Noorani kwenye mahojiano.

Akiongea kwa niaba ya wawekezaji wa sekta ya utalii na wamiliki wa hoteli za kifahari, Bw Noorani aliitaka serikali kuhakikisha bodi ya utalii nchini inafadhiliwa ili kuuza soko la Kenya kama kituo maalum cha utalii duniani.

Alisema endapo serikali itakubali sera hiyo, ndege nyingi zitapaa na kutua katika uwanja wa kimataifa wa ndege ya Moi na kuimarisha uchukuzi, utalii na biashara.

Uwanja huo ndio mkubwa zaidi sehemu ya Pwani.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa muungano wa wawekezaji wa utalii Bw Ishpal Oberoi, alisema biashara katika uwanja huo wa ndege unaweza kupigwa jeki endapo ndege zitakuwa zinapaa na kutua moja kwa moja.

“Kama tunataka kukuza eneo la Pwani kama soko la utalii, ni sharti tuweke mikakati kabambe ikiwemo kuhakikisha ndege zinatua na kupaa bila vikwazo. Ndege za kimataifa kutoka bara Uropa, Amerika na hata Asia zinaweza kuleta wageni,” alisema.

Bw Oberoi ambaye pia ni mkurugenzi wa kampuni maarufu ya kusafirisha watalii ya Kuldip, alisema sekta hiyo imeanza kuimarika hasa maeneo ya Diani, Kilifi, na Maasai Mara.

Hata hivyo alisema kuna matumaini ya utalii kuimarika kaunti ya Mombasa wakati wa likizo ya Agosti.

Lakini Waziri wa Utalii na Wanyama wa porini Bw Najib Balala alisema serikali itaweka mikakati kuhakikisha ndege za kimataifa zinatua uwanja huo.

“Ni dhahiri uchumi wa utalii umezorota duniani na kila mtu anaogopa. Kwa mfano barani Uropa, hakuna ndege ya inayokwenda Marekani sababu ya wasiwasi dhidi ya kuambukizwa virusi hivi. Tunaweka mipango ili uwanja huo upate ndege za kimataifa. Tuna Rwanda Air, Turkish Airways, Qatar Airways na Ethiopian Airways lakini tunataka ndege nyingine zisafirishe wageni Mombasa ili kukuza sekta hiyo,” alisema kwenye mahojiano wiki iliyopita.

Hata hivyo aliwataka wakenya kupiga jeki utalii wa humu nchini ili kufufua uchumi.

Tembeleeni mbuga zetu, Balala ahimiza Wakenya

Na MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Utalii na Wanyamapori, Bw Najib Balala ametoa wito kwa Wakenya kutumia muda huu ambao ada zimepunguzwa kuzuru mbuga za wanyama.

Bw Balala aliwahimiza wananchi kufanya hivyo ili kufurahia urithi wa wanyamapori na kama njia ya kuchochea ukuaji uchumi.

Waziri, hata hivyo, aliwakumbusha wananchi wote kuzingatia kikamilifu masharti yaliyowekwa na Wizara ya Afya ya kuvalia barakoa, kudumisha umbali unaofaa na kuosha mikono au kutumia dawa za kuua viini mara kwa mara ili kukabiliana na janga la COVID-19.

Bw Balala alisema hayo jana alipopokea pikipiki 15 na tairi 180 za magari kama ufadhili kutoka kwa Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Mihadarati na Uhalifu (UNODC), katika makao makuu ya Huduma za Wanyamapori Nchini, Nairobi.

Alieleza kuwa ufadhili huo umejiri wakati ambapo KWS na taifa lote kwa jumla linakabiliana na madhara ya janga la COVID-19, ambalo linasambaratisha mifumo ya kiuchumi duniani.

Mataifa na mashirika yanakabiliwa na changamoto za kupungua kwa mapato na kufanya kuwa vigumu kununua vifaa vya kutosha vya oparesheni za kawaida,” alisema.

Zuio la usafiri kuingia au kuondoka kwa baadhi ya kaunti kuondolewa?

Na CHARLES WASONGA

HUENDA vikwazo wa usafiri vikaondolewa hivi karibuni licha ya ongezeko kubwa la idadi ya visa vya Covid-19 nchini katika kipindi cha mwezi mmoja sasa.

Waziri wa Usalama Fred Matiang’i alisema Jumatano kwamba Wakenya wanafaa kuzoea kuendelea na maisha yao ya kawaida kwani imebainika kuwa virusi vya corona havitatokomezwa hivi karibuni.

“Sasa ni wazi kuwa virusi vya corona vitasalia nasi kwa muda mrefu na sharti tujiandae kuishi navyo na tuendelee na maisha yetu ya kawaida japo kwa tahadhari huku juhudi za kufatuta chanjo zikiendelea,” Dkt Matiang’i akasema katika jumba la KICC.

Alisema hayo alipowahutubia wadau katika sekta ya utalii wakati wa kuzinduliwa kwa mwongozo wa kuzuia maambukizi ya Covid-19 katika sekta ya utalii.

Dkt Matiang’i aliandamana na Waziri wa Utalii Najib Balala pamoja na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe.

“Hatuwezi kunyamaza na kusubiri miujiza fulani itendeke kabla ya kurejelea maisha ya kawaida. Sharti tuanze kujifunze namna na kuanza kusafiri huku tukizingatia kanuni za afya zilizowekwa kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu,” akasema.

Kauli yake iliungwa mkono na Bw Mutahi ambaye alisema Wakenya wanapaswa kujizoesha na virusi vya corona “kwa sababu dalili zinaonyesha kuwa janga hili litaisha nasi kwa kipindi kirefu.”

Bw Balala alisema mwongozo huo ndio utatumika wakati wa kufufuliwa kwa utalii wa humu nchini serikali itakapoondoa marufuku dhidi ya safari za ndege.

“Sekta ya utalii iliathirika pakubwa baada ya serikali kuzima safari za ndege za kuingia na kutoka nchini kuanzia mwezi Aprili. Kwa hivyo, mwongozo huu utasaidia kufufua sekta hiyo kwa kuruhusu usafiri wa ndege humu nchini,” akaeleza.

Serikali ya kaunti ya Mombasa yabuni mkakati wa kuipiga jeki sekta ya utalii

Na WINNIE ATIENO

WAWEKEZAJI wa sekta ya utalii wamepata afueni baada ya serikali ya Mombasa kutangaza mpango mpya wa kuwanusuru dhidi ya ada wanazotozwa kufuatia hali ngumu ya uchumi.

Aidha serikali hiyo inayoongozwa na Gavana Hassan Joho imesema itawanusuru wafanyabiashara wanaohudumu katika sekta ya utalii ambayo ndiyo inapitia changamoto kufuatia ukosefu wa watalii.

Sekta hiyo imeathirika kufuatia kusitishwa kwa safari za ndege za kimataifa katika nchi nyingi duniani ili kuzuia maambukizi ya homa ya corona.

Nchini Kenya hoteli nyingi za hadhi zimefungwa na wafanyakazi kusimamishwa kazi huku wengine wakilazimika kuchukua likizo.

“Serikali ya Kaunti ya Mombasa imeweka mikakati kabambe kuhakikisha wawekezaji wa sekta ya utalii wanakombolewa kutoka changamoto za kibiashara,” akasema Bi Asha Abdi, kaimu afisa mkuu wa Biashara na Utalii.

Bi Abdi alisema mipango hiyo itawasaidia kukabiliana na hali ngumu ya maisha hususan kibiashara.

