Habari Mseto

Wasioamini Mungu wapongeza serikali kulitandika kanisa la Mackenzie kiboko

February 2nd, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

CHAMA cha Wasioamini Mungu Kenya (ASK), kimeishukuru serikali kwa kuliorodhesha kanisa la Good News International Ministries, lake Mhubiri Paul Mackenzie, kama kundi la uhalifu.

Tangazo hilo lilitolewa na Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki mnamo Jumatano.

Kwenye taarifa, chama hicho kilitaja umaskini, kiwango cha chini cha elimu na ibada za makanisa zinazoendeshwa kwa njia ya mtandao kama hali ambazo zimechangia kuongezeka kwa makanisa kama hayo nchini.

“Wakenya wengi wamekuwa wakifika katika makanisa kama hayo wakiwa na matumaini ya kupata kazi, utajiri kati ya mafanikio mengine ya kidunia. Baadhi ya wahubiri, wengine wanaojibandika majina ya manabii au ‘watu wa Mungu’ , wamekuwa wakitumia njia hizo kuwapumbaza wafuasi wao,” kikasema chama hicho kwenye taarifa.

Kupitia kiongozi wake, Bw Harrison Mumia, chama hicho kilisema kuwa ijapokuwa viongozi wa kidini wana jukumu muhimu la kutekeleza katika jamii, hilo halimaanishi kuwapumbaza na kuwahangaisha wafuasi wao.

Mackenzie na watu wengine 94 wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji na ugaidi, kutokana na mauaji tata ya zaidi ya watu 400 yaliyotokea katika eneo la Shakahola, Kaunti ya Kilifi, mwaka 2023.

Mnamo Januari 16, 2024, Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (ODPP), ilisema kuwa baada ya uchunguzi wa kina, imebaini kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashtaka watu hao.

“Baada ya kumaliza uchunguzi wake, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilitukabidhi faili za uchunguzi huo, kubaini ikiwa kuna ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashtaka washukiwa. Baada ya kutathmini kwa kina ushahidi uliowasilishwa kwetu, tumeridhika kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuwashtaki wati hao 95,” ikasema ofisi hiyo.

Kulingana na mkurugenzi huyo, washukiwa hao watafunguliwa mashtaka ya mauaji, mauaji bila kukusudia na kuwashambulia watu na kuwajeruhi kwenye miili yao.