Onyo kwa wanahabari kuhusu ripoti za kisiasa

Na WANDERI KAMAU

WANAHABARI au vyombo vya habari ambavyo vitaonyesha mapendeleo kwa baadhi ya mirengo ya kisiasa vitaadhibiwa vikali uchaguzi wa 2022 unapokaribia, lilionya jana Baraza la Vyombo vya Habari Kenya (MCK).

Baraza hilo lilisema limepokea malalamishi kutoka kwa baadhi ya viongozi na wananchi kuwa baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikionyesha mapendeleo ya wazi kwa mirengo fulani ya kisiasa, licha ya hilo kuwa kinyume cha kanuni za uanahabari.

Kwenye uzinduzi wa Jopo Maalum litakalobuni mwongozo utakaozingatiwa na vyombo vya habari kwenye uchaguzi huo, Afisa Mkuu Mtendaji wa baraza hilo, Bw David Omwoyo, alisema wakati umefika kwa sekta ya uanahabari kuwajibikia vitendo vyake.

Aliwatahadharisha wadau katika sekta hiyo kufahamu kuwa vitendo vyao vinaweza kuijenga ama kuibomoa nchi, kulingana na taratibu watakazofuata katika kuangazia masuala ya uchaguzi mkuu.

“Lazima tufahamu kuwa Wakenya wote watakuwa wameelekeza macho yote kwetu kufuatilia masuala yanayohusiana na uchaguzi mkuu wa mwaka ujao. Ili kuhakikisha tumewafahamisha matukio yote ifaavyo, lazima tuchukue hatua za mapema kuhakikisha kuna mwongozo wa pamoja utakaozingatiwa na kila mmoja katika sekta hii,” akasema Bw Omwoyo.

Alirejelea chaguzi za 2013 na 2017, ambapo baraza lilipokea visa vingi vya wanahabari kushambuliwa au vyombo vya habari kususiwa na baadhi ya Wakenya kwa tuhuma za kuegemea mirengo fulani ya kisiasa.

Kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi tata wa 2007, vyombo vya habari vililaumiwa pakubwa kwa kuchangia hali hiyo, hasa vituo vya redio vinayotangaza kwa lugha asili.

Tafiti kadhaa pia zimevilaumu vituo hivyo kuwa kueneza ghasia na taharuki za kisiasa nchini.Bw Omwoyo alisema mwongozo huo unalenga kubuni mazingira ya wazi kwa vyombo hivyo kurejelea taratibu vinavyopaswa kuzingatia kabla ya kutangaza au kuandika masuala yanayohusiana na siasa za uchaguzi.

“Kama macho ya wananchi, jukumu letu linapaswa kuwafahamisha yanayojiri wala si kuendeleza ajenda za wanasiasa ama mirengo ya kisiasa,” akasema Bw Omwoyo.

Jopo linawashirikisha wanachama 21 kutoka vitengo mbalimbali vya sekta ya uanahabari na limepewa muda wa siku 20 kukamilisha kuandaa rasimu ya mwongozo huo.

Linaongozwa na Bw Joseph Odindo, ambaye aliwahi kuhudumu kama Mhariri Mkuu katika mashirika ya habari ya Nation (NMG) na Standard Group.

Baadhi ya wanachama wake ni Prof George Nyabuga, Bw Bernard Mwinzi (Mhariri Mkuu wa magazeti ya Saturday Nation na Sunday Nation), Bi Njeri Rugene kati ya wengine.

Akihutubu kwenye kikao hicho, Bw Odindo alisema watafanya kila wawezalo kubuni mwongozo bora ambao unalingana na mazingira ya kisiasa wakati huu.

“Jukumu letu halitakuwa jipya, kwani tutarejelea miongozo sawa iliyotumika mnamo 2013 na 2017. Hata hivyo, lengo kuu ni kuimarisha miongozo hiyo ili kuwiana na hali ya sasa,” akasema.

Baada ya jopo kumaliza kuandaa rasimu hiyo, itakabidhiwa wataalamu wa masuala ya habari, siasa na uchaguzi ili kupitiwa na kuboreshwa zaidi.

Baada ya hilo, itazinduliwa rasmi na kukabidhiwa vyombo vya habari.

Mtangazaji wa zamani wa KBC Gladys Erude afariki

Na Derick Luvega

MTANGAZAJI maarufu aliyevuma katika miaka ya 1980 na 1990 Gladys Erude, alifariki Jumatano usiku akiwa na umri wa miaka 70.

Kifo chake kilitokea wiki moja baada ya kurejea nchini kutoka Amerika ambapo amekuwa akitibiwa tangu alipogunduliwa kuwa na saratani mnamo 2019, kulingana na mwanawe, Bw Bonny Erude.

“Amekuwa akiendelea kupata nafuu. Pia alikuwa na matatizo ya moyo. Aliomba kurejea nyumbani (Kenya) ili awaone watu wake. Alikuwa kijijini kwa siku chache na alirejea Nairobi Jumapili,” alisema.

Alifariki nyumbani kwao Nairobi alipokuwa akisubiri ambulensi ya kumkimbiza hospitalini.Kaka yake Laban Kirigano alikuwa wa kwanza kuthibitisha kifo cha dada yake akieleza kwamba alikuwa nyumbani kwao kijijini baada ya kukaa kwa muda mrefu Amerika.

“Ni kweli amekufa. Amekuwa akiishi Amerika ambapo watoto wake wanne wanafanya kazi. Alirejea wiki iliyopita,”alisema Bw Kirigano.

Alipowasili nchini, alitembelea familia yake Vihiga, kisha akamtembelea dadake na hatimaye akaenda nyumbani kwake katika Kaunti ya Nandi.

Katika enzi zake, alivuma kwenye ulingo wa utangazaji kwa miaka 25 katika Idhaa ya Kitaifa (VoK) ambayo sasa inafahamika kama Kenya Broadcasting Corporation (KBC).

Alishinda zimwi la urithi wa wanawake akiwa na umri mchanga wa miaka 24, baada ya kifo cha mume wake Bw Erude, waliyejaaliwa naye watoto sita wa kiume.

Aliwahi kufichua jinsi jamaa zake walivyomgeuka na kuanza kumtesa hali iliyomlazimu kuhama Tigoi, Kaunti ya Vihiga na kwenda Kaunti ya Nandi ambapo alinunua ardhi na kuanza kuishi.

Watoto wake wanne wanafanya kazi Amerika kama daktari wa upasuaji, afisa wa polisi, mhandisi na mtaalam wa mitambo, huku wengine wakiwa mhudumu katika uwanja wa ndege na pasta.

TANZIA: Mhariri wa zamani wa Taifa Leo afariki

Na LEONARD ONYANGO

MHARIRI msanifishaji wa zamani wa gazeti la Taifa Leo Dennis Geoffrey Mauya, maarufu Mauya Omauya, amefariki baada ya kuzimia ghafla mtaani Donholm, Nairobi.

Kulingana na jamaa zake, Mauya alizimia na kufariki papo hapo Jumatatu mchana, alipokuwa akitoka dukani, mita chache kutoka Kituo cha Polisi cha Savannah, Donholm.

Maafisa wa polisi walifika katika eneo la tukio na kupeleka mwili katika mochari ya Hospitali ya Mama Lucy Kibaki. Lakini saa chache baadaye familia iliwasili na kuhamishia mwili katika Mochari ya Chiromo.

“Nilimpigia simu Mauya lakini ikapokelewa na afisa wa polisi ambaye aliniambia kwenda katika Hospitali ya Mama Lucy Kibaki baada ya kumfahamisha kwamba nilikuwa ndugu yake,” akasema Bw Sam Kiyaka, kaka yake mwendazake.

Kulingana na Bw Kiyaka, Omauya amekuwa akiishi mtaani Zimmerman kwa muda wa miezi minne iliyopita.

“Alikuwa akiishi kwangu mtaani Zimmerman baada ya kutofautiana kidogo na mkewe. Jumatatu asubuhi aliondoka kwenda kutembelea watoto wake wawili na mkewe mtaani Donholm na baadaye alifaa kwenda katikati mwa jiji la Nairobi kununua miwani.

“Lakini hatujui ikiwa alifika au alizimia akiwa njiani kuelekea huko. Hatujui alizuru maeneo yapi kati ya saa 2.00 asubuhi na saa 1.00 mchana alipopatikana akiwa amefariki ,” akasema Bw Kiyaka.

Polisi wanashuku kuwa huenda Omauya alifariki kutokana na matatizo ya kushindwa kupumua kutokana na ugonjwa wa corona.

“Tuna hakika kwamba hakuuawa na corona kwani alidungwa chanjo ya AstraZeneca wiki mbili zilizopita,” akasema Bw Kiyaka.

Mauya alijiunga na kampuni ya Nation Media Group (NMG) kama mhariri msanifishaji wa gazeti la Taifa Leo mnamo 2007. Baada ya kufanya kazi kwa mwaka mmoja, alipata ufadhili na kwenda kusomea Masuala ya Kimataifa, Mawasiliano na Diplomasia kiwango cha Uzamili katika Chuo Kikuu cha London, Uingereza.

Baada ya kukamilisha masomo yake, Mauya alirejea tena katika kampuni ya NMG ambapo aliendelea na majukumu yake ya mhariri msanifishaji wa Taifa Leo kati ya 2012 na 2014.

Baada ya kuondoka NMG alienda kufundisha katika vyuo vikuu vya Moi, Nairobi na Karatina. Omauya amekuwa akiandika maoni ambayo yamekuwa yakichapishwa katika gazeti la Taifa Leo kila Ijumaa.

Omauya pia alikuwa mtafiti na mwandishi wa gazeti la China linaloangazia masuala ya Afrika, ‘ChinAfrica’.