Alisema Bunge la Kaunti ya Mombasa litafanya mageuzi katika Mswada wa Fedha ili kuhakikisha ada wanazotozwa hususan hoteli na mikahawa zinapunguzwa maradufu.

Alisema pia itahakikisha wanafanya kampeni ya kusaka soko la utalii wa humu nchini raia waweze kuzuru mji wa kitalii wa Mombasa.

“Katika kampeni hiyo tunawaambia wale waliokuwa wanapania kuzuru Mombasa wasisitishe ratiba yao badala yake wabadilishe tu tarehe na mambo yatakaporejea sawa wamiminike mji huu,” alisema Bi Abdi.

Bi Asha Abdi kaimu afisa wa Utalii na Biashara akizungumzia mpango wa serikali ya Kaunti ya Mombasa kuwasaidia wawekezaji katika sekta ya utalii kuimarisha biashara zao. Picha/ Winnie Atieno

Hata hivyo, alifichua itachukua muda kabla sekta hiyo kuimarika tena kutokana na virusi vya corona.

Bi Abdi aliwahakikishia wawekezaji hao kwamba watawaunga mkono ili wafufue sekta hiyo.

Serikali ya kaunti ya Mombasa ilichukua jukumu la kusaidia zaidi ya maredeva 120 waliokuwa wakifanya shughuli za kusafirisha watalii sehemu kadha wa kadha ikiwemo mbuga za wanyama.

“Sekta hii iliathirika kabla hata ya Kenya kuthibitisha kisa cha kwanza cha corona ambapo tulipoteza wageni kutoka kwa soko letu kuu ikiwemo Amerika, Barani Asia na Italia ambazo ziliathiriwa pakubwa na janga hili,” alisema Bw Innocent Mugabe aliyekuwa akisimamia ugavi wa chakula hicho.

Amesema kaunti imechukua hatua hiyo kusaidia madereva hao ili wajimudu hadi pale mambo yatakapokuwa shwari.

Mikakati ipo kulainisha sekta ya utalii baada ya kunywea

Na WINNIE ATIENO

WIZARA ya Utalii imewahakikishia wawekezaji katika sekta ya utalii kwamba itaweka mikakati kufufua biashara zao.

Hii ni baada ya sekta hiyo kudorora kufuatia janga la Covid-19 ambalo lilisababisha hoteli nyingi za hadhi zifungwe na maelfu ya wafanyakazi kuachishwa kazi.

Kulingana na wizara hiyo, sekta hiyo kwa kawaida huwa imewaajiri takriban watu 500,000 moja kwa moja.

Lakini janga la Covid-19 limekuwa na athari hasi kwa utalii na inakadiriwa kwamba huenda ikazorota zaidi endapo ugonjwa huo hautomalizwa au kudhibitiwa.

Hata hivyo, serikali imewaahidi wawekezaji katika sekta hiyo kwamba wataendelea kujadiliana namna ya kufufua utalii ambao huchangia pato kubwa kwa uchumi wa Kenya.

“Wizara imeweka mikakati kufufua sekta ya utalii na kwa sasa tutaendelea na majadiliano na wawekezaji ili tupate mwafaka. Kama serikali tuna waahidi kuwapa uwezo n ahata mikopo ya kufufua biashara za utalii ili wakenya wasipoteze ajira,” amesema Katibu katika Wizara ya Utalii Bi Safina Kwekwe.

Kadhalika alisema serikali pia inajadili endapo wawekezaji was keta hiyo watapewa muda zaidi kulipa ushuru ili watumie fedha hizo kwenye biashara zao.

Alisema serikali inaanza kwa kuruhusu mikahawa kufungua kabla ya kujadili namna ya kufungua hoteli za kitalii.

Ugonjwa wa Covid-19 umesababisha serikali kuweka vikwazo vya usafiri sawia na ndege kusitisha usafiri.

Hata hivyo, Bi Kwekwe amewaahidi wawekezaji hao kwamba serikali inaweka mikakati kupunguza athari ya mikopo kwenye sekta hiyo akisisitiza kwamba mikakati hiyo inanuia kufufua utalii nchini.

“Tunafaa kuanza mjadala wa namna ya kuishi na hiki kirusi. Hivi ndio maisha yetu ya utalii yatakavyokuwa lakini tutaendelea kujadiliana na soko letu hususan lile ambalo hatujawai fikia ili kuwasihi waje kutemeba humu nchini,” alisema kwenye mjadala mtandao na wawekezaji wa utalii duniani walipokuwa wakizungumzia namna ya kufufua sekta hiyo.

COVID-19: Balala asema sekta ya utalii inapoteza Sh13bn kila mwezi

Na WINNIE ATIENO

WAZIRI wa Utalii Najib Balala amesema sekta hiyo inapoteza takribani Sh13 bilioni kila mwezi kufuatia mlipuko wa virusi vya corona duniani.

Akiongea kwenye mahojiano na runinga moja nchini, waziri Balala amesema ugonjwa wa Covid-19 umesababisha sekta hiyo kudorora.

“Sekta hii ni muhimu sana katika uchumi wetu ikizingatiwa inaajiri watu 1.6 milioni lakini sasa kila mwezi tunapoteza Sh13 bilioni. Zaidi ya asilimia 90 ya sekta hii imefungwa na tunapoteza ajira na ushuru,” akasema waziri.

Hata hivyo, ameelezea matumaini yake kwamba sekta hiyo itaimarika.

Amesema wawekezaji wa sekta ya utalii wanafaa kukumbatia utalii wa nyumbani ili kufufua sekta hiyo badala ya kushughulikia wageni wa kimataifa.

Amewashajiisha kuhakikisha wanafanya utalii wa humu nchini wa gharama nafuu kwa Wakenya.

“Tunafaa kujua wageni wetu wanataka nini ili tupunguze bei ya utalii wa humu nchini. Pia tunataka wageni watembee sehemu zote nchini ingawa changamoto zilizopo ni miundombinu duni,” akasema Bw Balala.

Waziri amesema baada ya jinamizi la mlipuko huu sekta hiyo itaimarika huku akiwataka wawekezaji kujitayarisha kupata wageni.

Amewataka wawekezaji wa mikahawa na hoteli kufuata maagizo ya Wizara ya Afya ili kukabiliana na ugonjwa huo.

Amesema hatua ya serikali kufungua baadhi ya mikahawa itasaidia kukuza uchumi.

Amesema licha ya ugonjwa huo kuyumbisha sekta ya utalii, Wakenya wanaweza kukabiliana nao.

“Kama mikahawa hiyo itafuata maagizo basi tutaendelea kupata wageni zaidi baadaye. Osha mikono na sabuni, vaa barakoa na uhakikishe unazingatia kuwa mbali kwa angalau mita chache baina yako na mwenzako,” amesema waziri huyo.

FORT JESUS: Historia, utamaduni, utalii, sanaa na utafiti

NA RICHARD MAOSI

Ngome ya Fort Jesus inasifika kote ulimwenguni kutokana na muundo wake wa kipekee, mbali na kuchangia kwa uchumi wa wakazi wengi wa pwani pamoja na kutengeneza nafasi nyingi za ajira miongoni mwa vijana.

Hata hivyo jambo lisilofahamika kwa wageni wengi wanaotua Mombasa ni kuwa, Fort Jesus ilitengenezwa na Waswahili halisi wa mwambao wa pwani na kuchukua umbo la binadamu ukiangalia kutoka mbali.

