Serikali yawataka wazazi walinde watoto dhidi ya dhuluma na habari potovu mitandaoni

Na WINNIE ONYANDO

SERIKALI inawataka wazazi kuwajibika na kuwalinda watoto wao dhidi ya habari potovu na dhuluma mtandaoni.

Waziri wa Mawasiliano, Joe Mucheru aliwalaumu wazazi kwa kukosa kukagua wavuti wanazoingia watoto wao, jambo linalosababisha kuongezeka kwa visa vya dhuluma za watoto mitandaoni.

Akizungumza jana katika hafla ya uzinduzi wa programu ya kuwalinda watoto mitandaoni iliyoasisiwa na Mama wa Taifa, Bi Margaret Kenyatta jijini Nairobi, Bw Mucheru alisema kuweka nywila (pin) kwenye simu au kwenye wavuti mbalimbali hakutoshi.

“Hatuwezi kuwalaumu watoto wetu. Lawama ni kwa wazazi ambao mara nyingi huwa wazembe baada ya kuwapa watoto wao simu. Ni jukumu letu sote kupambana na dhuluma za watoto mitandaoni. Wazazi lazima wawe katika mstari wa mbele katika kutekeleza hilo,” akashauri Bw Mucheru.

Alihusisha mavazi mabaya, matumizi ya lugha chafu, mitindo inayokiuka tamaduni za Kiafrika na vifo miongoni mwa watoto na ukosefu wa wazazi kuweka mipaka katika habari wanazofaa kuzitazama watoto wao.

“Wewe kama mzazi, hufai kumwacha mtoto wako huru kuingia katika wavuti yoyote. Weka mipaka ya matumizi ya simu. Usimwache atumie simu kwa muda mrefu,” akaonya Bw Mucheru.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano, Mercy Wanja, alisema matumizi ya mtandao yaliongezeka kwa asilimia nne mwaka huu kutokana na janga la corona. Aliwataka wazazi wahakikishe kuwa watoto wanapata tu fursa ya kufikia wavuti zinazohusiana na elimu bali si za kuwapotosha.

“Uzinduzi wa kampeni hii ni njia ya kuwalinda watoto wetu. Hatutaki wafikie habari za kuwapotosha,” akasema Bi Wanja.

Hata hivyo, Bi Wanja alisema watashirikiana na walimu na Taasisi ya Mtaala (KICD) ili kuunda wavuti itakayoangazia masuala ya watoto na kuwapa mafunzo ya kiakademia.

Alisema wanashirikiana na wadau mbalimbali kama vile Wizara ya Elimu, KICD, Ofisi ya wapelelezi wa makosa ya jinai na mahakama kuu ili kuwachukulia hatua watakaopatikana wakiwadhulumu watoto mtandaoni.

Jaji Mkuu, Martha Koome ambaye pia alihudhuria hafla hiyo alisema tayari wameunda programu mtandaoni itakayotumika kurekodi kesi zote na kuwawezesha polisi kufuatilia kesi zote za dhuluma.

DCI yachunguza kisa cha watoto kufungwa

Na STEVE NJUGUNA

IDARA ya Upelelezi Nchini (DCI) imeanzisha uchunguzi kuhusu kisa ambapo walimu wawili waliwafunga wanafunzi watatu wa Shule ya Msingi ya Thiru, Laikipia Magharibi, mitini kama adhabu ya kuchelewa kufika shuleni.

DCI jana ilianzisha uchunguzi dhidi ya Mwalimu Mkuu Shelmith Thimba na Naibu wake David Maina ambao wanadaiwa kuwafunga wanafunzi hao Ijumaa wiki jana.

Picha zilizosambaa mitandaoni zilionyesha wanafunzi hao watatu wakiwa wamefungwa kwa kamba mtini na kuzua ghadhabu miongoni mwa Wakenya.

Inadaiwa kuwa Naibu Mwalimu Mkuu alichukua picha za wanafunzi hao wa kisha akazituma kwenye ukumbi wa WhatsApp za wanafunzi hao kabla mwalimu mmoja kuzisambaza mitandaoni.

Hapo jana, maafisa wa DCI pamoja na Naibu Kamishina wa Kaunti ya Laikipia Moses Muroki walifika shuleni humo inayopatikana kilomita 15 kutoka mji wa Nyahururu.

Waliwahoji walimu pamoja na wanafunzi kuhusu kisa hicho hicho kilichokashifiwa na Wakenya na kutajwa kama tukio la uhayawani.

“Tumebaini kuwa ni kweli wanafunzi hao walifungwa mtini Ijumaa . Ni jambo la kukera na hatulifurahi hata kidogo. Tunasikitika kuwa wanafunzi hao walipitia hali kama hiyo. DCI imeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo,” akasema Bw Muroki.

Mkurugenzi wa Shirika la Watoto Kaunti ya Laikipia Ezekiel Mwanza na mkurugenzi wa Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) Irene Kadenge walikashifu kufungwa kwa wanafunzi hao wakisema ni jambo lisilothamini ubinadamu.

“Inashangaza kuwa watoto wetu wanapitia katika hali hiyo shuleni. Kama shirika la watoto tunakemea kitendo hicho na lazima tuwalinde watoto wetu,” akasema Bw Mwanza.

Alisisitiza kuwa shirika hilo litawalinda watoto hao watatu kisha kuwapa ushauri na nasaha na kufuatilia masomo yao .

WINNIE ONYANDO: Wazazi watafute muda kuwajenga watoto wao kifikra na kimaadili

Na WINNIE ONYANDO

Kutafuta pesa si mbaya ila ujenzi wa ukuruba na ukaribu na mwanao ni wa maana zaidi. Uwepo wako kama mzazi katika maisha ya mwanao huchangia pakubwa katika ujenzi wa tabia na mienendo kwa mwanao. Pia huchangia pakubwa katika alama atakazozizoa mtoto akiwa shuleni.

Watoto wanapokua, mara nyingi wanahitaji umakini kamili kutoka kwa wavyele wake. Mama au baba anapokuwa mbali na mwanawe hasa anapokua na kumwona pengine mara mbili kwa wiki, basi uhusiano kati ya wawili hao huwa na umbali wa Mashariki na Magharibi.

Mzazi mama huwa mlezi na hivyo huwa karibu sana na mwanawe na kumpa muda mwingi sana ikilinganishwa na mzazi wa kiume ambaye mara nyingi hufunikwa na majukumu ya kuwakimu familia.

Ila ni jukumu la kila mzazi kumtengea mwanawe muda wa kuwa karibu naye, ahisi uwepo wake katika maisha yake. Kazi isiwe kikwazo kwa mzazi na kumtenga naye maishani. Afya ya mwanao ni bora kuliko pesa unazotafuta.

Kando na kuhitaji uwepo wako, mtoto anahitaji kujengwa kifikra, kuhakikishiwa kuwa ni mrembo au mtanashati kila mara, kupongezwa, kushughulikiwa kiafya na mengineyo.

Uwepo wako unampa mtoto motisha, ujasiri, nguvu, kumjenga kihisia, utulivu wa mawazo na fikra, furaha na amani ya kipekee moyoni.

Anapocheza au hata kutangamana na wenzake, anapata kuwasimulia jinsi anavyopendwa na wazazi wake. Jinsi yeye hupigwa pambaja, kuambiwa kuwa ni mtanashati au mrembo na kukumbatiwa na wazazi wake kabla ya kulala.

Mtoto huathiriwa mno na anachokiona au kushuhudia. Anapomwona babake anaishi na mamake kwa upendo na amani, yeye ataufuata mkondo huo na kuishi vivyo hivyo na mkewe.

Anapomwona ukimtesa na kumpiga mamake, naye ataishia kujua kuwa wanawake ni viumbe dhaifu wanaofaa kuchapwa kila mara.

Cha muhimu mno ni kumlea mwanao katika njia za Mungu. Mfunze kuwa watu hawafai kula bila kuomba, waongoze katika kuomba na kusoma Bibilia au Kuraan nyumbani kama mzazi.

Mfunze njia za Mungu maana Bibilia inasema kuwa ‘mlee mtoto katika njia ipasavyo, naye hataiacha hata atakapokuwa mzee.’ Usifanye kazi au hata majukumu mengine yakutenganishe na mwanao.

Keti chini na mwanao, zungumza naye ili upate kufahamu mawazo, hofu, nguvu zake, udhaifu wake, talanta yake, rangi aipendayo, yanayompendeza na mahitaji zake za kibinafsi.

Usije ukajuta na kulalamika kuwa humfahamu mwanao ilhali wewe hukumtengea muda wa kumfahamu ipasavyo.Na WINNIE A ONYANDO

Wazazi wengi ‘wameolewa’ na kazi zao. Kutafuta pesa si mbaya ila ujenzi wa ukuruba na ukaribu na mwanao ni wa maana zaidi.

Uwepo wako kama mzazi katika maisha ya mwanao huchangia pakubwa katika ujenzi wa tabia na mienendo kwa mwanao. Pia huchangia pakubwa katika alama atakazozizoa mtoto akiwa shuleni.

Watoto wanapokua, mara nyingi wanahitaji umakini kamili kutoka kwa wavyele wake. Mama au baba anapokuwa mbali na mwanawe hasa anapokua na kumwona pengine mara mbili kwa wiki, basi uhusiano kati ya wawili hao huwa na umbali wa Mashariki na Magharibi.

Mzazi mama huwa mlezi na hivyo huwa karibu sana na mwanawe na kumpa muda mwingi sana ikilinganishwa na mzazi wa kiume ambaye mara nyingi hufunikwa na majukumu ya kuwakimu familia.

Ila ni jukumu la kila mzazi kumtengea mwanawe muda wa kuwa karibu naye, ahisi uwepo wake katika maisha yake.

Kazi isiwe kikwazo kwa mzazi na kumtenga naye maishani. Afya ya mwanao ni bora kuliko pesa unazotafuta.

Kando na kuhitaji uwepo wako, mtoto anahitaji kujengwa kifikra, kuhakikishiwa kuwa ni mrembo au mtanashati kila mara, kupongezwa, kushughulikiwa kiafya na mengineyo.

Uwepo wako unampa mtoto motisha, ujasiri, nguvu, kumjenga kihisia, utulivu wa mawazo na fikra, furaha na amani ya kipekee moyoni.

Anapocheza au hata kutangamana na wenzake, anapata kuwasimulia jinsi anavyopendwa na wazazi wake. Jinsi yeye hupigwa pambaja, kuambiwa kuwa ni mtanashati au mrembo na kukumbatiwa na wazazi wake kabla ya kulala.

Mtoto huathiriwa mno na anachokiona au kushuhudia. Anapomwona babake anaishi na mamake kwa upendo na amani, yeye ataufuata mkondo huo na kuishi vivyo hivyo na mkewe.

Anapomwona ukimtesa na kumpiga mamake, naye ataishia kujua kuwa wanawake ni viumbe dhaifu wanaofaa kuchapwa kila mara.

Cha muhimu mno ni kumlea mwanao katika njia za Mungu. Mfunze kuwa watu hawafai kula bila kuomba, waongoze katika kuomba na kusoma Bibilia au Kuraan nyumbani kama mzazi.

Mfunze njia za Mungu maana Bibilia inasema kuwa ‘mlee mtoto katika njia ipasavyo, naye hataiacha hata atakapokuwa mzee.’ Usifanye kazi au hata majukumu mengine yakutenganishe na mwanao.

Keti chini na mwanao, zungumza naye ili upate kufahamu mawazo, hofu, nguvu zake, udhaifu wake, talanta yake, rangi aipendayo, yanayompendeza na mahitaji zake za kibinafsi.

Usije ukajuta na kulalamika kuwa humfahamu mwanao ilhali wewe hukumtengea muda wa kumfahamu ipasavyo.

WANTO WARUI: Likizo ya majuma 18 kwa wanafunzi wa gredi ya 4 haifai

NA WANTO WARUI

HUKU wanafunzi wakijaribu kung’ang’ana ili warejelee hali ya kawaida ya masomo baada ya kuvurugwa na kuwepo kwa ugonjwa wa Covid-19, Wizara ya elimu tayari imetoa kalenda ya shule inayotoa mwelekeo hadi mwaka wa 2023.

Katika kalenda hiyo, wanafunzi wa Gredi ya 4 ambao iliwabidi kufungua mapema kidogo pamoja na darasa la 8 na kidato cha 4, wamepangiwa kukaa nyumbani kwa majuma kumi na manane – takriban miezi minne na nusu, katika likizo ijayo.

Hivi ni kusema kuwa baada ya wanafunzi wa Gredi ya 4 kufunga shule tarehe 19/03/2021 watakaa nyumbani hadi wafungue tarehe 26/07/2021.

Wizara ya Elimu imepanga kalenda hiyo hivyo kwa kutoa sababu kwamba wanafunzi wa Gredi ya 4 walitangulia shuleni wakati ya wenzao waliokuwa nyumbani. Aidha, inatazamiwa kuwa silabasi ya Gredi ya 4 itakuwa imekamilika kufikia Machi 19, wakati wa kufunga shule.

Jambo jingine ambalo huenda lilichangia wanafunzi hao kupangiwa hivyo ni kwa lengo la kurejelea mwaka wa masomo pamoja na wenzao hapo Julai 26, 2021 ili waingie Gredi ya 5.