Wanahabari wa gazeti la Taifa Leo, wakiongozwa na Mhariri Mkuu Peter Ngare, walimtaja Mauya kama mchapa kazi, mwaminifu, mpenda haki na mweledi wa masuala ibuka ya humu nchini na ngazi ya kimataifa.

King’ang’i na wanahabari tisa waachiliwa baada ya kulala seli

Na George Munene

MBUNGE wa Mbeere Kusini, Bw Geoffrey King’ang’i, pamoja na wanahabari tisa waliokamatwa Jumamosi katika eneo la Makima, Embu, waliachiliwa huru Jumatatu.

Bw King’ang’i na wanahabari hao walikamatwa na polisi waliokuwa wakifurusha wakazi katika ardhi inayozozaniwa. Maelfu ya watu waliachwa bila makao baada ya nyumba zao kubomolewa eneo hilo Jumamosi.

Bw King’ang’i na wanahabari hao walizuiliwa katika kituo cha polisi cha Matuu, Kaunti ya Machakos, hadi jana walipoachiliwa.

Maafisa wa polisi waliojihami kwa silaha walishika doria shughuli hiyo ya ubomoaji ikiendeshwa katika vijiji vya Ndunguni, Twanyonyi, Muthithu, Kituneni, Nunga na Mwanyani vilivyoko Mbeere Kusini.

Waliwalaumu wakazi kwa kuvamia ardhi ya ekari 66,000 ya Mamlaka ya Mito Tana na Athi (Tarda). Mtu mmoja alipigwa risasi na kujeruhiwa wakati wa kisa hicho.

Polisi walisema kwamba walikuwa wakitekeleza agizo la mahakama lililoruhusu Tarda kuwafurusha wakazi kutoka ardhi hiyo ili igawanywe.

Mnamo Februari 16, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tarda, Emilio Mugo, aliwapa wakazi ilani ya kuhama eneo hilo.

Kulingana na Tarda, ilani hiyo ilifuatia agizo la mahakama watu wahame ili ardhi hiyo igawanywe. Lakini wakazi wanasema kwamba wamekuwa wakiishi katika ardhi hiyo kwa miaka mingi na hawataondoka. Walidai kwamba watu wenye ushawishi wanataka kunyakua ardhi hiyo .

“Tunachukuliwa kuwa maskwota katika ardhi yetu. Hii haikubaliki,” alisema mkazi mmoja kwa jina Elizabeth Syombua.

Bw Kinga’ngi alidai kwamba watu matajiri wanataka kunyakua ardhi na kudhulumu masikini.

MCK yalaani mauaji katili ya mwanahabari wa KBC

WANDERI KAMAU na VINCENT ACHUKA

BARAZA la Vyombo vya Habari (MCK) jana limekashifu vikali mauaji ya kikatili dhidi ya Bi Betty Barasa, aliyehudumu kama mhariri wa video katika Shirika la Utangazaji la KBC.

Kulingana na taarifa za polisi, Bi Barasa aliuawa na majambazi mnamo Jumatano usiku nyumbani kwake katika eneo la Ololulua, Ngong, Kaunti ya Kajiado, alipongojea kufunguliwa lango ili kuingia.

Aliuawa na wanaume watatu waliobeba silaha kali.

Polisi waliiambia Taifa Leo kwamba wanashuku watatu hao walikuwa wamejificha katika nyumba ya karibu na kwake, ambayo bado inaendelea kujengwa.

Alifika kwenye lango la makazi yake mwendo wa saa mbili na unusu. Baada ya kumkabili mwanahabari huyo, majambazi hao waliingia kwa nguvu nyumbani kwake na kuanza kuitisha pesa.

Wezi hao waliwashinda nguvu mumewe, mwanawe na mfanyakazi wao wa nyumba.

Kwa wakati mmoja, mmoja wa majambazi hao alimlazimu Bi Barasa kuwapeleka kwenye ghorofa ya juu kutafuta pesa walizokosa.

Walipokosa pesa, walimpiga risasi mara mbili kichwani ambapo alifariki papo hapo.

Kufuatia mauaji hayo, MCK ilikashifu mauaji hayo, huku ikiwaomba polisi kuharakisha uchunguzi ili kubaini waliohusika.

Kwenye taarifa, Afisa Mkuu Mtendaji wa baraza hilo, Bw David Omwoyo alilalamikia ongezeko la visa vya mauaji dhidi ya wanahabari katika siku za hivi karibuni.

Mwaka uliopita, mwili wa mwanahabari maarufu na mwandishi wa vitabu, Prof Ken Walibora ulipatikana katika mochari ya Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) baada yake kukosekana kwa siku kadhaa.

Polisi walisema Prof Walibora aliuawa na watu wasiojulikana katika barabara ya Landhies, Nairobi.

Mwezi uliopita, aliyekuwa afisa wa mawasiliano katika Wizara ya Ardhi, Bi Jennifer Wambua, alipatikana ameuawa na mwili wake kutupwa katika msitu wa Ngong.

Visa vya wanahabari kuendelea kuhangaishwa na maafisa wa polisi na raia vinatia hofu, mmoja Milele FM akiuguza majeraha

Na SAMMY WAWERU

VYOMBO vya habari na wafanyakazi wake hasa watangazaji, waandishi na wapiga picha wamekuwa wenye mchango mkubwa kipindi hiki Kenya na ulimwengu unahangaishwa na janga la Covid-19.

Wamekuwa katika mstari wa mbele kuripoti yanayojiri, kuanzia visa vya maambukizi, maafa, waliothibitishwa kupona na mikakati iliyowekwa na serikali na wadauhusika kusaidia kudhibiti maenezi ya gonjwa hili ambalo ni kero la kimataifa.

Isitoshe, ni asasi ya kukusanya na kupasha habari ambayo imesaidia kulainisha serikali inapokosa na mtetezi mkuu wa haki ya wanyonge.

Sakata ya Covid Millionaires na iliyohusisha Mamlaka ya Usambazaji Dawa na Vifaa vya Kimataibabu Nchini (KEMSA) pamoja na baadhi ya maafisa wa idara ya afya, isingejulikana endapo vyombo vya habari visingejituma.

Ni kashfa iliyofukuliwa na kuangaziwa na runinga ya NTV, chini ya mwanahabari mpekuzi Dennis Okari.

Kimsingi, vyombo vya habari na wafanyakazi wake ni kati ya nguzo kuu katika kuboresha uchumi.

Licha ya bidii wanazotia, kuona kila mmoja amepashwa ujumbe kupitia magazetini, runinga, redio na pia tovuti za habari zinazomilikiwa na vyombo hivyo, waliotwikwa jukumu kukusanya habari hupitia kipindi kigumu hasa wanapokumbana na maafisa wa polisi na raia.

Si kisa kimoja, viwili au vitatu vimeripotiwa wanahabari kuhujumiwa na polisi.

Vinaendelea kushuhudiwa na vinaonekana kukita mizizi katika siku za hivi karibuni.

Tukio la hivi punde ni la mwanahabari wa Milele FM, kituo cha redio kinachopeperusha vipindi na matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili na kinachomilikiwa na Media Max Ltd, Bw David Omurunga ambaye alikamatwa na kushambuliwa Jumapili usiku, wakati akitekeleza majukumu yake.

Anauguza majeraha baada ya kutandikwa na maafisa wa polisi.

Ripota huyo wa Nakuru aliambia wanahabari kuwa aliingizwa kwenye gari la askari, akapitia unyama chini yao kabla ya kupelekwa katika kituo cha polisi cha Nakuru Central.

Bw Omurunga alisema alikamatwa baada ya saa mbili jioni, muda wa kafyu Nakuru, Nairobi, Kajiado, Machakos na Kiambu kuanza kutekelezwa, ambapo alikuwa akirekodi matukio.

Rais Uhuru Kenyatta alitangaza Machi 26, 2021 kukaza kamba sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kudhibiti virusi vya corona, katika kaunti hizo tano.

Maeneo hayo, kafyu ya kitaifa inatekelezwa kati ya saa mbili jioni hadi saa kumi alfajiri.

Vilevile, kaunti hizo na ambazo zimetajwa kuwa hatari kwa maambukizi ziliwekewa zuio la kuingia na kutoka.

“Walinishambulia licha ya kujitambulisha kuwa mimi ni mwanahabari (kupitia kitambulisho cha kazi, kinachotolewa na baraza la kusimamia vyombo vya habari na wanahabari nchini – MCK). Nilipata kichapo na kuuguza majeraha,”mwandishi huyo akasimulia, akitambua walivyokuwa baadhi ya maafisa.

Ni tukio la dhuluma ambalo limekashifiwa vikali na MCK, ikimtaka Inspekta Mkuu wa Polisi, IG Hillary Mutyambai kuchukulia hatua za kisheria maafisa wahusika.

“Waandishi wa habari ni miongoni mwa wafanyakazi wa huduma za dharura, waliorodheshwa na serikali. Sijajua ni kwa njia gani maafisa wa polisi wamejitwika jukumu la kutengeneza sheria, badala ya kuzitekeleza. Tunamhimiza Inspekta Mutyambai ahakikishe haki kwa mwanahabari aliyeshambuliwa imepatikana, uchunguzi ufanywe na wahusika waadhibiwe kisheria,” akasisitiza Bw David Omwoyo, afisa mkuu mtendaji wa MCK.

Cha kushangaza, kulingana na ripota aliyeshambuliwa Nakuru alisema askari waliohusika walimsuta “wanahabari hujifanya kama waliosoma sana na sisi (maafisa wa polisi) tutawatuliza”.

Ni matamshi ya dharao na kudunisha asasi ya upashaji habari, ambayo maafisa haohao wanaitegemea kupata habari muhimu kuwawezesha kutekeleza majukumu yao.