Kulingana na hifadhi ya kumbukumbu, wapwani walipata udhibiti wa ngome hii mwaka wa 1741 kabla ya mwingereza kutwaa hatamu 1895 enzi za ukoloni kama Protectorate of Kenya.

Mnamo mwaka wa 2001 UNESCO ikatoa kibali kwa Fort Jesus kama World Heritage Site na kuibuka kama mojawapo ya minara bora duniani iliyowahi kutengenezwa na kuhifadhiwa kwa muda mrefu.

Kuanzia hapo ndio mnara unaopokea wageni wengi zaidi katika ukanda wa Pwani na jumuiya ya Afrika Mashariki, na siku hizi ni makavazi ya kuhifadhi vyombo vya kale, michoro na miundo mbalimbali ya zana za kivita.

Taifa Leo Dijitali ilipiga kambi kubaini umuhimu wa ngome ya Fort Jesus kwa wakazi wa Pwani, hasa ikizingatiwa kuwa ni sehemu yenye utajiri mkubwa kwa utamaduni wa pwani, kuanzia chakula, mavazi, ufinyanzi , nyimbo na mashairi.

Mabaki ya wanyama wa majini

Mabaki ya nyangumi wa kiume aina ya Humback whale mrefu zaidi ulimwenguni aliyewahi kuishi, mwenye futi 48, yamehifadhiwa katika ngome ya Fort Jesus Mombasa na ni kivutio kikubwa cha watalii wa kigeni kutoka bara Asia na Uropa.

Huyu ni kiumbe ambaye anapatikana katika takriban bahari zote ulimwenguni, na anafahamika kutokana na maumbile ya kumiliki nundu,pamoja na uwezo wake wa kuimba, nyimbo za kawaida.

Humback whale hujumuika na nyangumi wenzake kwa makundi wakati wa kuwinda na kutafuta chakula majini, huku wakinengua densi na kuwavutia watalii wengi wanaotembea pwani ya Kenya kufurahia, mbwembwe za samaki hawa ambao husafiri kilomita nyingi.

Kwa mujibu wa akailojia ya pwani inayochungza na kudadisi mabaki ya viumbe wa kale,mabaki ya humback whale yalipatikana mnamo 1992 katika ufuo wa bahari Hindi akiwa amefariki.

Mabaki yenyewe yalipatikana katika sehemu ya Ungwana Bay Kipini katika kaunti ya Tana River ingawa chanzo cha kifo chake hakikubainika moja kwa moja, mpka wa leo.

Inasemekana kuwa umri wa nyangumi wa sampuli hii unaweza kuwa baina ya miaka 19-24.

Nyumba ya kihistoria ya Omani

Disemba tarehe 13 1698 ni mahali hapa ambapo waomani walishinda wareno na kuikomboa ngome ya Fort Jesus,Hatimaye waomani walijitahidi na kuimarisha hadhi ya ngome kwa kuzirefusha kuta, kila upande ili kuikinga ngome dhidi ya mashambulizi ya adui.

Walichimba mahandaki ya kujificha pamoja na kisima cha kuteka maji ya kunywa ,wakati wa kipindi cha muingereza 1980 nyumba hii ilirekebishwa na kufanywa kituo cha maonyesho.

Baadaye 2017 wizara ya michezo kupitia wizara ya Usultani wa Uomani walirekebisha na kuendeleza sehemu maalum kuwa ukumbi wa maonyesho, kwa watalii na wenyeji.

Hii iliwasaidia vijana wenge wanaofanya kazi za sanaa kujipatia ajira kama waelekezaji na walimu wa historia ndefu ya wapwani hususan Waswahili.

Sanaa

Taifa Leo Dijitali ilikutana na kijana Fadhili Swaleh ambaye ni mchoraji mahiri wa vibonzo na mabango ya kubandika ukutani, na amekuwa akifanya kazi hii tangu mwaka wa 2014.

Anasema alianza kazi yenyewe alipogundua alikuwa na kipaji cha kuchora na kuibua picha ya hali halisi ya mtu wa kawaida kwa watalii na wenyeji wa pwani ambao humiminika mara kwa mara katika Ngome ya Fort Jesus.

Yaonekana kazi yake inaendelea kupata mashiko kutokana na idadi kubwa ya wageni wanaosimama katika kibanda chake kufurahia kazi yake ya ubunifu, wengi wao wakiwa ni wanafunzi wa shule za msingi na upili.

Aidha amekuwa mchoraji wa kazi za nyumbani na hata kwenye matatu akiamini kuwa kipaji kama kazi nyingineyo kinalipa muradi tu msanii ajue kuwasilisha ujumbe wake kwa umma.

Alisema kuwa yeye hutumia kalamu ya wino, makaratasi, rangi ya majimaji na ile ya kupaka ukutani akiwa katika karakana yake.

Aliongezea kuwa mnara huo uliotengenezwa baina ya 1593 -1596 na wareno una historia pana ambapo ulilenga kuwakinga wareno dhidi ya maadui wakati wa kivita.

Hatimaye Fort Jesus iliingia katika orodha ya turadhi za kitaiifa manamo 2001 kupitia UNESCO World Heritage Committe.

Msanii anaweza kuibua michoro ya kuhamasisha, kuburudisha na kuzindua kwa sababu mara nyingi anatumia malighafi kutoka kwenye mazingira ya jamii halisia kama vile vipande vya miti mashina na kadhalika.

Utafiti

Katika mahojiano yake na Runinga ya NTV Fatma Twahir, mtaalamu wa miundo misingi anasema ngome ya Fort Jesus imekuwa ikisimama kwa miaka 420 bila kitu chochote kubadilika.

Anasema ni kumbukumbu ya kujivunia kwa sababu wakati wa shule wanafunzi wengi hufika hapa kujifundisha mambo mengi hasa yale yanayohusiana na somo la historia, Jiografia na somo la Kiswahili.

Anasema kuwa wamekuwa wakishirikiana na jamii ya waswahili kuwasaidia kufanya kazi ndani ya ngome kwa kuwafundisha namna ya kuwaelekeza wageni.

Alieleza kuwa kuna walimu wanaowafundisha wenyeji mambo ya ekolojia ya kisayansi ili waweze kuwa na njia ya kupambanua mambo yanahohitaji maelezo ya kitaaluma.

Aidha wamekuwa wakiwafundisha utamaduni wa jamii zingine kama vile Omani kwa kufananisha maisha yao ya kale na yale ya kisasa ambapo utandawazi umekuja na mabadiliko mengi kwa kizazi cha leo.

Wasomi vilevile wamekuwa wakipata nafasi ya kuendeleza taaluma zao katika kiwango cha juu kama vile shahada ya uzamili na uzamifu , hususan wale wanaojikita katika maswala na turadhi za waswahili.

Vilevile wanafunzi wanaosomea taaluma za Hospitality wamekuwa wakipata fursa ya kufanya majaribio baada ya kutimiza kozi zao katika ngome ya Fort Jesus.

“Maeneo mengine ya kuvutia ni kama vile Shimoni walipohifadhiwa waumwa, Jumba la Mtwana, Gedi na Rabai ,”akasema.

Alieleza kuwa ni ngome ambayo imedumu licha ya nyakati mbalimbali kubadilika kuanzia enzi za wakoloni mpaka kizazi cha leo.