Ingawa ni mpango mzuri, kuwataka wanafunzi kukaa nyumbani tena kwa miezi minne na nusu baada ya kusoma tu kwa mihula miwili mifupi ni kuwakosea.

Ni vyema ikumbukwe kuwa wanafunzi hao bado wangali na makovu ya vidonda vya Covid-19 kwa kukaa bila masomo kwa miezi tisa.Haina maana halisi kutoa sababu za kuwaweka nyumbani tena kwa muda mrefu vile. Mpango maalum ungeundwa wa kuhakikisha kuwa wanafunzi hawa wanaendelea na masomo yao badala ya kulaza damu tu kule nyumbani.

Wizara

Kwa mfano, Wizara ya Elimu ingeagiza baraza la mitihani nchini, KNEC, kuandaa mafunzo na majaribio angalau ya miezi miwili kama yale waliyofanya katika Gredi ya 3 ambayo yangewaweka wanafunzi hao katika hali bora zaidi ya kujitenga kutokana na ushawishi mbaya wakiwa nyumbani.

Mpango kama huu ungewaokoa wanafunzi hawa kutoka kwenye uzembe wa kukaa tu nyumbani. Aidha, ungetatua tatizo la kuwapa wazazi mzigo mkubwa wa kuwindana na wana wao mchana ilhali mahitaji ya kuwakimu yanahitajika.

Licha ya kuwa wanafunzi wa Gredi ya 4 wamekuwa shuleni kwa mihula miwili, bado kuna kazi nyingi sana ambazo hawajaweza kuzifanya ambazo zinahusiana na masomo yao.

Kwamba ndiyo gredi inayotanguliza mfumo wa CBC, kuna kila sababu ya kuwatayarisha wanafunzi hawa vyema kabisa wasije wakatetereka.Na huu ndio ungekuwa wakati mwafaka zaidi wa kuandaa wanafunzi hawa wa Gredi ya Nne badala ya kuwaelekeza nyumbani tena kwa majuma 18 wakakae bure!

Mungu ni mkuu, asema mkurugenzi baada ya kuondolewa mashtaka ya wizi wa watoto

Na RICHARD MUNGUTI

NAIBU wa Mkurugenzi wa huduma za afya katika shirika la utoaji huduma kaunti ya Nairobi (NMS) Dkt Musa Mohammed Ramadhan Jumatatu alimshukuru Mungu nje ya mahakama kuu ya Nairobi baada ya kuondolewa mashtaka ya wizi wa watoto katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki mwaka uliopita.

“Namshukuru Mungu kwa kuniondolea kesi niliyoshtakiwa nayo mwaka jana. Kama vile nilivyosema mbeleni kwamba sikuhusika na wizi wa watoto, hivyo ndivyo polisi wamepata baada ya uchunguzi wa kina. Sasa niko huru,” alisema Dkt Ramadhan alipohojiwa na Taifa Leo baada ya kuachiliwa.

Mshtakiwa huyo alipiga magoti nje ya mahakama kuu ya Milimani na kusema “(Alahu Akbara) Mungu ni mkuu”. Watu wa familia yake waliofika mahakamani kufuata kesi walifurahi wote.

Wote nje ya mahakama wakiongozwa na Dkt Ahmed Kalebi walisema “Alahu Akbar”. Dkt Ramadhan alipiga bismilahi tatu kisha akaanza kudodokwa na machozi.

Watu wa familia yake waliandamana kuenda nyumbani. “Tutasherehekea nyumbani,” Dkt Kalebi aliambia Taifa Leo.

Naibu wa Mkurugenzi wa huduma za matibabu kaunti ya Nairobi Dkt Musa Ramadhan asujudu nje ya mahakama ya milimani baada ya kuondolewa mashtaka ya kuwaiba watoto alipokuwa kinara wa hospitali ya mama Lucy na kuwauza. PICHA/ RICHARD MUNGUTI

Alisema Dkt Ramadhan amekuwa kielelezo chema kwa watu wa jamii ya Wanubi nchini “ikitiliwa maanani tuko na madaktari watano tu.”

Dkt Ramadhan alisema amewasamehe waliomwekelea madai ya uwongo.

“Sitaishtaki Serikali kwa kuniharibia sifa haswa kuniusisha na wizi wa watoto wachanga. Vile nimeondolewa lawama sina chuki na yeyote na nitaendelea kutoa huduma zangu kama hapo mbeleni,”alisema Dkt Ramadhan.

Daktari huyo aliondolewa lawama miezi minne baada ya madaktari wakuu katika hospitali hiyo Dkt Emma Mutioa na Dkt Regina Musembi kuachiliwa.

Madaktari hao wakuu walitiwa nguvuni kufuatia ufichuzi katika shirika la habari la BBC kwamba kuna kashfa inayoendelea na kuwauza watoto.

Shirika hilo lilitangaza kuwa watoto walikuwa wakiibwa kutoka kwa kina mama maskini na kuuzwa na maafisa wa hospitali hiyo kwa bei ya Sh45,000.

Dr Ramadhan aliondolewa mashtaka baada ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) kusema hakua ushahidi wa kumuhusisha na kashfa hiyo.

Watu wa familia yake waliofika mahakamani kufuata kesi walimpa busu. PICHA/ RICHARD MUNGUTI

Akiwasilisha ombi la kutamatisha kesi dhidi ya Dkt Ramadhan kiongozi wa mashtaka Bi Evalyene Onunga alimweleza hakimu mwandamizi Bi Esther Kimilu kuwa sasa mshtakiwa huyo(Ramadhan) atakuwa shahidi katika kesi dhidi ya maafisa wa masuala ya kijamii hospitalini humo Bw Makallaa Fred Leparan na Selina Adundo Awuor.

Bi Kimilu alitamatisha kesi dhidi ya Dkt Ramadhan kisha “akaamuru mshtakiwa arudishiwe dhamana ya Sh200,000 pesa tasilimu aliyokuwa amelipa kortini.”

Punde tu baada ya kuachiliwa kwa kinara huyo wa huduma za matibabu kaunti ya Nairobi shahidi wa kwanza, wakili Brian Kimeu Muia alisimulia jinsi alimuokota mtoto mchanga aliyekuwa ametupwa ndani ya kibanda cha kuuzia mboga kwenye barabara ya Outering Nairobi.

Bw Muia aliyekuwa na rafikie Bw Morris Nguyo Muki walimsikia mtoto huyo mchanga akilia kwa kutoa sauti kama ya Paka.

“Morrris alinieleza sauti hiyo ni ya jini..Nilimueleza hata mimi sijawahi ona jinni tuingie kibandani tumwone,” Bw Muia alisimulia.

Shahidi huyo alisema walimpeleka mtoto huyo kwa mzee wa kijiji mtaani Savana na hatimaye wakampeleka kituo cha polisi.

“Nilipewa barua nimpeleke hospitali ya mama Lucy ambapo tulimkabidhi Bw Leparan.

“Mtoto huyo aliyekuwa mchanga alipelekwa kuhifadhiwa katika idara ya watoto kisha nikamwandikia barua Dkt Ramadhan nikiomba niruhusiwe kumridhi mtoto huyo niliyempa jina Taji,” Bw Muia alisema.

Bw Muli aliyetoa ushahidi pia alitahadharishwa dhidi ya kuongea lugha ya Sheng kortini.

“Hiyo lugha unayoongea hapa kortini ya Sheng sio rasmi. Zugumza kishwahili sanifu,” Bi Onunga alimweleza Bw Muli.

Bw Muli alikuwa ameeleza mahakama jinsi yeye na Bw Muia na marafiki wengine walienda “kupiga tembo (kubugia pombe) kuchangamkia ubabe wa rafiki yao katika biashara yake.”

Aliposema hayo Bi Kimilu alimwuliza shahidi alichokuwa akisema na kuonywa asizugumze lugha ya sheng kortini.

Bw Muli alianza kuzugumza Kiswahili sanifu na kusimulia jinsi walimuokota mvulana aliyekuwa amezaliwa Mei 4 2020 na kutupwa.

Kesi inaendelea.

WANDERI KAMAU: Jamii imefeli ila ijikakamue kuelekeza watoto kimaadili

Na WANDERI KAMAU

KATIKA jamii, msingi wa kizazi cha baadaye huanza kuwekwa mara tu watoto wanapozaliwa. Msingi huo unaweza kuwa mbaya au mzuri.

Unaweza kuwa wa kukifaa kizazi hicho, kukielekeza ama kukipotosha. Msingi ambao kizazi husika hulelewa nao huja kujitokeza katika siku za usoni, hasa kwenye ukubwa wacho. Ni katika kiwango hiki ambapo maadili mema, sawa na maadili mabaya hudhihirika.

Vile vile, ni kwenye ukubwani ambapo mbivu na mbichi huonekana.Natoa urejeleo huu kufuatia ongezeko la visa vya utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi, hasa kwenye shule za upili, ambavyo vimeshuhudiwa kwa majuma mawili sasa baada yao kurejea shuleni.

Visa ambavyo vimeripotiwa kwa majuma hayo ni vya kusikitisha. Ni matukio ya kuatua moyo, kuhusu ikiwa yanafanywa na wanafunzi au watu razini waliogeuka kuwa wahalifu.

Katika siku za hapo nyuma, ilikuwa nadra kusikia kisa kuhusu mwanafunzi anayemshambulia mwalimu au mlinzi hadi akamuua. Visa vya wanafunzi kuwavamia wazazi wao vilikuwa matukio ambayo hayangesikika hata kidogo.

Hata hivyo, hali imebadilika.Sababu kuu ni kuwa vizazi vya wanafunzi wa hapo awali viliongozwa na maadili. Vilizingatia miiko na miongozo ya kijamii. Vilifahamu kuhusu umuhimu wa kuwaheshimu wakubwa wao. Vilielewa kwa undani athari za kutozingatia miongozo vilivyopewa na walezi wao.

Miongoni mwa athari hizo ni laana ambazo ziliaminika kutoka kwa “miungu.”Kimsingi, lengo kuu la tahadhari hizo lilikuwa kujenga uwepo wa kizazi ambacho kingeifaa jamii baadaye.

Lengo lake pia lilikuwa kuwajenga watu ambao wangeweza kupitisha maadili hayo kwa watoto, wajukuu, vitukuu na hata vilembwekeza wao.

Matokeo ya ulezi huo mzuri ulikuwa ni uwepo wa mashujaa waliopigania uhuru wa kwanza na wa pili, wasomi maarufu, wanamichezo wa kuheshimika, waalimu waadilifu, madaktari wasio wabinafsi kati ya wanataaluma wengine wenye utu na ubinadamu.

Enzi hizo, shule zilikuwa jukwaa nzuri lililoheshimika na kila mmoja kwani kando na wanafunzi kufaidika kimasomo, zilitoa mazingira mwafaka ya kimalezi kwa wanafunzi na jamii nzima.

Wazazi walikuwa huru kumwadhibu mtoto yeyote waliyempata akikosea. Chini ya mwelekeo huo, watoto kwenye vijiji waliwaheshimu wakubwa wao kwani waliwachukulia kama wazazi waliowalea.Hata hivyo, hali ni tofauti sasa. Badala ya mahali pa hekima na maadili, shule zimegeuka kuwa ngome za maafa, umwagikaji damu na utovu wa nidhamu.

Badala ya wanafunzi kuwa kioo chema cha maadili kwa wadogo wao, wamegeuka kuwa mifano ya kuogopwa kutokana na nyendo zisizofaa. Wanaogopwa na kila mmoja katika jamii.

Wakubwa kwa wadogo na vijana kwa wazee. Hawajali wala hawabali. Hawaambiliki wala hawasemezeki. Wamejifanya ‘wajuaji’; ‘wajuaji’ wasiojua watokako wala waelekeako.Kwa mkasa huu, nawalaumu wazazi, walimu na jamii ya sasa. Nawalaumu kwa kutoweka msingi ufaao kwa wanao.

Nawalaumu kwa kuwapa uhuru ambao sisi hatukupewa.Nawalaumu kwa kutowadhihirishia kuwa njia ya maisha si rahisi. Ni ndefu na yenye kujitolea kwingi. Ili kuokoa jahazi na kizazi chetu, ni wakati turejelee kanuni za awali kuhusu ulezi mwema.

akamau@ke.nationmedia.com

Sababu za kudhibiti filamu wanazotazama watoto

Na SAMMY WAWERU

Ni jambo la kuhuzunisha familia kupoteza watu watano kwa wakati mmoja, kupitia kitendo cha ukatili. Juma lililopita, taifa lilishtushwa na taarifa ya mvulana anayeshukiwa kuua babake, mamake, kaka yake na binamu pamoja na mfanyakazi katika Kaunti ya Kiambu.

Huku Idara ya Uchunguzi wa Jinai na Uhalifu (DCI) ikiendeleza uchunguzi baada ya mshukiwa huyo mkuu kufunguliwa mashtaka mahakamani, Lawrence Warunge, 22, alikiri kushawishiwa na filamu ya Kibritania (British) kutekeleza mauaji hayo ya kinyama.

Akikiri kutekeleza mauaji, kijana Warunge na ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha MKU, alieleza maafisa wa DCI kwamba filamu ‘Killing Eve’ ilimchochea kuondoa uhai wa jamaa zake.

