Afya na Jamii

Tatizo la ukungu wa macho na jinsi ya kukabiliana nalo

Na PAULINE ONGAJI August 6th, 2024 3 min read

MIAKA miwili iliyopita, Boniface Mwaka, 63, kutoka eneo la Ndithini, Kaunti ya Machakos, aliambiwa kwamba jicho lake la kulia lingepofuka, baada ya kugundulika kuugua ukungu wa macho, yaani cataracts.

Kabla ya hapo, Bw Mwaka ambaye alistaafu kama mtumishi wa umma, asema kwamba kwa miaka kadhaa alikumbwa na changamoto ya kusoma bila kutumia miwani.

“Tatizo la kuona pia lilikuwa likinikumba wakati wa usiku hasa kila nilipomulikwa na taa ya gari. Kando na hayo, jicho langu lilikuwa na maumivu ya macho kila mara,” aeleza.

Masaibu haya yalimlazimu kusaka huduma za kimatibabu katika hospitali kadhaa ambapo alikaguliwa na madaktari mbali mbali kabla ya kushauriwa kutafuta matibabu zaidi.

“Kila mara, nililazimika kuzuru hospitali ya macho ya Nairobi’s City Eye Hospital kufuatia ushauri wa wataalam,” aeleza.

Kulingana na Dkt George Ohito, mtaalam wa upasuaji wa kutibu maradhi ya ukungu wa macho,hali hii hutokea protini inapojiunda kwenye lenzi ya jicho na kulifanya lionekane kana kwamba imefunikwa na wingu.

“Wingu hili huzuia mwangaza kuingia jichoni na kumsababisha mgonjwa kupoteza uwezo wa kuona kwa kiwango fulani,”aeleza.

Kuna aina tofauti za ukungu wa macho, kulingana na mtaalam huyu.

“Kuna ukungu wa macho unaosababishwa na umri. Aidha kuna aina ingine inayofahamika kama congenital cataracts, ambapo huwakumba watoto wachanga hasa baada ya kukumbwa na maambukizi, majeraha au matatizo ya kukua kabla ya kuzaliwa au hata kukumbwa na hali hii wanapokua,” aeleza Dkt Ohito.

Mwanamume akijizatiti kusoma kwa sababu ya matatizo yaliyosababishwa na ukungu wa macho. Picha|Maktaba

Kisha kuna secondary cataracts, hali ambayo hujitokeza kutokana na matatizo ya kiafya kama vile kisukari au kuathiriwa na kemikali za sumu, aina fulani ya dawa, mwangaza au mnururisho.

“Pia, kuna traumatic cataracts. Aina hii hutokea baada ya jicho kukumbwa na jeraha,” aeleza Dkt Ohito.

Baadhi ya ishara za hali hii, asema mtaalam huyu, ni pamoja na kushindwa kuona vizuri, kushindwa kutofautisha rangi fulani, matatizo unapoendesha gari hasa wakati wa usiku, huku wakati mwingine mgonjwa akishindwa kuona vizuri kwenye mwangaza mwingi.

“Pia, ukishauriwa na daktari kubadilisha aina ya miwani unayotumia kila mara, unapaswa kufanyiwa uchunguzi zaidi kwani hii pia ni ishara,” aeleza.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani WHO, watu milioni 28 duniani kote wanakumbwa na matatizo ya kuona, miongoni mwao wakiwa Wakenya 750,000.

Kati ya watu milioni 39 wanaokumbwa na tatizo la upofu duniani kote, 224,000 ni Wakenya.

Aidha, asilimia 80 ya visa vya upofu nchini Kenya ni kutokana na sababu ambazo zaweza kuzuiwa hasa kupitia utambuzi na tiba ya mapema, na mojawapo ya sababu kuu ni ukungu wa macho.

Hali hii yaweza kuzuiwa?

Kutokana na sababu kuwa chanzo kikuu cha hali hii hakijatambuliwa vyema, wataalam wanasema kwamba hakuna njia kamili ya kuzuia hali hii.

Dkt Ohito asema, kutokana na sababu kuwa ukungu wa macho na matatizo mengine ya macho kama vile glaucoma huwakumba sana watu wenye umri mkubwa, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi wa macho kila wakati.

“Hii ni muhimu hasa ikiwa uko katika hatari ya kukumbwa na hali hii, au iwapo kuna historia ya maradhi haya kwenye familia,” asema.

Kulingana na wataalam, watu wenye umri mkubwa wanapaswa kukaguliwa na daktari wa macho angalau mara mbili kwa mwaka.

Utafiti unaonyesha kwamba watu wenye umri mkubwa wamo katika hatari kubwa ya kupofuka kutokana na ugonjwa huu.

Lakini licha ya kuwa maradhi haya kusababisha upofu miongoni mwa asilimia moja ya Wakenya, kuna teknolojia mpya ya upasuaji unaofahamika kama Phacoemlusification (phaco) surgery.

“Upasuaji huu ni teknolojia ya kisasa ya kutibu upofu unaosababishwa na maradhi ya ukungu wa macho. Utaratibu huu unahusisha matumizi ya mwangaza wa leza ambapo lenzi ya jicho lililoathirika linaondolewa na kuwekwa jipya, katika upasuaji unaochukua dakika 15 pekee,” aeleza Dkt Ohito.

Bw Mwaka ni mmoja wa watu walionufaika na tiba hii. Julai 7, 2024 , alibahatika kufanyiwa upasuaji huu.

“Nilibahatika kufanyiwa utaratibu huu ambapo dakika chache baadaye jicho langu lilikuwa sawa,” aeleza Bw Mwaka.

Dkt Ohito asema kwamba habari njema ni kwamba Wakenya wengi wanaokumbwa na tatizo hili wanatafuta matibabu mapema, na kulingana naye, teknolojia hii ni habari njema kwa wagonjwa humu nchini.

Ikiwa una wasiwasi kuhusu gharama ya matibabu, mtaalam huyu asema kwamba usiogope kwani itakugharimu tu kati ya Sh30,000 na Sh60,000.