Habari Mseto

Wabunge 34 wanaugua kansa, mbunge afichua

April 25th, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE 34 wanaugua maradhi hatari ya kansa, Mbunge wa Juja Francis Waititu alifichua Jumanne jioni.

Mbunge huyo alielezea kushangazwa na ongezeko la visa hivyo akisema miezi miwiil iliyopita alisafiri hadi India kutibiwa ugonjwa huo. Wakati huo, akasema, alifahamu wabunge 14 pekee waliogua, idadi ambayo imeongezeka kufikia sasa.

Bw Waititu ambaye alitibiwa kansa ya ubongo nchini India alisema alishangaa alipokutana na wenzake huko wakiugua ugonjwa huo.

“Nimeongea nao wote na kuwapa moyo kwamba kuna matumaini na kwamba watapona,” akasema bungeni.

Bw Waititu alikuwa akichangia hoja ya kusitishwa kwa mijdala bungeni ili kutoa nafasi kwa wabunge kutuma rambirambi zao kufuatia kifo cha Mbunge wa Baringo Kusini Grace Kipchoim.

Mbunge huyo alifariki wiki iliyopita baada ya kuugua ugonjwa wa kansa ya utumbo (colon cancer) kuanzia mwaka wa 2014.

Wabunge waliochangia alitoa wito kwa Serikali kupeleka mitambo ya kuchunguza kansa katika hospitali zote za kaunti.

“Taifa hili linahitaji mashine za kuchunguza kansa kwani hospitali nyingi za umma zinakosa mitambo hii. Uchunguzi wa mapema ndio njia mwafaka wa kupambana na ugonjwa huu hatari, Waititu akawaambia wenzake,

Mbunge mpya wa Kitui Magharibi Bi Edith Nyenze, alielezea jinsi mumewe Francis Nyenze, aligunduliwa kuugua ugonjwa huo.

Wabunge walimtaja marehemu Kipchoim kama mwanamke jasiri aliyepambana na wanaume na kushinda kiti hicho katoka jamii Endorois ambako jinsia ya kike hunyimwa nafasi ya kuwania nyadhifa za uongozi.

“Marehemu Kipchoim ni kielelezo cha kiongozi ambaye alivunja changamoto za kitamaduni katika jamii yake na kushinda katika uchaguzi mkuu mara mbili.

Wanawake wengine wanafaa kuiga mfano wake na kupigania nyadhifa za uongozi sambamba na wanaume,” akasema kiongozi wa wengi Aden Duale.