Habari

Washukiwa wakuu wa biashara ya mihadarati wauawe – Kamishna

June 18th, 2019 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

KAMISHNA wa Kaunti ya Lamu, Joseph Kanyiri amesema ametamani sana kuwa miongoni mwa wabunge wanaotunga na kupitisha sheria, ambapo angeunga mkono na kusukuma kupitishwa kwa sheria ya kuwapiga risasi na kuwaua papo hapo wasambazaji na watumiaji wa mihadarati nchini.

Akizungumza wakati wa kongamano lililowaleta pamoja vijana na mashirika mbalimbali ya kijamii kwenye Ukumbi wa hoteli ya Mwana Arafa mjini Lamu Jumanne, Bw Kanyiri alieleza kutamaushwa kwake na jinsi mihadarati inavyoendelea kuathiri na kuharibu maisha ya vijana wengi eneo la Lamu.

Alisema jambo la kuvunja moyo zaidi ni jinsi walanguzi wa mihadarati wanavyokamatwa na kisha baadaye kuachiliwa kwa dhamana mahakamani, ambapo hurejea kwa jamii na kuendeleza biashara yao mbovu.

Alisema ni bora sheria ipitishwe humu nchini, ambapo wahusika wakuu wa dawa za kuelvya watapewa adhabu ya kifo, ikiwemo kupigwa risasi na kuuawa iwapo watapatikana wakirandaranda na kutangamana na jamii.

Bw Kanyiri aidha aliiomba mahakama humu nchini kuibuka na mbinu mpya ya kuwanyima dhamana wahusika wa mihadarati kwani mbali na kuendeleza biashara yao haramu muda mfupi baada ya kupewa dhamana kortini, wao pia huwa hatari kwa usalama, hasa wa wale wananchi watukufu ambao hupeana taarifa kwa idara ya usalama zinazosaidia kukamatwa kwao.

“Idara ya usalama inafanya kazi kubwa ya kukabiliana na kumaliza janga la mihadarati. Kizingiti kilichoko ni kwamba mahakama zetu zimekuwa zikiwaachilia washukiwa wakuu wa mihadarati kwa dhamana punde wanapofikishwa mbele ya mahakama hizo.

“Ni sawa kwa sheria kutoa nafasi ya dhamana kwa washukiwa lakini omboli langu ni korti zetu kufikiria kuwanyima bondi hasa washukiwa wa dawa za kulevya ili wazuiwe kurudi kwenye jamii kuendeleza biashara yao haramu na hata kuhatarisha maisha ya raia wema wanaotoa habari kwa idara ya usalama kuhusiana na tabia za wahalifu hao,” akasema B Kanyiri.

Aliongezea kwa kuwaomba wabunge katika bunge la kitaifa nchini kupitisha sheria kali kwa wanaojijusisha na biashara ya dawa za kulevya chini, ikiwemo adhabu ya kifo.

“Ningekuwa katika nafasi ya kutunga sheria, ningepitisha sheria ya wahusika wote wa mihadarati wapigwe risasi na kuawa papo hapo badala ya kusumbuka kuwakamata washukiwa na kuwakabidhi mahakama na kisha baadaye wanaachiliwa kurudi kwa jamii kuendelea kuiharibu jamii hiyo kwa mihadarati.

“Hilo linafanya upande wetu wa usalama kulalamikiwa kwamba haufanyi kazi ilhali kazi tunaifanya ipasavyo,” akasema Bw Kanyiri.

Kauli ya kamishna huyo inajiri juma moja baada ya ofisi yake kutoa orodha ya majina ya washukiwa wakuu wanaoaminika kuendeleza biashara ya dawa za kulevya Lamu, ambapo washukiwa hao walitakiwa kujisalimisha kwa polisi kwa hiari.

Washukiwa hao ni pamoja na Kevin Kirui, Kelvin Opiyo, Mohammed Kale, Jackson Kang’ethe, Mwanaisha Hassan, Mwalimu Omar, Ali Hassan Nassir na mshukiwa mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Munar.

Idara ya usalama pia ilitaja vijiji vya Mtangawanda, Tchundwa, Myabogi na Kizingiti, Kaunti ndogo ya Lamu Mashariki na mitaa ya Kashmir, Kandahar, Milano, Wiyoni, Gadeni na Langoni, kaunti ndogo ya Lamu Magharibi kuwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na biashara ya mihadarati huku vijana wengi wakiharibiwa maisha.