Habari za Kitaifa

Ukarimu wa wanajeshi wa Uingereza na KDF kutoa huduma za matibabu Isiolo na Laikipia bila malipo   

Na MWANGI NDIRANGU September 15th, 2024 1 min read

ZAIDI ya wagonjwa 17,000 wamenufaika kwa kupata matibabu ya bure kutokana na kliniki ambayo inatarajiwa itaendelea kwa wiki tano kwenye kaunti za Isiolo na Laikipia.

Huduma hizo za matibabu zimekuwa zikitolewa kutokana na ushirikiano kati ya Kambi ya Mafunzo ya Majeshi ya Uingereza Kenya (BATUK), Majeshi ya Kenya (KDF) na serikali za kaunti za Laikipia na Isiolo.

Madaktari na wahudumu, wataalamu wa kimatibabu wamekuwa wakitoa matibabu hayo katika soko la Juakali na mjini Nanyuki, Kaunti ya Laikipia.

Wakazi wa wadi za Bulapesa na Kinna, Katika Kaunti ya Isiolo pia wamenufaika na ukarimu huo.

Kamanda katika kambi ya Batuk Kanali Edd Gordon alisema kati ya huduma ambazo zinatolewa ni tiba kwa maradhi na elimu ya afya kwa wakazi katika vijiji 11 vilivyoko mashinani kwenye kaunti hizo.

Kwa kawaida, wanaotoka vijiji hivyo hutatizika sana kupata huduma za kimatibabu.

Pia, wahudumu waliwashauri wenye tatizo la utapiamlo, kutibu wenye matatizo ya meno na kupima wengi maradhi mbalimbali kisha kupendekeza matibabu.

“Kati ya wale 17,494 ambao walifika, watu 5,000 walitibiwa papo hapo huku 614 ambao walikuwa chini ya umri wa miaka mitano wakipewa dawa. Kutoa huduma hizi ni fahari kwetu kama wanajeshi kwa sababu tunasaidia jamii,” akasema Kanali Gordon.

Brigedia Olly Bryant ambaye ni mshauri wa Ubalozi wa Uingereza kuhusu masuala ya ulinzi, alisema kuwa wao hawapambani tu na ugaidi bali pia wanashiriki miradi ya kuinua jamii.

Batuk imekuwa ikishiriki miradi ya kuinua jamii na mnamo 2022 ilitumia Sh200 milioni kuchimba visima, kukarabati hospitali na shule na pia imekuwa ikidhamini mashindano ya michezo.