Habari

Ruto ameanza kampeni rasmi?

May 10th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais Dkt William Ruto ameanza kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022 huku akitumia mbinu sawa na alizokuwa akitumia mlezi wake wa kisiasa Rais mstaafu Daniel Moi.

Dkt Ruto alianza siasa chini ya mabawa ya Rais Moi akiwa mmoja wa viongozi wa vijana wa chama cha Kanu.

Miongoni mwa mbinu alizokopa kutoka kwa Moi ambazo amekuwa akitumia katika siku za hivi majuzi, ni kualika jumbe za makundi mbali mbali na watu wenye ushawishi mashinani kutoka maeneo mbali mbali nchini katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi na nyumbani kwake Sugoi, Kaunti ya Uasin Gishu.

Wakati wa utawala wake, Moi alikuwa akikutana na jumbe hizi katika Ikulu na nyumbani kwake Kabarak, Kaunti ya Nakuru.

Kupitia jumbe hizo, Moi alijenga umaarufu wake hadi mashinani huku akijivumisha kupitia shirika la utangazaji la serikali na utawala wa mikoa.

Japo anasisitiza kuwa, kwa kukutana na jumbe hizo na kuzuru maeneo tofauti anatekeleza majukumu yake kama Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya, wadadisi wanasema kwamba, jumbe hizo ni sehemu ya kampeni zake za urais kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

“Dkt Ruto anataka kujenga mtandao mpana wa washirika waaminifu kwake kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022. Hataki kuacha nyuma yeyote au sehemu yoyote nchini na anaendelea kuimarisha mbinu zake,” asema mdadisi wa masuala ya kisiasa Tom Maosa.

Dkt Ruto alikumbatia mbinu hii kikamilifu baada ya kuhisi kuwa, huenda maafisa wa utawala wa mikoa na usalama walikuwa na maagizo ya kutodumisha usalama katika mikutano aliyokuwa akiandaa kote nchini.

Hii ni kutokana na hali iliyotokea katika hafla moja aliyohudhuria kaunti ya Nyeri, maafisa wa polisi walipokosa kufika. Washirika wake wa kisiasa walilaumu maafisa wakuu katika Wizara ya Usalama wa Ndani.

Dkt Ruto amekuwa akikumbatia viongozi wa kidini, kuandaa mikutano ya harambee na kutambua wanasiasa maarufu wa kuendeleza ajenda yake katika kila eneo jinsi Moi alivyokuwa akifanya kwa miaka 24 aliyotawala Kenya.

Wanasiasa ambao ametambua wamepachikwa jina la Tanga Tanga kwa kuandamana naye maeneo tofauti.

Miongoni mwao ni mbunge wa Kikuyu Kamau Ichungwa, mwenzake wa Malindi Aisha Jumwa na Didimus Barasa wa Kimilili na Dkt Boni Khalwale.

Katika kila mkutano anaohudhuria, Dkt Ruto amekuwa akiwataka viongozi kuhubiri amani na kuzingatia maendeleo. Hata hivyo, wafuasi wake wamekuwa wakimpigia debe wakisema ndiye anayefaa kuongoza Kenya baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu 2022.

Dkt Ruto amekutana na jumbe, zikiongozwa na wanasiasa wanaomuunga mkono kutoka Nakuru, Kisii, Kakamega, Kiambu, Meru, Bungoma, Nyeri na kaunti za Kaskazini mwa Kenya miongoni mwa maeneo mengine.

Aidha, amekutana na makundi na viongozi wanawake na vijana.

Ametembelewa na viongozi wa madhehebu tofauti ambao wameunga michango ambayo amekuwa akitoa kusaidia makanisa na miradi ya serikali licha ya wapinzani wake kumlaumu.

Waliohudhuria mikutano hiyo wanasema, huwa wanaandaliwa mlo na kuburudishwa vilivyo. Yakiwa makazi yake rasmi, mikutano hiyo hugharimu mlipa ushuru mamilioni ya pesa kupitia bajeti ya ofisi ya Rais.

Bi Jumwa ambaye ameibuka kuwa mmoja wa wafuasi wake sugu, anasisitiza kwamba Ruto atakuwa Rais 2022.

“Hatuwezi kusimamisha jambo ambalo wakati wake umefika. 2022, kwa mapenzi ya Mungu, itakuwa ni zamu yake William Ruto,” Bi Jumwa amekuwa akisema.

Wazi

Mbunge mmoja kutoka eneo la Magharibi ambaye amehudhuria mikutano kadhaa aliambia Taifa Leo kwamba, Dkt Ruto huweka bayana nia yake ya kugombea urais 2022.

“Katika mkutano mmoja, aliambia waliohudhuria kwamba anataka wawe mabalozi wake kwenye safari ya kuelelea Ikulu 2022,” alisema mbunge huyo ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Seneta mmoja mwandani wa Dkt Ruto pia alidokeza kuwa akiwa mwanasiasa mwenye azima kuu, naibu rais hawezi kuepuka siasa za 2022 anapokutana na jumbe tofauti.

“Naibu Rais ni mcha Mungu na huwa anaita viongozi wa kidini awasikilize na kumuombea ili wabariki safari yake ya kuelekea Ikulu 2022,” alisema.

Kasisi mmoja alisema waliombwa na naibu rais kuzuru boma lake kwa ajili ya kumuombea na taifa kwa jumla wala mkutano huo haukuwa na maudhui ya siasa za 2022.

“Iwapo kulikuwa na siasa katika boma hilo, basi hiyo siasa ilikuwa matamshi ya naibu rais ya kutilia mkazo kwamba ataendelea kutoa sadaka kanisani kwa lengo la kubarikiwa na Mungu licha ya wapinzani wake kukosoa tabia yake ya ukarimu kwa makanisa,” alisema kasisi husika.

Kulingana na mbunge wa Nyeri Mjini, Bw Ngunjiri Wambugu, japo Ruto mwenyewe amekuwa akijaribu kuepuka kuzungumzia kampeni katika mikutano anayoandaa, wafuasi wake katika wamekuwa wakimpigia debe.

Hata hivyo, Bw Wambugu anasema kwa kufanya kampeni za mapema wabunge hao hawamsaidii Bw Ruto.

Mbunge wa Cherangany Joshua Kutuny alitaja hatua ya Naibu Rais kualika makundi ya watu katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi kama “siasa za ugali”.

“Namuomba rafiki yangu Naibu Rais kuachana na siasa hizo za enzi za zamani ambapo Rais alikuwa akiwaalika Ikulu wanasiasa fulani kula ugali ili wafuate misimamo yake. Hizi ni siasa zilizopitwa na wakati,” akaambia Taifa Leo.

Vilevile, Bw Kutuny alisema Dkt Ruto amekumbatia mtindo huo wa kualika watu nyumbani kwake Karen, Nairobi ili kubuni marafiki wake.

Na Mbunge Maalumu Maina Kamanda alisema ni makosa kwa Naibu Rais kufuja ‘rasilimali za umma’ na muda wake kualika watu katika makazi yake.

Alimshauri Ruto kutii agizo la Rais Uhuru Kenyatta kwa kukomesha kampeni hizo ambazo hazina maana,” mbunge huyo akaamba Taifa Leo kwenye mahojiano ya simu.