Mwanamfalme Karim al-Hussaini Aga Khan IV kuzikwa leo
MWADHAMA Mwanamfalme Karim al-Hussaini Aga Khan IV, Imamu wa 49 wa Waislamu wa Shia Ismailia anazikwa leo katika mji wa Aswan, Misri, kufuatia hafla ya mazishi iliyokuwa na hisia kali iliyofanyika Lisbon, Ureno hapo jana.
Mazishi ya Aga Khan IV, aliyefariki Jumanne akiwa na umri wa miaka 88, yatakuwa sherehe ya faragha.
Mtangulizi wake na babu yake, Sir Sultan Mahomed Shah Aga Khan III, pia amezikwa huko Aswan kwenye Makaburi ya Aga Khan yaliyo kando ya Mto Nile.
Taarifa iliyotolewa jana na Diwan wa Maimamu wa Ismailia ilisema kwamba mwili wa Mwadhama utalala kwenye kaburi la babu yake kwa muda.
‘Atazikwa katika kaburi la babu yake, marehemu Sir Sultan Mahomed Shah Aga Khan III, hadi kaburi jipya litakapojengwa kama mahali pake pa kupumzika kwenye ardhi iliyo karibu,’ ilisema taarifa hiyo.
Sherehe ya mazishi ya jana, iliyofanyika katika Kituo cha Ismaili huko Lisbon, ilihudhuriwa na Mwanamfalme Rahim Aga Khan V, Imam wa 50 wa Ismaili, na watu wengine wa familia ya Aga Khan.
Viongozi wa jamii ya Ismailia na Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan pia walihudhuria, pamoja na viongozi wa kimataifa.
‘Miongoni mwa viongozi wa kimataifa waliohudhuria ni Rais Rebelo de Sousa wa Ureno, Waziri Mkuu Trudeau wa Canada, na maafisa wakuu kutoka Jordan, Kyrgyzstan, Pakistan, Ureno, Qatar, Uhispania, Umoja wa Falme za Kiarabu na Uingereza miongoni mwa wengine,’ ilisema taarifa hiyo.
‘Jamii ya kimataifa ya Ismailia ilikusanyika ulimwenguni kote katika Jamatkhanas (maeneo ya ibada) ili kushuhudia sherehe kwa njia ya moja kwa moja kwenye runinga, na kuenzi maisha ya ajabu ya Imam wao.
“Jeneza la Muadhama lilikuwa limefunikwa kwa kitambaa cheupe kilichopambwa kwa dhahabu. Iliingizwa ndani ya ukumbi wa sherehe na watu wa kujitolea kutoka jamii ya Ismailia, huku sala zikisomwa za kuomba baraka kwa Mtume Muhammad na kizazi chake (amani iwe juu yao). Aya za Qur’ani Tukufu zilisomwa na, baada ya hapo, wageni walipita kando ya jeneza kutoa heshima zao za mwisho,’ ilieleza taarifa hiyo.
Kwingineko, nchini Pakistan, Jumamosi ilikuwa siku ya kitaifa ya maombolezo.
Kufuatia agizo la Baraza la Mawaziri siku ya Alhamisi, bendera ya taifa ilipeperushwa nusu mlingoti. Waziri wa Fedha wa Pakistan, Seneta Muhammad Aurangzeb, alikuwa miongoni mwa waliohudhuria hafla ya mazishi huko Lisbon.
Baada ya mazishi ya leo, Jumanne itakuwa tarehe muhimu katika kalenda ya Waislamu wa Ismailia kwani hiyo ndiyo siku ambayo sherehe ya kumtawaza Aga Khan mpya itafanyika.
‘Sherehe maalum ya heshima itafanyika Lisbon, Ureno. Mwanamfalme Rahim al-Hussaini Aga Khan V atakutana na viongozi wakuu wa jamii ya Ismailia, ambao watatoa kiapo cha utiifu wao, kwa niaba ya jamii ya kimataifa ya Ismailia, kwa Imamu wa 50 wa Waislamu wa Ismailia,” ilisema taarifa ya Ismailia Imamat siku ya Alhamisi.