Habari

Wafuasi wa Waititu wamkabili diwani wa Thika Township

March 7th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO
 
MKUTANO wa Gavana wa Kiambu ulizua taharuki wakati wafuasi wake walimkabili diwani wa Thika Township.
Ilidaiwa kuwa Bw Ferdinand Waititu alikuwa amezuru kijiji cha Kiandutu kwa minajili ya  kujadili maswala ya  ardhi ambayo yamekuwa kero kubwa katika eneo hilo.
Hata hivyo kwa muda mrefu diwani wa eneo la Thika Mjini, Bw Andrew Kimani amekuwa na uhusiano mbaya na Bw Waititu lakini mnamo Jumatano, alihudhuria mkutano huo uliopangwa na gavana.

Hata hivyo baada ya Bw Waititu kuhutubia wakazi wa Kiandutu, alitaka diwani wake awasalimie wananchi kabla ya kukamilisha hotuba yake.

“Mnataka diwani wenu awasalimie  kabla niendelee na hotuba yangu? Mnanisikia vyema?” Bw Waititu alisikika akiuliza wananchi.

Nao wananchi kwa hasira walisema hawataki salamu za diwani huyo ambaye walidai huwa hatembei sehemu hizo, na hafahamu yale yanayoendelea eneo hilo.

Hata hivyo diwani naye alitaka kuhutubia watu japo kwa lazima kwani hata yeye alikuwa na wafuasi wake waliokuwa katika hafla hiyo.

Je, ilikuwa ni kuchochea?

Ilidaiwa ya kwamba hatua ya gavana  kuuliza wananchi iwapo diwani huyo alikuwa na wakati wa kuhutubia ilikuwa  ni njia moja ya kuchochea watu dhidi ya diwani huyo ambaye alionyesha hasira.

“Jambo muhimu hapo lilikuwa kuhusu maswala ya ardhi lakini liligeuka kuingizwa siasa,”diwani Kimani alisikika akisema.

Wafuasi wa diwani huyo pia waliteta ya kwamba diwani wao amekuwa akihangaishwa na gavana wao kwa kunyimwa fedha za CDF matokeo yakiwa ni watu wa eneo lake kutaabika.

Wengi wa wale waliohudhuria hafla hiyo hawakuridhika na jinsi mambo yalivyoendeshwa kwa sababu siasa ndiyo ilitawala mkutano huo.

Naye Bw Waititu alisema wakati wa kugawanya ardhi hiyo ni wakongwe ndio watanufaika kwanza kwa sababu ni wao wameishi mahali hapo kwa muda mrefu.

“Tutahakikisha ugavi wa ardhi ukianzishwa tutafanya juhudi kuona ya kwamba wakongwe wanakuwa mstari wa mbele kunufaika kwanza,” alisema Bw Waititu.

Hata hivyo, mkutano huo ulikamilika kwa taharuki kila mmoja akijali zaidi maisha yake.

Ilidaiwa kwa miezi kadha madiwani wachache wamekuwa katika maelewano mabaya na Gavana wao huku wengine wakinyimwa fedha za maendeleo.