Habari za Kitaifa

Uzembe wa polisi wafanya serikali iamriwe kufidia waliokufa chuoni Sh496 milioni

Na RICHARD MUNGUTI August 1st, 2024 2 min read

SERIKALI imeagizwa kulipa fidia ya Sh496 milioni kwa wanafunzi waliojeruhiwa na wazazi waliopoteza watoto wao wapendwa wakati wa shambulio la kigaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa miaka tisa iliyopita.

Majaji watatu wa Mahakama Kuu waliamua kwamba serikali ilishindwa kuzuia watu kupoteza maisha kwani kulikuwa na ushahidi kwamba shambulio lingetokea katika chuo kikuu hicho mnamo Aprili 2015.

Majaji Anthony Ndung’u, Mugure Thande na David Kemei walisema ingawa vikosi vya usalama vinaweza kupongezwa kwa juhudi zao ambapo wanafunzi 600 waliokolewa katika chuo hicho mnamo Aprili 2, 2015, kuchelewa kupeleka kikosi cha Recce, kulisababisha vifo zaidi.

Wakati wa shambulio hilo la alfajiri, magaidi waliokuwa na silaha waliwateka wanafunzi kwa saa kadhaa na kuwasababishia mateso ya kiakili, maumivu na uchungu kabla ya kuwapiga risasi na kuwaua.

Watu 148, wengi wao wakiwa wanafunzi walikufa wakati wa shambulio hilo na wanaume mnamo 2019 watatu walipatikana na hatia na kufungwa jela kuhusiano na shambulio hilo.

Mahakama ilimpa kila mwanafunzi aliyejeruhiwa kati ya Sh1.2 milioni na Sh10 milioni kulingana na kiwango cha majeraha.

Kwa waliofariki, majaji waliagiza Serikali kulipa kila mmoja Sh3 milioni.

Majaji Mugure Thande (kushoto) Daniel Ndung’u na Daniel Kemei walipoamuru Serikali ilipe wazazi wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Garissa waliouawa kwenye shambulio la kigaidi 2015. Picha|Richard Munguti

“Kulikuwa na uzembe kwa upande wa washtakiwa, ambao walichukua hatua kutokana na tukio hilo la kusikitisha,” majaji walisema.

Majaji hao walisema ushahidi uliowasilishwa mahakamani ni kwamba kikosi cha Recce, ambacho kinafaa zaidi kwa shughuli kama hiyo hakikufika hadi saa kadhaa baadaye.

“Kwa hivyo, inafuata kwamba matarajio halali ya walalamishi yalikiukwa. Iwapo polisi wangewajibika kwa njia ya kitaalamu zaidi kwa kuzuia kwa ufanisi na umakini, shambulio hilo lingezuiwa au angalau, mauaji hayo yangepunguzwa,” walisema majaji.

Mahakama ilisema uongozi wa serikali na chuo kikuu ulishindwa kulinda wanafunzi waliosafiri kutoka mbali katika harakati zao za kutafuta elimu na kuweka msingi thabiti wa maisha yao ya baadaye.

Mahakama ilisema kuwa kulikuwa na ushahidi kwamba mkuu wa chuo hicho aliomba kuimarishwa kwa usalama katika taasisi hiyo lakini ombi hilo halikuzingatiwa vya kutosha na polisi.

Hii ni kwa sababu, idadi ya maafisa wa polisi iliongezwa kutoka wawili hadi wanne.

“Ni dhahiri kwamba tishio la shambulio katika chuo kikuu lilikuwa halisi. Kwa hivyo, kwa kukubali kwao, idara za usalama zilifahamu shambulio lilikuwa litokee na hivyo walikuwa na jukumu la kuimarisha usalama,” wakaongeza majaji.

Kituo Cha Sheria kiliwasilisha kesi hiyo kwa niaba ya wanafunzi 14 waliopigwa risasi na kupata majeraha wakati wa shambulio hilo na kwa niaba ya wazazi waliopoteza watoto wao.

Walalamishi walilaumu serikali kwa kukosa kutuma maafisa wa polisi ili kuhakikisha kuwa usalama wa kutosha ndani ya chuo.