Habari za Kitaifa

Watu 15 waaga dunia katika ajali eneo la Twin Bridge

January 9th, 2024 1 min read

NA MERCY KOSKEI

WATU 15 wameaga dunia huku saba wakijeruhiwa katika ajali iliyotokea Jumanne alfajiri katika eneo la Twin Bridge, Mau Summit katika barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.

Polisi wamesema ajali ilitokea saa tisa alfajiri na ilihusisha matatu ya Northways Shuttle na basi la Classic Kings of Congo.

Kamanda wa Polisi wa Kuresoi Kaskazini Judah Gathenge, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, ambapo ameeleza kwamba walioangamia ni pamoja na watu wazima wanane na watoto saba.

Basi lilikuwa likielekea Nairobi huku matatu ikielekea upande wa Eldoret.

Waliojeruhiwa wamepelekwa katika hospitali ya mjini Molo huku miili ya walioangamia ikipelekwa mochari ya Molo.

Mbali na Twin Bridge, maeneo mengine ambayo ni hatari katika barabara kuu ya Nairobi-Nakuru-Eldoret ni Ngata-Sobea-Salgaa, Migaa, Karai, ambapo watu 40 waliangamia mwaka 2017.

Mengine ni Kinungi, Mbaruk, Gilgil, na St Mary’s katika barabara kuu ya Nakuru-Nairobi.

Pia kuna ukanda wa Gilgil-Nakuru-Kasambara-Kikopey, na sehemu za Timboroa na Makutano katika eneo la Burnt Forest.

Ajali ya Jumanne inajiri mwezi mmoja tu baada ya watu watano kuangamia kwenye ajali iliyotokea eneo la Eveready katika barabara kuu ya Nakuru-Eldoret. Ajali ilihusisha matatu ya abiria 14 na lori la trela katika mzunguko wa Eveready.