Hali kadhalika, ni maafisa haohao hukimbilia wanahabari wanaponyanyaswa na mwajiri wao, na pia kutetea haki zao za kimsingi.

Kisa cha Jumapili, si cha kwanza wanahabari kuhujumiwa.

Machi 2021, katika uchaguzi mdogo wa wadi ya Londo Nakuru, wanahabari walishambuliwa na raia wakati wakifuatilia zoezi hilo.

Ni aibu na fedheha kuona wanaoitwa kupeperusha na kupasha taifa kuhusu takwimu za maambukizi ya Covid-19, wakihangaishwa na idara ya usalama.

Serikali inadai kutambua uwepo wa wanahabari nchini, ila haiwalindi.

Kenya ni nchi inayothamini demokrasia, na waandishi wanapohangaishwa wakati wanatekeleza majukumu yao wananyimwa haki yao Kikatiba, kwa mujibu wa kipengele cha 35, ambacho kimeweka wazi haki ya kupata taarifa popote pale.

Wanahabari wa spoti wa NMG watwaa tuzo

Na MWANDISHI WETU

Wanahabari wa spoti wa kampuni ya Nation Media Group (NMG) walitawala hafla ya utoaji tuzo za Muungano wa Wanahabari wa Spoti Kimataifa (AIPS) 2020 kwa kutwaa mataji kwa wingi.

Tuzo hizo zilitolewa kwa waandishi wa spoti bora barani Afrika.Wanahabari hao wakiongozwa na mhariri wa spoti Elias Makori, walidhihirisha kwamba janga la corona halikuwa kizingiti kwao kujitolea na kujituma kazini.

Waandishi wa magazeti, Runinga na wa mitandaoni waliotambuliwa kwenye hafla hiyo ya Alhamisi jioni walijumuisha Elias Makori (Daily Nation) na Idah Waringa (NTV).

Ripota wa NTV Stephen Keter alitwaa taji la Mwanaripota bora Chipukizi Afrika huku mpigapicha wa Taifa Leo na Daily Nation Sila Kiplagat akiburura mataji mawili kwa kupiga picha za kusisimua.

Sila Kiplagat aliibuka bora zaidi barani katika kitengo cha mpigapicha chipukizi na kuchukua nafasi ya pili kwa kupiga picha murua za spoti.

Wengine ni? Jeff Kinyanjui, Samuel Gacharira na Cellestine Olilo wote wa Daily Nation. Idah Waringa alitwaa tuzo tatu.

Aliibuka wa kwanza barani Afrika kwa kuwa na stori bora zaidi kuhusu upelelezi. Waringa alipata matuzo mengine kwa kutoa video bora. Mhariri Elias Makori aliibuka wa pili barani wa kuandika stori iliyopendeza zaidi kuhusu kikosi cha Shujaa kilichoshirika mashindano jijini Vienna.

 

Mtangazaji wa zamani wa NTV afariki kutokana na corona

NA WANGU KANURI

Aliyekuwa mtangazaji wa habari katika runinga yaNTV Winnie Mukami amefariki. Mukami aliaga dunia Alhamisi baada ya matatizo ya ugonjwa wa Covid-19.

Mnamo 2010, Mukami aliondoka NTV, kampuni inayomilikiwa na Aga-Khan, baada ya kuhudumu kwa miaka saba.

“Nilifurahia sana kipindi ambacho nilikuwa kwenye vyombo vya habari na wakati ambapo kipindi changu kilitamatika, nilikumbatia mabadiliko hayo na nikaanza kufikiria jinsi nitasonga mbele. Sasa mimi ni mwanabiashara aliyejisimamia ambaye anafikiri namna ya kusaidia jamii hata ingawa kufikia hapa haijakuwa kazi rahisi,” alisema wakati huo.

Mukami alijulikana mnamo mwaka wa 2003 wakati ambapo alipeperusha habari za NTV wakati wa uzinduzi wake.

Alianza kazi yake ya uanahabari katika kituo cha KBC kama mwanahabari na mtayarishaji wa redio na televisheni wa masuala ya hivi sasa.

Kifo chake kinatujia siku mbili baada ya kifo cha mwanahabari wa Royal Media Services, Robin Njogu aliyefariki kutokana na ugonjwa huu wa Covid-19.

Wakati ambapo alikuwa akifanya kazi katika Nation Media Group, nyota yake iling’aa na akawa analinganishwa na wanahabari wa ngazi ya juu kama Katherine Kasavuli, Swaleh Mdoe, Sophie Ikenye na Louis Otieno miongoni mwa wengine.

Katika mahojiano ya hapo awali, Mukami alieleza kuwa tukio ambalo anakumbuka sana alipokuwa akifanya kazi katika televisheni ni wakati wa vurugu za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, ambapo alikuwa studioni siku nzima akiripoti uhalisia wa matukio jinsi yalivyochipuka.

Mnamo 2018, aliteuliwa kwenye bodi ya kampuni ya Kenya Pipeline kwa kipindi cha miaka mitatu na aliyekuwa sekretari wa mafuta ya petrol John Munyes. Zaidi ya ushupavu wake kwenye vyombo vya habari na serikali, Mukami alifichua kuwa alikuwa akiuza uji kwa wafanyikazi wa mijengo kabla hajapata uajiri rasmi.

Winnie Mukami alieleza uchapishaji huo kuwa angezunguka mtaa wa Kitengela akitafuta mahali ambapo ujenzi ulikuwa ukifanywa na kuuza uji wake. Aliyatumia mapato ya biashara hiyo kuwasaidia wazazi wake na ndugu zake watatu.

Uhuru amwomboleza mwanahabari aliyefariki kutokana na corona

CHARLES WASONGA na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta ametuma risala za rambirambi kwa familia ya mwanahabari Robin Njogu ambaye alifariki Jumatatu usiku baada ya kuugua Covid-19. Marehemu alifariki katika hospitali ya Aga Khan ambako alikuwa amelazwa akipokea matibabu.

Kwenye taarifa ilitolewa na kitengo cha habari za rais (PSCU), Rais Kenyatta alimtaja Njogu kama mwanahabari shupavu ambaye mchango wake katika vitengo vya redio na uanahabari wa mitandaoni umestawisha sekta ya uanahabari na mawasiliano.

Hadi kifo chake, marehemu alikuwa Mhariri Msimamizi wa Habari katika kitengo cha Redio katika Shirika la Habari la Royal Media Services (RMS).

“Robinson alikuwa mwanahabari mwenye tajriba na uzoefu mkubwa ambaye aliwafunza chipukizi wengine katika tasnia ya uanahabari. Daima tutaendelea kuenzi weledi wake, haswa katika kitengo cha redio ambapo alikuwa kielelezo cha ufanisi,” akasema Rais Kenyatta.

Kiongozi wa wa taifa aliongeza kuwa Njogu alikuwa mwanahabari wa kutegemewa zaidi alipohudumu katika kitengo cha habari katika Ikulu kati ya 2013 na 2017.

“Nilifaidi pakubwa katika kutangamana kwangu na Robin wakati ambapo alifanya kazi katika Ikulu pamoja na wanahabari wengine wa kitengo cha habari za rais. Alikuwa mfanyakazi wa kuaminika na kupigiwa mfano,” Rais Kenyatta akasema.

Kwa upande wake Naibu Rais William Ruto alimtaja marehemu Njogu kama mtaalamu aliyependa kazi yake ambayo aliifanya kwa bidii na moyo wa kujitolea.

“Alizingatia maadili ya uanahabari na kutoa mchango wake katika kuendeleza taalamu hii,” Dkt Ruto akasema kwenye taarifa aliyotuma kupitia ukarasa wake wa twitter.corona

Njogu amefariki siku chache tu baada ya kifo cha mama yake.

Waandishi wa Thika wapewa hamasisho kuhusu wajibu wao

Na LAWRENCE ONGARO

WAANDISHI wa habari wamehimizwa kuwa makini wanapoandika habari zao ili ziweze kuaminika.

Walishauriwa kuwa mstari wa mbele kufika kwenye tukio la habari wanazoripoti ili kupata ukweli wa habari hizo.

Baraza la Vyombo vya Habari Nchini Kenya (MCK), liliendesha warsha ya siku moja katika mkahawa mmoja mjini Thika ambako waandishi wa Thika wapatao 20 walihudhuria.

Afisa msimamizi kwa maswala ya mawasiliano MCK Bw Victor Bwire, alieleza kuwa mwandishi anastahili kuripoti jambo aliloshuhudia wala sio la kusikia kutoka kwa watu.

” Ili uweze kujivunia kazi yako kikamilifu kama mwandishi utalazimika kwanza kuchunga usalama wako. Hufai kufanya kazi katika mazingira yanayohatarisha maisha yako,” alisema Bw Bwire.

Aliwahimiza waandishi wawe na umoja wanapofanya kazi yao.

“Kufanya uandishi ukiwa peke yako ni hatari kwa usalama wako. Kwa hivyo, ni vyema kuwa kituo kimoja na wenzako,” alifafanua.

Aliyasema hayo mnamo Ijumaa alipokuwa akiwahamasisha waandishi jinsi ya kujiandaa wanapotekeleza kazi hiyo.

Aliwataka waandishi watakaopata nafasi ya kuripoti uchaguzi mdogo wa Juja utakaofanyika Mei wawe makini kwa kuangazia kila mwaniaji kiti hicho bila kubagua.

“Kila mwaniaji ana haki yake kupewa nafasi ya kujieleza na kupewa nafasi katika vyombo vya habari. Wewe kama mwandishi ni sharti uweke ubinafsi kwa uzito mkubwa.

Alisema waandishi wa habari wanategemewa na mashirika mengi ili kuangazia mambo yao.

Alisema waandishi wamelindwa pakubwa na sheria na kwa hivyo ni bora kuandika ripoti iliyo na ukweli.

