Habari Mseto

Wabunge Kitui wazozana na bintiye Ruto kuhusu viatu

June 6th, 2024 1 min read

NA KITAVI MUTUA

WABUNGE wawili wa mrengo wa Kenya Kwanza wamemkemea vikali Charlene Ruto kwa kusambaza viatu katika shule za Kitui bila ya kuwahusisha.

Mbunge wa Kitui Kusini, Dkt Rachel Nyamai, alimlaumu waziri wa Afrika Mashariki na Maeneo Kame, Bi Penina Malonza, kwa kumpotosha mtoto wa Rais kuhusu itifaki.

“Ninajua kuna njama ya kutonifahamisha kuhusu yanayojiri ndani ya eneobunge langu. Aliyepanga mambo haya aache kumhusisha mtoto katika siasa za Kitui,” akasema.

Lakini Waziri Malonza alisema afisi yake iliandika barua za mwaliko kwa viongozi wote, wakiwemo MCA wa Kitui Kusini.

Mbunge wa Kitui Mashariki, Nimrod Mbai aliudhihaki wakfu wa Zero Bare Foot Campaign unaoendeshwa na Charlene, akidai kuwa viatu vinavyosambazwa kwa watoto wa shule havifai.

“Kwanza ni viatu vya plastiki isiyo na thamani. Vingi ni vikubwa kwa wanafunzi. Wamelazimika kurudi navyo Nairobi kwa sababu hakuna hata kimoja kilichokuwa saizi ya miguu ya watoto wetu,” akasema.

Bi Charlene Jumanne alipokuwa akisambaza viatu hivyo katika shule ya msingi ya Kyoani eneo la Ikutha, aliwajibu wabunge hao.

“Sielewi kwa nini wananiandama na maneno ilhali mimi si mwanasiasa wala mtu wa rika lao,” akasema.