Habari Mseto

Wayne Rooney pazuri kumbwaga Rafael Benitez na kuwa kocha mpya wa kikosi cha Derby County

November 20th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

WAYNE Rooney, 35, amesema kwamba atakosa kuwa na maono iwapo hataanza kuwazia fursa ya kuwa kocha mkuu wa kikosi cha Derby.

Nyota huyo wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza amepokezwa kwa muda mikoba ya ukocha kambini mwa klabu ya Derby kwa pamoja na Liam Rosenior, Shay Given na aliyekuwa kocha wa zamani wa chipukizi wa Derby, Justin Walker.

Wanne hao walipokezwa mikoba ya Derby baada ya kuondoka kwa kocha Philip Cocu mnamo Novemba 14, 2020.

Mnamo Novemba 16, 2020, Rooney na wenzake walikutana na mmiliki wa sasa wa Derby County Mel Morris, Afisa Mkuu Mtendaji wa kikosi Stephen Pearce na wawakilishi wa Sheikh Khaled anayepigiwa upatu kuwa mmiliki mpya wa kikosi cha Derby.

Rooney ndiye anayepigiwa upatu wa kumbwaga kocha mzoefu Rafael Benitez katika vita vya kuwania fursa ya kuwa mkufunzi mpya wa Derby kwa mkataba wa kudumu.

Kikubwa zaidi kinachomwaminisha Rooney ni ufanisi unaojivuniwa kwa sasa na wachezaji wenzake wa zamani kambini mwa Uingereza – Steven Gerrard, Frank Lampard na Scott Parker katika ulingo wa ukufunzi wa soka.