Bw Jacob Nyongesa afisa wa mawasiliano katika MCK aliwashauri waandishi wawe makini na habari za uwongo zinazoangaziwa kila mara mitandaoni.

“Habari nyingi ambazo zinaangaziwa mitandaoni huwa sio za kweli bali huwa ni za kuchochea hisia za wasomaji kwa manufaa ya mwandishi mwenyewe,” alisema Nyongesa.

Alisema iwapo mwanahabari ataangazia stori za aina hiyo bila kudhibitisha ukweli wake mhusika huweza kupigwa faini nzito ama kifungo cha jela.

Alisema waandishi wengi huandika habari za uwongo ili kujinufaisha kifedha na kuleta hofu kwa wasomaji.

Wanahabari wataka waorodheshwe kwa watakaopewa chanjo ya corona

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha kutetea masilahi ya Wanahabari Nchini (KUJ) sasa anaitaka serikali kujumuisha wanachama wake miongoni mwa wafanyakazi watakaopewa chanjo ya corona kwanza.

Kwenye taarifa, Katibu Mkuu wa chama hicho Eric Oduor alilalama kuwa mwongozo wa utoaji chanjo ya Covid-19 haujaorodhesha wanahabari kama wa kwanza kupewa chanjo hiyo.

“KUJ inataka wanahabari wajumuishwe kwenye orodha ya wafanyakazi ambao watapewa kipaumbele na kuwa wa kwanza kupewa chanjo ya corona inayowasilishwa nchini wiki hii,” akasema.

Bw Oduor pia alimtaka Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kutambua vyombo vya habari kama asasi muhimu katika kampeni ya kitaifa ya kupambana na Covid-19.

Kauli ya KUJ inajiri kufuatia tangazo la Wizara ya Afya kwamba wahudumu wa afya, walinda usalama na walimu ndio wafanyakazi ambao watapewa chanjo hiyo kwanza. Hii ni kutoka na majukumu yao ambayo yanawafanya kutangama na wananchi na hivyo kuwaweka katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona.

Kenya itapokea shehena ya kwanza ya dozi 1.02 milioni ya chanjo aina ya AstraZeneca kutoka Uingereza mnamo Jumanne usiku. Hii ni sehemu ya dozi au vipimo 4.1 milioni ambayo Kenya inatarajia kupokea na kusambaza katika awamu ya kwanza ya usambazaji chanjo hiyo ambayo ni kati ya mwezi Machi hadi Juni.

KUJ sasa inasisitiza kuwa wanahabari wanafaa kuwa miongoni mwa wafanyakazi wa kupewa chanjo hiyo kwa sababu kazi yao inawalazimu kutagusana na wananchi kila siku na hivyo kuwaweka katika hatari ya kuambukizwa Covid-19.

“Wanahabari pia wanafaa kukingwa dhidi ya corona. Inasikitisha kuwa hawajajumuishwa miongoni mwa wafanyakazi walioko mstari wa mbele kupewa chanjo. Isiwe kwamba wanahabari ni muhimu tu nyakati za dharura wakati ambapo huduma zao zinahitajika lakini masilahi yao hayathaminiwi,” akalalama Bw Odour.

Tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kuripotiwa nchini mnamo Machi 13, 2020, wanahabari ni miongoni mwa wale ambao wameambukizwa vizuri corona vinavyosababisha homa hiyo hatari.

Mwaka jana, Rais Uhuru Kenyatta alipotangaza mwongozo kuhusu udhibiti wa Covid-19, wanahabari waliorodheshwa miongoni mwa makundi 13 ya wafanyakazi wanaotoa hudumu muhimu na ambao wanafaa kusazwa wakati wa utekelezaji wa kafyu.

WANTO WARUI: Kuzuia wanahabari shuleni kunaficha maovu

NA WANTO WARUI

Hatua ya hivi juzi ya Wizara ya Elimu kupiga marufuku vyombo vya habari shuleni huenda ikasababisha hasara zaidi kuliko faida.

Ingawaje kwa upande mmoja vyombo vya habari vinaweza kuzusha hali ya taharuki shuleni hasa wakati huu tunapokumbwa na janga la maradhi ya Covid-19, lakini pia kuna maovu mengine sugu ambayo huenda yakafanyika shuleni na yakakosa kumulikwa.

Kuporomoka kwa madarasa ya shule ya Talent Academy ambapo wanafunzi kadhaa walipoteza maisha yao, kwa mfano, ni tukio ambalo lilifungua serikali macho.

Aidha wawekezaji wengine katika sekta hii ya elimu walichukua tahadhari kutokana na kisa hicho. Kama si vyombo vya habari kuangazia suala hilo, huenda kufikia leo wanafunzi wengine wengi wangekuwa wamepoteza uhai wao kutoka na ulegevu kama huo wa wamiliki wa shule.

Mfano mwingine wa maovu yanayoendeshwa shuleni ni kuadhibu wanafunzi kwa kuwatandika kinyume cha sheria. Aidha wanafunzi wengi hasa wale wa kike hupitia dhuluma za kimapenzi ambazo zahitaji kuwekwa wazi ili jamii iweze kukosoa matendo kama hayo. Kumekuwa na kesi nyingi shuleni za mioto na hata matumizi ya dawa za kulevya.

Hofu kubwa ya Wizara ya Elimu katika suala hili ni taharuki inayoweza kuzushwa na vyombo vya habari endapo kutatokea mkurupuko wa maradhi ya Covid-19 shuleni.

Bila shaka ni kweli kuwa jambo kama hilo linaweza kuzua wasiwasi mwingi sana kwa walimu, wanafunzi na zaidi kwa wazazi. Hata hivyo, mtu akificha mwiba na kutoung’oa hatimaye mwiba huo hutunga usaha na maumivu zaidi.Je, serikali imebuni mikakati bora ya kukabiliana na hali ya Covid-19 endapo ugonjwa utakurupuka shuleni?

Ni vipi wengine watajua na kuweza kuchukua tahadhari hasa jamii ambayo inaweza kuwa imezingira shule iliyoathirika?Ni kweli kama alivyosema Waziri wa Elimu kuwa wanafunzi ni wengi zaidi na hawawezi kutoshea madarasa yaliyoko katika shule zetu. Ikiwa kabla maradhi ya Covid-19 hayajaingia madarasa yalikuwa hayatoshi, sembuse sasa?

Ni wazi kuwa sheria ya kujikinga na maradhi haya ambayo ni kutokaribiana ndiyo ngumu zaidi kutekelezwa kwa wanafunzi. Sidhani kuna shule hata moja nchini ambayo itaweza kuhakikisha wanafuzi hawagusani hasa uwanjani wanapocheza.

Jambo la muhimu zaidi ambalo Wizara ya Elimu ingefanya ni kuwaita waandishi wa habari na kufikia muafaka wa mazungumzo nao ili kuwaelekeza yale ambayo wasingependa yawasilishwe hewani huku wakipatia vyombo hivyo fursa ya kukagua maendeleo ya masomo au upungufu wa kimaadili katika shule.Kwa kufanya hivyo, maovu mengi ambayo yanaweza kutokea shuleni yatapunguzwa.

Hali ilivyo sasa, huenda kuna mambo mengi sana mabaya ambao hayatajulikana au kuweza kurekebishwa.

CMIL-Kenya yatoa mafunzo ya kuboresha uanahabari nchini

NA FAUSTINE NGILA

Kituo cha Unahabari na Elimu ya Mawasiliano nchini (CMIL-Kenya) kimeshirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (CA) kupitia ufadhili wa UNESCO kuwaelimisha wananahabari, washikadau na asasi za udhibiti wa habari kuhusu mbinu za kuboresha utendakazi katika sekta hiyo.

Mafunzo hayo ya mtandaoni kwa jina ‘Kuimarisha Uwezo wa Washikadau wa Uanahabari na Asasi za Udhibiti kuhusu Elimu ya Mawasiliano’ yalifanyika kwa siku tatu kuanzia Jumanne hadi Alhamisi wiki hii.

Dhamira ya mafunzo hayo ni kuwaelimisha wanahabari wa mashirika mbalimbali pamoja na wataalamu wa mashirika ya serikali yanahohusika na mawasiliano ili kukuza uelewa wa sera za kituo hicho.

Mkurugenzi wa CMIL Kenya executive Jakubu Mwongera aliambia Taifa Leo kuwa mafunzo hayo yatasaidia kutolewa kwa maoni yatakayotumikwa kuboresha mwongozo wa UNESCO kuhusu mtaala wa elimu ya habari nchini.

“Mafunzo hayo yatasaidia pakubwa hasa katika hali ambazo serikali ya Kenya inatekeleza miradi mbalimbali kukuza uelewa wa habari katika enzi hii ya kidijitali kwa wananchi,” alisema.

Kutekelezwa kwa miradi hii kunaweza kuongezea kiwango cha wananchi cha kung’amua jinsi ya kupata habari muhimu zitakazowasaidia kufanya maamuzi ya busara katika maisha yao, hasa kuhusu masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

“CMIL Kenya pia itawalinda wananchi dhidi ya habari feki na kuwawezesha kushiriki katika maendeleo ya kijamii na kisiasa, huku ikiwapa fursa kufaidika na nafasi za ajira zinazotolewa na teknolojia za kisasa,” aliongeza.

Kuinua viwango vya ushindani katika tamaduni mbalimbali huenda kukapiga jeki juhudi za kuwapa maarifa wananchi kupitia vyombo vya habari vinavyofurahia uhuru wa kuchapisha na kutangaza habari, hali ambayo itasaidia kuleta uongozi bora nchini.

