Habari za Kitaifa

Wanaume wanne wakamatwa kwa kuvizia makazi ya Kiptum

February 14th, 2024 2 min read

NA TITUS OMINDE

WANAUME wanne ambao inadaiwa walivizia nyumbani kwa marehemu mwanariadha Kelvin Kiptum siku nne kabla ya kutokea kwa ajali iliyosababisha kifo chake, hatimaye wamekamatwa. 

Polisi kutoka kituo cha polisi cha Kaptagat walisema kuwa washukiwa walikamatwa baada ya kujiwasilisha kituoni humo wakitumia gari ambalo walikuwa nalo walipofika nyumbani kwa marehemu.

Kiptum aliaga dunia Jumapili usiku kuamkia Jumatatu kupitia ajali ya barabarani katika barabara ya Eldoret-Ravine.

Akithibitisha kukamatwa kwa washukiwa afisa mkuu wa polisi Kaunti ndogo ya Keiyo Kusini Abdullahi Aden amesema Jumatano kuwa washukiwa walifanyiwa mahojiano kabla ya kuhamishiwa hadi makao makuu ya upelelezi CCIO Kaunti ya Elgeyo Marakwet yaliyoko mjini Iten.

“Washukiwa wamekamatwa baada ya kujiwasilisha hapa na baada ya mahojiano mafupi, tumeamua kuwapeleka katika makao makuu ya CCIO mjini Iten,” akasema Bw Aden.

Afisa mkuu wa Polisi Keiyo Kusini Bw Abdullahi Aden akihutubia wanahabari katika kituo cha polisi cha Kaptagat baada ya washukiwa waliovizia makazi ya marehemu Kelvin Kiptum kukamatwa. PICHA | TITUS OMINDE

Afisa huyo hakutaka kuzungumzia zaidi suala hilo japo alisema washukiwa walitambuliwa na babake marehemu ambaye alipiga picha gari ambalo walikuwa nalo walipofika nyumbani kwake.

“Washukiwa na wenyeji wa kaunti jirani ya Uasin Gishu, baba wa marehemu amewatambua,” alisema Bw Aden.

Babake Kiptum, Mzee Samson Cheruiyot, ambaye alifika katika kituo cha polisi alisema gari ambalo washukiwa walikuwa nalo ni sawa na gari ambalo alipiga picha washukiwa walipofika bomani mwake.

“Hili ndilo gari ambalo walikuwa nalo, ndiyo hii picha,” akasema Mzee Cheruiyot huku akionyesha picha aliyopiga akitumia simu yake ya mkononi.

Tayari washukiwa wamefikishwa katika makao makuu ya CCIO mjini Iten.

Washukiwa waliandamana na wakili wao.

Wakati huo huo, familia ya Kiptum imependekeza marehemu kuzikwa mnamo Februari 24, 2024.

“Tungependa kumpumzisha marehemu mnamo Februari 24 lakini tunasubiri kusikia kutoka kwa serikali ikizingatiwa kuwa kulikuwa na pendekezo la kumpa mazishi ya kiserikali,” akasema mtawala mmoja kutoka kata ya Chepkorio ambaye hakutaka kutajwa kwa sababu za itifaki ya serikali.

Kiptum ambaye alikuwa mshikilizi wa rekodi ya mbio za marathon alikuwa akiendesha gari lake aina ya Toyota Premio lenye nambari za usajili KDL 566F akiwa na kocha wake raia wa Rwanda Gervais Hakizamana ambaye pia alipoteza maisha.

Lakini mwanamke kwa jina Sharon Kosgey aliyekuwa na wawili hao alinusurika ambapo alifikishwa hospitalini na kutibiwa.