Habari za Kitaifa

Ufichuzi: Matiang’i ameajiri kampuni ya kumchorea mipango ya 2027

Na VICTOR RABALLA August 8th, 2024 2 min read

ALIYEKUWA Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Okengo Matiang’i, ameanza kujipanga kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Dkt Matiang’i aliyefahamika kama ‘waziri mkuu’ wakati wa utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ameajiri kampuni inayotambulika duniani kumwandalia kampeni yake ya kutwaa urais wa Kenya.

Kampuni ya Dickens & Madson, yenye makao yake nchini Canada, italipwa Sh32.5 milioni ili kushawishi serikali na, au, mabunge ya mataifa yenye nguvu kama vile Amerika, Uingereza, Japan na nchi au serikali nyingine zozote zitakazokubaliwa, na mashirika ya kimataifa kwa niaba ya Dkt Matiang’i.

“Kampuni hii pia itatoa huduma nyingine kusaidia kubuni na kutekeleza sera kwa maendeleo yenye manufaa na uthabiti wa malengo yako ya kisiasa na kukusaidia kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya,” ilisema sehemu ya makubaliano yaliyotiwa saini mnamo Julai 13, 2024 yaliyoonwa na The Africa Report.

Dkt Matiang’i ambaye hajaonekana hadharani tangu aondoke afisini 2022, pia anatumai kutumia utendakazi wake alipohudumu katika wizara za ICT na Elimu, ambao ulivutia wengi.

Licha ya upinzani mkali, aliongoza uhamaji kutoka kwa utangazaji wa analogi hadi dijitali akiwa katika wizara ya ICT huku akisifiwa kwa kuanzisha hatua za kuzuia udanganyifu uliokithiri katika mitihani ya kitaifa akiwa Waziri wa Elimu kati ya 2015 na 2018.

Azima yake ya urais inaweza kuwasisimua baadhi ya waandamanaji vijana ambao walitumia mitandao yao ya kijamii kumuunga mkono wakati wa maandamano ya hivi majuzi dhidi ya serikali.

Hata hivyo, katika ngazi ya mashinani, Dkt Matiang’i atalazimika kubuni mkakati wa kukabiliana na muungano kati ya Rais William Ruto na kinara wa Upinzani Raila Odinga iwapo wataungana katika uchaguzi wa urais wa 2027.

Ingawa Dkt Matiang’i anatumai kutambuliwa kimataifa kupitia kampuni hiyo yenye makao yake makuu mjini Montreal, rekodi za hapo zamani za shirika hilo zinaweza kuongeza au kuhatarisha azima yake.

Dickens & Madson imezua mizozo kadhaa kimataifa.

Mnamo 2021, ililazimika kuacha kandarasi ya Sh260 milioni (Dola za Amerika 2m) na jeshi la Myanmar kutetea mapinduzi ya kijeshi ya Februari 1 katika nchi hiyo ya kusini-mashariki mwa Asia, baada ya kushindwa kupata kibali kutoka Amerika na Canada.

Miaka miwili kabla ya mzozo huo, kampuni hiyo ilitia saini mkataba wa Dola milioni 6 kutafuta fedha na kutambuliwa kidiplomasia kwa Jenerali Hamdan Dagalo wa Sudan, anayejulikana kama Hemedti, ambaye vikosi vyake vimeshutumiwa kwa mauaji ya waandamanaji mjini Khartoum.

Mpango huo, ulioripotiwa na The Globe and Mail, unajumuisha “kujitahidi kupata ufadhili na vifaa kwa jeshi la Sudan”.

Kampuni hiyo pia ilitaka “kusaidia kubuni na kutekeleza sera kwa malengo ya kisiasa ya Hemeti”.

Kwa wakati huu, Hemedti, kiongozi huyo wa kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) kinachopigana na Wanajeshi wa Sudan, ameshutumiwa na shirika la Human Rights Watch kwa kufanya uhalifu mkubwa wa kivita dhidi ya raia Darfur na maeneo mengine ya Sudan.