 

 

MUTUA: Serikali haijali maslahi ya raia ndani na nje ya nchi

Na DOUGLAS MUTUA

MWANAHABARI Mkenya, Bw Yassin Juma, atapandishwa kizimbani nchini Ethiopia wiki ijayo kujibu mashtaka yanayoaminika kuwa ya kusingiziwa.

Kando na kwamba atakuwa kwenye mahakama ya nchi nyingine, Bw Juma atakabiliwa na changamoto tatu kuu: kutokuwa na wakili, kutoielewa lugha rasmi ya Ethiopia na kupuuzwa na Serikali ya Kenya.

Hiyo ni hali isiyotamanisha kwa mtu yeyote kujipata akikabiliwa nayo hata kama ametenda kosa gani.

Bw Juma, ambaye ni mwanahabari wa kujitegemea na mtaalamu anayewashauri watu kuhusu mawasiliano, alikamatwa mapema mwezi jana baada ya maandamano dhidi ya serikali ya Ethiopia ambapo yapata watu 240 waliuawa.

Alitiwa nguvuni alipopatikana nyumbani kwa mteja wake, Jawar Mohammed, ambaye ni mwanasiasa wa upinzani na mwanzilishi wa shirika la habari la Oromo Media Network (OMN).

Miongoni mwa matatizo niliyokwisha orodhesha hapo juu, la kukosa wakili ni la muda tu na labda kabla ya wakati huo mashirika ya kimataifa yatakuwa yamemtafutia uwakilishi tosha.

Lile la lugha pia huenda lisiwe hoja kwa maana iwapo atapata wakili mzuri Mwethiopia huenda akafanikiwa kupata mkalimani bora.

WIZARA YA MASHAURI YA KIGENI

Lakini tatizo la tatu ni kama ugonjwa wa saratani unaomla mgonjwa polepole japo kwa maumivu tele huku akijua fika kwamba pepo wa mauti anamnyelemea muda wote, hivyo karibuni anaelekea kaburini.

Mkenya yeyote aliyewahi kuwa na hitaji au kupata tatizo japo dogo namna gani atakwambia kuwa Bw Juma hana bahati! Wizara ya Mambo ya Nje na Serikali ya Kenya kwa jumla haijalikuhusu matatizo ambayo raia wake wanapata nje ya nchi!

Ingekuwa inajali, Bw Juma hangelala ndani siku mbili kwani juhudi za kidiplomasia, urafiki na ujirani mwema zingefanywa kuhakikisha yuko huru.

Ijapokuwa sasa Dkt Monica Juma si Waziri wa Mambo ya Nje tena, angetumia ushawishi wake kwa namna fulani kuisaidia Wizara hiyo kumtoa Bw Juma jela.

Nimetoa mfano wa Dkt Juma kwa sababu nakumbuka alitumika kama balozi wa Kenya nchini Ethiopia wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, na hivyo lazima ushawishi wake nchini humo ulikita mizizi alipoteuliwa Waziri wa Mambo ya Nje na Rais Uhuru Kenyatta.

UFISADI KATIKA BALOZI

Rais Kenyatta mwenyewe anajulikana kuwa na uhusiano mzuri sana na watawala wa sasa wa Ethiopia na watangulizi wao, hivyo kumkomboa Bw Juma si kazi ngumu.

Lakini sijashangaa kwamba Serikali ya Kenya kwa jumla haijamfaa mwanahabari huyo wakati huu anapowahitaji zaidi.

Inavyoonekana ni kuwa kuna sera fiche ya kuwatelekeza Wakenya wanaojipata katika hali tatanishi nje ya nchi.Wakenya wanaoishi ughaibuni watakwambia hakuna kitu wanachochukia kama balozi za Kenya zilizo kwenye mataifa wanamoishi.

Ule mtindo wa maafisa wa serikali kujibeba kana kwamba kuwahudumia walipa ushuru ni kuwafanyia hisani ni maradhi yaliyoenea na kuvuka mipaka na bahari.Hata mtu anayetaka huduma za kawaida tu ubalozini huzungushwa akaishia kutoa ‘chai’.

Niliyashuhudia haya kwa macho yangu mwenyewe kwenye Ubalozi wa Kenya jijini Washington D.C, watu wakitoa hongo wapewe Huduma Namba!

Mtindo huu wa kuyakosea thamani na heshima maisha ya Wakenya, ndani na nje ya nchi, unapaswa kukomeshwa mara moja.

Hebu na tuanzie hapo pa Bw Juma, arejeshwe nchini bila masharti yoyote. Mwanahabari huyo ndiye mlezi wa ndugu zake mayatima na wao pamoja na familia yake changa wanamtegemea pakubwa.

mutua_muema@yahoo.com

Wanahabari 3 wa NMG watambuliwa na Rais

Na LUCY KILALO

WANAHABARI watatu wa shirika la Nation Media Group, Nasibo Kabale, Vera Okeyo na Angela Oketch ni miongoni mwa watu waliotambuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kwa uzalendo wao.

Waandishi hao wa masuala ya afya, wamekuwa katika mstari wa mbele katika uandishi wa taarifa kuhusiana na maambukizi ya virusi vya corona miongoni mwa masuala mengine ya kiafya.

Wanahabari wengine kadhaa kutoka kwa mashirika mbalimbali ya habari pia walitambuliwa kupitia kwa tuzo hiyo.

“Kwa kufanya zaidi ya wajibu wao wa kujuza, kuelimisha na kuhamasisha Wakenya kuhusu ugonjwa wa Covid 19, mara nyingi wakiwa wanahatarisha afya yao wenyewe, wanahabari hawa wameonyesha uzalendo wa kweli na kujipatia tuzo kuu la kitaifa,” taarifa hiyo ilieleza.

Mkurugenzi Mkuu wa Afya, Dkt Patrick Amoth aliyekuwa pia kati ya maafisa wa afya ambao wanaongoza katika kushughulikia janga la corona nchini, pia alituzwa. Madaktari wengine kadha pia walitambuliwa kwa juhudi zao katika kukabiliana na maambukizi ya maradhi yanayotokana na virusi hivyo.

 

Wanahabari 250 wamo jela kote duniani – Ripoti

Na MASHIRIKA

MATAIFA ya Misri, Eritrea na Cameroon yanaongoza kwa kudhulumu wanahabari barani Afrika.

Kulingana na ripoti ya Kamati ya Kimataifa ya Kulinda Wanahabari (CPJ) ya mwaka huu, idadi kubwa ya wanahabari wamefungwa gerezani katika mataifa hayo matatu.

Wanahabari 26 walifungwa gerezani mwaka huu nchini Misri kwa madai ya kueneza habari za uongo na kuchochea ugaidi.

Wengi wa wanahabari nchini Misri walikamatwa kufuatia maandamano makubwa yaliyofanyika Septemba 19 ambapo raia wa nchi walilalamikia ongezeko la ufisadi jeshini na kumtaka Rais Abdul Fattah al-Sisi kujiuzulu.

Wanahabari 16 walisukumwa gerezani nchini Eritrea, Cameroon (7), Burundi (4), Rwanda (4), Nigeria (1), Chad (1), Comoros (1), DR Congo (1), Sudan Kusini (1), Ethiopia (1), Tanzania (1) na Somalia (1).

Kulingana na ripoti ya CPJ, China na Uturuki zinaongoza kwa kutatiza uhuru wa wanahabari kote ulimwenguni.

Katika ukanda wa Mashariki ya Kati, Saudi Arabia inaongoza kwa kuwafunga wanahabari bila hatia.

Ripoti ya CPJ inaonyesha kuwa wanahabari 250 wamefungwa kote duniani. Ripoti ya 2018 ilionyesha kuwa wanahabari walikuwa gerezani kote ulimwenguni. Mwaka wa 2016 ulivunja rekodi kwa kuwa na jumla ya wanahabari 273 waliokuwa wanatumikia vifungo vya jela.

Kimataifa, China inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanahabari wanaotumikia vifungo magerezani ikifuatiwa na Uturuki, Saudi Arabia, Misri, Eritrea, Vietnam na Iran.

Wengi wa wanahabari hao waliofungwa wanakabiliwa na makosa ya kueneza habari za ‘uongo’ dhidi ya serikali.

Kulingana na ripoti, idadi ya wanahabari ambao wamefungwa kwa ‘kueneza habari za kupotosha’ imeongezeka hadi 30 mwaka huu ikilinganishwa na 28 mwaka jana.

Mwaka jana, mataifa ya Urusi na Singapore yalipitisha sheria ya kupiga marufuku uchapishaji wa habari za kupotosha.

Wanahabari 47 wamefungwa gerezani nchini Uturuki mwaka huu ikilinganishwa na 68 mwaka jana.

Rais Recep Tayyip Erdo?an mwaka jana alifunga vituo 100 vya habari na kufikisha mahakamani wafanyakazi wake kwa madai ya kuendeleza ugaidi.

Serikali ya Uturuki mnamo Oktoba ilipitisha sheria iliyoruhusu wafungwa waliopatikana na hatia ya kueneza habari za kupotosha na propaganda kukata rufani..

Wengi wa wanahabari wanaozuiliwa nchini humo wamekata rufani na kesi zao zinaendelea kusikizwa wakiwa kizuizini.

Ripoti ya CPJ ya 2019, imebaini kuwa wanahabari 48 wamezuiliwa gerezani nchini China.

Upinzani Bolivia wazima vituo vya habari vya serikali

NA AFP

VIONGOZI wa upinzani nchini Bolivia Jumapili walivamia kituo cha runinga na kile cha redio, vyote vinavyomilikiwa na serikali na kuvikomesha kupeperusha matangazo hewani.

Hayo yalijiri huku uhasama wa kisiasa ukiendelea kutanda nchini humo.

Uhasama huo umechochewa na vuta ni kuvute kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais ambapo Rais wa sasa Evo Morales alitangazwa mshindi mwezi uliopita.

