Habari za Kitaifa

Waziri Mbadi atoa kima cha Sh40 bilioni kwa idara mbalimbali za serikali

Na WYCLIFFE NYABERI August 22nd, 2024 1 min read

WIZARA ya Fedha imetoa kima cha Sh40 bilioni kwa idara mbalimbali za serikali, ili kufanikisha utendakazi wa serikali.

Bw John Mbadi ndiye Waziri wa Fedha na Hazina ya Kitaifa.

Fedha hizo zimesambazwa kama ifuatavyo:

Idara ya Elimu ya Msingi imepokea Sh1.6 bilioni kufadhili elimu ya bure katika shule za msingi, ilhali Sh 14.1 bilioni zingine zitatumika kwa masomo ya sekondari ya bure katika shule za kutwa.

Kitita kingine cha Sh6.1 bilioni, kimetengewa Idara ya Elimu ya Sekondari Msingi.

Bodi ya Kufadhili Elimu ya Juu (Helb) na Bodi ya Hazina ya Vyuo Vikuu, zimetengema Sh5.1 bilioni na Sh2.8 bilioni, mtawalia.

Idara ya Barabara imepewa Sh2 bilioni huku ile ya Unyunyiziaji imekabidhiwa Sh2.6 bilioni.

Katika kilimo, Bodi ya Mazao na Nafaka (NCPB) itapokea Sh2 bilioni kulipa madeni ya mbolea nafuu katika Mwaka wa Kifedha 2023|2024 kulipokuwa na mvua chache na kubwa.

Shirika la Maziwa (KCC), limepokezwa Sh800 milioni katika Idara ya Mashirika.

Hazina inayolenga kuwainua wafanyabiashara wadogo wadogo, ambayo ilibuniwa na Rais William Ruto alipotwaa uongozi 2022 maarufu kama Hustler Fund, imeongezewa kima cha Sh500 milioni kupiga jeki operesheni zake.

Sh1 bilioni zimetengewa Wizara ya Viwanda ili zitumike katika ujenzi wa Viwanda vya Uzalishaji Mazao ya Kilimo, maarufu kama County Aggregation and Industrial Parks (CAIPS).

Idara ya Uwekezaji, imetengewa Sh600 milioni ili kufaidi shughuli za usindikaji wa bidhaa za kusafirisha nje ya nchi.