Habari za Kitaifa

Wakenya wamuomboleza Shari Martin aliyevuma kwa wimbo wake wa ‘Rafiki Pesa’

Na ELIZABETH NGIGI August 6th, 2024 1 min read

WAKENYA wamejitokeza katika majukwaa tofauti kumuomboleza mwanamuziki maarufu Shari Martin, aliyevuma sana kwa wimbo wake ‘Rafiki pesa’.

Martin aliaga dunia mnamo Agosti 2, 2024, akiwa na umri wa miaka 54 alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta.

Kifo chake kilithibitishwa na rafiki yake wa karibu na msanii mwenzake, ambaye alijitambulisha kama Bi Pauline.

Kulingana na Bi Pauline, mwanamuziki huyo alianza kuugua Julai 27, 2024, na akakimbizwa hospitalini, ambapo alipatikana anaugua nimonia.

“Martin alikuwa akiendelea kupata nafuu na alifaa kuruhusiwa kuenda nyumbani. Lakini akaanza kukumbwa na tatizo la kupumua. Kwa bahati mbaya, alifariki dunia Agosti 2, 2024. Baadaye tulifahamu kwamba alikuwa akiugua ugonjwa huo kwa muda na hakuwa ameenda hospitalini kupata matibabu,” akasema Bi Pauline.

Familia na marafiki wanakutana eneo la Chokaa, Kangundo Road-Nairobi kwa Mzee Matthew Komora kupanga mazishi yake.

Msanii mwenzake Japheth Kasanga aliambia Taifa Dijitali kuwa tayari kundi la WhatsApp limeundwa ili kuchanga hela za kusaidia shughuli za kumpumzisha.

Shari Martin anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya muziki nchini, haswa wimbo wake wa ‘Rafiki Pesa’, ambao uliwagusa wengi kutokana na ujumbe mzito.

Katika mahojiano na Taifa Leo Februari mwaka huu, Martin alisifu msukumo wa wimbo wake wa Rafiki Pesa, alioutoa mwaka wa 1998.

Nyimbo za Shari Martin ziliambatana na uzoefu na changamoto za kila siku ambazo vijana hukabiliana nazo.

Alikuwa mpishi stadi na alifanya kazi katika sekta ya hoteli kabla ya kuwa mwanamuziki.

  • Imetafsiriwa na Winnie Onyando