Ni kisa cha kuhuzunisha na kinachopaswa kuwa mwamko wa wazazi na taifa kwa jumla kufahamu kwa kina filamu na michezo ya kuigiza inayopeperushwa kwenye runinga na pia kupakiwa mitandaoni.

Warunge kukiri filamu hiyo potovu kimaadili na kimatendo kwa watoto na vijana wetu, ilimchochea kuua wanafamilia ni jambo linalopaswa kututia wasiwasi, wasiwasi mkubwa mawazo ya watoto wetu yakitekwa bakunja na ‘maisha na tabia za ughaibuni’.

Kitendo hicho kiwe mwamko, wazazi wawe makini wanachotazama wanao.

Isemwavyo, udongo uwahi ukiwa maji na pia samaki mkunje akiwa angali mbichi, maisha ya baadaye ya watoto na vijana yanategemea msingi wa malezi hasa wakiwa wangali wadogo kiumri.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Kukagua Filamu Nchini (KFCB), Dkt Ezekiel Mutua amekuwa akikariri mara kwa mara haja ya runninga kuchuja filamu zinazopeperushwa.

Huku baadhi ya wakosoaji wake wakimsuta kutokana na msimamo wake mkali, Dkt Mutua amekuwa akiweka wazi mmomonyoko wa kimaadili na nidhamu unaoshuhudiwa miongoni mwa watoto wetu na vijana unachangiwa na wanachotazama kwenye runinga na pia machapisho mitandaoni, video na picha zinazopakiwa.

“Tunaposema kinachotazamwa na watoto wetu kinachangia kudorora kwa usalama wa kitaifa, tukio kama hili (Lawrence Warunge kukiri kuchochewa na filamu potovu kuua jamaa zake) ndilo tunamaanisha.

“Baadhi ya yanayopeperushwa na vyombo vya habari yanachangia kuathiri tabia na fikra za wateja, hususan watoto. Watoto wanaotazama filamu za kivita huishia kushiriki vita mara kwa mara wanapokomaa,” Dkt Mutua anaelezea.

Akionya vyombo vya habari, Afisa huyo Mkuu wa KFCB anasema matangazo mengi ya vyombo vya habari hasa vituo vinavyolipiwa ada, yanasifia vita na uhalifu, dawa za kulevya, ngono, ubakaji na lugha chafu.

“Wazazi hulipia ada watoto kutazama vituo hivyo bila kujua programu zinazopeperushwa. Hatimaye wanapotoka kimaadili machoni pao,” Dkt Mutua anasema, akionya tahadhari isipochukuliwa huenda maadili ya vijana yakageuzwa na filamu wanazotazama.

“Umewadia wakati tukaze kamba sheria kudhibiti yanayopeperushwa katika vyombo vya habari.”

Kwa hakika kauli na msimamo wa Dkt Mutua ni bayana na yenye ukweli, hasa unapotazama watoto mitaani wakicheza, baadhi utawaona wakiwa na vifaa vya kuchezea vyenye muundo wa bastola au bunduki.

Wakiiga wanayotazama kwenye filamu, utawaona wakifyatulia wenzao ‘risasi’, ishara ya kushawishiwa na program hizo hatari.

Ili maji yasizidi unga, kisa cha mauaji ya Kiambu kiwe mwamko kwa wazazi na vyombo vya habari yanayopeperushwa yadhibitiwe.

Teknolojia inavyozidi kuimarika kila uchao, ni muhimu kufahamu ina mchango mkubwa katika malezi ya watoto na vijana, ambao ni wazazi na viongozi wa kesho.

Kwa hakika, wanahitaji malezi bora na yenye uadilifu wa hali ya juu ili wawe kielelezo katika jamii na kwa vizazi vijavyo.

Ni muhimu watoto kuruhusiwa kushiriki michezo

Na MISHI GONGO

MICHEZO ni kiungo muhimu katika ukuaji na uimarikaji wa mtoto katika nyanja mbalimbali.

Michezo huchangia katika ukuaji wa akili, mawazo, kuwafanya watoto kuwa na uwezo wa kutatua mizozo baina yao na hata kuwapa ujuzi wa kutangamana na watu wengine.

Zamani watoto wakishiriki michezo mengi iliyohusisha wao kukimbia, kurukaruka na kadhalika.

Mifano ya michezo iliyochezwa na watoto wa miaka ya tisini hadi 2000 ni kama mpira wa kulengana kwa wasichana, kupika, kuruka blada, uku na mingineyo huku wavulana wakicheza mpira wa miguu, michezo ya kutengeneza magari, kujenga nyumba, kuigiza taaluma mbalimbali ,kulenga shabaha, kuogelea na kadhalika.

Michezo hiyo iliwawezesha watoto kunyoosha viungo vyao na kuwa wachangamfu.

Hata hivyo, michezo hiyo kwa sasa imepotea mijini ambapo watoto wengi kwa sasa wanapendelea kuchezea simu aina ya smartphone, michezo ya kudhibitiwa na rimokonto au kuangalia sinema katika runinga.

Kulingana na utafiti uliofanywa hivi majuzi na shirika la utafiti la watoto Mudorch, ni kwamba watoto kuangalia runinga au kipakatalisha kwa zaidi ya muda wa saa moja kwa siku kunawaathiri akili zao na pia kupunguza uwezo wao wa kukumbuka vitu.

Utafiti uliyofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2019 ulipendekeza watoto kuanzia umri wa miaka miwili hadi mitano kuangalia televisheni kwa saa moja kwa siku huku wale wa chini ya umri wa miaka miwili ikipendekezwa kutoruhusiwa kuangalia runinga.

Aidha mtoto kuangalia televisheni kwa muda mrefu pia kumehusishwa na watoto kupata athari za kiafya kama kuwa wazito kupindukia na kufanya vibaya katika masomo yao.

Bi Dolicate Oloo mwalimu mkuu katika shule ya mmiliki binafsi ya Skyways alisema kuwa ni muhimu kwa watoto kucheza michezo ya kurukaruka.

Alisema watoto wanaofaulu zaidi darasani ni wale walio wachangamfu uwanjani.

“Katika shule yetu tunawahimiza watoto kucheza. Mara kwa mara tunaandaa warsha za michezo ambazo tunawahusisha wazazi na watoto wao. Hili pia husaidia wazazi na watoto kuwa na uhusiano mwema,” akasema.

WATOTO: Ujasiri wa kuwa mwanamitindo kuanzia umri mdogo

Na PHYLLIS MUSASIA

Clara Mereso ni mwanafunzi wa Darasa la Kwanza katika shule ya Melvin Jones Lions Academy mjini Nakuru.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka sita ana uraibu katika maswala ya unamitindo ambao alianza akiwa na miaka mitatu.

Hadi sasa, ameweza kushinda mataji matatu ikiwemo, Little Miss Peace Nakuru, taji ambalo alishinda mnamo mwaka wa 2017, Tiny Miss Kenya Nakuru, mnamo 2018 na Tiny Miss World Kenya mnamo 2019.

Ujasiri alionao umemwezesha kupata fursa ya kushiriki katika matangazo ya bidhaa za kampuni ya Dura Coat pamoja na mashindano ya Rosy.

Mereso amewai pia kushiriki katika tamasha za wasanii ambazo zilihusisha watoto kama vile Churchil Kids Festival na makaribisho ya msanii Avril nyumbani kwao Nakuru.

Taifa Leo Dijitali ilipokutana naye nyumbani kwao katika kaunti ndogo ya Nakuru Mashariki, Mereso alisema kuwa hatolegeza Kamba katika ndoto yake ya kuwa mtunza amani atakapokuwa mkubwa.

Kulingana naye, mamake amekuwa wa msaada sana katika juhudi zake licha ya umri wake. Katika kushinda taji zote, mamake amemwelekeza na kumshauri vilivyo.

“Ninaamini kuwa nilizakuwa kuwa mshindi na nitafanya bidii kuhakikisha kuwa ninashinda katika kila jambo nitakalo shiriki,” akasema.

Aliongeza kuwa, “mama amenifunza kuwa mvumilivu, kumtegemea Mungu na kuamini kuwa kila jambo linawezekana.”

Mereso anaamini kuwa yeye ni msichana mrembo na mwenye akili zaidi ulimwenguni.

Clare Mereso mwenye umri wa miaka 6 ni mwanafunzi wa gredi ya kwanza katika shule ya Melvin Jones Lions Academy mjini Nakuru. Yeye ni mwanamitindo na ameshinda tuzo tatu tangu 2017. Picha/ Phyllis Musasia.

Aidha, anatazamia kushinda taji zaidi siku zijazo.

“Nilipokuwa na umri mdogo kuliko sasa, watu wengi walinieleza kuwa mimi ni mrembo na hadi sasa bado wao husema hivyo. Wakati huo, sikuelewa walimaanisha nini lakini leo hii, ninazidi kujifunza jinsi ya kufanya makuu ili mafanikio yangu iandamane zaidi na urembo wangu,” akasema.

Kabla kuzuka kwa janga la corona, Mereso alishiriki katika mafunzo ya modeli kila Jumamosi katika shule ya Little Big Talents ambayo huendesha shughuli zake katika hoteli ya Kunste mjini Nakuru.

“Mwalimu wangu anaitwa Bi Joan Musumba na amenifunza mambo mengi sana. Ana fadhili na ni mkufunzi bora zaidi kati maswala ya modeli ya watoto,” akasema Mereso.

Wakati huu wa janga, Mereso hutumia wakati wake mwingi kusoma akiwa nyumbani kupitia mtandao wa zoom.

Anajifunza pia kuhusu nyimbo katika mtandao kwa kutumia simu ya mkononi ya mamake.

“Kila wakati niapokuwa nimemaliza masomo ya siku, mimi hujihusisha katika kusikiza mziki na kujifunza kuimba kwa sauti nzuri. Ningependa pia kuwa msanii wa nyimbo za kuhubiri amani,” akasema.

Tayari Mereso anasaidiwa na mamake kutunga wimbo ambao unahusu usalama wa wototo wakati huu wa janga la Covid-19.

Kulingana naye, wakati huu ambapo hafla na sherehe zimesitishwa ili kuzuia maambukizi ya Covid-19, kutangamana na watoto wengine imekuwa vigumu na ndio sababu anatunga wimbo ili kuwafikia wengi mahali ambapo walipo.

Anasema kupitia wimbo huo atatumia mitandao za kijamii kama vile Facebook na Youtube ili kuwasilisha ujumbe wake.

“Wakati huu ambapo siendi katika mafunzo, mama yangu ndio mwelekezi na anafanya kazi nzuri. Ananipa mifano ya watu ambao walianza kama mimi na sasa wamefaulu. Ananishauri pia nikaze mwendo,” akasema Mereso.

Licha ya kwamba, Mereso anauraibu katika maswala mbalimbali, masomo yatasalia kuwa kipaumbele siku zote.

Watoto wa kurandaranda waokolewa

Na WINNIE ATIENO

ZAIDI ya watoto 1,400 wa kurandaranda humu nchini walikusanywa, kurekebishwa tabia na kujumuishwa na familia zao tangu Kenya ianze kukabiliwa na janga la corona Machi.

Kulingana na mwenyekiti wa bodi ya Street Families Rehabilitation Trust Fund (SFRTF), Bi Linah Jebii Kilimo, watoto hao wa kurandaranda sasa wanapokea malezi bora kutoka kwa familia zao.

Hata hivyo, Bi Kilimo alieleza namna watoto hao wanaendelea kudhulumiwa kingono, akisema wengi wanalazimika kutumia dawa za kulevya, kujihusisha na sinema chafu na ukahaba wa watoto.

“Waototo wa kurandaranda wanaendelea kudhulumiwa huku haki zao zikikiukwa kutokana na mazingira wanamoishi,” alisema Bi Kilimo alipozuru makao ya watoto wa kurandaranda wanaorekebishwa tabia ya Onesmus Good Boys Centre.

Mkurugenzi wa Onesmus Good Boys Centre Joseph Matheka. Picha/ Winnie Atieno

Hata hivyo, Bi Kilimo aliwasihi wazazi na wale waliotwikwa jukumu la kulea watoto kuhakikisha wanapata malezi bora ili wasitokomee mitaani.

“Wapatie watoto hao mazingira na malezi bora; wale waliorekebishwa tabia nao msiwanyanyapae. Tunajizatiti kuokoa watoto wa kurandaranda ili wajumuike na familia zao,” alisisitiza Bi Kilimo.

Akinukuu ripoti ya kitaifa ya watoto wa kurandaranda, Bi Kilimo alitaja sababu za kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaotokomea kuishi mitaani ikiwemo ufukara, familia kutengana, vita na dhuluma nyumbani kwao, maradhi, malezi mabaya na wengine kuachwa peke yao kujilea.

Hata hivyo, Bi Kilimo alisema watoto hao wanaendelea kupewa mafunzo ili waweze kujikimu kimaisha.

Mkurugenzi wa Onesmus Good Boys Centre Joseph Munyasya Matheka alisema watoto hao hunyanyapaliwa licha ya kwamba ni watoto tu wa kawaida ambao wasipoelekezwa wanapotoka kimaadili, lakini wakipewa ushauri na maelekezo wanakuwa watu wazuri katika jamii.

Wazazi washauriwa wasiwe wakifarakana mbele ya watoto wao

Na MISHI GONGO

MAAFISA katika idara za watoto mjini Mombasa wamewataka wazazi kutogombana mbele ya watoto wao, wakisema hali hii huwaathiri watoto kisaikolojia.