Ombi

Joy Mwangeka muuzaji wa shanga katika ngome ya Fort Jesus anasema ni sehemu inayofaa kuboreshwa ili isipoteza thamani yake kwa wakazi wa pwani kwa ujumla.

Akiwa mfanyibiashara anaona kuwa serikali ya kaunti inaweza kupaka rangi na kuziba baadhi ya nyufa ambazo zimeanza kutokea katika sehemu za mjengo huu wa kale.

“Ingawa Fort Jesus inatoa taswira nzuri ukiangalia bahari na upepo mtulivu, vijana wengi bado sio wabunifu vya kutosha kujifaidisha na ngome hii,”akasema.

Alieleza kuwa utalii katika Pwani ya Kenya umekuwa ukiwasaidia wakazi wengi kupigana na janga la umaskini, hasa kwa mapato ya nje kuinua uchumi wa kitaifa.

Qatar Airways yazindua safari ya ziada kutoka Doha hadi Mombasa

Na MAGDALENE WANJA

IDADI ya watalii nchini inatarajiwa kuongezeka hii ikiwa ni baada ya shirika la Qatar Airways kuzindua safari (trip) ya ziada kutoka Doha kwenda Mombasa.

Safari hii inafikisha tano idadi ya safari za kila wiki katika jiji la Mombasa kutoka Doha na inatarajiwa kuwaleta watalii wakati wa msimu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

Safari hiyo inatarajiwa kuanza Desemba 20, 2019, hadi Machi 27, 2020.

Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Akbar Al Baker alisema kuwa kuzinduliwa kwa safari hiyo ni mojawapo ya njia zitakazosaidia katika kudumisha uhusiano kati ya Kenya na Qatar na kutasaidia katika kuongeza nafasi za kazi katika maeneo ya Pwani mwa Kenya.

“Kufikia sasa, tuna zaidi ya safari 160 katika sehemu mbalimbali duniani na tunatarajia uhusiano mwema zaidi na nchi ya Kenya,” akasema Bw Al Baker katika taarifa.

Aliongeza kuwa shirika la Qatar Airways litahudumu safari hiyo ya ziada kwa kutumia ndege aina ya Airbus A320 ambayo ina viti 12 katika sehemu ya abiria wa kiwango cha business class na viti 120 katika sehemu ya economy class.

“Shirika hili litakuwa na jumla ya safari 26 kila wiki kati ya Doha na Kenya, zikiwemo tatu za kila siku kutoka Doha hadi Nairobi,” akasema Bw Al Baker.

Pwani mwa Kenya kuna vivutio vingi vya watalii hasa Old Town, Fort Jesus, Haller Park na Mbuga ya Kitaifa ya Mombasa Marine.

Kenya kutuma ombi kuandaa kongamano la UN kuhusu utalii wa kimataifa

Na MAGDALENE WANJA

KENYA ni miongoni mwa nchi ambazo zimeonyesha nia ya kuwa mwenyeji wa kongamano la baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu Utalii wa Kimataifa ambalo litafanyika mwaka wa 2021.

Kulingana na Waziri wa Utalii Najib Balala, Kenya itawasilisha maombi yake rasmi wiki hii.

Waziri Balala alisema kuwa nchi ya Kenya imeonyesha ukomavu katika kuandaa hafla za kimataifa na hii inaiweka katika nafasi nzuri ya kuandaa mkutano huo.

Mataifa mengine yaliyoonyesha nia hiyo ni Morocco na Ufilipino.

“Tutawasilisha ombi letu la kuandaa kongamano hilo na tutakuwa nchi ya kwanza ya Afrika Mashariki kuandaa mkutano huo iwapo azma yetu itafua dafu,” alisema Bw Balala.

Ikifaulu, nchi hii bila shaka itapata faida kubwa kutokana na biashara za kigeni kwani idadi kubwa ya watalii wanatarajiwa kuzuru kipindi hicho.

“Hii itakuwa hatua kubwa katika kufungua njia kwa nchi ya Kenya kuandaa mikutano ya haiba kama hii siku zijazo,” akasema waziri.

Wizara yawataka watalii waepuke mitego ya matapeli mitandaoni

Na MAGDALENE WANJA

WIZARA ya Utalii na Wanyamapori imeanzisha uchunguzi kuhusu ripoti za watu ambao wanawalaghai watalii mitandaoni.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotiwa sahihi na mkurugenzi wa mawasiliano wa wizara hiyo Bw Mulei Muia, kuna visa vingi vya ulaghai ambavyo vimeripotiwa katika ofisi za wizara hiyo.

Kulingana na habari hiyo, walaghai hao hawana kibali cha kufanya kazi wala ofisi zozote.

“Utafiti wa hivi punde unaonyesha kwamba wahudumu hao walaghai hawana leseni kutoka kwa mamlaka ya kudhibiti shughuli za utalii (TRA) na wala ya kutoka kwa muungano wa wahudumu wa kitalii wa Association of Tour Operators (Kato),” inasema taarifa hiyo.

Habari hiyo pia inasema kuwa uchunguzi tayari umeanzishwa na washikadau mbalimbali katika sekta ya utalii.

“Hata hivyo, tunawataka watalii wote wa humu nchini na wale wa kutoka nje kuwa makini sana wanapotumia mitandao kutafuta sehemu za kutembelea ili kujikinga dhidi ya walaghai. Tunawashauri kutembelea tovuti maalum kama vile htts://www.tourismauthority.go.ke.”

Haya yanajiri siku mbili baada ya habari zilizofichua jinsi watalii wengi wanaotembea humu nchini hujipata taabani baada ya kulaghaiwa mitandaoni.

Waziri wa Utalii na Wanyamapori ni Najib Balala (pichani).

Uchafuzi wa maziwa ya Bonde la Ufa unavyoathiri utalii

NA RICHARD MAOSI

SHIRIKA la Huduma za Wanyamapori nchini (KWS) mwaka 2018 ilitoa ripoti yenye utata iliyosema kuwa kiwango cha maji katika ziwa Nakuru kilikuwa kimepanda na kuzamisha baadhi ya mijengo.

Aidha waziri wa utalii Najib Balala miezi miwili iliyopita, alipozuru mbuga ya wanyama ya Ziwa Nakuru, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema ziwa hilo lilikuwa limechakaa na kupoteza hadhi yake, kinyume na siku za mbeleni lilipokuwa na uhai.

Ingawa washikadau wamepinga mawazo haya, wanasayansi kwa upande mwingine wamefichua kuwa maziwa yanayopatikana katika Bonde la Ufa yanaangamia kutokana na uchafuzi wa mikondo ya maji inayoelekea kwenye mbuga za wanyama na maziwa.

Mwanasayansi Daktari Silas Simiyu anasema hili limechangiwa na ongezeko la idadi ya watu, wanaoishi kandokando ya maziwa makuu na mito inayobeba maji kuelekea mbuga ya wanyama ya Ziwa Nakuru.

Mbuga ya ziwa Nakuru ni kivutio cha The Big Five yaani simba, ndovu, vifaru, chui na duma. Isitoshe, ni mbuga ya kipekee Afrika Mashariki yenye vifaru weupe ambao wameadimika kutokana na uwindaji haramu.

Kumbukumbu za miaka miwili iliyopita, tangu watu tano waangamie katika ziwa Nakuru baada ya mkasa wa ndege kutumbukia ziwa Nakuru,hali ya uchafuzi haionekani kukoma kwa sababu ya maji taka yanayoingia ziwani.