Waandamanaji ambao ni wafuasi wa kiongozi wa upinzani Carlos Mesa, ambaye pia aliwahi kuwa rais, walivamia runinga ya Bolivia TV na kituo cha redio ya Patria Nueva kueleza ghadhabu yao kwamba vituo hivyo vimekuwa vikiegemea upande wa Rais Morales.

Kulingana na mkurugenzi wa kituo cha redio cha Patria Nueva, Ivan Maldonado, waandamanaji hao waliwafurusha watangazaji hao na kuwaamrisha waondoke baada ya kupokeo jumbe za vitisho katika siku za nyuma.

Wafanyakazi zaidi ya 40 walionekana wakiondoka kwenye vituo hivyo huku waandamanaji waliokuwa nje wakiwamiminia kila aina ya matusi vituo hivyo vikiruhusiwa kucheza muziki pekee.

Tukio hilo lilikuwa kisa cha hivi punde kudhihirisha kero ya upinzani ambao unalalamikia udanganyifu kwenye uchaguzi huo uliompa Rais Morales nafasi ya kuongoza kwa muhula wa nne.

Rais Morales naye alishtumu kitendo cha uvamizi wa vituo hivyo, akisema wameonyesha kwamba hawaheshimu demokrasia.

“Wanasema wanapigania demokrasia lakini wanajifanya kwa kuwa vitendo vyao vinaonyesha udikteta. Pia wamevamia redio inayomilikiwa na Muungano wa wakulima,” akaandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mapema jana, Rais huyo alikuwa ametoa wito kwa viongozi wa upinzani wakubali kufanya mazungumzo naye ili waafikiane jinsi taifa hilo linaweza kusonga mbele na kumaliza visa vya utovu wa usalama vinavyotekelezwa na waandamanaji.

Hata hivyo, Mesa alikataa kuridhia ombi hilo akisema hawana chochote cha kuzungumza na Rais huyo wanayedai aliwaibia kura zao.

Uwezekano wa Rais huyo kuendelea kusalia mamlakani unaendelea kuwa finyu baada ya mgawanyiko kuanza kushuhudiwa kwenye vitengo vya polisi huku baadhi waliokuwa wakilinda afisi yake wakiondoka Jumamosi.

Ni maafisa wachache tu ndio walisalia kutoa ulinzi kwenye afisi hizo kufikia jana, ishara tosha kwamba hii huenda ikawa mwanzo wa kuporomoka kwa utawala wake.

Viongozi wa upinzani nao wametoa wito kwa jeshi la taifa hilo kufuata nyayo za polisi hao huku wakisisitiza kwamba uchaguzi huru ndio utatuliza mambo nchini humo.

Uhuru wa wanahabari utiliwe mkazo Afrika – BBC

Na VALENTINE OBARA

SHIRIKA la kimataifa la habari la BBC, Jumatano lilitoa wito kwa mashirika mengine ya habari Afrika kutilia mkazo umuhimu wa uhuru wa kutekeleza wajibu wao bila ushawishi kutoka nje.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Bw Tony Hall alisema uhuru wa vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika kukomesha maovu barani na kutetea wanyonge katika jamii.

“Uhuru wa vyombo vya habari unahitajika sasa kuliko wakati mwingine wowote wa enzi zilizopita. Uhuru huu unazidi kukandamizwa. Kuna mataifa mengi ambayo yamepitisha sheria za kukandamiza vyombo vya habari. Haya ni masuala tunayohitaji kuwazia na kuweka pia mikakati ya kulinda wanahabari zaidi,” akasema.

Alikuwa akizungumza kwenye hafla iliyoleta pamoja wadau wa sekta ya vyombo vya habari Nairobi Jumatano usiku, akiwemo afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Nation Media Group, Bw Stephen Gitagama.

Wakati huo huo, shirika hilo lilitangaza mpango maalumu wa kusaidia wanahabari walemavu kupata nafasi ya kujistawisha katika taaluma zao.

Bw alisema mpango huo unaofahamika kama Aim High utatoa mafunzo kwa wanahabari walemavu kuanzia Aprili mwaka ujao.

Wale watakaofuzu kwa nafasi hizo watapewa nafasi kufanya kazi wakijinoa kitaaluma katika afisi za BBC zilizo Nairobi.

Nairobi ina afisi kubwa zaidi ya BBC barani Afrika baada ya makao makuu ya shirika hilo London, Uingereza.

Bw Hall alikuwa nchini kwa sherehe za shirika hilo kuhusu mafanikio yake barani Afrika ambako inatangaza habari kwa lugha 13 tofauti ikiwemo Kiswahili kupitia kwa runinga, redio na mitandao.

Wamiliki vyombo vya habari waonywa dhidi ya kudunisha wanahabari kimalipo

Na JUMA NAMLOLA

BARAZA la Vyombo vya Habari nchini (MCK) limewaonya wamiliki wa vyombo hivyo wanaowakandamiza wanahabari kimalipo kuwa litalazimika kuwanyima leseni.

Afisa Mkuu Mtendaji, Bw David Omwoyo, alisema jana kwamba kuwaacha wanahabari kwa miezi kadhaa bila mshahara kunachangia kiwango kikubwa cha ufisadi katika taaluma hiyo.

“Tuna taarifa kwamba baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari hawajalipa wanahabari kwa karibu miezi minne. Hili ni jambo lisilokubalika. Hawa wanahabari wana familia zinazowategemea na pia wana kodi za kulipa. Hatutakubali jambo hili,” akasema.

Bw Omwoyo alikuwa akizungumza wakati wa kupokea ripoti ya Kamati Maalum iliyoundwa kukusanya takwimu kuhusu vyama na mashirika ya wanahabari na wafanyakazi katika sekta ya uanahabari nchini.

Alieleza kuwa kwa kuwacheleweshea mishahara wanahabari au kuwalipa mshahara duni, wengi huishia kutegemea vyakula vya bure kwenye mikutano ya wanahabari au kuomba pesa.

“Unatarajia vipi mwanahabari anayehongwa kwa chakula au nauli kuandika habari isiyoegemea upande wowote? Iwapo tabia hii haitakoma, huenda tukalazimika kuwanyima vyeti vya kuwaruhusu kukata upya leseni zao,” akasema Bw Omwoyo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw Mutegi Njau, alisema mojawapo ya changamoto kubwa waliyokumbana nayo wakati wa kusajili makundi ya wanahabari, ni kukosekana kwa mafunzo maalum yanayoenda na wakati.

“Tuligundua kuwa wanahabari wamejiunga katika vikundi kutegemea na majukumu wanayotekeleza. Ilibainika kuwa wengi hawajapata mafunzo yanayowafaa,” akasema.

Makundi 27 ya wanahabari yalisajiliwa.

Waajiri wahimizwa wafidie waandishi wanapovamiwa

Na WANDERI KAMAU

ASASI za kusimamia waandishi wa habari nchini zimehimizwa kuhakikisha wanahabari wanalipwa ridhaa wanaposhambuliwa ama vifaa vyao kuharibiwa wakiwa kazini.

Akihutubu Jumatno kwenye ufunguzi wa Kongamano la Wanahabari Kuhusu Ugatuzi jijini Nairobi, aliyekuwa Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Nyeri Bi Priscilla Nyokabi alisema kwamba, wanahabari wengi hawajakuwa wakilipwa ridhaa wanaposhambuliwa, licha ya masaibu yao kuangaziwa.

Alisema asasi za kuwatetea kama Baraza la Vyombo vya Habari Kenya (MCK) hazijakuwa zikichukua hatua za kutosha kutetea maslahi ya wanahabari, licha ya kukashifu mashambulio dhidi yao.

“Licha ya MCK kujitokeza kuwatetea sana wanahabari, juhudi zaidi zinahitajika katika kuhakikisha wanalipwa ridhaa ikiwa wanajeruhiwa ama vyombo vyao kuharibiwa,” akasema Bi Nyokabi.

Visa vya wanahabari kushambuliwa na kujeruhiwa ama vyombo vyao kuharibiwa wakiwa kazini vimekuwa vikiongezeka, hasa katika kiwango cha kaunti.

Baadhi yao hata wameuawa katika hali tatanishi, huku waliohusika katika visa hivyo wakikosa kuchukuliwa hatua.

Mwaka uliopita, mwanahabari Barack Oduor wa Shirika la Habari la Nation (NMG) alinusurika kifo, baada ya kutekwa nyara na watu wasiojulikana pamoja na mwanadada Sharon Otieno katika Kaunti ya Homa Bay, ambapo baadaye msichana huyo alipatikana akiwa ameuawa.

Mnamo Juni, wanahabari wa shirika la habari la Standard Group Carolyne Bii, Boniface Magana (mpiga picha) na Immaculate Joseph (dereva) walinusurika kifo baada ya gari lao kushambuliwa na kuchomwa na wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya St Joseph’s katika Kaunti ya Machakos.

Kulingana na Bi Nyokabi, asasi zilizopo hazijakuwa zikizingatia sheria kuhakikisha wanahabari wanaojipata matatani wanalipwa ridhaa kutokana na hasara wanayopata.

“Kuna sheria inayoeleza jinsi wanahabari wanaoshambuliwa wakiwa kazini wanapaswa kulipwa ridhaa kwa hasara wanayopata,” akasema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari wa Kandarasi (KCA) William Janak alisema kuwa, tangu Januari, wamepokea visa 38 vya wanachama wao ambao wameshambuliwa wakiwa kazini.

Alisema wameanza mikakati ili kushinikiza asasi husika kuchukulia kwa uzito na kufuatilia visa vya wanahabari wanaoshambuliwa.

