Habari za Kitaifa

Wandani wa Gachagua sasa wataka ‘BBI’ ifufuliwe kuhusu mshindi wa urais

Na MWANGI MUIRURI August 21st, 2024 2 min read

WANDANI wa Naibu Rais Rigathi Gachagua sasa wanataka hitaji la mshindi wa urais kupata asilimia 50 na kura moja zaidi liondolewe kupitia kura ya maamuzi ya kubadilisha katiba.

Uhusiano kati ya Bw Gachagua na Rais William Ruto umeendelea kudorora hasa baada ya mawaziri wanne kutoka ODM kuteuliwa serikalini.

Matakwa haya yamefasiriwa kama yanayolenga uongozi wa nchi baada ya uchaguzi wa 2027. Viongozi wanaoegemea mrengo wa Bw Gachagua waliandaa mkutano usiku wa Jumapili katika hoteli moja mjini Thika ambapo waliazimia kuwa eneo hilo sasa lazima liamue mkondo litakaouchukua mwaka wa 2027.

Wanasiasa hao walisema kuwa wamechoshwa na tabia ya wandani wa Bw Raila Odinga kuingizwa serikalini na marais wanaotumia kura za eneo hilo kuingia mamlakani.

Mbali na Rais Ruto, mtangulizi wake Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta pia alishirikiana na Bw Raila katika muhula wa pili wa utawala wake.

Aidha, wanataka chama chochote ambacho kitabuni serikali kiwe na asilimia 60 za kura na kikishindwa basi kisheria kiruhusiwe kuunda serikali ya muungano.

Bw Odinga alikuwa katika serikali ya ‘nusu-mkate’ na Rais Mwai Kibaki kati ya 2008-2013 baada ya uchaguzi wa 2007/08 kugubikwa na ghasia.

Masharti mengine ambayo wanasiasa wa Mlima Kenya sasa wanataka yatimizwe kupitia mabadiliko ya katiba ni Afisi ya Kiongozi wa Upinzani kutengewa bajeti na pia rasilimali za nchi zigawanywe kwa kuzingatia idadi ya watu na siyo ukubwa wa maeneo.

Aliyekuwa Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu ambaye sasa ni msaidizi wa kibinafsi wa Bw Gachagua anasema licha ya kuwa bosi wake hakuhudhuria mkutano huo, anaunga mkono yaliyojadiliwa na kuafikiwa.

“Kama mkutano haujaandaliwa kumpiga vita mtu yeyote basi hana tatizo. Mkutano unaolenga kuunganisha watu na kutafuta mwongozo wa kulisaidia eneo letu hauna chochote kibaya,” akasema Bw Wambugu.

Wakili wa Mahakama Kuu Mwangi Kariuki ambaye alinakili yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo alisema kuwa kutakuwa na mikutano mingine ya kushauriana kuhusu mustakabali wa kisiasa wa Mlima Kenya.

“Kwa sasa wanaoshindwa kura wanatumia fujo serikalini lakini tunataka mabadiliko ya kisheria ili hilo liwe rahisi. Kura za Mlima Kenya zimekuwa zikitumika kuwasaidia watu kutwaa uongozi lakini wanapigwa kumbo baada ya baadhi ya watu kutumia fujo kuingia serikalini na hilo husababisha mauti ya raia,” akasema Bw Kariuki.

Kwa mujibu wa Mbunge wa Naivasha Jayne Kihara ambaye alihudhuria mkutano huo, wanalenga kuwashirikisha Gen-Z ili wawe na ushawishi wa kuamua nani ataunda serikali mwaka wa 2027.

Bi Kihara alisema ni mikutano kama hiyo ndiyo ilimsaidia Rais Ruto kupenya ukanda wa Mlima Kenya, Bw Kenyatta alipokuwa mamlakani, huku wanasiasa wa eneo hilo wakimuunga Bw Raila.

Mbunge wa zamani wa Gatanga Nduati Ngugi aliyesema anawakilisha Bw Kenyatta katika mkutano huo, alisema kuwa eneo hilo lazima liungane la sivyo hesabu za kisiasa zitawachenga 2027 na 2032.

Wanasiasa wa Mlima Kenya waaminifu kwa Bw Gachagua wamekuwa wakisema kuwa kuna mipango inayoendelezwa kichinichini na mrengo wa Raia/ Ruto ili kubadilisha katiba na kufungia eneo lao kutawala siasa za nchi.