Habari MsetoSiasa

Mzee Moi arejea nchini baada ya matibabu Israeli

March 19th, 2018 1 min read

Na WYCLIFFE KIPSANG

RAIS Mstaafu Daniel Moi alirejea nchini Jumamosi usiku baada ya kupokea matibabu nchini Israeli.

Kulingana na taarifa kutoka kwa afisi yake, Mzee Moi aliwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa ndege maalum mwendo wa saa mbili jioni, ambapo baadaye alielekea katika makazi yake ya Kabarnet Gardens, Nairobi.

“Mzee Moi yuko katika hali nzuri. Hata hivyo, madaktari wataendelea kufuatilia hali yake ya afya. Walisema kuwa hayuko hatarini hata kidogo,” ikasema taarifa.

Kiongozi huyo alilazwa katika hospitali ya Ichalov, mjini Tel Aviv Jumapili iliyopita, ambapo alifanyiwa ukaguzi wa kiafya hasa katika goti ambalo limekuwa likimsumbua kwa muda.

Kabla ya kurejea nyumbani, Moi, aliye na umri wa miaka 93, alitembelea maeneo kadhaa ya kihistoria mjini Jerusalem.

Alikuwa ameandamana na daktari wake wa kibinafsi, Dkt David Silverstein na mwanawe Seneta Gideon Moi.

Alionekana mara ya mwisho hadharani mnamo Oktoba 26, 2017 akipiga kura yake katika Chuo Kikuu cha Kabarak wakati wa uchaguzi wa marudio wa urais. Lakini kinyume na chaguzi za hapo awali, alipigia kura katika gari lake.

Mzee Moi amekuwa akiendesha maisha yake kimya kimya katika makazi ya Kabarak, ambapo amekuwa akipokea jumbe mbalimbali.

Mnamo Januari, 27, 2017 alifanyiwa upasuaji wa goti katika hospitali ya Aga Khan, Nairobi. Matatizo ya goti hilo yalianza 2006 alipopata ajali wakati katika eneo la Rukuma View Point, Limuru.

Bw Moi alikuwa akirejea nyumbani kwake Kabarak kutoka Machakos, baada ya kuhutubu katika hafla ya kuhitimu kwa mahafala katika Taasisi ya Mafunzo ya Kidini ya Scotts.

Mnamo Juni, 5, 2000 Moi alihusika katika ajali nyingine ya barabarani katika eneo la Museum Hill, Nairobi. Aliongoza Kenya kama rais kwa miaka 24, kati ya 1978 na 2002.

Aling’atuka uongozini mnamo 2002 baada ya Kanu kushindwa vibaya kwenye kinyang’anyiro cha urais na muungano wa Narc, ulioongozwa na Rais Mstaafu, Mwai Kibaki.