Habari za Kitaifa

Tutatamba bila Raila, asema Karua

Na KEVIN CHERUIYOT August 23rd, 2024 2 min read

KIONGOZI wa chama cha Narc Kenya, Martha Karua, amesema kuwa muungano wa upinzani utaendelea kutamba hata bila uwepo wa kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Akizungumza Alhamisi, Agosti 22, 2024 katika makao makuu ya chama hicho jijini Nairobi, Bi Karua alisema atasimama na Wakenya na kupigania haki yao.

Huku akimtakia Bw Odinga mema katika azma yake ya kuwania wadhifa wa uwenyekiti wa AUC, Bi Karua alishikilia kwamba ataendelea kumkosoa Rais William Ruto kila anapokiuka katiba.

“Msimamo haubadiliki. Tutaendelea kuwapigania Wakenya. Japo Bw Odinga ameachana na siasa za humu nchini, sisi bado tupo imara na tutaendelea kuiwajibisha serikali ya Kenya Kwanza. Kuwa katika upinzani hakutegemei uwepo au kutokuwepo kwa ndugu yetu (Bw Odinga). Ni jukumu tunalochukua kwa uzito,” Bi Karua alisema.

Karua amewahakikishia Wakenya bado anasimama na waathiriwa wa ukatili wa polisi na utekaji nyara.

“Chama hiki kitaendelea kusimamia ukweli. Hatupo ndani ya serikali, sisi ni wapinzani na tumezoea kuwa kwenye mrengo wa upinzani kwa muda mrefu zaidi. Unaweza kutarajia kwamba tunaendelea kufanya hivyo na wenzetu wanaotaka kufanya hivyo, tutashirikiana nao,” Bi Karua alisema.

Pia, chama hicho kimesema kitaendelea kumpa shinikizo Rais Ruto hadi maafisa wa polisi walionaswa kwenye kamera wakiwadhulumu waandamanaji wakati wa maandamano dhidi ya serikali watiwe mbaroni.

“Tunadai uwajibikaji kwa ukiukaji wa haki za binadamu, vifo, kwa mashambulizi ya raia na vyombo vya habari. Hatupaswi kukubali, kusahau na kukosa kuiwajibisha serikali. Tunasubiri maafisa ambao walinaswa kwenye kamera wakikiuka sheria wachukuliwe hatua.”

Kauli hiyo inajiri huku kukiwa na mchakato unaoendelea wa Narc Kenya kutaka kujiondoa kwenye muungano wa Azimio La Umoja One Kenya, hatua ambayo ilichochewa na uamuzi wa Bw Odinga kujiunga na serikali.

Chama hicho kilisema kwamba kitawasilisha maelezo ya ukatili wa polisi kwa Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu (ACHPR), Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu na mashirika mengine husika.

Alisikitika kuwa licha ya kuwepo kwa ghasia juu ya ukatili wa polisi na matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji, watu kukamatwa bila makosa na utekaji nyara unaendelea kulenga watu wanaodai uwajibikaji.

“Tunakataa kukaa kimya. Tunakataa kuwasaliti Wakenya. Ni lazima tuzungumze kwa ajili ya wale ambao hawawezi kuzungumza.”

Kuhusu mjadala mkali wa mtindo wa ufadhili wa elimu ya juu, Bi Karua alisema kuwa ni usaliti kwa Wakenya.

“Ikitekelezwa bila ushirikishwaji wa umma sio tu ni kinyume cha Katiba, bali pia ni ubaguzi. Inazidisha ukosefu wa usawa wa kijamii na wa kiuchumi.”

Imetafsiriwa na Winnie Onyando