Akili MaliMakala

Uboreshaji masoko ya vyakula asilia freshi

Na SAMMY WAWERU September 15th, 2024 2 min read

ONGEZEKO la idadi ya watu linaendelea kushinikiza mahitaji ya chakula kupanda, kiwango cha 

mashamba ya kilimo kikipungua. 

Hilo linachochea kubisha hodi haja ya kuboresha mifumo kuzalisha chakula na kinakouziwa.

Licha la ongezekeo la watu, maeneo mengi nchini yanaendelea kutegemea masoko ambayo hali yake kimazingira ni ya kutatanisha, hatua inayoibua hofu ya masuala ya afya.

Masoko ni majukwaa ambapo wakulima, wafanyabiashara wa bidhaa za kula na walaji, yaani wanunuzi, hukongamana  hivyo basi kuleta utangamano mkubwa wa mtandao wa chakula.

Masoko ya zamani ndiyo yanatumika, japo wafanyabiashara hawana uwezo vile kuyaboresha.

Ruth Okowa, Mkurugenzi Mkuu GAIN Kenya. PICHA|SAMMY WAWERU

Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN), wakfu usio wa kiserikali kutoka Uswizi uliozinduliwa 2002 na Umoja wa Mataifa (UN), ukiwa na lengo la kuangazia masuala ya utapiamlo, umekuwa katika mstari wa mbele kuimarisha hali ya baadhi ya masoko ya chakula Kenya.

Aprili mwaka huu, 2024, shirika hilo liliandaa kongamano lenye kauli mbiu ‘Masoko Imara na Utawala wa Mifumo ya Chakula’, ambapo wadau kutoka serikali ya umma na kibinafsi kwenye mtandao wa kilimo na chakula walikutana.

Aidha, mkutano huo ulifanyika Jijini Nairobi.

Shirika la Chakula na Kilimo chini ya UN, ndilo FAO na lile na Afya Duniani (WHO), yalikuwa kati ya mashirika yaliyohudhuria, shabaha ikiwa jinsi ya kuboresha miundomsingi ya chakula, kuanzia shambani hadi sokoni.

Ruth Okowa, Mkurugenzi Mkuu GAIN Kenya akizungumza wakati wa Kongamano la Shirika hilo 2024 kuhusu mifumo ya masoko na chakula, jijini Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Kando na kuimarisha mazingira ya masoko, GAIN vilevile inaendeleza nchini mpango kuhakikisha yanafanya kazi, Keeping Food Markets Working (KFMW).

“KFMW ilizinduliwa Kenya ilipokumbwa na Covid-19, madhumuni yake yakiwa kulinda wafanyabiashara dhidi ya virusi vya corona na kuhakikisha chakula bora na chenye virutubisho faafu vinapatakina sokoni,” anasema Ruth Okowa, Mkurugenzi Mkuu GAIN Kenya.

Mikakati kuzuia msambao zaidi wa Corona iliathiri utendakazi wa maeneo muhimu, masoko yakiwa miongoni mwa yaliyohisi makali yake.

Ruth anasema GAIN iliona mwanya kuinua jamii kupitia uzinduzi wa KFMW.

Purity Ndunge, mmoja wa wafanyabiashara katika Soko la Marikiti, Machakos walionufaika kupitia mpango wa GAIN. PICHA|SAMMY WAWERU

Mpango huo ulitangulia na Kaunti ya Machakos na Kiambu, na sasa umepaa hadi Nairobi, Nakuru na Mombasa.

Purity Ndunge na Veronica Nguli, ni kati ya wafanyabiashara katika Soko la Marikiti, Machakos waliofaidika kupitia mpango wa shirika hilo.

“Mbali na kuboreshewa vibanda vyetu, GAIN imejitolea kuhakikisha mazingira tunayofanyia kazi ni safi na nadhifu,” Ndunge anasema.

Shirika hilo linajizatiti kuboresha miundomsingi ya majitaka, vibanda vya wafanyabiashara kwa kuvirembesha, kuwawekea vifaa vya kunawa mikono kuhakikisha chakula wanachouza kinasalia safi, kati ya huduma zingine.

Purity Ndunge, akipanga nyanya zake katika Soko la Marikiti, Machakos. PICHA|SAMMY WAWERU

Inakadiriwa zaidi ya asilimia 70 ya watu wanaoishi Afrika Mashariki, Afrika ya Kati, Kusini na Magharibi, hutegemea masoko ya zamani kununua chakula.

Hivyo basi, itakuwa busara endapo mazingira ya wafanyabiashara kwenye masoko hayo yataboreshwa ili kudumisha kiwango cha usafi.