Habari Mseto

Wakazi wa Juja wataka hospitali ya Gachororo iboreshwe

November 29th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

HOSPITALI ya Gachororo iko katika hali ambayo si nzuri kuweza kuhudumia wagonjwa kikamilifu.

Afisa mkuu wa hospitali hiyo Bw Daniel Mukabi, alisema kwa muda mrefu hospitali hiyo imekuwa kwa hali mbaya huku wagonjwa wakikosa kupata huduma jinsi inavyofaa.

“Hata wahudumu katika hospitali hii wamekuwa wakilalamika kuhusu ukosefu wa vifaa bora ili kuwahudumia wagonjwa kikamilifu. Tungetaka Kaunti ya Kiambu ishirikiane na serikali kuu kukipa kituo hiki sura mpya ili kuwapa wagonjwa matumaini ya kutibiwa,” alisema Bw Mukabi.

Alisema wakati huu wa janga la Covid-19 kuna changamoto tele kwa sababu hata wagonjwa wenyewe hawapati huduma nzuri.

“Kwanza wahudumu wa afya wanakosa magwanda muhimu ya kujilinda wawapo kazini; hali inayowaweka katika hatari ya kuambukizwa Covid-19. Serikali ifanye hima kuona ya kwamba magwanda hayo yanapatikana haraka iwezekanavyo,” alisema Bw Mukabi.

Bw JM Kariuki ambaye ni mkazi wa Juja alisema hospitali hiyo inastahili kuzingirwa na ukuta ili kuweka ulinzi unaostahili.

“Hospitali hiyo ya Gachororo iko katika hali mbaya sana na inastahili marekebisho ya dharura,” alisema Bw Kariuki.

Akafafanua: “Tungetaka kuwa na hospitali safi yenye dawa za kutosha kwa sababu idadi ya wakazi wa Juja iko juu zaidi.”

Alisema serikali ya kaunti ni muhimu ifanye mazungumzo na serikali kuu ili kuikarabati hospitali hiyo ambayo inastahili kufanyiwa marekebisho haraka iwezekanavyo.

Alisema hospitali hiyo ina zaidi ya miaka 10 tangu ifunguliwe na kwa hivyo inastahili kupandishwa hadhi hadi daraja la 4.

Alisema wakazi wengi wa Juja hulazimika kusafiri hadi hospitali ya Thika Level 5 ama Ruiru Level 4 kutafuta matibabu.

“Jambo hilo linawapa wakazi hao wakati mgumu na kwa hivyo jambo la dharura linastahili kuzingatiwa,” alisema mkazi huyo wa Juja.

Alisema hata ambulensi ambayo ilikuwa ikisaidia wagonjwa katika hospitali hiyo ilipata hitilafu na haiko katika hali nzuri.

Aliongeza kusema ya kwamba wagonjwa wengi huamua kuenda kutibiwa katika hospitali za wamiliki binafsi lakini pia kulipa ada ya juu ya matibabu.