Habari

Waiguru sasa asimamisha ada za madaktari

May 25th, 2019 1 min read

Na GEORGE MUNENE

GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru ameagiza serikali yake kusimamisha ada za madaktari wanaofanya kazi kaunti hiyo kwa Chama cha Madaktari Kenya (KMPDU) mara moja.

Bi Waiguru alikilaumu chama hicho kwa kuidharau na kutoiheshimu serikali yake.

Kutokana na hayo, aliwaagiza maafisa wa idara ya fedha kutekeleza agizo hilo mara moja.

Bi Waiguru alisisitiza kwamba serikali yake haitatuma michango kwa chama ambacho kinaingilia na kusambaratisha shughuli za utoaji huduma za afya katika kaunti hiyo.

“Hakuna vile tunaweza kuendelea kutuma ada kwa chama ambacho kinanipiga vita bila sababu zozote. Chama kitalazimika kuwashinikiza wanachama wake kutoa michango hiyo wao binafsi bila kuihusisha serikali yangu,” akasema.

Gavana huyo alishikilia kwamba chama hicho kinaingiza siasa katika malalamishi yake, kwani bado kinaishambulia serikali yake ya hali ya usafi kurejeshwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kerugoya.

Aliwaambia wafanyakazi katika sekta ya afya kupuuzilia mbali mwito chama chao kususia kazi na kuendelea kuwahudumia wakazi.

Kuimarika

Akihutubu Ijumaa mjini Kutus, Bi Waiguru alisema kuwa sekta hiyo imeimarika, hasa hali ya usafi, hivyo wafanyakazi hao hawapaswi kushiriki katika mgomo.

Alikilaumu chama hicho kwa kuwapotosha wafanyakazi hao kushiriki katika mgomo, kwa manufaa yake binafsi.

“Chama hiki kinatumiwa na wanasiasa kuwachochea wafanyakazi kugoma ilhali Hospitali ya Rufaa ya Kerugoya na zingine zinaendesha shughuli zao bila matatizo yoyote. Hizi ni siasa tu. Wafanyakazi wanapaswa kuendelea na shughuli zao bila kukubali kuingiliwa kwa namna yoyote,” akasema.