Wahariri waonya wanaodhuru wanahabari

Na KALUME KAZUNGU

BODI ya wahariri wa Habari nchini (Editors Guild) imeonya vikali tabia ya baadhi ya watu kuwashambulia wanahabari wanapokuwa kazini.

Katika kikao kilichowakutanisha wananchi na wahariri hao kwenye ukumbi wa hoteli ya Mwana Arafa mjini Lamu Jumamosi, Rais wa bodi hiyo, Bw Churchill Otieno, alisema hawatamsaza yeyote atakayejaribu kuingilia au kuzuia utendakazi wa wanahabari kupitia kuwavamia na kuwapiga au kuharibu vifaa vyao vya kufanyia kazi.

Bw Otieno alisema kuwashambulia wanahabari ni sawa na kuushambulia umma, hivyo akasisitiza haja ya wenye nia hiyo mbovu kukoma.

Pia aliwataka viongozi na wakazi kuwa mstari wa mbele katika kudhibiti usalama wa wanahabari kwenye maeneo yao ili watekeleze jukumu lao la kuupasha umma habari ipasavyo na kwa wakati ufaao.

Katibu Mkuu wa Muungano wa kutetea Maslahi ya Wanahabari (KUJ), Bw Eric Oduor, alisema tayari wamehakikisha wote waliojaribu kuwashambulia wanahabari wanakamatwa na kufikishwa kortini hapa nchini.

Alitaja kisa cha kupigwa kwa mwanahabari wa gazeti la Standard anayefanya kazi Lamu, Bi Jane Wangechi Mugambi na Mwakilishi Maalum wa Bunge la Kaunti ya Lamu, Bi Monica Njambi, kuwa mojawapo ya mifano ambapo KUJ imehakikisha haki inatendeka kwa wanahabari wanaodhulumiwa nchini.

Kamishna motoni kwa kuhangaisha wanahabari

Na WAIKWA MAINA

BARAZA la Habari (MCK) limepuuzilia mbali agizo la Kamishna wa Kaunti ya Nyandarua, Bw Boaz Cherutich kwa vyombo vyote vya habari kuwasilisha taarifa zao kwa Shirika la Habari la Kenya (KNA) kabla ya kuzichapisha.

MCK ilieleza wasiwasi wake pia kuhusu visa vinavyoongezeka vya kuhangaishwa kwa wanahabari na maafisa wa serikali za kaunti na hata ya kitaifa.

Wiki iliyopita, Bw Cherutich alitoa agizo hilo wakati wa kongamano kuhusu vita dhidi ya ugaidi na itikadi kali za kidini mjini Ol Kalou, akisema habari zinazofikia wananchi zinafaa kufanyiwa utathmini na kuruhusiwa na KNA.

Akizungumza alipokuwa Nyandarua kuchunguza kisa ambapo wanahabari walihangaishwa na kutishiwa na maafisa wa polisi wiki iliyopita, Meneja wa Uhuru wa Wanahabari katika MCK, Bi Dinnahh Ondari alisema agizo hilo lilikuwa na lengo la kunyamazisha wanahabari.

“Agizo hilo ni la kunyanyasa vyombo vya habari na tunalipinga. Tuna uhuru wa vyombo vya habari katika nchi hii na umelindwa kikatiba,” akasema Bi Ondari.

Kwenye kisa kilichokuwa kikichunguzwa, maafisa watatu wa polisi na mmoja wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walihangaisha na kutishia kuwapiga risasi wanahabari waliokuwa wakikusanya habari kuhusu gari lililohusishwa na uhalifu.

Gari hilo lilichomwa katika kituo cha polisi baada ya kunaswa na wananchi. Lilipatikana Ol Kalou likiwa na watu wanne walioshukiwa kuhusika kwa uhalifu mjini Ol Kalou na Nakuru.

Bi Ondari alisema inatia wasiwasi jinsi polisi wanavyojitahidi kuzuia wanahabari kutekeleza majukumu yao.

ONGAJI: Wakati wa vyombo vya habari vya Kiswahili kuzinduka ni sasa

Na PAULINE ONGAJI

NINA uhakika kwamba umepata fursa ya kukutana na picha za kejeli mtandaoni almaarufu kama ‘meme’ wakati wowote unapopekua mitandao ya kijamii.

Majuma kadha yaliyopita, nilikutana na meme moja kwenye mtandao wa kijamii ambapo kulikuwepo picha ikilinganisha habari zinazopewa kipaumbele na vyombo vya habari humu nchini na zile ambazo huwa zinapeperushwa na stesheni nyingine za kimataifa.

Picha mbili za kwanza zilikuwa zinaonyesha vituo fulani vya kimataifa ambapo mada ilikuwa kuhusiana na ustawi wa vijana na masuala ya kiteknolojia.

Kwa upande mwingine, picha ya tatu ilikuwa ya habari za lugha ya Kiswahili za stesheni moja hapa nchini, ambapo mada ilikuwa iwapo mabinti wanapaswa kuvalia chupi au la.

Hii ni meme iliyoibua hisia kali mtandaoni huku maoni mengi yakiwa kuhusu ni habari zipi zinazopewa umuhimu na vyombo vya habari vya humu nchini, hasa vinavyopeperusha matangazo yao kwa lugha ya Kiswahili kwenye redio na runinga.

Maoni mengi yalionekana kukemea baadhi ya vitengo vinavyopeperusha matangazo yao kwa lugha ya Kiswahili kwa kutawaliwa na mada za mzaha na zisizo na kina.

Wengi walitaja hizo kama baadhi ya sababu zinazowafanya wasitazame taarifa za habari kwa lugha ya Kiswahili, na badala yake kusubiri zile zinazopeperushwa kwa Kiingereza ili kupata kina cha matukio yanayoendelea nchini na kimataifa.

Ilikuwa ni hoja ambayo nakubaliana nayo kwa asilimia fulani. Majukwaa mengi ya habari za Kiswahili yameshushwa thamani na kuwa ya kuzungumzia masuala ya kipumbavu wakati mwingi kuliko muda unaotolewa kujadili masuala yaliyo na umuhimu katika jamii. Hii inafanyika huku yakitarajiwa kushindania hadhara na mengine yanayopeperusha matangazo kwa lugha ya Kiingereza ambayo mara nyingi huzungumzia masuala ya kina na yenye umuhimu mkubwa kwa jamii kama vile ustawi wa kiuchumi, teknolojia na sayansi.

Ni kana kwamba hadhara ya wanaotazama au kusoma taarifa kwa lugha ya Kiswahili ni watu wasio na elimu au wasioelewa mambo yanavyoendelea ulimwenguni.

Ni kwa sababu ya haya ambapo lugha hii imezidi kudharauliwa kiasi cha kwamba imekuwa kawaida kwa watu wakomavu waliopitia mfumo wa elimu humu nchini unaohusisha masomo ya Kiswahili, kusema bila aibu kwamba hawawezi kuzungumza lugha hii.

Inahuzunisha sana hasa ikizingatiwa kuwa Kiswahili kimevuka mipaka kiasi cha kuwa sasa kinazungumzwa katika mataifa mengi barani, huku Afrika Kusini ikitangaza hivi majuzi kwamba kinapangiwa kuhusishwa katika mtaala wa masomo nchini humo.

Wakati umefika kwa vyombo hivi vya habari kuipa lugha hii heshima inayostahili na kuwekeza kuhakikisha kwamba utaalamu unaotumika kupeperusha taarifa kwa lugha ya Kiingereza, pia unazingatiwa katika vitengo vya Kiswahili.

Ikiwa tunataka kukuza na kuipa lugha ya Kiswahili heshima inayostahili sharti basi tupanue hadhara, jambo litakaloafikiwa kwa kuhakikisha kuwa habari zinazopeperushwa kwa lugha hii zinavutia watu kutoka ngazi mbali mbali kijamii, kimasomo, kitaaluma na hata kiuchumi.

pongaji@ke.nationmedia.com

Wakenya wanaamini vyombo vya habari – Ripoti

Na WANDERI KAMAU

WAKENYA wengi wanaviamini vyombo ya habari kwa kuangazia masuala muhimu yanayoikumba nchi, imeonyesha ripoti mpya.

Ripoti hiyo, ambayo ilitolewa na Baraza la Vyombo vya Habari (MCK) kwa ushirikiano na shirika la utafiti la Infotrak, inaonyesha kuwa karibu robo ya wananchi wanaviunga mkono kwa kuripoti masuala hayo.

Masuala mengine yaliyoibukia kupendelewa ni uangaziaji wa habari za mashinani, habari zinazochipukia, ufuatiliaji wa habari muhimu, umaarufu wa wanahabari mbalimbali, uhuru wa habari zinazopeperushwa na uangaziaji wa watu maarufu.

Kwa mara nyingine, Wakenya zaidi wangali wanaviamini vyombo vya habari kama mojawapo ya taasisi zinazoaminika.

Utafiti ulionyesha kuwa zaidi ya nusu ya Wakenya wanaviamini vyombo hivyo kama asasi inayoaminika zaidi.

Kando na hayo, televisheni ziliibuka kama vyombo vinavyotegemewa na Wakenya wengi, zikifuatwa na redio, mitandao ya kijamii na magazeti.

Na huku mitandao ya kijamii ikiendelea kuwa maarufu miongoni mwa Wakenya, robo ya waliohojiwa walisema huwa wanaitumia kubuni urafiki na watu wengine.

“Kuibuka kuwa watu wengi wanaotumia mitandao hiyo kubuni urafiki inaonyesha kuwa watu wanaanza kutambua umuhimu wa matumizi yake katika maisha yao ya kila siku,” ikasema ripoti.

Kando na kubuni urafiki, mitandao ya kijamii pia iliibuka kama mihimili muhimu kwa Wakenya kupata habari.

TAHARIRI: Afisa aliyedhulumu wanahabari akamatwe

NA MHARIRI

MASHAMBULIZI dhidi ya wanahabari yameanza kuwa jambo la kawaida hapa nchini.

