Habari za Kitaifa

Tanzania yasema Raila tosha, achaguliwe mwenyekiti wa AUC

Na BENSON MATHEKA August 27th, 2024 1 min read

RAIS wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan amemtaja mgombea wa Kenya wa kiti cha uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC), Raila Odinga kama kiongozi mwerevu anayetosha kwa wadhifa huo.

Akimwidhinisha Bw Raila kwa wadhifa huo, Rais Samia alisema kwamba Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Kenya ana sifa zote za kuongoza tume hiyo ya Afrika.

Rais William Ruto amezindua rasmi Jumanne, Agosti 27, 2024 azma ya Bw Raila kuwania kiti hicho cha hadhi ya juu Barani Afrika.

“Tanzania inasema kwamba Baba anatosha, achaguliwe,” alisema.

Baba, jina la lakabu analotambulika nalo Raila Odinga ambaye ni kiongozi wa upinzani Kenya.

Mama Samia alisema kwamba Tanzania haibahatishi kwa kuunga mkono kiongozi huyo wa ODM na pia muungano wa Azimio la Umoja – One Kenya, kwa wadhifa wa bara.

“Chini ya uongozi wa Raila, tunaona Afrika yenye nguvu na ustawi. Tanzania inahakikishia Kenya kwamba inamuunga mkono Raila Odinga,” alisema, akiongeza kuwa kinara huyo wa upinzani nchini kwa muda mrefu ni mwaniaji wa Afrika Mashariki.

Ujumbe wake ulihusisha pia Rais mstaafu wa Tanzania Jakwaya Mrisho Kikwete.