Wakizungumza katika Maadhimisho ya Mtoto wa Kiafrika walisema zaidi ya watoto 52 wameokolewa kutoka mitaani baada ya kutoroka majumbani mwao kufuatia mizozo kati au baina ya wazazi.

Afisa wa watoto mjini Mombasa Bw Philip Nzege alisema kufuatia mafarakano ya wazazi, baadhi ya watoto huamua kutoroka na kuanza maisha barabarani.

“Wanapokuwa mitaani, wanajiweka katika hatari mbalimbali zikiwemo kunajisiwa, kushawishiwa kushiriki katika utumiaji wa mihadarati na hata kupewa mimba za mapema,” akasema.

Aliwaomba wazazi kuhakikisha wanatatua mizozo yao mbali na watoto.

Bi Selina Maitha afisa wa polisi aliyeongea kwa niaba ya kamishna wa Mombasa Bw Gilbert Kitiyo, alisema tangu kuzuka kwa janga la Covid-19 watoto mjini Mombasa wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali.

Aidha aliwaonya wazazi wanaowatumia watoto wao kama vitega uchumi.

Alisema baadhi ya wazazi wanawatumia watoto kuokota chupa barabarani kwa akili ya kuuza bila kuzingatia hali yao ya afya.

“Katika doria zetu tunakutana na watoto wanaokota chupa na vyuma barabarani bila maski ambapo tunapowashika na kuwadadisi watoto hao husema kuwa wametumwa na wazazi wao,” akasema.

Hata hivyo, alisema wameungana na wazee wa mitaa kuhakikisha kuwa watoto hawadhulumiki mitaani nyakati hizi ambapo shule zimefungwa.

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kiafrika husherehekewa kila mwaka baina ya Juni 15 na Juni 16 kuwakumbuka watoto walioleta mageuzi mwaka 1976 Soweto, Afrika Kusini.

AFYA: Kucheza na sabuni kwaweza kumletea mtoto asthma

Na LEONARD ONYANGO

Unahifadhi wapi sabuni baada ya kufua nguo, kuoga au kuosha vyombo nyumbani? Ikiwa unaweka katika sehemu ambayo inaweza kufikiwa na watoto, basi umekuwa ukiwaweka hatarini kupatwa na maradhi ya pumu (asthma) bila kujua.

Watafiti sasa wanasema kuwa watoto wachanga wanaochezea sabuni mara kwa mara wako katika hatari ya kupatwa na maradhi ya asthma.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Simon Fraser cha nchini Canada ulihusisha watoto 2,000 wa umri wa chini ya miezi minne.

Watoto hao hawakuwa wamewahi kuwekwa katika mazingira yaliyo na moshi ya wavutaji wa sigara na zaidi ya asilimia 70 kati yao hawakuwa na mtu katika familia yao ambaye amewahi kuugua maradhi ya asthma.

Watoto hao walilelewa kwenye mazingira yaliyokuwa na sabuni kwa muda wa miaka mitatu. Baadaye walipimwa kubaini ikiwa walikuwa na maradhi ya asthma au la.

Watafiti hao walibaini kuwa karibu asilimia 40 ya watoto hao walikuwa na ugonjwa wa asthma walipofikisha umri wa miaka mitatu.?Karibu ya asilimia 100 ya watoto waliopatikana na maradhi ya asthma walilelewa kwenye mazingira yaliyokuwa na sabuni ya kuoshea vyombo vya jikoni, kufulia nguo na kusafishia sakafu.

Asthma ni ugonjwa unaoathiri njia ya kutoa au kuingiza hewa kweye mapafu.?Njia ya kupitisha pumzi huwa nyembamba, hufura na kutoa kamasi jingi zaidi. Kamasi hilo humfanya mwathiriwa kupumua kwa shida na huanza kukohoa na kuhisi kuishiwa pumzi.

Wakenya zaidi ya milioni 4 wanaaminika kuugua maradhi ya asthma.?Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) Evanson Kamuri, idadi kubwa ya Wakenya wanaougua asthma wanapatikana katika maeneo ya mijini.

“Hii ni kwa sababu maeneo ya mijini yako na hewa chafu zaidi ikilinganishwa na maeneo ya vijijini. Hewa ya maeneo ya mijini inachafuliwa na viwanda, magari mengi, marundo ya takataka, kati ya mambo mengineyo,” anasema.

Ugonjwa wa asthma hauna dawa lakini dalili zake zinaweza kudhibitiwa kwa kutumia dawa. Ugonjwa huo unapotambuliwa mapema, makali yake yanaweza kupunguzwa.

Kwa kawaida waathiriwa wa asthma hutumia kifaa kinachojulikana kama ‘inhaler’ ili kupunguza makali ya ugonjwa huo.

Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa jiji la Nairobi na mji wa Eldoret zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa asthma na wengi wa waathiriwa ni watoto wakati ya umri wa miaka 10 na 14.

Kulingana na watafiti wa Chuo Kikuu cha Simon Fraser sabuni za unga au majimaji zinazotoa harufu ndizo zinahusishwa zaidi na maradhi ya asthma.

Watafiti hao wanasema watoto wa umri wa chini ya mwaka mmoja wako katika hatari kubwa ya kupatwa na asthma kwa sababu kinga zao za mwili zingali hafifu na mfumo wa upumuaji haujakomaa.

Watoto pia hutumia muda wao mwingi wakichezea vitu mbalimbali kama vile sabuni na kutambaa kwenye sakafu iliyosafishwa kwa sabauni.

“Tafiti za hapo awali pia zimewahi kuhusisha sabuni na maradhi ya kupumua hivyo hatukushangazwa na matokeo hayo,” wakasema watafiti hao.

Wataalamu wa afya wanasema kuwa baadhi ya aina ya sabuni zinatengenezwa kwa kemikali zinazojulikana kama formaldehyde na 1,4-dioxane, ambazo hudhuru mapafu. Asilimia 22 ya sabuni zinazotumiwa nyumbani zimesheheni kemikali zinazosababisha asthma.

Kemikali inayojulikana kama benzalkonium chloride, ambayo hupatikana katika sabuni za kuua bakteria pia husababisha asthma.?Kemikali nyingine inayojulikana kama borax au boric acid ambayo hupatikana kwenye sabuni inatatiza homoni mwilini.

Wataalamu wanashauri wazazi kuepuka kutumia sabuni zinazotoa harufu kama njia mojawapo ya kuwakinga watoto dhidi ya kupata asthma.

Wataalamu wa afya wanashauri watu kununua sabuni zisizo na kemikali ambazo si hatari kwa watoto kwa kusoma viungo vilivyotumiwa kuitengeneza.

Kulingana na madaktari, maradhi ya asthma hayawezi kuambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine.

“Ugonjwa wa Asthma unaweza kurithishwa kutoka kwa mzazi hadi kwa mtoto. Lakini hauwezi kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine. Kadhalika, ugonjwa huu hauna dawa mara nyingi mwathiriwa hupewa dawa ya kuutuliza tu,”anasema Dkt Torooti Mwirigi.

Mtu aliye na ugonjwa wa asthma anaweza kuhisi ugumu wa kupumua anapokuwa kwenye mazingira ya vumbi, moshi wa magari na manukato yenye harufu kali.

Mgonjwa wa asthma ambaye tayari ameonyesha dalili za kuwa na ugumu wa kupumua anaweza kusaidiwa kwa kumsihi kupumu kwa utaratibu.

Mletee mwathiriwa kifaa cha inhaler ambacho hutumika kusukuma dawa kwenye mapafu kupitia mdomoni.

Madaktari pia wanashauri kuwa unaweza kumketisha wima mwathiriwa na kulegeza nguo ili apate hewa ya kutosha.

Watoto wawili wapatikana katika shimo la choo Juja wakiwa wameuawa

Na LAWRENCE ONGARO

WATOTO wawili wamepatikana katika shimo la choo wakiwa wameuawa katika kijiji cha Riuriro, Murera mjini Juja.

Nyanya ya watoto hao wawili alikuwa amepiga ripoti kituo cha polisi cha Ruiru baada ya kupata habari za kifo chao na kushuhudia miili yao ilipotolewa kwenye shimo hilo.

Imeelezwa kwamba mkazi mmoja wa eneo hilo aliwaona watoto hao wawili wakiandamana na mtu fulani ambaye hakuweza kutambuliwa na baada ya siku moja, miili yao ilipatikana kwenye shimo hilo.

Kulingana na ripoti za polisi ni kwamba mshukiwa huyo alikuwa mume wa mama ya mmoja wa watoto hao na baada ya kukosana walikorofishana na kuachana.

Hata hivyo, mama huyo aliwaacha watoto hao na nyanya yao huku akisafiri nchini Italia kwa shughuli za kikazi.

Watoto hao ambao waliachwa na nyanya yao ni Linus Macharia (7), na Prince Muchina (6), ambao waliripotiwa kupotea baada ya kukosa kurejea nyumbani kutoka shuleni.

Nyanya wa watoto hao Joyce Wangechi alisema alisema yeye ndiye mlezi wa watoto hao baada ya mama huyo kwenda ng’ambo kwa shughuli za kikazi.

Miili hiyo ilitolewa katika shimo hilo walipatikana na majeraha mabaya sana ya visu huku miili hizo zikionekana kuharibika.

“Mimi nilipata habari kuhusu mauaji hayo kutoka kwa wakazi wa hapa baada ya kusema ya kwamba miili miwili ilionekana imetupwa katika lindi la choo,” alisema Bi Wangechi.

Alizidi kuelezea polisi ya kwamba mshukiwa alikuwa mtu wa fujo nyingi kwa muda wa miezi kadha walipokuwa pamoja – na mwanamke aliyesafiri ng’ambo – kama wachumba.

“Alikuwa akimpiga ovyo bila sababu. Hata kuna wakati nilitaka aachane naye ili apate amani,” alisema Bi Wangechi, nyanya ya watoto hao.

Kulingana na kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Juja Bi Dorothy Migarisha, tayari wamemshika mshukiwa wa mauaji hayo na anaendelea kuzuiliwa kabla ya kufikishwa mahakamani ili afanyiwe mashtaka.

“Tutaendelea kumzuilia mshukiwa huyo kwa siku chache ili tujue ukweli wa mambo kabla ya kumwasilisha mahakamani ashtakiwe,” akasema Bi Migarisha.

Kwa wakati huu mshukiwa amezuiliwa katika kituo cha polisi cha Juja huku akiendelea kuhojiwa zaidi kuhusiana na mauaji hayo ya watoto hao.

Miili ya wawili hao imehifadhiwa katika chumba cha maiti cha General Kago mjini Thika, huku familia ikingoja kupata ripoti kamili kuhusu mauaji hayo.

Tume kuchunguza vifo vya watoto 14 shuleni

CHARLES WANYORO na BENSON AMADALA

TUME ya Utendaji Haki kwa Umma, leo imepanga kutembelea Shule ya Msingi ya Kakamega kuchunguza vifo vya wanafunzi 14 walioangamia walipokanyangana wiki iliyopita.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Bi Florence Kajuju anasema watachunguza iwapo afisa yeyote wa serikali alizembea katika wajibu wake.

Akiongea na Taifa Leo, Bi Kajuju alisema watakagua jengo hilo lenye orofa tatu na kuona ikiwa linafaa kutumiwa na wanafunzi wa shule ya msingi.

Wakati wa upasuaji wa miili uliofanywa Ijumaa wiki iliyopita, baadhi ya wazazi wa wanafunzi waliokufa walisema hawakuridhishwa na jinsi upasuaji ulivyofanywa.

Bi Kajuju alisema pia wataangalia ikiwa Mamlaka ya Ujenzi wa Kitaifa ilichunguza na kuidhinisha jengo hilo kuwa salama kwa wanafunzi kusomea, na ikiwa tathmini yao iko sawa.

“Tutaangalia ikiwa mipango ilifuatwa, kama kulikuwa na vyuma vya kujishikilia kwa sababu ninaambiwa hakukuwa na vyuma hivyo kati ya mahali ambapo wanafunzi wangeshikilia. Pia tutaangalia jengo hilo kuona kama mpango na muundo ulikuwa kwa kiwango sahihi,” akasema.

Bi Kajuju aliongeza kuwa ikiwa afisa yeyote wa serikali atapatikana na hatia, tume yake inaweza kupendekeza kwamba mkosaji azuiliwe kuwa ofisini yoyote ya umma, aondolewe kutoka ofisi ya umma na kulipia uharibifu huo.

“Kifo cha wanafunzi 14 hakiwezi kuchukuliwa kimzaha. Tutachukua hatua za kisheria,” Bi Kajuju akaonya.

Wanafunzi wawili ambao walikufa kwenye kisa hicho walizikwa Jumamosi.

Nicole Achola, mwanafunzi wa Darasa la tano alizikwa nyumbani kwa wazazi wake mtaani Maraba. Alikuwa katika shule hiyo kwa miaka miwili pekee.

Babake Nicole, Bw Dalmas Khalusi Masayi, akitiririkwa na machozi alielezea jinsi binti yake alivyofanya bidii masomoni na jinsi alivyokuwa mchangamfu.

“Nitampeza binti yangu sana. Alikuwa kipenzi cha watu wengi,” Bw Masayi akanena.