Kila mtu anayehisi kubanwa hukimbilia kuwatusi, kuwalaumu au hata kuwashambulia wanahabari. Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria, ni wa punde zaidi kuwashambulia wanahabari wa kampuni ya Nation Media Group kwenye mtandao wa Twitter, kwa kuwaita “watumwa wa mwajiri wao”.

Kisa na maana ni kuwa, gazeti la Sunday Nation lilichapisha kibonzo cha Bw Kuria akiwa ametokwa na ulimi mrefu na maandishi ‘Kijana wa zamani wa kanisa mwenye ulimi wa sumu.’

Mchoraji katuni na wahariri wa gazeti hilo wanaamini kuwa japokuwa Bw Kuria anadai kuwa aliwahi kuwa kijana wa kutumika madhabauni, tabia zake, matamshi yake na mienendo haviendi sawa na sifa hiyo.

Amekuwa akitoa cheche za matusi, kuwaombea wanasiasa wengine kifo n ahata wakati mmoja alimwita Kinara wa chama cha ODM, Raila Odinga majina yasiyochapishika na kudai angemfanyia kitendo fulani.

Naibu Kamishna wa Kaunti eneo la Miharati naye Ijumaa aliwashambulia wanahabari waliokuwa kazini wakati wa maandamano ya wakongwe. Aliwaamuru maafisa wa polisi wa Utawala wawapokonye wanahabari hao vifaa vyao vya kazi na kuhakikisha hawakurekodi matukio hayo.

Wanahabari hao wa runinga za Njata na Gikuyu walikuwa wakitekeleza wajibu wao wa kufahamisha umma kuhusu yaliyokuwa yakitokea.

Kifungu cha 35 cha Katiba kinaeleza haki ya umma kupata habari. Ukijumuisha na kifungu cha 33 kuhusu Uhuru wa Vyombo vya Habari, inasikitisha sana kuona Bw Kuria na Naibu huyo wa Kamishna wa Kaunti wakiwa wangali kazini.

Wizara ya Usalama wa Ndani imetangaza kuwa inachunguza madai dhidi ya Naibu wa Kamishna wa Kaunti. Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) inapaswa kujibu maswali kuhusu maafisa inaowaajiri kutumikia umma.

Kwa afisa huyo kutangaza kuwa hakuna mwanahabari atakayefanya kazi yake katika eneo analosimamia bila ya ruhusa yake, ni wazi haelewi katiba ya nchi hii inavyosema.

Afisa kama huyo anatumia vibaya afisi yake, jambo ambalo ni ukiukaji wa Sura ya Sita kuhusu Maadili. Inashangaza kuwa bado yupo kazini kufikia leo.

Wanahabari wakejeli wahubiri wanaowatishia maisha kwa kuanika maovu yao

Na ANITA CHEPKOECH

VYAMA vya waandishi habari nchini vimeelezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la visa vya viongozi wa kidini kuwatishia wanahabari wanaofichua maovu na hadaa ndani ya makanisa yao.

Kupitia taarifa, Muungano wa Sekta ya Vyombo vya Habari (KMSWG) ambao hujumuisha Muungano wa Wanahabari (KUJ) na vyombo vya Habari vya Kenya (MCK), uliwashtumu viongozi wa makanisa wanaowatishia wanahabari kwa lengo la kuwazuia kufanya kazi zao kikamilifu.

Taarifa hiyo inajiri huku mhubiri wa Kanisa la Neno Evangelism, James Ngáng’a alinakiliwa kwenye kanda ya video akimtishia mwanahabari wa runinga ya Citizen, Linus Kaikai, akisema ‘ataona moto’ iwapo hatakoma kuwadharau wahubiri.

Majuzi, wafuasi sugu wa mhubiri anayejidai kwa nabii pekee wa Mungu, Dkt David Owuor walijitosa kwenye mitandao ya kijamii na kuvamia vyombo vya habari na maripota, baada ya kuangazia madai ya kutwaa mali ya muumini yaliyokuwa yakimkabili nabii wao.

“Tumesikitishwa na tabia inayochipuka ya viongozi wa makanisa wenye maadili ya kutiliwa shaka kugeukia vyombo vya habari, kuwatisha wanahabari na kuvuruga uhuru wa kujielezea.”

“Uanahabari ndiyo nguzo ya nne ya utawala nchini na una jukumu ya kuanika mambo yanayokwenda mrama kwa umma, wakiwemo viongozi wa makanisa wanaowahadaa waumini wao. Kazi za wakuu wa dini zina athari katika jamii na lazima ziangaziwe bila uoga wala aibu,” ikasema taarifa ya KMSWG.

Nabii Owuor na Kasisi Ngángá ni baadhi ya viongozi wa kidini ambao wamewachochea waumini wao kuzama mitandaoni sio tu kuwakashifu wanahabari bali pia kuwatishia kwa kuendelea kuwaangazia.

“Tumeshtushwa kuwa Ngángá, mtumishi wa Mungu amewatishia wanahabari kwa kumwaangazia. Tunataka kuwaeleza Bw Ngángá na Bw Owuor kwamba, hata wanahabari wanaamini Mungu na hakuna vitisho vyovyote vitakavyowazuia kuanika maovu yanayoendelea katika maeneo ya kuabudu,” ikaongeza taarifa hiyo.

Wakinukuu kifungu cha Bibilia, viongozi wa KMSWG walisema hata Yesu aliingia hekaluni na kuwacharaza viboko watu waliokuwa wakishiriki maovu ndani ya nyumba ya Mungu.

“Uanahabari si uhalifu na utaendelea kuwa macho yanayoangazia taasisi zote na uongozi wa nchi. Hatuwezi kukaa kitako na kutazama tu jinsi wahubiri wanavyowafilisi kondoo wao kwa kisingizio kwamba hawawezi kukabiliwa kisheria,” ikasisitiza taarifa hiyo.

KMSWG hata hivyo ilizitaka Tume ya Kitaifa ya Huduma ya Polisi(NPS) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma(DPP) kuwachukulia hatua kali Bw Owuor na Bw Ngáng’a kwa kuwatishia wanahabari na wafuasi wao wanaoendeleza shutuma kwenye mitandao ya kijamii kwa walio na mitazamo tofauti.

Wito raia kuwaripoti wanahabari wafisadi

NA CECIL ODONGO

TUME ya kupokea malalamishi ya Baraza Kuu la Vyombo vya Habari nchini imewataka raia kupiga ripoti kwake kuhusu wanahabari wafisadi na visa vya kuharibiwa jina kabla ya kuziwasilisha mahakamani.

Kulingana na Mwenyekiti wa tume hiyo Henry Maina, wamiliki wa vyombo vya habari hupoteza kati ya Sh100 milioni na Sh150 milioni kila mwaka kutokana na kesi mahakamani ilhali kesi zenyewe zinaweza kutatuliwa nje ya mahakama.

“Wanahabari siku za nyuma hawajamakinika jinsi wanavyoripoti visa au kuandika habari kuhusu ufisadi. Wao huwalaumu washukiwa hata kabla ya hawajafunguliwa mashtaka mahakamani. Hii huvutia kesi ambazo wanahabari huishia kupoteza,” akasema Bw Maina.

Akizungumza katika mkutano wa kutoa mafunzo kwa wahariri uliofadhiliwa na Chama cha Wahariri nchini jijini Kisumu, Bw Maina aliwaomba wale wote wanaohisi kudhulumiwa na wanahabari, kutosita kuwasilisha malalamishi yao ili tume ifanye uchunguzi na kuwaangushia wahusika adhabu kali. Na Caroline Mundu

Wanahabari wavamiwa kwenye kesi ya aliyebaka mtoto wa waziri

Na MAGDALENE WANJA

BARAZA la Wanahabari nchini (MCK) limetoa onyo kwa wanaowavamia wanahabari wakiwa kazini kuwa watakabiliwa na sheria.

Hii ni baada ya wanahabari wawili kupata majeraha Alhamisi walipovamiwa katika mahakama ya Nakuru wakati wa kusikizwa kwa kesi ya mshukiwa wa ubakaji ya mtoto wa waziri serikalini.

Mkurugenzi mkuu wa MCK David Omwoyo aliyezungumza na wanahabari baada ya kupiga ripoti kuhusu kisa hicho na maafisa wa polisi katika kituo ca Central mjini Nakuru alilaani kitendo hicho  akisema kuwa ni kinyume na haki za wanahabari.

Mkurugenzi mkuu wa MCK Bw David Omwoyo aungana na wanahabari kukemea uvamizi dhidi ya vyombo vya habari katika kituo cha polisi cha Central mjini Nakuru Desemba 27, 2018. Picha/ Magdalene Wanja

“Yeyote atakayewavamia wanahabari wakiwa kazini atachukuliwa hatua kali za kisheria kwani hiyo ni kukiuka haki za vyombo vya habari na zile za kibinafsi,” alisema Bw Omwoyo.

 Baadhi ya waliojeruhiwa ni mwanahabari wa KTN  Peter Kimani,  na mwenzake wa Mount Kenya Tv Eliud Mwangi.

Bw Kimani alisema kuwa kutokana na shambulio hilo, alipata majeraha katika sehemu zake za siri.

Bw Omwoyo alisema kuwa baadhi ya kaunti ambazo zimerekodi visa vingi vya mashambulizi dhidi ya wanahabari ni pamoja na Kilifi, Bungoma, Tharaka Nithi, Murang’a, Embu, Mombasa na Nairobi.

Aliongeza kuwa ofisi ya Mashtaka ya Umma pamoja na ile ya Huduma za Polisi imehakikishia MCK kwamba visa vyote vilivyoripotiwa vitashughulikiwa.