Habari za Kitaifa

Wetang’ula ashtakiwa kwa kushindwa kulipa deni la mbwa wawili

Na CAROLINE WANJUGU August 20th, 2024 1 min read

SPIKA wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula amejipata kwenye kikaango moto kwa kukosa kulipa deni la mbwa wawili analodaiwa, kilele chake kikiwa kusukumwa kortini.

Bw Wetang’ula anadaiwa deni la Sh298, 100 kutokana na malimbikizi ya kusambaziwa mbwa wawili aina ya German Shepherd na mafunzo waliyopewa.

Kwenye kesi iliyowasilishwa katika Mahakama ya Milimani, korti inayoshughulikia masuala ya fedha na deni, mlalamishi Isokat Bethwel anadai kwamba manmo Juni 2021, ‘alimuuzia’ Wetang’ula mbwa mwenye umri wa mwaka mmoja, na mwingine wa miezi sita na huduma zingine, chini ya makubaliano.

Kwenye stakabadhi za mashtaka zilizotazamwa na Taifa Dijitali, Bw Bethwel anahoji huduma zote ziligharimu jumla ya Sh348, 100.

Mlalamishi aliambia korti kwamba Bw Wetang’ula alimuomba kuwapa mbwa hao wa ulinzi mafunzo ambapo walikubaliana amlipe Sh50, 000.

Hata hivyo, kulingana na Bethwel makubaliano yao ya Juni 2021 yalifanyika kwa njia ya ‘mdomo’ tu.

Analalamika kuwa Spika Wetang’ula alikataa kutii mkataba wao, unaojumuisha mbwa aliosambaziwa na gharama kuwapa mafunzo.

“Baada ya kujaribu kumfuata, mshtakiwa alilipa Sh100, 000 pekee, akasalia na deni la Sh298, 100…” nakala iliyowasilishwa kortini inasema.

Inazidi kueleza, “Mlalamishi aliendelea kumfikia na kuwasiliana naye ili apate haki yake, ila mshtakiwa alimweleza kwa ukatili na ukaidi kwamba hatamlipa deni lililosalia”.

Aidha, mlalamishi alitumia njia za kisheria, na kumuandikia Spika barua kupitia wakili mnamo Julai 11, 2024, ombi lake likikosa kujibiwa.

Bw Bethwel sasa anaitaka mahakama kuingilia kati, kumsaidia kupata haki – alipwe deni hilo.

Anasema ametatizika kiakili na kimawazo, na endapo korti haitamsaidia, atapoteza jasho lake.

Kesi hiyo, amewakilishwa na Ashioya Mogire na Nkatha advocates, kampuni ya kutoa huduma za uwakili, kufuatia stakabadhi zilizotua kortini Julai 25, 2024, akitaka kulipwa deni la Sh298, 100, ikiwa ni pamoja na hasara aliyokadiria na gharama kufungua kesi.

Imetafsiriwa na Sammy Waweru