Habari za Kitaifa

Wazee waishtaki serikali ya Kaunti ya Homa Bay na kuhatarisha mradi wa Ruto

Na GEORGE ODIWUOR August 29th, 2024 2 min read

SERIKALI ya Kaunti ya Homa Bay imekumbwa na mzozo mpya wa kisheria ambao unaweza kutatiza mradi wa mamilioni uliozinduliwa na Rais William Ruto mapema mwaka huu, 2024.

Baadhi ya wakazi wanaopinga eneo Maalum la Kiuchumi la Riwa huko Rachuonyo Kaskazini, sasa wanadai kuwa serikali ya Kaunti inanyakua ekari 532 za ardhi ya jamii.

Walidai kuwa serikali ya kaunti haikushauriana nao ilipoamua kuanzisha mradi huo.

Bw Ager Kirowo ambaye ni miongoni mwa wakazi walioathirika alisema kuwa kituo hicho kitawanyima wakazi fursa ya kulisha mifugo wao.

“Wakulima wanatumia ardhi hiyo kwa kilimo na ndiyo tegemeo letu la maisha, kikichukuliwa ina maana hatutakuwa na pa kulima,” alisema.

Bw Kirowo alisema kuwa kuwekwa ua kwenye ardhi kutasababisha jamii kufa kwa njaa.

“Itasababisha upatikanaji mdogo wa chakula kwa watu wanaoishi karibu na bustani ya viwanda,” alisema.

Bw Kirowo alidai kuwa serikali ya kaunti ilitumia njia za kutiliwa shaka kupata hati miliki ya ardhi hiyo.

“Hati ya umiliki wa ardhi hiyo bado ilikuwa katika hatua ya awali na wakazi walikuwa na nambari za ploti wakijiandaa kupata hati miliki. Hata hivyo, tulishangaa kujua kwamba serikali ya kaunti ina hati miliki ya ardhi hiyo ambayo ni yetu,” Bw Kirowo alisema.

Kesi iliyowasilishwa mahakamani huenda ikapunguza kasi ya kazi katika eneo hilo la viwanda.

Wakazi wanaozunguka Riwa wamekuwa na vita vya muda mrefu kuhusu umiliki wa kipande kimoja cha ardhi.

Wazee walisema mzozo huo umedumu kwa angalau karne moja.

Wakazi wa koo za Koyugi, Kokoth na Kakdhimu walipigana kudai sehemu hiyo ambayo ilitumiwa tu kwa kilimo na malisho ya mifugo.

Baadhi ya wakazi waliamua kusuluhisha suala hilo mahakamani.

Kesi hiyo iliwasilishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama Kuu ya Kisii mwaka wa 2011.

Ilihamishiwa hivi majuzi katika mahakama ya Ardhi na Mazingira huko Homa Bay.

Mahakama ya kwanza ilikuwa imesuluhisha suala hilo hapo awali kabla ya rufaa kuifufua na kuzuia serikali ya kaunti kutekeleza shughuli zozote katika ardhi hiyo.

Kesi hiyo iliwasilishwa na watu saba wa ukoo wa Kakdhimu ambao wanataka kuzuia serikali ya kaunti na mashirika ya serikali kujihusisha na shughuli zozote katika eneo maalum la kiuchumi.

Walalamishi hao saba pia wanataka hati miliki ya eneo maalum la viwanda la Riwa iliyosajiliwa kwa majina ya serikali ya Kaunti ya Homa Bay ibatilishwe.

Imetafsiriwa na Benson Matheka