Habari za Kitaifa

Vijana wahimizwa kutumia ubunifu kupigana na zimwi la ufisadi

Na FRIDAH OKACHI September 6th, 2024 1 min read

VIJANA jijini Nairobi wametakiwa kuwa wabunifu ili kukabiliana na ufisadi katika sekta mbalimbali.

Msimamizi wa mradi wa USAWA unaoleta pamoja mashirika ya kijamii kupambana na ufisadi Bw Titus Gitonga, aliwataka vijana hao kutoa michango ya maana kwa jamii kwa kuwa wabunifu wanapotumia njia za kidijitali ili kuimarisha sekta muhimu kama vile huduma ya afya.

Bw Gitonga alisema sekta muhimu nchini zinakabiliwa na changamoto ya udanganyifu katika utoaji huduma kwa umma.

Alisema vijana walio na ujuzi wa uvumbuzi wana uwezo wa kutoa suluhu kwenye sekta hiyo.

“Vijana wengi wanaweza kubuni vifaa ambavyo vinaweza kuthibitishia umma pesa zilitumika au kutolewa na mwananchi wakati wa kupata huduma. Tunataka kuhakikisha watu wanapata taarifa za kutosha na wanaweza kushiriki kwenye uongozi na kutoa uamuzi,” alisema Bw Gitonga.

Mwanaharakati Bw Kennedy Sakara, alisema sekta ya afya ambayo iligatuliwa ina jukumu kubwa zaidi na hupokea rasilimali nyingi. Jukumu lao, ni kuhakikisha wananchi wanaweza kushiriki kukuza uwajibikaji.

Bw Kennedy Sakara akieleza kuhusu mbinu za kukabiliana na ufisadi. PICHA|FRIDAH OKACHI

 “Lengo letu ni kuleta pamoja wananchi, wafanyabiashara na viongozi wa kidini ili kuongeza ufahamu kuhusu haki zetu kama watumiaji wa huduma hizo,” alisema Bw Sakara.

“Sisi ni kizazi kilichounganishwa na taarifa na tuwe tayari kuleta mabadiliko. Tujifahamishe jinsi fedha zilizotengewa jamii zinatumika kwenye sekta muhimu kwa kutumia mitandao ya kijamii kuangazia masuala yanayohusiana na bajeti za afya na ripoti za miradi. Tutumie kile tulicho nacho kuepusha ufisadi,” aliongeza.