Operesheni ya kutafuta miili ya walioaga dunia wakati huo, iliwaachia wazamiaji maradhi ya ngozi ambayo yamechukua muda mrefu kutibika,jambo hili likiakisi hali halisi ya kiwango cha uchafuzi katika ziwa Nakuru.

Shughuli ya uokozi ilichukua muda mrefu ikiaminika kuwa baadhi ya wazamiaji wa majini walihofia kuingia ndani ya ziwa, ili wasipate madhara ya ngozi.

Ndege za kijeshi ndizo zilitumika kutafuta mabaki ya manusura,juhudi za wazamiaji na meli zilipokosa kuzaa matunda wiki moja hatimaye.

Miaka kumi iliyopita maeneo yanayozunguka ziwa Nakuru hayakuwa na makazi rasmi ya watu, lakini watu walianza kujenga ndiposa mitaa kama vile Rhonda,Langalanga,Kivumbini na Madaraka ikatokea.

“Baadae mitaa karibu na Lake view ilianza kukua na kukaribia ziwa Nakuru,kwani serikali husika haikutilia maanani mpangilio wa ukuaji wa mji,”alieleza Simiyu.

Anasema kwa sababu ya miundo mbinu duni,serikali ya kaunti ya Nakuru ilishindwa kutekeleza wajibu wake wa kuzoa taka mitaani ipasavyo,huku mirundiko inayobaki ikisombwa na kuingia kwenye mitaro ya maji.

Kulingana naye ongezeko la idadi ya watu umesababisha ukataji miti kiholela na kusababisha mmomonyoko wa udongo unaochafua maji,”akasema Silas Simiyu.

Alieleza kuwa mchanganyiko wa kemikali kutoka kwenye viwanda,pamoja na maji chafu yanayotokea kwenye makazi ya watu ndio jinamizi linalokodolea macho ziwa Nakuru,ikionekana kuwa swala hili haliwezi kuepukika,

Changamoto nyingine inayokumba ziwa Nakuru ni ukaribu wake na ziwa Elementaita ambayo ina kiwango kikubwa cha maji ya chumvi.

Wakati wa joto jingi mvua hunyesha na kuongeza idadi ya chumvi ndani ya ziwa Nakuru hali ambayo ni hatari kwa maisha ya ndege na wanyama wanaotegemea ziwa Nakuru.

Hali hiyo hufanya samaki kuhamia pembeni mwa bahari na kutaga mayai ambayo hayawezi kuangua kwa wakati, kutokana na msukosuko wa maji.

Aidha Simiyu alieleza idadi ya flamingo wanaopatikana katika ziwa Nakuru imepungua kutoka milioni moja hadi famingo 200 tu,katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

“Ndege wengi walipoteza maisha na waliobaki kuhamia ziwa Bogoria katika juhudi za kutafuta mazingira tulivu,”akasema.

Mbali na makazi ya watu kulaumiwa kwa sababu ya kumwaga maji taka yanayoingia ziwani,wenye viwanda vya kutengeneza bidhaa za plastiki pia hawajasazwa kwa kukosa njia mbadala ya kutupa bidhaa zao.,

Mtaalam wa mazingira James Wakiba anasema ingawa UNESCO inatambua ziwa Nakuru kama eneo lenye chemichemi za maji na kivutio cha watalii,kiwango cha uchafuzi kimepoteza hadhi yake.

Katika matembezi yake kwenye ziwa Nakuru, aligundua kuna mito midogo 26 inayoingiza maji chafu ndani ya ziwa Nakuru sita yazo ikiwa ni kutoka kwenye viwanda.

Wakiba anaona kuwa kuna mito zaidi ambayo bado haijatambuliwa,lakini ameachia jukumu hilo KWS tawi la Nakuru, kupekua mazingira ya mbuga ya ziwa Nakuru kwa kina.

Anasema vianzo vya maji pia vipo hatarini ,ishara tosha kutokana na mmomonyoko wa udongo unaoteremsha mchanga kutoka kwenye milima ya Dundori kupitia eneo la Lanet na baadae ziwa Nakuru.

Mto Makalia,Nderit na Njoro ndiyo ilikuwa ikibeba maji safi hadi kwenye ziwa Nakuru lakini kufikia wakati wa upekuzi wa Taifa dijitali mito hiyo imekauka, labda msimu huu wa mvua ndio maji kidogo yanatiririka.

Kwa upande mwingine baadhi ya mito inayotoa maji safi kama vile Rongai, imefungiwa na wawekezaji wa kibinafsi wanaokuza maua.

Licha ya kutolewa marufuku kuhusu utumiaji wa mifuko ya plastiki,inaonekana kuwa idadi kubwa ya wanyama pori wanaoangamia katika ziwa Nakuru ni kwa sababu ya kutafuna mifuko ya plastiki inayoingia mbugani.

“Idadi kubwa ya wanyama wanaopoteza maisha ni pundamilia,swara,viboko,nyani na flamingo wanaopigania kunywa maji kwenye mito inayoingia ndani ya ziwa Nakuru,”akasema.

Mnamo 2016 Christine Mwinzi anasema takriban kilo 540 ya taka zilikuwa zikizolewa kila siku kutoka ndani ya Ziwa Nakuru.

2019 Taifa dijitali ilishuhudia usimamizi wa uzoaji taka kutoka ziwa Nakuru ambapo tani 6 zilitolewa kwa siku mbili.Usimamizi wa mbuga ya Nakuru uliajiri jumla ya vibarua 8 waliozoa taka na kupakia ndani ya malori.

” Wanyama wanaokaa ndani ya ziwa hunywa maji haya,hawana njia mbadala na ndio sababu huenda baadhi ya wanyama wamekuwa wakiugua na hata kufa mkurupuko wa maradhi yanapotokea,”akasema

Ziwa la pili lililopata pigo ni ziwa Naivasha kilomita chache kutoka Nakuru, ambalo hutegemewa kwa shughui za uvuvi na utalii kwa sababu ya maji yake safi.

Mbali na ziwa hili kuwa mojawapo wa maziwa makubwa katika bonde la ufa, washikadau wanasema huenda ziwa Naivasha lisiwe la manufaa yeyote kwa wakazi siku za mbeleni.

Mbali na uvuvi kupita kiasi baadhi ya watu wameanza kuweka makazi yao kando ya ziwa hilo kwa sababu ya uwekezaji katika ukulima na upungufu wa kipande cha ardhi.

Kwa kipindi cha miaka miwili kiwango cha samaki wanaovuliwa kutoka ziwa Naivasha kimepungua kutoka takriban tani 1,180 hadi tani 964.

Jambo hili lilifanya onyo kali kutolewa na serikali dhidi ya wavuvi wanaofanya shughuli zao wakati wa giza.

Mkurugenzi anayesimamia matumizi ya maji katika ziwa Naivasha Enock Kiminta anasema uvuvi haramu ndio chanzo cha ushukaji wa kiwango cha maji katika ziwa Naivasha.

Pili ongezeko la magugu maji ndani ya ziwa Naivasha ni jambo linalofanya samaki kukosa virutubisho na oksijeni.Wengi wa samaki hapa wamehamia maji ya kina kirefu wasipatikane kwa urahisi.

Mbwana Mbogo Kamau mtaalam wa mazingira anasema ongezeko la shuguli za binadamu kando ya mito pia ina mchango katika upatikanaji wa magugu katika ziwa Naivasha.

