Habari za Kaunti

Wafanyakazi Uasin Gishu wapinga mpango wa bima ya afya

Na TITUS OMINDE August 25th, 2024 1 min read

ZAIDI ya wafanyikazi 3600 wa serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu ambao ni wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Kaunti (KCGWU) tawi la kaunti hiyo, wanaitaka serikali hiyo kujiondoa katika mpango wa bima ya afya ya thamani ya  Sh255 milioni unaotolewa na kampuni ya Bima ya Trident.

Wafanyikazi hao wenye ghadhabu wanadai viwango vya huduma zinazotolewa katika hospitali  zilizoteuliwa na kampuni hiyo kuwahudumia ni duni zaidi.

Walidai kuwa hospitali  za kibinafsi zisizojulikana mjini Eldoret ndizo zimepewa kandarasi na kampuni hiyo.

Wakizungumza wakati wa mkutano wa wafanyakazi wa kaunti mjini Eldoret  Jumamosi Agosti 24, 2024, wafanyakazi walidai hawapati huduma bora katika hospitali hizo zisizo na dawa, vifaa na wahudumu wa kutosha.

“Ukweli wa mambo ni kwamba hospitali zilizoteuliwa na kampuni hiyo ya bima hazina uwezo wa kutoa bima ya matibabu kwa wafanyakazi wote wa serikali hii akiwemo gavana Jonathan Bii,” alisema mwenyekiti wa KCGW tawi la Uasin Gishu,  Isaac Kiptallam.

Kwa hivyo, wamemtaka Gavana Bii kusitisha kandarasi ya bima ya afya aliyotoa kwa kampuni hii.

Bw Kiptallam alifichua kuwa serikali ya kaunti haikushirikisha maoni ya wafanyikazi kabla ya kuwasajili wanachama wake katika mpango huo wa bima ya afya.