Habari

Uchunguzi waanika uozo unaokumba shule za umma

March 25th, 2018 2 min read

Na WAANDISHI WETU

MAAFISA wa elimu wa ngazi za juu waliozuru kaunti 46 wameshtushwa na uozo unaokumba taasisi za elimu nchini Kenya.

Kundi hilo ambalo lilijumuisha maafisa kutoka Wizara ya Elimu, Baraza la Mitihani ya Kitaifa (KNEC), Taasisi ya Kuunda Mtaala (KICD) na Taasisi ya Elimu Maalum (KISE), limebaini kuwepo kwa idadi kubwa ya mimba za mapema, ndoa za mapema, utumizi wa dawa za kulevya na pia wanafunzi kukosa kufika shuleni.

Katika baadhi ya kaunti, takriban asilimia 60 ya wasichana wachanga wanaozwa mapema na kukosa kutumia nafasi ya elimu bila malipo, matokeo ya mijadala ambayo imekuwa ikiendelea kuhusu ubora wa elimu iliyomalizika Ijumaa yameonyesha.

Waziri wa Elimu, Amina Mohamed alisema midahalo hiyo ni muhimu katika kukusanya maelezo ambayo yatasaidia mageuzi yanayoendelea shuleni, baadhi ambayo yameegemezwa katika mitazamo iliyopitwa na wakati.

“Mageuzi yetu lazima yatekelezwe kulingana na data iliyokusanywa moja kwa moja kutoka kwa wadau walioathiriwa,” alisema.

Midahalo hiyo iliyohudhuriwa na wafanyakazi wa kitaifa na kaunti ilibainisha kuwa idadi ya wanafunzi wanaokosa kufika shuleni ni kubwa katika baadhi ya kaunti zaidi ya inavyotarajiwa.

“Tulishtushwa na viwango vya wanafunzi kukosa kufika shuleni katika baadhi ya shule, hali ambayo imechangia idadi ya wanaojiandikisha shuleni kupungua kwa sababu wanafunzi wengine wanaacha shule,” alisema mkurugenzi wa Elimu ya Mahitaji Maalum, Bi Maria Cherono.

Hali ni mbaya zaidi katika kaunti ya Kirinyaga ambapo wadau waliafikiana kuunda kundi maalum la kuchunguza changamoto za dawa za kulevya na wanafunzi kukosa kufika shuleni.

Katika Kaunti ya Meru, kundi hilo lilibaini kuwa mimba za mapema, utafunaji miraa, ukeketaji wa wasichana na ajira ya watoto kuwa changamoto zinazoathiri watoto.

Walimu kadha katika Kaunti ya Mombasa walilalamikia kukosa vitabu vya kutosha kuweza kufunza vilivyo. Katika Kaunti za Kisii na Nyamira, makanisa yalipigwa darubini kufuatia tuhuma kuwa yanaingilia kati usimamizi wa shule.

Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu Kaunti ya Kisii, Dkt Henry Onderi alisema baadhi ya wadhamini wanawajibikia kuanguka kwa shule zilizotambuliwa kwa sababu ya kuvuruga usimamizi.

Katika Kaunti ya Kilifi, mila na desturi za Wamijikenda zilitajwa kuchangia mimba za mapema na matokeo mabovu, hasa disko zinazochezwa matangani.
Gavana wa Kilifi, Amason Kingi ambaye alihudhuria kikao katika kaunti yake aliwahimiza wakazi kuachana na desturi potovu. Aliongeza kuwa ukosefu wa miundomsingi na walimu umeongeza kudorora kwa elimu.

Katika Kaunti ya Nakuru, msongamano madarasani ulibainika kuwa shida kubwa, darasa moja likiwa na wanafunzi zaidi ya 100.

Taarifa ya Ouma Wanzala, Diana Mutheu, Magati Obebo, Kalume Kazungu, Charles Lwanga, Barack Oduor, Francis Mureithi, Ruth Mbula, Francis Mureithi na Steve Njuguna.