Kiminta anasema wizara ya mazingira kwa ushirikiano na NEMA zina wakati mgumu kukabili maji taka yanayoingia kwenye mito hususan msimu wa mvua.

Ziwa Nakuru limejaribu kuweka kichujio kabla ya maji kuingia kwenye mbuga lakini hali hii haijasaidia kitu kwa sababu mifuko ya plastiki inapoziba mikondo ya maji,mchanga hupenya na kuingia ndani ya mbuga..

Kenya yapoteza watalii 2,000 wakihofia usalama

Na Winnie Atieno

KENYA imepoteza watalii 2,000 wa kimataifa baada ya meli mbili za kifahari, zilizokuwa zitie nan’ga katika Bandari ya Mombasa, kubadilisha mkondo na kuelekea nchi nyingine.

Meli hizo ambazo huleta raia wa Ulaya kuzuru mbuga za wanyama nchini Kenya zilibadilisha mkondo kufuatia onyo la Amerika kwamba kutakuwa na shambulio la kigaidi.

Waziri wa Utalii, Najib Balala alielezea ghadhabu yake kufuatia hatua hiyo.

“Nitawasiliana na wizara ya mambo ya kigeni kuhusiana na suala hili. Onyo la Amerika limeleta taharuki na hata meli mbili za watalii kubadilisha mkondo.”

Akiongea kwenye warsha na wabunge katika hoteli ya Whitesands huko Mombasa, Bw Balala alisema meli hizo zingeleta Zaidi ya wageni 2000.

Bw Balala alisema onyo hilo litapelekea kuharibika kwa biashara za wakneya na uchumi wa taifa.

Alisema baada ya shambulizi la kigaidi huko Nairobi katika mkahawa wa DusitD2 mnamo Januari 15, alikutana na mabalozi wa nchi za kigeni ikiwemo ile ya Marekani na wakakubaliana dhidi ya kutoa onyo la usafiri kwa raia wao.

“Tulikubaliana kuwa ugaidi si swala la nchi hii bali jinamizi la ulimwengu, lazima tushirikiane. . Onyo la Marekani kwa raia wake linanuia kuwataka wawe waangalifu na makini kufuatia tishio la shambulizi la kigaidi,” Bw Balala alisisitiza.

Waziri huyo alisema vikosi vya usalama nchini vimeimarisha usalama kwa watalii na raia wake huku akisisitiza kuwa kuna usalama wa kutosha.

Aliwataka mabalozi kushirikiana na serikali kabla ya kutoa onyo la usafiri.

“Msifanya kuwe na wasiwasi, Kenya iko salama na tumekabiliana na tishio lolote,” Bw Balala alisisitiza.

Jumapili meli ya watalii ya, MS Nautica ambayo ilinuiwa kutia nang’a katika bandari ya Mombasa ilielekea Ushelisheli kufuatia onyo la Marekani.

Sekta ya utalii ilipata pigo kubwa kufuatia onyo hilo.

MENENGAI CRATER: Mali asili inayofumbiwa macho na serikali

NA RICHARD MAOSI

KULINGANA na utafiti uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (UNEP), kati ya miaka ya 1990-2010 Kenya imekuwa ikipoteza asilimia 0.32 ya misitu kila mwaka, kutokana na shughuli za kibinadamu.

Hali yenyewe imeendelea kupunguza kiwango cha maliasili, hasa pale tunaposhuhudia miti iliyokomaa ikigeuzwa majivu kwa muda mfupi.

Japo serikali imejaribu kila mbinu kuweka kanuni imara za kudhibiti ukataji miti na kutoa uhamasisho kwa jamii, bado kuna mashaka makuu.

Msitu wa Menengai Crater ukiteketea na kuhatarisha maisha ya wakazi wanaozunguka msitu huo. Picha/Richard Maosi

Kubana vibali ama kuwakamata wahalifu wanaochoma makaa porini haitoshi. Huenda labda maafisa wa misitu watalazimika kubadilisha mbinu za kushika doria.

Taifa Leo Dijitali ilipozuru msitu wa Menengai Crater, ilipata maliasili inayoelekea kuangamia baada ya ushirikiano kati ya raia na maafisa wa usalama kuulinda kutozaa matunda.

Msitu wa Menengai katika Kaunti ya Nakuru unazungukwa na wakazi wanaotegemea bidhaa zinazotokana na miti kama vile mbao, makaa na asali. Ni mlima wenye kasoko (volkano) kileleni.

Daniel Ole Kuntai (kulia) mfugaji wa kuhamahama kutoka Gilgil akielezea masaibu anayopitia akitafutia lishe mifugo wake tarehe 2, Februari 2019. Picha/Richard Maosi

Unapatikana mwendo wa kilomita 10 hivi kutoka mjini Nakuru karibu na eneo la Milimani, mkabala na Olo Rongai katika upande wa Magharibi .

Vilevile, kuna baadhi ya miradi ya serikali iliyostawishwa ndani ya Menengai, mojawapo ikiwa ni mitambo ya kutuma mawimbi ya mawasiliano kwa vituo vya redio na televisheni, na pia uzalisha kawi ya mvuke (Geothermal Power).

Licha ya kutumika kama kituo cha utalii, wageni wengi humiminika hapa kutazama spishi mbalimbali za mimea , wanyama na ndege ingawa taswira ya Menengai Crater imechakaa kinyume na zamani iliposheheni uzuri wa rangi ya kijani kibichi.

Mwendeshaji bodaboda akisafirisha makaa kuelekea eneo la Subukia. Biashara hii imenoga mjini Nakuru. Picha/Richard Maosi.

Pametengwa sehemu maalum ya wageni kubarizi ili kufurahia mazingira tulivu yasiyokuwa na shughuli nyingi kila siku za wiki, lakini hata hivyo bali na uzuri wote huu visa vya moto vimekuwa ni jinamizi la kila mwaka.

Mnamo 2015, ekari 400,000 ya miti iliteketea .Waziri wa Mazingira kaunti ya Nakuru Richard Rop alisema moto huo ulisababishwa na kiangazi pamoja na upepo mkali uliosambaza moto katika sehemu kubwa.

Changamoto kubwa ikiwa ni ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kuzima moto.

Mradi wa serikali wa kuzalisha kawi ya mvuke unaoendeshwa ndani ya msitu wa Menengai. Picha/Richard Maosi

Kulingana na wakazi wanaoishi karibu na msitu wa Menengai, serikali imekuwa ikifumbia macho jambo hili huku baadhi ya watu wakipendekeza mitaro ichimbwe ili kuzuia moto kuenea.

Upekuzi wa Taifa Leo Dijitali kwa mbali ulishuhudia moshi ukifuka angani kutoka kwenye vichaka, ila hatungeweza kufika katika sehemu yenyewe kutokana na miinuko ya ardhi.

Allan Kibor, mkazi wa Crater anasema moto umekuwa ukizuka kutokana na mambo madogo kama vile uvutaji sigara.

Ndege la Shirika la Huduma za Misitu (Kenya Forest Service) lilipotua kudhibiti hali ya moto. Picha/Richard Maosi

Baadhi ya wakazi wamekuwa wakipuuza na kutupa sigara kabla haijazima kwenye nyasi zilizokauka bila kufahamu ingeleta madhara makubwa baadaye.

Pia analaumu kampuni ya GDC inayozalisha kawi ya umeme , kwa kutumia vilipuzi akiamini huenda vimekuwa vikichochea na kuanzisha cheche zo moto .

