Habari za Kitaifa

Ustadh aomba dua kwa Mungu mswada wa nyumba uanguke

January 30th, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

KIOJA kilizuka mjini Mokowe, Lamu, wakati ustadh mmoja wa dini ya Kiislamu aliomba dua kwa Mwenyezi Mungu akitaka Mswada wa Nyumba za Bei Nafuu kuangushwa na kalamu ya Muumba.

Umati uliofika kushiriki mjadala kuhusu Mswada wa Nyumba za Bei Nafuu uliangua kicheko pale aliposimama mbele ya hadhira na kuuombea dua mswada huo ‘kupigwa kalamu’ ya kutotimia na Mwenyezi Mungu endapo unaweza ukawa na ‘shoti’ kwa wananchi wanyonge ambao huenda wadhulumiwe haki yao.

Ustadh Omar Athman Hamisi, ambaye pia aliwakilisha vijana, alisimama wima mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa Kuhusu Fedha na Uendelezaji wa Vikao vya Kushirikisha umma nchini kuhusu Mswada wa Nyumbaza za Bei Nafuu, ambapo aliweka wazi shauku ya wananchi kuuhusu mswada huo, akishikilia kuwa ipo hofu inayowazonga Wakenya wengi wanaohisi kudhulumiwa kupitia mpango huo.

Zaidi ya Wabunge 10 wanachama wa kamati hiyo waliohudhuria kikao hicho mjini Mokowe wakiongozwa na Mwenyekiti wao, ambaye pia ni Mbunge wa Molo Kuria Kimani, pia waliachwa na mshangao kufuatia ujasiri wa ustadh huyo wakati akiukosoa Mswada na hata kuuombea Allah (Mungu) mwenyewe kuuangusha.

Wabunge wanachama wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Fedha wakiongozwa na mwenyekiti wao, Kuria Kimani (Molo) wakati wa kikao chao Mokowe, Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Kikao hicho kilifanyika kwenye ukumbi wa kijamii wa Mokowe, ambapo ulihudhuriwa na mamia ya wakazi.

Kulingana na ustadh Hamisi, inavyoonekana ni kwamba wanaosukuma kufaulishwa kwa mswada huo wana ajenda fiche ambazo siyo za kumfaidi mwananchi wa kawaida ila tu wale wa tabaka la juu.

Bw Hamisi alilinganisha ushawishi na shinikizo zinazoendelezwa na wabunge na hata Rais mwenyewe, William Ruto kuhusu kukumbatiwa kwa Mswada wa Nyumba za Bei Nafuu kuwa sawa na msemo wa Uswahilini kwamba ‘anayetaka kumshika na kumchinja kuku lazima ambembeleze kwa kumwagia punje za mtama, wimbi na mahindi badala ya kumkimbiza na kumkamata ndege huyo moja kwa moja.

Aliendelea kueleza kuwa punde kuku huyo ‘anapoingia boksi’ na kukamatwa basi huwa hana ujanja tena, akisema wakenya pia wanaelekea huko kupitia mpango huo wa Nyumba za Bei Nafuu.

“Namaanisha licha ya mpango huo wa Nyumba za Bei Nafuu kuonekana kuwa jambo zuri lakini kwa upande mwingine ni mtego tu. Ni wazi kwamba Wakenya wana hofu, hasa kulingana na ulimwengu wetu wa leo ambao ni wa madeni. Ukitazama leo hii utaona kuna simu za mkopo, pikipiki za mkopo, taa za mkopo na inavyoonekana sasa tunaelekea kwa hizi nyumba ambazo huenda zikageuka kuwa za mkopo pia,” akasema Ustadh Hamisi.

Alisema kuna tashwishi ama hofu inayogubika Wakenya wengi kuwa endapo mwananchi atalipia nyumba za bei nafuu na kisha kushindwa kulipia kinachotakikana njiani huenda asirudishiwe fedha zake kama inavyoshuhudiwa kwenye mashirika ya kukopesha nchini.

“Kutokana na hilo, basi ningemuomba Mwenyezi Mungu, ikiwa mradi ni wa kheri na manufaa kwa wananchi, basi auajalie utimie na ikiwa ni wenye shoti kwa wananchi wanyonge ambao huenda wadhulumiwe haki yao, basi Mwenyezi Mungu apitishe kalamu yake ya kutotimia mradi huu, Ameen,” akasema Ustadh Hamisi huku umma ukiangua kicheko ukumbini.

Ni wakati huo ambapo Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge la Kitaifa Kuhusu Fedha, Bw Kuria Kimani, alisimama tisti ukumbini na kuwahakikishia Wakenya kwamba mradi ni wenye kumfaidi mwananchi wa mapato ya chini na yule wa mapato ya juu, ambapo wote watawezeshwa kuishi kwenye nyumba za hadhi nzuri.

“Ningewasihi nyote tuungane kupitisha mpango huu. Nyumba za Bei Nafuu zitafaidi wananchi wa kila tabaka, iwe ni la juu au la chini. Isitoshe, mpango huu unanuia kuinua mitaa ya mabanda nchini, hivyo kufanya maisha ya wananchi yawe ya kutamanika popote walipo. Hakuna nia yoyote mbaya ya kudhulumu mwananchi kupitia mpango huu. Hiyo ndiyo sababu tumefika hapa Lamu kuchukua maoni yenu kwa uwazi na uwajibikaji kwa mujibu wa Katiba yetu ya Kenya,” akasema Bw Kimani.

Baadhi ya wenyeji wa Mokowe wakisikiliza mawasilisho wakati wa kushirikisha umma suala la Mswada wa Nyumba za Bei Nafuu. PICHA | KALUME KAZUNGU