Kongamano la 2 la Kimataifa la Kiswahili la Jumuiya ya Afrika Mashariki lilivyovuma Mombasa, Kenya
JUMAPILI, Julai 7, 2024 ilikuwa siku maalum kwa wakazi wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa sababu maadhimisho ya tatu ya Siku ya Kiswahili Duniani (SIKIDU) yalifanyika.
Vilevile, Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili lililoasisiwa na Jumuiya ya EAC liliandaliwa kwa usambamba.
Ilikuwa fahari hata zaidi kwa Wakenya kwa sababu sherehe za mwaka huu zilifanyika jijini Mombasa.
Sherehe hizo zilizowaleta pamoja wadau mbalimbali wa Kiswahili kutoka ukanda huu wa EAC na kwingineko Afrika na duniani, zilianza Ijumaa, Julai 5 na zilifikia kilele chake Julai 7.
Mnamo Novemba 23, 2021, wakati wa kikao cha 41 cha mataifa wanachama kilichofanyika jijini Paris, Ufaransa, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), lilitangaza Julai 7 kuwa Siku ya Kiswahili Duniani.
Kutokana na tangazo hilo la UNESCO, Baraza la Afrika Mashariki kuhusu Elimu, Sayansi na Teknolojia, Utamaduni na Michezo, katika kikao cha 17, liliidhinisha Julai 7 kama siku maalumu ya kusheherekea Lugha ya Kiswahili kote ulimwenguni.
Hatua hii ya UNESCO ilikifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN).
Kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni Kiswahili, Elimu na Wingi-lugha katika Ufanikishaji wa Amani ni faafu wakati huu ambapo kuna haja ya kuhubiri amani kutokana na migogoro mingi inayoshuhudiwa katika mataifa mengi duniani. Hivyo basi, siku hii ilitoa wito kwa mataifa yote ulimwenguni kuishi kwa amani.
Kiswahili kina historia pevu na tamaduni za kina, sio ajabu kwamba kinasherehekewa.
Chimbuko la lugha yenyewe
Lugha ya Kiswahili ilijijenga kutokana na mtagusano wa wafanyabiashara wa kigeni na wenyeji wa Pwani ya Afrika Mashariki kati ya Karne ya 11 na 16 (Kabla ya Masihi); na sasa tunajivunia maendeleo na maenezi ya Kiswahili ambacho kimevuka mipaka ya kihistoria kote ulimwenguni.
Utandawazi na utandaridhi ambao umeshuhudiwa katika Bara la Afrika mwanzoni mwa Karne ya 21 una misingi thabiti katika historia ya bara letu kinyume na baadhi ya nadharia potovu kuhusu asili ya ustaarabu wa Afrika ambazo zinafumbia jicho mchango mkubwa wa wenyeji.
Shughuli za biashara ziliimarika katika janibu za Pwani ya Afrika Mashariki kwa kuvutia watu kutoka ughaibuni kama vile Amerika, Indonesia, India, Uhabeshi, Maeneo ya Maziwa Makuu ya Afrika na Uropa walipokuwa wakitagusana.
Hii ilimaanisha kwamba dini na lugha mbalimbali zilitagusana pakubwa na kukuza mawasiliano na mitagusano ya Kiswahili kama lugha iliyowaunganisha watu.
Ustaarubu huu katika maeneo ya Pwani ya Afrika Mashariki unathibitishwa na utamaduni wa kufua vyuma, utengenezaji wa mavazi, shanga, ujenzi wa maeneo ya ukumbusho kama vile misikiti ya mawe, makaburi na makasri pamoja na utengenezaji wa glasi na ufinyanzi.
Ustaarabu huu unatokea Pwani ya Afrika Mashariki takribani kilomita 3,000 kutoka Mogadishu (Somalia) Kaskazini hadi Msumbiji Kusini mwa Afrika.
Masalio mengine yanayothibitisha ustaarabu wa Uswahili ni pamoja na Maeneo ya Turathi za Kimataifa za UNESCO za Mji Mkongwe wa Lamu, Mji wa Mawe wa Zanzibari, Magofu ya Kilwa Kisiwani, Mnara wa Songo na Iha ya Msumbiji.