Uchomaji msitu wa Menengai umekuwa ukifanya mifugo kukosa malisho, Wafugaji wakilazimika kutembea mwendo mrefu kutafutia ng’ombe wao nyasi na maji.

Afisa wa kulinda misitu akiwa kazini. Picha/Richard Maosi

“Endapo hali itaendelea kuwa hivi miaka nenda miaka rudi sehemu hii ambayo wakati mmoja ilisheheni miti itakuja kugeuka jangwa,”alisema.

Charles Kemita ni mmiliki wa hoteli ya kitalii ndani ya Menengai Crater kwa zaidi ya mwongo mmoja sasa.

Anasema amekuwa akishirikiana na jamii kwa mambo mengi hasa ijapo nafasi ya kutoa ajira kwa vijana wanaoishi karibu na Menengai Crater.

Wakazi wenye wasiwasi wakitazama makazi yao yaliyoteketezwa na moto katika msitu wa Menengai. Picha/Richard Maosi

Kinachomtia hofu ni kuwa biashara imeshuka maana watalii wengi hawatembelei eneo hili la kivutio kama awali .

“Mikahawa iliyokuwa ikisheheni wageni sasa imebaki kuwa mahame,”alisema.

Badala yake wageni wamenza kuzuru sehemu nyingine kama vile Nyahururu,Naivasha na Baringo kujivinjari.

Utalii ulivyokwamishwa na moto unao enea kwa haraka na kuwafanya wageni kujivinjari kwingine. Picha/Richard Maosi

“Hali ya kiangazi pamoja na familia za wafugaji wa kuhamahama ndio chanzo cha masaibu yetu, kila mwaka moto unapozuka. Japo idara husika inafahamu hili hawajachukua hatua yoyote,” alisema.

Fred Ogombe anayesimamia msitu wa Mau , alitupambanulia kwa kina hali halisi akisema kila mwaka msitu wa Menengai umekuwa ukishika moto.

“Japo ni vigumu kubaini chanzo moja kwa moja, wenyeji ndio wa kulaumu kwani wamekuwa wakiwaficha wahalifu wanaofanya biashara ya kuuza makaa,” alisema.

Sehemu ya msitu wa Menengai iliyochomeka. Picha/ Richard Maosi

Hata hivyo anasifia juhudi za serikali ya kaunti kuwasaidia wakazi kuzima moto kila mara mkasa unapotokea.

Anaamini wamekuwa nguzo muhimu sio tu kuwashauri bali pia kuchukua hatua ya haraka mkasa wa moto ukiripotiwa .

Kaunti imekuwa ikitoa magari na ndege kufikia sehemu zisizofikika ili kudhibiti makali ya moto ambao umekuwa ukiwalemea wakazi kuuzima.

Maafisa wa KFS wakitoka kutathmini kiwango cha uharibifu uliosababishwa na moto. Picha/ Richard Maosi

Jambo hili lilifanya waziri wa mazingira wa kitaifa Keriako Tobiko kufanya ziara ya ghafla kwenye msitu wa Menengai mnamo Februari 2,2019 kutathmini hali.

Akishirikiana na maafisa wa misitu(Kenya Forest Service)walitembelea msitu wa Menengai na baadaye kuzungumza na wakazi.

Ilibainika moto umekuwa ukisababishwa na wachomaji makaa ambao wamefanya misitu kuwa makao yao ya muda.

Maafisa wa KFS wasemezana baada ya kuzima moto. Picha/ Richard Maosi

Kando na kupatiwa ulinzi na maafisa wa usalama, wao huchoma makaa peupe.

Wakazi wanasema biashara ya kuuza makaa ilikuwa imenoga katika eneo la Subukia, Solai na Lanet.

Aidha wazima moto wamekuwa wakichukua muda mrefu kufika kwenye eneo la mkasa kutokana na mabonde ya kina kirefu.

Tobiko alihimiza vijana kushirikiana na viongozi wa mtaa kuanzisha mchakato wa kupanda miti tano kila mmoja ili kufikisha asilimia 10 inayohitajika.

Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko akitathmini hali katika msitu wa Menengai ambao uliteketea siku nne mfulululizo Februari 2019. Picha/Richard Maosi

“Serikali haitalegeza vita dhidi ya ukataji miti kiholela, kwa sababu ndio chanzo cha mito na mvua”aliongeza

Misitu mingine iliyo kwenye hatari ya kuangamia ni kama vile Narasha (Baringo), Ndoinet, Olposimoru , Sabatia, Eburru (Nakuru), Londiani (Kericho) na Olrabel (Baringo).

“Baadhi ya misitu inateketezwa na wafugaji ambao hukita kambi ndani ya misitu wakisaka lishe kwa mifugo yao,” alisema.

Baadhi ya wafugaji waliafiki maelezo haya wakisema wamekuwa wakigombania raslimali na wachomaji makaa.

Sehemu kubwa ya msitu iliyochomeka. Picha/ Richard Maosi

“Wakati mwingine vita huzuka pindi maelewano yanapokosekana miongoni mwetu kwa sababu ya uhaba wa nyasi na majani ya miti,” Daniel Ole Kuntai ambaye ni mfugaji alisema.

Anaeleza tangu 2014 amekuwa akifunga safari kutoka kaunti ndogo ya Gilgil, kusaka lishe kwa mifugo wake na hangekubali watu wachache wenye tamaa za kujitajirisha wamfanye ataabike.

Mnamo 2018 Bw Tobiko alihimiza wakenya milioni 45 kupanda miti mitano kila mmoja lakini hilo halijashuhudiwa kufanyika mpaka sasa.

Hili linajiri baada ya wakenya kushuhudia siasa kuingizwa katika swala la kuhifadhi misitu.Kila mara watu walipofurushwa kutoka msituni ilisemekana ni jamii fulani ilikuwa ikilengwa.

Muafaka umeimarisha utalii nchini – Ripoti

Na BERNARDINE MUTANU

Sekta ya utalii imeimarika kwa asilimia kubwa ikilinganishwa na mwaka wa 2017.

Mapato katika sekta hiyo yaliimarika kwa asilimia 31.2 mwaka wa 2018 kulingana na data mpya kutoka kwa Wizara ya Utalii na Wanyamapori.

Wizara hiyo ilitangaza mapato ya Sh157.38 bilioni kutoka Sh119.0 bilioni mwaka wa 2017. Kulingana na serikali, mapato hayo yaliimarika kutokana na kuimarika kwa usalama nchini na hatua ya serikali kudhibiti ugaidi.

Pia hali dhabiti ya kisiasa baada ya muafaka imepelekea kuongezeka kwa watalii nchini, ilisema wizara hiyo.

Sekta hiyo imeshuhudia ongezeko la asilimia 68 ya watalii kutoka nje ya nchi hadi 2.025 milioni kutoka 1.46 milioni mwaka wa 2017.

Utalii wa humu nchini uliimarika kwa asilimia 9.03 kutoka siku 3.64 hadi 3.97 kiwango cha vitanda vilivyohifadhiwa.

Idadi ya watalii kutoka Afrika ilipita watalii kutoka kwingineko kwa asilimia 40.76 (825,489).

Watalii kutoka Tanzania walikuwa ni 212,216 ilhali wale kutoka Uganda walikuwa 204,082.

Waliotoka Uropa walikuwa 611,969 au asilimia 30.33 (Ujerumani 48,189 Ufaransa, Uhispania 25,027 na Sweden 22,028).