Mamake Nicole alishikwa na huzuni tele kiasi cha kutoweza kuongea na waombolezaji.

Prince Vermaline, 10, mwanafunzi katika darasa la nne alizikwa Khumusalaba katika kaunti ndogo ya Khwisero.

Mamake, Bi Lavender Akosa hakuweza kuzuia machozi yake na kusema kifo kilimpokonya mtoto wake wa pekee.

Wanafunzi wengine wawili, Fidel Kumbutie kutoka Chimoi katika kaunti ndogo ya Kakamega Kaskazini na Samuel Simekha kutoka Bunyore katika Kaunti ya Vihiga walizikwa jana.

Wanafunzi wengine watatu, Antonnet Iramwenya, Venesa Adesa na Simon Waweru watazikwa leo katika kijiji cha Chamakoti katika Kata ya Vihiga, Navakholo, Eshisiru katika Kaunti ya Kakamega na Milima Mitatu eneo la Molo, Kaunti ya Nakuru.

Wanafunzi wengine, Bertha Munywele, Catherine Aloo na Lavenda Akasa watazikwa Jumamosi ijayo.

Huzuni Kakamega wanafunzi 13 wakifariki shuleni

Na BENSON AMANDALA

BIWI la simanzi Jumatatu lilitanda katika Kaunti ya Kakamega baada ya wanafunzi 13 wa Shule ya Msingi ya Kakamega kuaga dunia shuleni huku  39 wakijeruhiwa.

Maafa hayo yalisababishwa na purukushani iliyozuka wanafunzi hao wakitoka madarasani kuelekea nyumbani.

Walikanyagana na wengine kuanguka kutoka orofa ya tatu.

Wanafunzi wengine 39 nao walipata majeraha mabaya na wanaendelea kulazwa katika hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Kakamega huku wengine 20 wakitibiwa na kuruhusiwa kuenda nyumbani.

Kamanda wa Polisi, ukanda wa Magharibi Peris Kimani alithibitisha idadi ya walioaga dunia katika kisa hicho cha kusikitisha nyakati za jioni.

Aidha, wazazi walikita kambi katika hospitali ya rufaa ya Kakamega wakiwatafuta wanao huku waliowapoteza watoto wao wakipiga nduru na baadhi hata kuzirai kwa kuzidiwa na machungu.

Hali ilikuwa mbaya zaidi hospitalini humo ikizingatiwa wahudumu wachache tu ndio walikwepo kutokana na mgomo unaoendelea wa madaktari katika gatuzi hilo.

Hadi tukienda mitambono, Kamishina wa kaunti ya Kakamega Pauline Dola na Bi Kimani walitarajiwa kuhutubia wanahabari kuhusu mauti hayo.

Kauli za watoto kuhusu Krismasi

Mwanahabari wetu Sammy Kimatu alitangamana na wanafunzi wa  Amazing Grace Academy, Kaiyaba, Kaunti ya Nairobi kuhusu uelewa wao wa Sikukuu ya Krismasi.

Swali: Naomba unipe hoja yako kuhusu jinsi unavyoielewa Sikukuu ya Krismasi

Fridah Nzisa, 10 (pichani juu)

Siku hii ni kubwa kwangu kwa sababu ndiyo Mwokozi Yesu Kristo alizaliwa ili anifilie kwa ajili ya dhambi zangu.

Caroline Mugambi. Picha/ Sammy Kimatu

Caroline Mugambi, 11

Huku Bwana Yesu anaposherehekewa kuzaliwa kote duniani, wazazi huwa wanawapamba wanao kwa mavazi mapya.

Shantel Mwikali. Picha/ Sammy Kimatu

Shantel Mwikali, 10

Ni siku kubwa kwa familia kupeleka watoto nje kutembea na kubarizi na pia kwenda kanisani kwa maombi.

Winnie Ndinda. Picha/ Sammy Kimatu

Winnie Ndinda, 10

Licha ya wanaopinga na kubishania tarehe kamili ya Yesu kuzaliwa, naamini muhimu ni kuwa alizaliwa kuokoa wanadamu.

Eunice Njeri. Picha/ Sammy Kimatu

Eunice Njeri, 8

Ni kukumbuka Yesu wetu alipozaliwa Bethelemu, nchi ya Juda wakati wa enzi ya mfalme Herodi kutawala.

Mercy Wambui. Picha/ Sammy Kimatu

Mercy Wambui, 7

Ni siku kubwa ulimwenguni kuona watoto walifurahia nguo mpya na kupikiwa vyakula pamoja na kutangamana na wageni.

Kelvin Mutuku. Picha/ Sammy Kimatu

Kelvin Mutuku, 10

Krismasi ni siku kunapowekwa baluni na maua nyumbani na maeneo ya burudani kuashiria ukubwa wake.

Prince Kilunda. Picha/ Sammy Kimatu

Prince Kilunda, 8

Ni siku ya nyimbo, kupamba miti kwa maua huku mifugo kama vile kuku, mbuzi na ng’ombe wakiwa vitoweo kwa binadamu.

Evans Mutambu. Picha/ Sammy Kimatu

Evans Mutambu, 10

Licha ya wakristo kuiweka kama ukumbusho wa kuzaliwa kwa Yesu, inatakiwa sisi kuwakumbuka wasiobahatika katika jamii.

Reagan Machuki. Picha/ Sammy Kimatu

Reagan Machuki, 7

Ni siku ambayo wakristo huamini Yesu alifariki na kufufuka tena kwa ajili ya dhambi zao.

Joseph Mburu. Picha/ Sammy Kimatu

Joseph Mburu, 12

Ni siku yenye mbwembwe zake kuanzia jumbe za kutakiana mema na baraka zake Rabuka.

James Mutemi. Picha/ Sammy Kimatu

James Mutemi, 9

Kila kalenda huandikwa Disemba 25 kwa wino mwekundu kumaanisha Mkombozi alizaliwa kama binadamu duniani.

NTV huru kupeperusha kipindi korti ikitupilia mbali kesi

Na Sam Kiplagat

MAHAKAMA moja Nairobi imefutilia mbali kesi ambapo Shirika la kupigania Maslahi ya Watoto Nchini (CWS) lililenga kuizuia NTV dhidi ya kupeperusha kipindi kinachofichua maovu yanayotendeka katika taasisi hiyo ya umma.

CWS ilikuwa imefika katika korti ya watoto na kupata amri ya kuzuia upeperushwaji wa kipindi hicho.

Kampuni ya Nation Media Group ilitii amri na kusitisha upeperushaji wa kipindi hicho baada ya kukabidhiwa agizo la mahakama.

Kupitia mawakili wake wakiongozwa na Bw Gitonga Mureithi, NMG iliwasilisha kesi ikitaka kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo ikihoji kuwa mahakama ya watoto ni korti maalum na inajishughulisha tu na masuala ya watoto wala si kuchafuliwa jina.

Kulingana na Bw Mureithi, kesi ya CWS ililenga kutetea sifa yake na haikuwa na lolote kuhusu maslahi ya watoto.

Korti ilisisitiza kuwa CWS ilikuwa ikidai fidia katika kesi hiyo na haikuwa na mamlaka ya kuendelea kusikiza.Hakimu alitoa uamuzi kuwa hakukuwa na uhusiano kati ya kesi hiyo na ulinzi wa watoto kwa sababu kesi hiyo ilidai fidia kwa kuchafuliwa jina.

 

Mapuuza yazua mauti shuleni

Na VALENTINE OBARA

SHULE ya Msingi ya Precious Talents iliyo katika Wadi ya Ngando, eneobunge la Dagoretti Kusini ilikuwa sawa na mtego wa maafa kwa zaidi ya watoto 800, wataalamu wa masuala ya ujenzi wamesema.

Shule hiyo ya orofa moja iliyojengwa kwa mbao, mabati na nyaya bila vyuma, iliporomoka mwendo wa saa moja asubuhi jana na kusababisha vifo vya watoto saba waliokuwa darasani.

Watoto wengine 64 walipelekwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta ambapo wawili kati yao ndio waliopatikana na majeraha mabaya na wengine kuruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kutibiwa.

Katibu wa Taasisi ya Wahandisi wa Kenya, Bw Nathaniel Matalanga alisema ukaguzi wa vifusi vya shule hiyo ulionyesha kuwa hapakuwa na msingi thabiti, slabu (sakafu ya orofani) ilikuwa hafifu bila vyuma, na ukuta wa mabati haukufaa kwa jengo kama hilo.

“Ujenzi wa jumba haufai kufanywa namna hii. Lazima uchimbe msingi thabiti na ujenge ukuta unaoweza kushikilia uzito. Slabu inafaa kujengwa kwa kokoto. Hii ilikuwa kama inchi mbili hivi na badala ya vyuma, ilikuwa na waya kama wa kujengea kibanda cha kuku. Hata mtu anayejenga choo mashambani hawezi kamwe kujenga jinsi hii,” akasema.

Kisa hicho kilionyesha picha ya hali mbaya ambayo Wakenya wengi hupitia katika mitaa ya mabanda kote nchini wanakoishi.

Katika wadi hiyo ya Ngando, ilibainika hakuna shule yoyote ya umma wala hospitali ya umma. Shule pekee inayoweza kusemekana ni ya umma ni ile ya upili ya Lenana, ambayo ni shule ya kitaifa.

Wazazi na wananchi waliowasili eneo la mkasa kwa haraka kuokoa watoto, walilazimika kutegemea bodaboda kuwasafirisha hadi katika zahanati ndogo inayosimamiwa na Kanisa Katoliki ili kupokea huduma ya kwanza ya matibabu.

Baadhi ya wazazi walisema haingewezekana zahanati hiyo kuhudumia idadi kubwa ya watoto waliokuwa wakikimbizwa huko.

“Nilipompata mtoto wangu amejeruhiwa mguuni na kichwani, nilimchukua mara moja nikamweka kwenye pikipiki na kumkimbiza zahanati ya Katoliki lakini wahudumu wakaniambia hawataweza kumtibu. Nilibahatika kupata ambulensi ikamleta KNH,” akasema Bw Maurice Muthomi, mmoja wa wazazi.

Mbunge wa Dagoreti Kusini, Bw John Kiarie alisema wadi hiyo iliyo na idadi ya watu wapatao 30,000 haina ardhi ya umma ndiposa hakuna shule wala hospitali ya umma.

Ijapokuwa Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alisema serikali itazingatia kujenga shule eneo hilo, kuna shule ya umma iliyo kilomita mbili pekee kutoka wadi hiyo ambayo watoto wanaweza kupelekwa.

“Serikali itajitahidi kuanzisha shule iwapo inahitajika. Suala la mipaka ya wadi halifai kuwa tatizo bali umbali wa shule kutoka mahali ambapo watoto wanaishi. Tutatafuta ardhi kwa njia yoyote ile na kujenga shule hapa miezi mitatu au minne ijayo,” akasema Prof Magoha.

Mmiliki wa shule hiyo, Bw Moses Wainaina, alidai kisa hicho kilisababishwa na mtaro wa maji-taka unaochimbwa karibu, ingawa hili halinwgethibitishwa.

Alisema shule hiyo huwa na wanafunzi karibu 800 kwa jumla na baadhi ya walioathirika walikuwa wakijiandaa kwa Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) unaoanza mwezi ujao.

TEKNOLOJIA: Wanafunzi wako tayari, nani atawafundisha usimbaji wa programu?

NA FAUSTINE NGILA

NI Jumatano mchana katika mji wa Meru, ambapo Taifa Leo Dijitali imetembelea Shule ya Msingi ya St Paul iliyoko mita chache kutoka katikati ya mji wa Meru. 

Wanafunzi kadhaa wamekusanyika darasani huku wakiongeleshana kwa sauti za chini na wengine wakiingia kuketi. Taswira ya nyuso zao na jinsi wanavyotembea kwa mwendo wa asteaste zinadhihirisha fika ujasiri na umakini wao.

Katika kona moja ya darasa hili ni wasichana walioonekana kuzama katika simu zao kwa mapenzi na tabasamu kana kwamba wamesheherekea siku yao ya kuzaliwa jana.

Katikati kuna marijali ambao wanashiriki katika mdahalo kwa kunong’onezeana, wengine wakivitingisa vichwa na wengine wakigongesha mikono yao kwenye madawati kusisitiza maoni yao.

Ghafla mwanamume wa miaka 25 anaingia darasani na kusimama tisti mbele ya darasa, kisha kujitambulisha kama Bw Alex Guantai, mratibu wa mradi wa Code Mashinani katika shule za msingi na upili mwaka eneo la Meru.

Mratibu wa mradi wa Code Mashinani katika shule za msingi na upili mwaka eneo la Meru Bw Alex Guantai akielezea wanafunzi manufaa ya teknolojia. Picha/ Faustine Ngila

WARSHA

Warsha ya teknolojia ya siku tatu imeandaliwa na wazazi wametakiwa kuwashirikisha wana wao wa umri wa miaka 6 hadi 18 kwenye warsha itakayotoa mafunzo ya teknolojia, ili kukuza viongozi wa baadaye.

“Tumepanga kambi ya kufunza kodi ili kuwasaidia wanafunzi kuimarisha fikra zao kufuatia changamoto katika mazingira wanamoishi na jinsi uvumbuzi wa kiteknolojia unaweza kuleta suluhu, ” anasema Bw Guantai.