Ustaarabu huu unazidi kukua katika karne hii ya 21 kupitia mavazi, fasihi simulizi na teknolojia ya baharini ambavyo ni thibitisho la utamaduni wa Waswahili wa Pwani unaopenyeza ukanda wa Afrika Mashariki kijamii na kiuchumi.
Ukuaji wa kijamii na kiuchumi
Katika miaka ya 1950, Umoja wa Mataifa ulianzisha kitengo cha Redio cha Lugha ya Kiswahili cha Umoja wa Mataifa, na leo hii, Kiswahili ndiyo lugha pekee ya Kiafrika katika mamlaka ya Mawasiliano ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa (UN).
Mwanzoni mwa miaka ya 1960, wakati ambamo nchi nyingi za Afrika zilikuwa katika harakati za kujikomboa dhidi ya ukoloni, waandishi na wataalamu wa Kiswahili kama vile Wole Soyinka walianza kutoa wito wa matumizi ya Kiswahili kama lugha ya Bara la Afrika.
Ni wazi kwamba, mwito huu ulitekelezwa kwa sababu, mwaka wa 2004, Umoja wa Afrika (AU) uliidhinisha Kiswahili kama mojawapo ya lugha zake rasmi.
Baadaye, kikao cha 40 cha Baraza Kuu la Umoja wa Afrika kilichofanyika Januari 20 hadi Februari 12, 2022, kiliidhinisha Kiswahili kama lugha ya mawasiliano ya Umoja wa Afrika.
Lugha ya Kiswahili pia ni mojawapo ya lugha rasmi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Kiswahili ni chombo adimu ambacho kimefanikisha Maendeleo Endelevu, Ruwaza ya 2030 na katika mshikamano wa fani mbalimbali hususan katika utekelezaji wa Makubaliano ya Biashara Huru Barani Afrika.
Sherehe za siku ya Kiswahili zilianza mwaka wa 2022. Ziliandaliwa kisiwani Zanzibar na mwaka uliofuatia wa 2023 zikaandaliwa nchini Uganda, Kampala.
Mwaka huu wa 2024, Kenya imeandaa kongamano hilo. Sambamba na sherehe za Siku ya Kiswahili Duniani, nchi hii pia imeandaa Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili jijini Mombasa. Kilele cha sherehe hizi kilikuwa katika ngome ya Fort Jesus, Mombasa. Zilianzia katika hoteli ya Sarova Whitesands.
Kongamano la kwanza la Jumuiya ya Afrika Mashariki lilifanyika mwaka wa 2017 kisiwani Zanzibar.
Kongamano hili lilifunguliwa Rasmi na Waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Turathi za Kitaifa, Mheshimiwa Aisha Jumwa Katana.
Kongamano hili lilileta pamoja wataalamu na wasomi wa Kiswahili katika kuchambua na kujadiliana mada tofauti zinazohusu ukuaji na uendelevu wa lugha ya Kiswahili.
Waziri Jumwa katika hotuba yake alitambua juhudi za wasomi, wakereketwa na wataalamu wa Kiswahili katika kujizatiti na kuhakikisha kuwa lugha hii imepewa taadhima inayostahili.
Bi Jumwa pia aliangazia mada mbalimbali zilizojumuishwa na kujadiliwa kwa undani na wataalamu.
Mada hizi ni pamoja na Kiswahili na Utangamano; Kiswahili na Elimu; Maarifa ya Usalama; Kiswahili na Amani; Kiswahili na Wakimbizi; Fasihi ya Kiswahili; Kiswahili na Vyombo vya Habari; Kiswahili, Amani na Teknolojia ya Kidijitali; Kiswahili, Utangamano na Vyombo vya Habari; Kiswahili, Amani na Maendeleo Endelevu na Kiswahili na Lugha Asili za Afrika.
Kwa taarifa zaidi, bofya hapa.