Watalii kutoka Marekani nchi walikuwa ni asilimia 11.12 au 225,157.

Sarafu mpya zitastawisha utalii na kulinda wanyamapori – Balala

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Utalii na Wanyama Pori Najib Balala amepongeza hatua ya serikali ya kuweka picha za wanyamapori katika sarafu mpya zilizozinduliwa Jumanne.

Kwenye taarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari mnamo Jumatano Waziri Balala alisema sarafu hizo mpya zilizozinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta “zinasheheni thamani ya Wakenya na inalingana na kujitolea kwa serikali kustawisha utalii kwa kulinda wanyama pori, mazingira na utamaduni.”

Waziri Balala aliongeza kuwa “picha za wanyama pori hao itakuwa ni kumbukumbu ya kila siku kwamba wanyama hao wana nafasi muhimu katika maisha ya Wakenya.”

“Hii inakumbusha kwamba ni wajibu wetu kuwadumisha na kulinda wanyama hawa kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” akasema Waziri Balala.

Mnamo Jumanne Benki Kuu ya Kenya ilizindua sarafa mpya ambazo zinawiana na viwango vilivyowekwa na Katiba. Sarafu hizo hazina picha za marais wa Kenya wa sasa na wa zamani na badala yake zimewekwa picha za wanyamapori.

Sarafu ya Sh5 ina picha ya Kifaru, ya Sh10 ina picha ya simba nay a Sh20 ina picha ya Ndovu. Upande wa pili wa sarafu hizo kuba picha za simba wawili kwenye mchoro wa jina “Harambee” nembo ambayo imekuwepo katika sarafu za zamani.

Akiongoza sherehe ya uzinduzi wa sarafu hizo alipozuru Benki Kuu ya Kenya Rais Uhuru Kenyatta alisema zinaazishia mwanzo mpya wa Kenya katika juhudi za kuijenga kwa kuhifadhi historia yake.

“Sarafu mpya ni njia ya kujijenga, kuhifadhi historia ba utamaduni na kulinda mazingira yetu. Zinaakisi mambo makuu ambayo ni yenye umuhimu mkubwa kwa historia ya nchi hii,” akasema Rais Kenyatta.

Mwanaharakati Okiya Omtata ameishtakiwa CBK kwa kuendelea kutumia safaru zenye picha za marais wa zamani akidai hiyo ni kinyume cha Katiba.

NGILA: Safari za moja kwa moja hadi Amerika ziimarishe utalii nchini

NA FAUSTINE NGILA

MAENDELEO ambayo yameshuhudiwa katika sekta ya utalii mwezi Oktoba yanastahili pongezi. Wakati nilihudhuria kikao cha pamoja kati ya Wizara ya Utalii na kampuni ya Google mtaani Westlands, Nairobi, nilijionea juhudi za hakika za kuimarisha utalii nchini.

Waziri Najib Balala aliishukuru Google kwa kuzindua huduma ya Street View ambapo watalii watajionea mandhari ya mbuga zetu kwa simu zao popote walipo duniani, kabla ya kuzuru humu nchini.

Na hapo jana, ndege ya kwanza ya safari ya moja kwa moja kutoka Kenya ilitua nchini Amerika katika mchakato uliochukua miongo sita na kuifanya nchi hii kuwa ya kwanza Afrika Mashariki kujivunia huduma hiyo ya kipekee.

Na sasa serikali inalenga kuvutia watalii zaidi ya 2.5 milioni kila mwaka kufikia mwaka 2022. Idadi hii inamaanisha utalii nchini utakua kwa asilimia 72 kutoka kwa watalii 1.14 milioni ambao walifika nchini 2017.

Si siri tena kwamba utalii wa Kenya kwa sasa uko katika hali nzuri. Kulingana na Baraza la Kimataifa la Utalii na Safari, utalii wetu unachangia asilimia 15.2 ya mauzo yote katika mataifa ya kigeni na asilimia 8.9 ya ajira.

Ninatumai kuwa hata wakati serikali inaonyesha jitihada zake katika kuimarisha sekta hii, haitasahau changamoto zinazotishia kuyumbisha uchumi wetu.

Tunajua fika kuwa usalama ni nguzo muhimu ya kuvutia raia wa nchi za kigeni kuzuru mbuga zetu. Hivyo basi, wanajeshi wetu wanafaa kuilinda mipaka ya Kenya dhidi ya uvamizi huku pia wakizuia utovu wa usalama humu nchini.

Utegemezi

Wakati sasa umefika kwa serikali kukoma kutegemea watalii kutoka nje ya nchi. Inafaa kuzidisha juhudi za kuwahamasisha Wakenya kuzuru taifa lao wenyewe na miundombinu iwekwe.

Bila hili, tutazidi kukumbana na hali ngumu katika sekta hii wakati ambapo mataifa ya kigeni yanawashauri raia wake dhidi ya kusafiri kuja Kenya.

Pia, iwapo kampuni yetu ya ndege ya Kenya Airways inalenga kuvuna vizuri kutokana na safari za moja kwa moja hadi jijini New York, basi inafaa kuhakikisha nauli yake haizidi ile ya kampuni shindani za ndege.

Itakuwa aibu kwa watalii kuondoka nchini Kenya wakielekea Amerika, au Amerika wakija nchini kwa kampuni pinzani za ndege kutokana na sababu kuwa eti nauli za Kenya Airways ni ghali mno.

Kauli mbiu ya kampuni hiyo ni ‘Fahari ya Afrika.’ Inafaa kukuza imani katika kaulimbiu yake kupitia kwa utendakazi wake wa kuvutia watalii wa bara hili.

Mbuga ya Maasai Mara bado namba wani Afrika

Na GEORGE SAYAGIE

MBUGA ya wanyamapori ya Maasai Mara kwa mara nyingine imeorodheshwa katika nafasi ya kwanza Barani Afrika kwenye tuzo za Utalii duniani, World Travel Awards.

Ufanisi huo wa kupigiwa mfano sasa unaiweka pazuri sekta ya utalii nchini haswa baada ya kipindi kigumu cha uchaguzi uliojaa utata mwaka jana na kuathiri sana sekta hiyo.

Kando na Maasai Mara, nyota hiyo ya jaha pia iling’aa katika hoteli za kitalii na hifadhi nyingine za wanyamapori nchini zilizoshinda tuzo za hadhi Kwenye sherehe iliyoandaliwa katika hoteli moja mjini Durban, Afrika Kusuni Jumapili.

Maasai Mara ambayo ni maarufu kote duniani ilichukua nafasi ya sita ulimwenguni na kuzibwaga hifadhi maarufu katika mataifa ya Afrika Kusini, Tanzania na Uganda. Vile vile mbuga hiyo inayopatikana katika Kaunti ya Narok imekuwa ikishinda tuzo hiyo kwa miaka minne mfululizo tangu mwaka 2013.

Kwenye kitengo cha mataifa, Kenya ilishinda tuzo za ufuo bora, mbuga bora ya wanyamapori na tuzo ya bodi bora ya kitalii barani Afrika, ufanisi ambao wamepata miaka ya 2013, 2014, 2015, 2016 na sasa 2017.

Hoteli ya kifahari ya Villa Rosa Kempinsky ilitajwa bora zaidi barani Afrika kwa kutoa huduma zinazoana na tamaduni ya wazungu pamoja na ukarimu wa Wakenya wanaofanyakazi hotelini humo.