Brian Mutuma, mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Upili ya Mang’u anapania kuwa wakili atakapofuzu chuoni. Kulingana naye, ni wakati mwafaka kwa watu kuwa na uzoefu wa mabadiliko yanayochangiwa na teknolojia mpya.

“Teknolojia inasambaa kwa haraka na watu watakuwa wakiitegemea . Hii ni kwa sababu mtu hawezi kuwa hodari asilimia 100 ila utumiaji wa teknolojia utarahisisha mambo hata katika kazi tunazofanya,” anasema Brian.

Aidha anapinga madai kuwa teknolojia itawafanya wafanyikazi kutowajibika kwani itakuwa na manufaa zaidi.

“Watu lazima wajifunze kuikumbatia teknolojia na kuachana na hofu kuwa itawabandua na kuchukua nafasi asilia zote. Wanafaa kuona manufaa yake, ” anasema.

Anafunguka kuwa iwapo atapewa fursa, ataanzisha mtandao wa kijamii ambao utapunguza utumiaji wa karatasi hasa katika sekta ya uanasheria. Kulingana naye, visa vya kesi kutoendelea kutokana na ukosefu wa ushahidi vinaweza kusuluhishwa na teknolojia.

Hata hivyo Edwin Ikaria kutoka Shule ya Upili ya Thura anasema kuwa teknolojia imeleta madhara mengi.

“Napenda teknolojia ila imeleta madhara, wezi wanatumia mitandao kuiba, wanadukua benki na mitandao ya kijamii ,” analalamika Edwin.

Hata hivyo alishikilia kwamba ili kuinasua serikali kwenye mazimwi ya ufisadi, ni lazima teknolojia itumike.

TEKNOLOJIA KUZIMA UFISADI

“Mie huchukia visa vya ufisadi vinavyotendeka nchini. Naamini ipo siku uvumbuzi wa teknolojia itakayotambua wafisadi itaundwa ili kutatua tatizo hili,” anatoa matumaini Edwin.

Aliongeza kuwa mahakama zinachukua miaka na mikaka kukamilisha kesi zilizopo, jambo ambalo linafaa kusitishwa. Alitoa mifano ya waathiriwa wa dhuluma ambao hawawezi kupokea matibabu hospitalini kwa sababu ya kukosa fomu ya P3 ambayo kulingana naye, huchukuwa mda mrefu kutolewa.

Akiwa na miaka 18, Edwin anahofia ukosefu wa ajira kutokana na kuwepo kwa roboti. Hata hivyo,  Elizabeth Wanjiru, mwanafunzi wa darasa la nane katika Shule ya St Paul Academy ana maoni tofauti na na Edwin.

“Mimi na ithamini teknolojia kwa sababu inaboresha maisha kwani hizo roboti haziwezi kufanya kazi bila kudhibitiwa na mwanadamu, watu wanafaa kujifunza jinsi ya kuzimudu tu, ” anasema Elizabeth.

Anasisitiza kuanzishwa kwa jukwaaa la kuwasaidia wanafunzi ambao wazazi wao wanashindwa kulipa karo.

“Licha ya kukosa fedha za karo, ni haki kwa kila mtoto kupata elimu bora. Wazazi wenye mapato ya chini wanafaa kusaidiwa.”

Elizabeth anapania kuwa mwigizaji na angependa kuanzisha teknolojia ya kuboresha vipaji kama hivyo pamoja na kuhakikisha kuwa wanapata malipo kwa wakati.

Katoka Shule ya Upili ya Wasichana ya Kaaga, Jasmine Nkatha, mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza analenga kuwa mtangazaji na angependa kutangaza taarifa za runinga siku moja ila kulingana naye, jambo hilo haliwezi kutimia hadi teknolojia iweze kuboreshwa.

Wanafunzi washiriki katika warsha ya teknolojia katika Shule ya Msingi ya St Paul’s mjini Meru. Picha/ Faustine Ngila

5G

“Ukitazama teknolojia ya hologram na video za 5G katika mtandao wa YouTube na kufikiria jinsi taarifa za siku za usoni zitakavyokuwa, utatambua kwamba kweli changamoto zipo.

“Nataka kuwa na uzoefu wa teknolojia na kuwasaidia watu hasa kule mashinani kupata taarifa za runinga,” anasema Nkatha.

Kulingana naye, ili kuepuka madhara ya teknolojia, ni lazima watu waifahamu teknolojia .

“Tumesikia madaktari wa upasuaji wakitumia roboti kuimarisha uhakiki katika operesheni zao, ila wao wamejifunza teknolojia hiyo kwanza,” anasimulia.

Jesse Nkatha, mwenye umri wa miaka 10 katika Shule ya Msingi ya St Paul’s Academy  anataka kuwa mchezaji bomba na mtajika wa kandanda, sio tu humu nchini bali hadi kimataifa.

“Napenda jinsi Messi alivyowalambisha sakafu wapinzani na kufuma mabao, najua ana bidii na baadhi ya makocha hutumia uchanganuzi wa data ili kumuongoza, ” alisema Jesse.

Pia anafahamu kuwa teknolojia zinazohusishwa na kandanda kama Video Assisted Referee (VAR) na ile ya kutambua mpira ukipita laini ya goli zinaleta usawa katika sekta hiyo. “Sipendi kuona timu ikishinda kwa kupendelewa,” anamalizia Jesse.

UZEMBE WA SERIKALI

Licha ya kuwepo kwa wanafunzi ambao wapo tayari kuisoma teknolojia, serikali na sekta binafsi zimezembea katika uanzilishi wa programu za usimbaji (coding) shuleni ili kuwasaidia wanafunzi.

Katika mataala mpya wa elimu , teknolojia ambayo ni nguzo kuu katika kuimarisha uchumi miaka inayokuja, imeachwa nje licha ya wanafunzi kuwa na ujuzi na hamu yake.

Bw Jesse Muchai ambaye ndiye afisa mkuu mtendaji na mwanzilishi wa Code Mashinani alisema kuwa ameweka mikakati ya warsha ya mafunzo ili kuwasaidia wanafunzi kuwa na fikra bora na bunifu.

“Wanadamu hawawezi kusoma vizuri hasa wakiwa na dharba. Tumewekeza kwa watoto kwa sababu wao wanafikiria umuhimu na manufaa na pia hupenda kujaribu vitu vipya na huamini wanachofunzwa bila kubisha, ”alisema Bw Muchai katika mahojiana na Taifa Leo Dijitali.

Licha ya juhudi zake, Bw Muchai anadai kuwa bado kuna mengi ya kufanywa ili kutimiza malengo hayo.

“Malengo yetu ni kuchochea wanafunzi wajiulize maswali muhimu kwani hata kuunda programu lazima uwe na elimu ya teknolojia,”  aliiongeza Bw Muchai.

Bi Peris Waithera, mwasisi mwenza wa Code Mashinani alisema ni njia bora ya kuwaelimisha wasichana kuthamini teknolojia na kuhakikisha kuna usawa wa 1:1 katika mafunzo yote. Hata, wanawake wanaonekana kuachwa nyuma.

“Wanawake wanaogopa teknolojia, wanahofia kujifunza sayansi, tekmolojia, hesabu na uhandisi. Tunataka kuto aiyo hofu na kuwaelewesha umuhimu wa teknolojia pamoja na kutatua chanagamoto wanazopata kama ukeketaji,” alisema Bi Waithera.

Baada ya ziara yetu maswali mawili ynaibuka: Je, ni nani atawafunza wanafunzi ujuzi huu iwapo taifa hili linalenga kujiandaa kwa mageuzi ya kiteknolojia? Nani atawafunza jinsi ya kusimba (code) programu na tovuti zitakazoleta suluhu?

Watoto kutoka China hufunzwa jinsi ya kusimba kuanzia wakiwa miaka mitano ili kuwawapa uzoefu katika ulingo wa teknolojia mapema.

Austria, Bulgaria, Denmark, Estonia, Ufaransa, Hungary, Ireland, Lithuania, Malta, Uhispania, Poland, Ureno, Finland, Slovakia na Uingereza pia zimeanzisha mfumo huo wa usimbaji katika shule za msingi na upili.

Kennedy Kanyi, mwenye miaka 27, mwanaprogramu ambaye alianzisha lugha ya usimbaji ya BraceScript mwaka wa 2017, ni mfano bora wa vipaji vilivyomo humu nchini.

Miradi kama African Girls Can Code Initiative ambao unafanywa kuanzia mwaka wa 2018 hadi 2022 ni hatua mwafaka ila serikali za Afrika zinafaa kufunza na kukuza vipaji vya kusimba katika shule za umma.

Bitange Ndemo, profesa wa masuala ya biashara katika Chuo Kikuu cha Nairobi anasema kwamba miradi kama ya Code Mashinani ni mizuri na serikali inafaa kuwafunza wanafunzi kusimba kuanzia umri mdogo.

“Tunafaa kuanza kuwasaidia watoto kusoma na kutatua shida zilizopo wangali wachanga. Wanafunzi wa chekechea wanafaa kuzoeshwa kutumia programu ambazo zitawapanua akili,” anasema Prof Ndemo.

Shule ya Montessori ndiyo anayoamini kuwa mfano bora katika kutekeleza mtaala mpya wa elimu unaowatayarisha wanaafunzi kuwa viongozi wa baadaye na kukabili mawimbi ya kiteknolojia yanayokuja.

“Mfumo unaowafanya wanafunzi kujibu maswali kwa kuchagua jibu sahihi hautosaidia kamwe.Serikali inafaa kuiga mfumo unaotumika katika shule ya Montessori katika mtaala mpya wa elimu na pia kuufanya nafuu kwa wazazi,” anaeleza Prof Ndemo.

 

Imetafsiriwa na Fatuma Bugu 

Kenya yasifiwa kupunguza vifo vya watoto wachanga

Na PAUL REDFERN

KENYA imepiga hatua katika juhudi zake za kupunguza vifo vya watoto wachanga walio chini ya umri wa miaka mitano katika miaka 25 iliyopita. Haya ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB).

Ripoti hiyo inasema kuwa vifo hivyo vimepungua hadi kufikia watoto 41 kati ya 1,000 ilhali kiwango cha vifo hivyo duniani ni 39 kati ya watoto 1,000.

Mnamo 1996 idadi ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano waliofariki ilikuwa 114 kati ya watoto 1,000, hali inayoashiria kuwa vifo hivyo vimepungua kwa kiwango cha asilimia 60 kwa kipindi cha miaka mitatu.

Na idadi hiyo ni chini zaidi ikilinganishwa na idadi wastani ya vifo vya watoto wachanga katika mataifa yote yaliyoko kusini mwa jangwa la Sahara.

Ingawa Kenya ingali na nafasi ya kupiga hatua zaidi, takwimu za hivi punde ni bora zaidi ikilinganishwa na zile za mataifa kadhaa ya Afrika.

Mataifa ya Somalia, Nigeria, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sierra Leone na Guinea ni miongoni mwa mataifa yenye viwango vya juu vya vifo vya watoto wachanga barani Afrika ambapo ni zaidi ya watoto 100 kati ya 1,000.

Benki ya Dunia inasema kwamba licha ya Kenya kuandikisha rekodi nzuri, hali si nzuri katika mataifa yaliyoko Kusini mwa jangwa la Sahara.

Mnamo mwaka wa 2018 mtoto mmoja kati ya 10 wenye umri wa miaka mitano kuenda chini walifariki katika Afrika ikilinganishwa na mtoto mmoja kati ya 24 katika mataifa yaliyoko kusini mwa bara Asia. Hii ina maana kuwa Afrika na Asia ndio waliongoza kwa vifo vya watoto wachanga mwaka huo.

Umri

Ripoti hiyo pia inasema kuwa asilimia 40 ya vifo vya watoto walioko chini ya umri wa miaka 15 hutokea kuanzia mwezi wa kwanza baada ya wao kuzaliwa.

Inakisiwa kuwa jumla ya watoto 2.5 milioni kote duniani walifariki mwezi mmoja baada ya kuzaliwa mnamo mwaka wa 2018. Kiwango hicho ni sawa na watoto 7,000 wachanga kila siku.

Aidha, imebainika kuwa idadi ya watoto ambao hufariki wakiwa na umri mdogo inapungua kwa kasi kuliko idadi ya watoto wanaofariki wakiwa na umri mkubwa.

Serikali yapiga marufuku raia wa kigeni kuchukua na kulea watoto wa humu nchini

Na MARY WANGARI

RAIS Uhuru Kenyatta amepiga marufuku mara moja raia wa kigeni kuchukua na kuwalea watoto wa nchini Kenya huku akiagiza Wizara ya Leba kuunda sera mpya ya kudhibiti upangaji watoto na raia wasio Wakenya.

Hatua hiyo ilitangazwa jana katika mkutano maalum wa Baraza la Mawaziri uliofanyika Ikulu, Nairobi, na ulioongozwa na Rais akiwa ni mwenyekiti wake na kuhudhuriwa na Naibu Rais William Ruto.

Kiongozi wa Taifa pia ameagiza Wizara ya Leba na Ulinzi wa Jamii kubuni sera mpya za kudhibiti shughuli ya upangaji wa watoto na raia wa kigeni nchini Kenya.

Aidha, Wizara hiyo imeagizwa kulainisha shughuli za Shirika la Maslahi ya Watoto Kenya pamoja na shughuli za makao ya watoto nchini.

