Habari Mseto

Utapiga mfuko zaidi kutumia ‘barabara ya ghorofa’ Nairobi Expressway

January 1st, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

SERIKALI imetangaza kuongeza ada zinazotozwa magari tofauti kwa kutumia barabara ya Nairobi Expressway.

Hatua hiyo inafuatia notisi iliyochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali na Waziri wa Uchukuzi, Bw Kipchumba Murkomen mnamo Desemba 19, 2023, ambapo aliidhinisha kuongezwa kwa ada hizo.

Bw Murkomen alitaja nyongeza hiyo kuchangiwa na kudorora kwa thamani ya Shilingi ya Kenya dhidi ya dola ya Amerika, ambayo kwa sasa inauzwa kwa Sh156.46

“Kutokana na mamlaka niliyopewa na Sehemu 4B (3) ya Sheria ya Ada za Usafiri, Waziri wa Barabara na Uchukuzi ameidhinisha kuongezwa kwa ada zinazotozwa magari katika barabara ya Nairobi Expressway,” ikaeleza notisi hiyo.

Kutokana na hilo, waendeshaji magari watakaolipa ada za chini zaidi watalipa Sh170 kutoka Sh120, kwa kutumia barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 27.

Ada itakayotozwa magari madogo (kama yale ya kibinafsi) imeongezeka kutoka Sh310 hadi Sh500.

Ada zinazotozwa magari hayo zitakuwa kama ifuatavyo:

  • Westlands hadi Mlolongo na Syokimau —-Sh500
  • Westlands hadi JKIA na Easter Bypass —-Sh410
  • Westlands hadi Southern Bypass —-Sh330
  • Westlands hadi Haile Selassie na Capital Centre —-Sh250
  • Westlands hadi Museum Hill —–Sh170

Magari makubwa makubwa kama malori na matrela yatatozwa Sjh2,500 kutoka Sh1,550.

Hata hivyo, Wakenya wamekosoa hatua hiyo, wakiitaja kuwa isiyofaa, hasa wakati huu ambapo wengi wanakabiliwa na gharama ya juu ya maisha.

“Haya ni mateso ya wazi kwa Wakenya, Waziri Murkomen. Tushachoshwa na nyongeza kubwa ya ushuru!” akalalama Wakili  Ahmednasir Abdullahi kupitia mtandao wa ‘X’.

Wakenya wengine walimuunga mkono wakili huo, baadhi wakisema watapinga ada hizo mpya mahakamani.