Habari Mseto

SHAIRI: Ushairi tujifunze, tupate kuumaizi

April 2nd, 2018 1 min read

Na KULEI SEREM

Istilahi za shairi, zimepangwa kwa mpororo, 
Mishororo ni mistari, kama kamba na nyororo,
Wengi wanatahadhari, ila ni jambo jororo,
Ushairi tujifunze, tupate kuumaizi.

Mistari ina vipande, wahitaji kumaizi,
Sikizeni chondechonde, mambo ni ya waziwazi,
Ukwapi kwanza kipande, utao na mwandamizi,
Ushairi tujifunze, tupate kuumaizi.

Sitasahau ukingo, ndicho kipande cha mwisho,
Hili ni la mwitu gongo, nitasema kwa fupisho,
Nisemayo si uongo, ni mazuri mafundisho,
Ushairi tujifunze, tupate kuumaizi.

Tukija kwenye ubeti, fungu moja la shairi,
Naomba mjizatiti, msijione mahiri,
Muweze kutofauti, kuna wa vina urari,
Ushairi tujifunze, tupate kuumaizi.

Tuangazie mizani, ni ya silabi idadi,
Tunazama ndanindani, nyuma kamwe haturudi,
Tuzifuate kanuni, kwa hilo hatuna budi,
Ushairi tujifunze, tupate kuumaizi.

Wengine wajiuliza, vipi nako kwenye vina,
Wacheni kujiumiza, vichwani mnajikuna,
Mimi nitawaeleza, silabi nazofanana,
Ushairi tujifunze, tupate kuumaizi.

Mishororo ina vyanzo, chemichemi zake mito,
Ni zile za beti nyenzo, kama kuni kwenye moto,
Ule kwanza ndio mwanzo, wa pili ndio mloto,
Ushairi tujifunze, tupate kuumaizi.

Katika beti mleo, ni mshororo wa tatu,
Kote kule maeneo, wafaa kujua watu,
Ya baharini komeo, ndio ushairi wetu,
Ushairi tujifunze, tupate kuumaizi.

Arudhi ni maagizo, kanuni huzingatiwa,
Mshororo kibwagizo, betini unarudiwa,
Kutuo pia ni wazo, ni ule usorudiwa,
Ushairi tujifunze, tupate kuumaizi.

Nini maanake toni, muwe ange kusikia,
Neno hili silo geni, mbona mnaliwazia,
Iwapenye akilini, za mshairi  hisia,
Ushairi tujifunze, tupate kuumaizi.

Sabilia ni shairi, lisilo na kibwagizo,
Msiseme nakariri, ninatilia mkazo,
Za ushairi bahari, ni nyingi sana kunazo,
Ushairi tujifunze, tupate kuumaizi.

Ninawaaga jamani, kwa mahadhi ya sauti,
Iwanate akilini, kama pembe zake nyati,
Haya yamo vitabuni, endelea kutafiti,
Ushairi tujifunze, tupate kuumaizi.

MALENGA KULEI SEREM