Baraza hilo pia liliidhinisha Sh6.9 bilioni kwa lengo la kuendeleza miundomsingi katika eneo maalum lililotengwa Naivasha pamoja na ukamilishaji wa awamu ya pili ya Standard Gauge Railway (SGR).

Katika baraza hilo vilevile, uidhinishaji wa kuandaliwa kwa warsha ijayo Nairobi ya Kongamano la Kimataifa kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo awamu ya 25 (ICPD), ulipitishwa.

Kongamano hilo lililopangiwa kufanyika kuanzia Novemba 12 hadi 14, 2019, linatarajiwa kuvutia wajumbe zaidi ya watu 6,000 kutoka mataifa 179.

Warsha hiyo inatazamiwa kupiga jeki sekta ya utalii nchini Kenya kwa kutoa picha nzuri na kuimarisha nafasi ya Kenya kama kituo mwafaka cha kongamano na usafiri wa ndege.

NGILA: Tuwape watoto fikra za kutatua changamoto maishani

NA FAUSTINE NGILA

WIKI iliyopita wanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari wenye umri wa kati ya miaka minane na 17 katika Kaunti ya Meru walikongamana kupokea mafunzo ya kufikiria kidijitali kutoka kwa waasisi wa mradi wa Code Mashinani.

Wengi walisema wanapendezwa na jinsi teknolojia imeboresha maisha huku wakionekana kuchangamkia masuala ya teknolojia.

Walitaja uanasheria, uanahabari, udaktari, uhandisi na uigizaji kama baadhi ya taaluma ambazo zinawapendeza, huku wakikiri teknolojia itatumika kuboresha kila sekta.

Hata hivyo, afisa mkuu mtendaji wa mradi huo, Jesse Muchai aliwafafanulia kuwa kabla ya kung’amua jinsi ya kuunda programu za simu na kompyuta, wanafaa kuelewa fikra zote zinazochochea kuundwa kwake.

Huu ndio msingi kwani kampuni zote kubwa za teknolojia duniani kama Amazon, Facebook, Google, Twitter au Tesla zilianzishwa baada ya waasisi wake kujiuliza maswali mengi kuhusu dunia ya mbeleni.

Uwezo wa kutambua changamoto kisha kuitafutia suluhu ni nguzo kuu katika maendeleo ya kila taifa duniani. Na ukimfundisha mtoto kufikiria jinsi ya kutatua matatizo, atakuwa mwananchi wa kutegemewa katika uchumi wa nchi.

Na si hilo tu, wanafunzi wanapozoea kukabiliana na visiki, wao huwa wakomavu wa akili na mwenendo wanapohitimu masomo yao. Tatizo tulilo nalo hapa Kenya ni kuwa watoto wanalelewa kwa kubembelezwa, wasijue tabu wala vizingiti maishani. Utawaona wakiitisha wazazi wao vitu kwa lazima na wasiponunuliwa wanatisha kujinyonga!

Tukiendelea kulea watoto wetu hivi watakuwa tu vifyefye maishani, hawatajisaidia kwa lolote wala kujikwamua kwa tatizo lolote. Na kizazi kizima cha usoni hakitaweza kukabiliana na mawimbi ya teknolojia kama 5G, Blockchain na Sayansi ya Data ambazo zitafuta nafasi za ajira zilizopo huku zikiunda zingine mpya.

Wazazi wanafaa kutambua kuwa unapomzoesha mtoto maisha ya kupewa kila kitu bila kung’ang’ana, kumtatulia changamoto zake, yeye huishia kukosa ubunifu ambao unahitajika katika dunia ya sasa iliyojaa ushindani.

Mustakabali wa uchumi wetu kwa sasa umo mikononi mwa ubunifu katika teknolojia. Kwa hivyo, iwapo mwanafunzi wa chuo kikuu atahitimu kwa shahada ya uanasheria na hajui jinsi ya kutumia teknolojia kuwasilisha ushahidi kortini kwa niaba ya mteja wake, atapoteza ajira.

Kuanzia umri mdogo, kama miaka mitano hivi, tunafaa kuwafundisha watoto baadhi ya teknolojia zinazotumika kwa sasa.

Hata unapomnunulia vifaa vya kuchezea, hakikisha vinaimarisha akili yake, mpe changamoto azoee angali mchanga. Akikomaa atakuwa mbunifu kiasi cha kuunda programu za kipekee.

Hivyo, ukomavu wa mtoto unadhibitiwa na wazazi wake. Tusipowafunza jinsi ya kufikiria suluhu za changamoto, basi kizazi kijacho kitakuwa cha watu wazembe wanaotegemea usaidizi wa wazazi, wasioweza kubuni mifumo ya maana inayotoa nafasi za ajira.

Mwalimu ajitolea kutetea haki za watoto

NA RICHARD MAOSI

Bw Sigei Justice Kiprono amegonga vichwa vya habari kutokana na juhudi zake kupigania haki za watoto hususan wa kike chini ya mwavuli wa kampeni inayofahamika kama Child Protection.

Anasema tamaduni za kale na ukosefu wa uhamasisho wa kutosha kuhusu haki za binadamu, ndicho chanzo kikubwa cha kurudisha nyuma ndoto za watoto kupata mafanikio maishani.

Akiwa mwalimu katika Shule ya Msingi ya Kimari inayopatikana kaunti ya Bomet, alishirikiana na hospitali ya Nairobi Women kuchunguza na kabiliana na wale wanaokiuka haki za watoto.

Alieleza kuwa watoto wanastahili kulindwa dhidi ya taasubi za kiume ili kuhakikisha maisha yao hayamo hatarini kwani sheria inawalinda.

Sigei anasema walilenga kufundisha jamii namna mbalimbali za kukiuka haki za mtoto,mbali na kuwapatia wanafunzi ujuzi wa kujitegemea kimaisha.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, alisema kwanza alibuni makundi ya kuigiza shuleni yanayotumia mashairi na nyimbo kuhamasisha jamii.

Bw Sigei Justice Kiprono. Picha/ Richard Maosi

Hatua yenyewe ilimsaidia kuvutia idadi kubwa ya wanafunzi, ikizingatiwa wao huchukua muda mfupi kujifunza kitu kipya muradi kitawafurahisha.

Katika mradi huo alijaribu kuhimiza wanafunzi,wake na walle wa shule jirani kutumia elimu wanayopata shuleni kuimarisha nidhamu kwenye makuzi yao ya kila siku.

“Tangu Gender Violence Recovery Centre kuchukua usukani visa vya ukiukaji wa haki za watoto katika kaunti za Kericho na Bomet vimepungua kwa asilimia kubwa,” akasema.

Aidha amefanikiwa pamoja na washikadau kuwawezesha watoto kupata elimu na ufadhili ili wasikatize masomo yao wakiwa njiani,kabla ya kujitimu na kupata cheti.

Sigei anasema hususan mtoto wa kike amekuwa kwenye hatari zaidi kutokana na mimba za mapema au ubakaji.

Lakini hata hivyo anawalaumu wazazii kwa kuwasukumia walimu jukumu hilo na badala yake kutumia wakati wao mwingi wakifanya kazi.

Anapendekeza wazazi kuwapatia watoto wao pesa za kutosha kwa sababu ya mahitaji ya kila siku,kwani hali ngumu ya maisha inaweza kuwasukuma watoto kwa utumiaji wa mihadarati.

Akitoa mfano katika eneo la pwani ambapo visa vya ulanguzi wa watoto vimekuwa vikiongezeka kutokana na mfumo mpya wa teknolojia na utandawazi.

Biashara hiyo imechangiwa na mitandao ya kijamii kwa asilimia kubwa na wazazi hawajakuwa wakichukua jukumu la kuangalia watoto wao wanazungumza na akina nani kwenye mitandao.

“Ulanguzi wa binadamu hasa watoto umekuwa ukiongezeka kutokana na mahitaji ya kimaisha kama vile umaskini na idadi kubwa ya vijana wanaotafuta ajira mtandaoni,”akasema.

Pia walezi wamekuwa wanyonge na woga hasa ijapo katika swalla la kuwaelimisha watoto kushiriki mapenzi wakiwa wachanga.

Sigei aliteuliwa kama mwenyekiti anayesimamia kaunti ya Bomet na Kericho kama balozi atakayepitiza ujumbe kuhusu haki za watoto na maeneo mengineyo Bonde la ufa.

Akiwa mwalimu amefanikiwa kufikia familia nyingi hasa mashinani ambao awali hawakuona umuhimu wa kuwapeleka watoto wao shuleni.

Aidha kutokana na ushawishi wake amepigana na tamaduni zilizopitwa na wakati na akafanikiwa kuonyesha kuwa mtoto wa kike ni sawa na mtoto wa kiume.

Kwa ushirikiano na usimamizi wa shule ya Kimari walifanikiwa kubuni chama cha Kings and Queens ambacho kinawahimiza wanafunzi wazifahamu haki zao za kimsingi.

Kings and Queens

Kings and Queens ni kikundi cha wanafunzi wenye ndoto za kuja kuwa watu wa maana katika jamii siku za mbeleni,hivi sasa wakiwa wanafunzi 41 maaazimio yao ni ya kutia moyo.

Mwalimu Sigei alitaka kuwaleta pamoja wanafunzi kutoka tabaka la juu na tabaka la chini na kuwaonyesha jinsi masomo yangeweza kuwaunganisha wawe sawa.

“Ni kupitia elimu tu ambapo jamii itafanikiwa kupigana na chagamoto zinazomkabili mtoto,”aliongezea.

Brenda Chepkoech ni mwanafunzi wa darasa la nane,anasema yeye ni mshiriki wa michezo ya kuigiza ambapo anatumia kipaji chake kuhimiza maadili miongoni mwa wenzake.

Anawashauri watoto wengine kutafuta msaada wa haraka endapo watagundua maisha yao yako hatarini.

“Wanafunzi wengi wanazingatia ushauri wa kufanya kazi kwa bidii ili kujitengenezea maisha yao ya siku za mbeleni,”aliongezea.

Ni kwa sababu hiyo kupitia serikali ya ugatuzi wizara imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa mtoto wa kike haponzwi na taasubi za kiume.

Ambapo sheria inatoa utaratibu dhidi ya ukiukaji wa haki za mtoto akiwa mdogo,aidha sheria inaunga mkono ajenda ya kulinda maslahi ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa kwani wana haki ya kurithi mali ya wazazi wao.

BALLET: Densi ya majuu inavyonoa akili za watoto Nakuru

NA RICHARD MAOSI

Densi ya Ballet yenye asili ya Uhispania na Uingereza inahitaji miondoko ya aina yake, utafiti ukionyesha kuwa watoto kati ya miaka 2-12 wataimarisha afya, upevu na ukomavu wa akili wakishiriki.

Densi yenyewe haiwezi kufananishwa na zile za kawaida kwa sababu mshiriki anahitajika kuwa makini, katika harakati za kuboresha stadi yenyewe hatua ya mwanzoni kabla hajahitimu na kuwa mahiri.

Taifa Leo Dijitali ilipatana na wanafunzi kadhaa wanaojifundisha Ballet kutoka mtaa wa Pipeline, Lanet viungani mwa mji wa Nakuru, siku ya Jumamosi baada ya masomo.

Bi Rosie Njoroge ,mwalimu wao alianzisha studio ndogo ya kunoa vipaji vya mabinti hawa wadogo akilenga kutumia fursa yenyewe kama hamasa ya kushinikiza umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.

Bi Njoroge anaungama kuwa wanafunzi wanaoshiriki densi walikuwa ni mahiri sana darasani hasa ijapo katika somo la hisababi, miongoni mwa masomo mengineyo yanayotahiniwa shuleni.

“Wanatakiwa kujihami na stadi ya kuhesabu nambari za tarakimu, kwa sababu hii ndiyo njia ya kipekee itakayowafanya kukumbuka mafunzo yaliyotangulia,” Bi Rosie akasema.

Ingawa baadhi yao ni wadogo, wao huchukua muda mfupi sana kuiga na hatimaye wakabobea kwa kutegemea kasi ya mtoto kujifundisha.

Muziki tulivu ni kiungo muhimu kinachohitajika kunogesha shughuli hapa, ikizingatiwa kuwa kila hatua inategemea midundo inayoendana sawia na miondoko.

Kulingana na Bi Rosie, densi ya Ballet imekuwa ikiwasaidia wanafunzi kuongeza nguvu katika viungo vyao vya mwii, hasa wenye umri mdogo wanaoendelea kukua.

Humsaidia mwanafunzi kupata uzoefu na kufanya mambo ya kawaida kwa njia rahisi kama vile kucheza mpira na kushiriki michezo ya yoga inayohitaji viungo dhabiti vyenye unyumbufu.

Mbali na kufanya umbo la mshiriki kukomaa kwa haraka, Ballet humsaidia mwanafunzi kupata umbo linalopendeza.

Rosie anaona kuwa ipo haja kubwa kwa wanafunzi kuhimizwa kuhusu utumiaji wa vipaji vyao,kwa mujibu wa nyanja mbalimbali ili kujiendeleza kwenye nyanja mbalimbali za kimaisha.

Mshiriki anaweza kufanya vyema hata akahitimu na kufikia kiwango cha kimataifa kisha akajiajiri na kuwaajiri wengine katika ulingo unaokaribiana na huu ama huu.

