Habari Mseto

Waombolezaji wavumilia mvua, kibaridi kikali wakimzika mwanajeshi Rose Nyawira

April 25th, 2024 1 min read

NA GEORGE MUNENE 

RISALA nyingi za rambirambi zilitawala hafla ya mazishi ya mwanajeshi Sajini Rose Nyawira Alhamisi ambaye aliuawa kwenye mkasa wa helikopta Elgeyo Marakwet wiki iliyopita.

Nyawira alizikwa katika boma la wazazi wake eneo la Kagio, Kaunti ya Kirinyaga.

Mamia ya waombolezaji wakiwemo Gavana Anne Waiguru, maafisa wa KDF walifika kutoa heshima zao za mwisho.

Walimuomboleza kama afisa aliyejitolea, aliyekuwa na bidii na aliyependa watu ambaye maisha yake yalikatizwa kikatili na kifo kupitia ajali.

Waombolezaji walivumilia mvua kubwa, kibaridi kikali huku wengine wakilia kwikwi wakati wakimzika mwanajeshi huyo hodari.

Familia ilieleza kwamba Nyawira alikuwa mtu mzuri na kwamba kifo chake kitabaki akilini mwao milele.

“Nyawira alikuwa msichana mzuri na mkono wa mauti umemchukua akiwa mchanga mno. Nafurahia mafanikio yake maishani. Tumepata pigo lakini tutasalia imara,”akasema Bw Timothy Kamau, mjomba wa mwendazake.

Bw Kamau alieleza jinsi Nyawira alikuwa na tabasamu usoni kila mara na kwamba hakuwa na uwezo wa uadui wowote.

“Alitabasamu kila mara kama mamake, hangeweza kukosea yeyote, tulimpenda sana na nakumbuka maisha yake yote. Alikuwa nyota na kifo chake ni pigo kubwa kwetu kama familia. Tunaomba Mungu atufariji,” akasema Bw Kamau akipangusa machozi.

Mamake Nyawira, Irene Wanjiku alimsifia bintiye kama aliyekuwa mrembo na mwenye kupendeza wakati wote.

“Kwaheri mwanangu nilikuthamini sana, najua tayari upo mbinguni ukitutabasamia kama kawaida yako. Ulikuwa na mapenzi ya dhati na roho ya utu na nitathamini kumbukumbu zote baina yetu,” akasema.