Habari Mseto

Wakulima raha tele Sony Sugar ikilipa deni la Sh1 bilioni


KIWANDA cha Sony, ambacho kimekuwa kikikabiliwa na changamoto, sasa kipo katika mchakato wa kurejesha hadhi yake baada ya kulipa deni kubwa la kihistoria la Sh1 bilioni kwa wakulima wa miwa.

Afisa Mtendaji Mkuu mteule, Martine Dima alisema kuwa malipo ya wiki iliyopita ya deni hilo sasa inawapa ari ya kupambana na changamoto nyingine katika jitihada za kukifufua kiwanda hicho.

Katika malipo ya awali, Hazina ya Kitaifa ilichangia asilimia 92.5, sawa na Sh686 bilioni huku Sh181 bilioni zilizobaki zikilipwa kwa wakulima wa miwa wiki iliyopita.

“Kama kampuni, tuliongezea kiasi hicho kwa Sh125 milioni kutoka kwa mapato tunayokusanya na kupunguza mzigo hadi mapema Juni,” alisema.

Bw Dima alidokeza kuwa kampuni inafanya kazi kwa lengo la kupunguza muda wa wakulima ambao wanasubiri baada ya kuwasilisha mazao ya hadi mwezi mmoja pekee.

“Kama mazao yanayohitaji mtaji na ajira nyingi, hatufai kuwaweka wakulima kwa muda mrefu kabla hawajalipwa kwa kazi yao,” alisema.

Bw Dima aliongeza kuwa mfumo wa malipo unaozingatia aliyeleta miwa kwanza kiwandani umewapa imani wakulima ambao walikuwa wameacha kilimo cha miwa na kukumbati kilimo cha mimea mingine.

“Kampuni imepata ongezeko la kiasi cha tani 15,000 za miwa kila wiki,” Dima alisema.

Hata hivyo, alibainisha kuwa changamoto kubwa bado ni kulipa Sh800 milioni kwa wafanyakazi, deni ambalo limerundika kwa miezi 12 iliyopita.