“Ni njia mwafaka ya kupitiza muda miongoni mwa wanafunzi hasa wikendi ambapo wao huwa nje ya darasa,wanaweza kupata ujuzi wa maisha vilevile,” aliongezea.

Densi ya Ballet inalenga wanafunzi kutoka familia za tabaka la chini na wale wa tabaka la juu.

Hususan hii ikiwa ni densi ya kigeni inawahimiza watoto kujivunia tamaduni zao, na kuheshimu desturi za jamii nyinginezo zinazokaa pembe mbalimbali duniani.

Kinyume na zamani ambapo mchezo huu ulihusishwa kwa asilimia kubwa na wale wanaotokea katika tabaka la juu lakini kufikia sasa Ballet imepenya.

Maeneo mengine ambayo watoto wanashiriki densi hii ni kaunti ya Nairobi mtaa wa Kibera na Mombasa.

Rosie anawashauri wazazi kuwaruhusu watoto wao kujifunzi mambo mchanganyiko wangali wachanga,,kwa sababu hili litawasaidia kujitambua na kujielewa wakiwa na umri mdogo.

“Watoto kutoka kwenye familia maskini wanaamini kuwa hii ni mojawapo ya njia itakayowakwamua kutoka kwenye lindi la umaskini siku za usoni,” alisema.

MUTANU: Wazazi wasipowaelekeza watoto, upotovu utazidi

Na BERNARDINE MUTANU

Kilikuwa kisa cha kushangaza kwa vijana wa umri mdogo walipomteka nyara na kumuua mvulana wa umri mdogo mbali na kuitisha fidia kutoka kwa wazazi wake ili wamwachilie.

Hiyo ni taswira kamili ya jamii yetu ilivyo nchini. Uhayawani umewatoka wanyama na kuwaingia binadamu.

Cha kushangaza ni kuwa kisa hicho kilihusisha watoto wa umri mdogo, karibu wote wakiwa wenye umri kati ya miaka 15 na 18.

Ingawa wataadhibiwa kisheria, hilo si suluhisho la kinachoendelea katika jamii na huenda visa kama hivyo vikaendelea kuripotiwa mara kwa mara katika siku zijazo.

Wakati wa sherehe za kuadhimisha Sikukuu ya Madaraka, Rais Uhuru Kenyatta alizungumzia suala la mauaji miongoni mwa wananchi yanayoendelea kuripotiwa kila siku.

Rais alikashifu vikali visa hivyo, zaidi ya kutambua viwango vya juu vya mafadhaiko miongoni mwa wananchi. Visa vya mauaji au kujiua vinatokana na shinikizo za mambo katika jamii.

Ingawa kuna haja kubwa ya kufanya utafiti ili kutambua kiini kamili cha visa hivyo vya kuhuzunisha, ukweli ni kwamba jamii imechangia pakubwa.

Ingawa sitaki kuhukumu, watoto wa umri mdogo kama hao wa Kakamega hawawezi kufanya hivyo bila kuiga kutoka kwa watu wengine au kupata mafunzo.

Aidha, watoto wanaweza kuhusika katika uhalifu kama huo kwa kusukumwa na hali katika jamii au kutazama video au filamu zinazoonyesha uhalifu.

Ukifuatilia zaidi, utapata kuwa watoto kama hao huwa wanachama wa madhehebu ambayo huwapotosha.

Ingawa kuna masuala mengi ambayo huchangia mauaji au hatua ya kujitoa roho, ni vyema wananchi kuelewa kuwa ‘mtoto umleavyo ndivyo akuavyo’.

Watoto wengi hukua wakijua kuwa vurugu ni kawaida, kutusi ni kawaida, kudanganya ni kawaida, kuiba ni kawaida au hata kumchapa mtu ni kawaida. Hii ni kwa sababu hukua wakiona mambo hayo yakifanywa katika jamii na wazazi wao, ndugu zao wakubwa, majirani au hata marafiki.

Wanapokuwa watu wazima, inakuwa ni vigumu kujizuia kuhusika katika mambo kama hayo na ndiposa kuna idadi kubwa ya wafungwa wa umri mdogo nchini.

Ninachosema ni kwamba watoto, ambao ni viongozi au wazazi wa kesho, wamekosa mwelekezi au mtu wanayeweza kumuiga au kuwashauri.

Wazazi wamewafeli watoto wao kwani zaidi ya kuwa hawapatikani tena kuwaelekeza watoto wao kutokana na shughuli za hapa na pale, baadhi yao hawawafunzi maadili na umuhimu wa kuwa waadilifu. Zaidi, baadhi ya wazazi huwa hawawaelekezi watoto wao makanisani, misikitini au mahekaluni ili kupata ‘chakula’ cha kiroho.

Kutokana na hilo, wengi hukua wakiwa watupu kiroho, hivyo, hujipata wamevunjika moyo au kutamauka maishani, kisha kuona heri wafe kwa kujitoa uhai au waondoe uwepo wa mtu au watu walio ‘kikwazo’ katika maisha yao.

Na ndiyo maana kuna visa vingi vya mauaji au kujitoa uhai. Tunachohitaji kwa sasa ni kujirudi kama wazazi na kuchukua hatua za kimsingi katika malezi.

Hisia kali kuhusu pendekezo watoto wa miaka 16 kuruhusiwa kufanya ngono

Na PETER MBURU

PENDEKEZO la Majaji wa Mahakama ya Rufaa kuwa umri wa watoto kuruhusiwa kujihusisha na ngono unafaa kupunguzwa kutoka miaka 18 hadi 16 limeanza kuvutia hisia kali, baadhi ya washikadau wakilipinga.

Majaji Roselyn Nambuye, Daniel Musinga na Patrick Kiage wakitoa uamuzi walisema kuwa umri wa watoto kuwa na haki ya kujiamulia kufanya mapenzi kwa hiari unafaa kupunguzwa, kutokana na visa vingi ambapo wanaume wamefungwa jela kwa makosa ambayo walioshtakwa kuwanajisi walikuwa wameelewana.

Majaji hao walisema hayo walipokuwa wakitupilia mbali kifungo dhidi ya mwanamume aliyefungwa miaka 15 jela, kwa kumtia mimba msichana wa miaka 17.

Walisema taifa linafaa kujadili kuhusu kupunguzwa kwa umri huo kwani wanaume wengi wanaozea jela, wakati walihukumiwa kwa kuwanajisi wasichana ambao walikuwa na hiari na walikaa kama watu wazima.

Lakini mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Kuhusu Elimu Julius Melly jana alipinga pendekezo la Majaji hao, akisema miaka 16 ni umri mdogo kwa mtoto kuruhusiwa kujiamulia, kwani hilo litaathiri elimu.

“Watoto wengi wa miaka 16 wako aidha kidato cha pili ama cha tatu na hata kwa wanochelewa masomoni shule za msingi. Hivyo kuruhusu watoto wa kiwango hicho kujiamulia tutaanza kushuhudia visa vya wanafunzi kupata mimba na kuacha masomo ovyoovyo,” akasema Bw Melly, ambaye pia ni mbunge wa Tinderet.

Mbunge huyo alisema umri huo unafaa kusalia miaka 18 kama ilivyo sasa, kwani watoto wengi huwa wamekamilisha masomo ya shule za upili, wamekomaa kutosha na wameanza kuelewa maisha vyema.

Lakini majaji hao, katika uamuzi wao, walikuwa wamesema “Inawezekana wakawa hawajafikisha umri wa ukomavu lakini wanaweza kuwa wamefikisha umri wa kujiamulia kizuri na kibaya kwa maisha na mili yao.”

Majaji hao walisema sheria kuhusu makosa ya kingono dhidi ya watoto sasa inafaa kukaguliwa vyema na kurekebishwa ili kutatua baadhi ya changamoto, ambazo zimewapeleka watu wengi gerezani.

Mjadala huo umeibuka wakati kumekuwa na visa vya mara kwa mara vya wanaume, ikiwemo walimu, kushtakiwa kwa kushiriki ngono na wanafunzi ama watoto wengine wa umri huo, ama wa chini.

Baadhi ya wazazi aidha wanahoji kuwa umri wa miaka 16 ni wa chini kwa mtoto kuwa na uhuru wa kujiamulia, wakihofia watoto wengi watafanya maamuzi ya kupotosha katika maisha yao.

Wasamaria kutoka kuzimu

Na VALENTINE OBARA

TABIA ya wahisani kutoka ng’ambo kuwadhulumu watoto mayatima na wanaotoka familia maskini, imefikia upeo mpya baada ya Idara ya Upelelezi ya Amerika (FBI) kuanza kuchunguza mume na mkewe kwa madai ya unajisi katika makao ya watoto Bomet.

FBI inachunguza raia wake wawili, Gregory Dow na mkewe Mary Rose, kwa madai ya kudhulumu watoto kimapenzi katika makao ya watoto waliyosimamia katika eneo la Boito.

Ufichuzi huu umetokea siku chache baada ya mahakama kuagiza makao ya watoto ya Martyrs of Uganda katika Kaunti ya Machakos

ifungwe, baada ya kufichuliwa wavulana katika makao hayo wamekuwa wakilawitiwa.

Ingawa wavulana karibu tisa walilalamika kuhusu ulawiti waliotendewa na mpishi wa kiume, hakuna hatua zilichukuliwa hadi watetezi wa haki za binadamu walipoingilia kati.

Ongezeko la visa hivi limefanya Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kuanzisha kitengo kipya cha kupambana na dhuluma dhidi ya watoto.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Kenya Alliance for Advancement of Children, Bw Timothy Ekesa alisema hatua za dharura zinahitaji kuchukuliwa.

“Ukichunguza vyema utakuta visa vingi huwa haviripotiwi kwa sababu wahusika hutoa vitisho,” akasema mwanasaikolojia wa watoto, Bi Loice Okello.

Kwa miaka kadhaa sasa, kumekuwa na visa zaidi ya saba ambapo raia wa kigeni wamechunguzwa na baadhi kupatikana na makosa ya kudhulumu watoto katika makao ya mayatima.

Mwaka jana, Hans Egon Dieter Vriens, ambaye ni raia wa Uholanzi alikamatwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kwa kubaka wasichana wa umri wa kati ya miaka minane na kumi.

Ilisemekana kulikuwa na wasichana wanane waliokuwa wakiishi nyumbani kwake wakipokea misaada kama vile elimu.

Mwaka huo huo, Keith Morris, 72, ambaye ni raia wa Uingereza, alipatikana na hatia ya kudhulumu wasichana kimapenzi na akahukumiwa miaka 18 na miezi sita gerezani Uingereza.

Mapema 2011, Kasisi Kizito wa Kanisa Katoliki aligonga vichwa vya habari kwa madai ya kudhulumu watoto kimapenzi katika makao ya watoto aliyosimamia mtaani Dagoretti. Hata hivyo, wavulana waliohusika baadaye walidai walilazimishwa kumharibia sifa kasisi huyo.

Mnamo 2015, Mwingereza Simon Harris alihukumiwa miaka 17 na miezi minne gerezani na mahakama ya Uingereza iliyompata na hatia ya kulawiti wavulana wa kurandaranda mitaani katika eneo la Gilgil.

Mwingereza mwingine, Simon Wood, alijitoa uhai 2014 alipokumbwa na mashtaka ya ubakaji wa wasichana wenye umri wa kati ya miaka mitano na 13, alipokuwa akitoa misaada katika shule na makao mbalimbali ya watoto Kenya, Uganda na Tanzania.

Nchini Amerika, Matthew Lane Durham, aliyekuwa na umri wa miaka 21 alihukumiwa miaka 40 gerezani kwa kudhulumu watoto kimapenzi katika makao ya mayatima ya Upendo jijini Nairobi, kati ya Aprili na Juni 2014.

Mwanamke mwingine ajifungua watoto 6 kwa dakika 9

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

Houston, Amerika

MWANAMKE mmoja kutoka Amerika amejifungua watoto sita kwa kwa mpigo kwa kipindi cha dakika tisa pekee.

Bi Thelma Chiaka ambaye ni mkazi wa Houston alijifungua watoto wanne wa kiume na wawili wa kike mnamo Jumapili katika Hospitali ya Wanawake ya Texas.

Wahudumu wa hospitali walisema watoto hao wamewekwa katika kitengo cha kuwatunza watoto wachanga ambako wataendelea kuhudumiwa. Walizaliwa kati ya saa kumi na dakika 50 na saa kumi na dakika 59 alfajiri.

Tukio hilo linajiri siku tano baada ya Bi Evelyn Namukhula kutoka Kaunti ya Kakamega, Kenya kujifungua watoto watano mara moja kwa njia ya upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya kaunti hiyo.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 28 alijifungua wavulana wawili na wasichana watatu.

Hata hivyo, watoto hao walihamishwa hadi Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH), Eldoret baada ya wawili kati ya kupatwa na matatizo ya kupumua.

Mama Namukhula ni mkazi wa kijiji cha Sikokhe katika eneo bunge la Navakholo. Mumewe ambaye anajulikana kama Herbert Nambwire ni kiziwi na husaka riziki kwa kufanya kazi za vibarua kijijini Sikokhe.

Hata hivyo, Bi Thelma Chiaka amempiku Bi Namukhula kwa idadi ya watoto wanaozaliwa kwa mpigo  mwaka huu.