Akili MaliMakala

Ukuzaji avokado Kenya waendelea kustawi

Na SAMMY WAWERU August 21st, 2024 2 min read

KILIMO cha avokado nchini kinaendelea kunawiri kiwango cha idadi ya mashamba yanayolimwa kikiongezeka.

Hatua hiyo ni kutokana na wakulima kupevuka, na kukumbatia ukuzaji wa matunda haya ambayo pia yanajulikana kama maparachichi.

Nchi za Bara Uropa, China na Milki za Kiarabu (UAE) ndio wanunuzi wakuu wa avokado za Kenya.

Kakuzi PLC, ni kati ya kampuni na mashirika yaliyoidhinishwa na Mamlaka ya Mseto wa Mimea inayochukua muda mfupi kukomaa (HCD) kuuza maparachichi ng’ambo, na kwenye mahojiano ya kipekee Akilimali, Meneja Mkuu wa kitengo cha mimea mseto (horticulture), Jonathan Kipruto alisema wakilinganisha idadi ya mashamba waliyokuwa wakilima avokado miaka mitatu iliyopita kuna ongezeko kubwa.

“Kiwango cha ardhi tuliyokuwa tukipanda maparachichi sasa kimegonga Hekta 1, 057 kutoka Hekta 800 miaka mitatu iliyopita,” akasema afisa huyo.

Jonathan Kipruto, Meneja Mkuu wa kitengo cha mimea mseto Kakuzi PLC akielezea kuhusu kilimo cha maparachichi wakati wa Maonyesho ya Kimataifa Barani Afrika kuhusu Avokado 2024 yaliyofanyika Sarit Expo Centre, Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Hilo linaashiria kuimarika kwa sekta ndogo ya kilimo cha avokado nchini, mfano huo ukitoa taswira ya kampuni na wakulima wengine.

Kakuzi inaendeleza ukuzaji wa matunda hayo katika eneo la Makuyu, Kaunti ya Murang’a.

Isitoshe, ina kandarasi na wakulima Kipruto akidokeza kwamba kwa sasa inahudumu na wakuzaji wapatao 3, 500.

Aidha, hukagua, kupakia na kuuza maparachichi nje ya nchi.

Kando na matunda hayo yenye thamani na ambayo yanazidi kuwa na mvuto, pia hulima na kutafutia soko ughaibuni macadamia na blueberry.

Kulingana na Kipruto, katoni ya kilo 4 wakulima hulipwa Sh160, japo kuna viwango vingine vya uzani kwa mujibu wa saizi ya matunda.

Uzani unachezea kati ya kilo 4 hadi 10.

“Hayo ni malipo ya kwanza wanapotusambazia, na tuna mpango wa kutuza wanaohudumu nasi (CSR) ambapo baada ya kuuza mazao huwapa bonasi,” anaelezea.

Meneja Mkuu wa kitengo cha mimea mseto Kakuzi PLC, Jonathan Kipruto akionyesha tunda la avokado wakati wa Maonyesho ya Kimataifa Barani Afrika kuhusu Avokado 2024 yaliyofanyika Sarit Expo Centre, Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Hata hivyo, si wakulima wote wanaohudumu na Kakuzi huisambazia maparachichi kila wakati au msimu, afisa huyo akisema wengine huegemea kwa mashirika yenye bei bora.

Mwaka uliopita, 2023, Kipruto wakati wa mahojiano alifichua kwamba Kakuzi iliuza ng’ambo makontena 572.

Machi 2024, Halmashauri ya Kilimo na Chakula nchini (AFA) kupitia HCD ilifungua awamu ya uuzaji avokado ng’ambo kwa msimu wa mavuno unaoendelea.

Kulingana na data za HCD, kitengo kilichotwikwa jukumu na AFA kutoa mwelekeo na kudhibiti uuzaji wa mazao ya mimea yanayochukua muda mfupi kukomaa, uuzaji wa maparachichi ng’ambo umeongezeka kutoka tani metri (MT) 121, 068 mwaka 2002 hadi 468, 438 mwaka uliopita, 2023.

Mwaka jana, mauzo hayo yaliingiza mapato ya Sh157 bilioni.

Masoko yaliyochangamkia avokado za Kenya ni Uholanzi (asilimia 27), Uingereza (14), Ufaransa (13), UAE (5.8), Ujerumani (5.1) na Monaco (4.6).

Jonathan Kipruto, Meneja Mkuu wa kitengo cha mimea mseto Kakuzi PLC akihudumia wakulima wakati wa Maonyesho ya Kimataifa Barani Afrika kuhusu Avokado 2024 yaliyofanyika Sarit Expo Centre, Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Zaidi ya kaunti 32, zinazalisha maparachichi na 2023 Kenya ilizalisha 518, 500 MT kwenye Hekta 29, 150.

Kaunti inayoongoza katika ukuzaji wa matunda haya ni Murang’a ikiwakilisha kwa asilimia 23.2 ikifuatwa na Nakuru (12), Kisii (11), Kiambu (9), Nyamira (5), Meru (4), Uasin Gishu (4) na Bomet (3).

Kenya ndiyo inaongoza Barani Afrika katika uuzaji wa avokado ng’ambo, ulimwenguni ikiorodheshwa ya sita bora, baada ya Mexico, Colombia, Peru, Indonesia na Demokrasia ya Dominican.

Boniface Ngacha ni mmoja wa wakulima wa maparachichi katika Kaunti ya Nyeri, na licha ya kilimo cha matunda haya kuendelea kunoga analalamikia bei duni wanayolipwa na mabroka.

“Tunda moja bei ya langoni ikienda juu sana ni Sh5,” anateta. Yeye hukuza avokado asilia, Fuerte.

Jonathan Kipruto, Meneja Mkuu wa kitengo cha mimea mseto Kakuzi PLC akipanga maparachichi kwenye katoni wakati wa Maonyesho ya Kimataifa Barani Afrika kuhusu Avokado 2024 yaliyofanyika Sarit Expo Centre, Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Maparachichi yaliyoboreshwa aina ya Hass ndiyo yanalimwa kwa wingi.

Yote tisa, kumi, licha ya ukuzaji wa avokado kuimarika na kubobea, Kipruto anahimiza wakulima kuwa kwenye miungano au vyama vya ushirika ili kuwa na ushawishi wa soko.

“Itawasaidia kushirikiana na kampuni za kuuza mazao ng’ambo ili wawahi soko bora.”

Kakuzi ilikuwa miongoni mwa washirika waliohudhuria Maonyesho ya Kimataifa Barani Afrika kuhusu Avokado 2024 yaliyofanyika Sarit Expo Centre, Nairobi.

Yakiwa ni Makala ya Nne, yaliandaliwa na Chama cha Ushirika cha Maparachichi Kenya, ndicho Avocado Society of Kenya.