Uncategorized

Njia ni hii: Walimu wakuu watoa pendekezo la kusaidia CBE ifaulu

Na WINNIE ATIENO November 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HUKU Kenya ikijiandaa kuanzisha Shule za Upili chini ya Mfumo wa Elimu Unaotegemea Umilisi (CBE), wadau wa elimu wametaja vipaumbele vya msingi vinavyolenga kudumisha usawa, ubora, na maendeleo katika mageuzi ya elimu yanayoendelea.

Akizungumza katika kongamano la kila mwaka la Chama cha Wakuu wa Shule za Msingi Kenya (Kepsha) lililofanyika Mombasa, Mwenyekiti wa Kitaifa, Bw Fuad Ali Abdalla, alisema kuwa awamu inayofuata ya mageuzi ya elimu itazingatia uelewa wa mtaala, kuboresha miundombinu ya shule, na kuimarisha uwezo wa walimu ili kuhakikisha mpito mzuri na utekelezaji wenye mafanikio.

“Kenya inapokita mafanikio katika Shule za Msingi na kujiandaa kwa Shule za Upili, ni lazima  tuhakikishe kila mwanafunzi, bila kujali asili yake, anapata elimu bora, jumuishi, na yenye mabadiliko,” alisema Bw Abdalla.

Miongoni mwa vipaumbele vilivyotajwa ni kuboresha ushauri kuhusu ajira na uelewa wa mtaala ili kusaidia wanafunzi na wazazi kufanya maamuzi sahihi kuhusu  mikondo  ya CBE. Shule zinaandaa pia mipango ya ushauri wa kina ambapo walimu maalum watatoa mwongozo na kuwapa wanafunzi fursa za kuunganishwa na sekta za viwanda na vyuo vikuu.

Chama pia kinaomba uwekezaji mkubwa katika miundombinu na teknolojia, hasa katika Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisbati (STEM), sanaa, na michezo.

Bw Abdalla alitoa wito kwa serikali kutumia ushirikiano kati ya sekta ya kibinafsi na umma ili kupanua maabara, vituo vya ICT, na miundombinu ya michezo ili kuziba mapengo yaliyopo.

“Mabadiliko ya kidijitali shuleni lazima yaendane na upanuzi wa miundomsingi. Upatikanaji sawa wa vifaa vya kisasa vya kufunza si  hiari tena bali ni lazima,” alisisitiza.

Kipaumbele kingine ni uwezo na walimu wa kutosha, ambapo kuna wito kwa maendeleo endelevu ya taaluma katika ufundishaji wa kisasa, uelewa wa kidijitali, na tathmini inamlenga mwanafunzi.

Kuhusu ufadhili, chamna kimeomba serikali kuanzisha mfumo wa ufadhili unaohusiana na utendaji kama ilivyoelezwa katika Sheria ya Elimu ya Msingi (2025), unaolenga kuhakikisha usambazaji wa rasilmali kwa wakati na kwa usawa kulingana na matokeo na mahitaji.

Bw Abdalla pia alisisitiza ushirikiano wa wazazi na jamii kama msingi wa mageuzi ya elimu yenye mafanikio, akihimiza mipango kama Elimu Mashinani.