MWANASIASA wa NASA, Miguna Miguna (aliyevaa kofia) akiwa katika Mahakama ya Kajiado jana asubuhi. Bw Miguna alionekana kwa mara ya kwanza alipofikishwa katika mahakama hapo jana, siku tano baada ya kukamatwa na polisi. Picha/KANYIRI WAHITO

Mahakama yaagiza polisi wasinase wakuu wa NASA

 

MWANASIASA wa NASA, Miguna Miguna (aliyevaa kofia) akiwa katika Mahakama ya Kajiado jana asubuhi. Bw Miguna alionekana kwa mara ya kwanza alipofikishwa katika mahakama hapo jana, siku tano baada ya kukamatwa na polisi. Picha/KANYIRI WAHITO
MWANASIASA wa NASA, Miguna Miguna (aliyevaa kofia) akiwa katika Mahakama ya Kajiado Februari 5, 2018 asubuhi. Bw Miguna alionekana kwa mara ya kwanza alipofikishwa katika mahakama, siku tano baada ya kukamatwa na polisi.
Picha/KANYIRI WAHITO

Na RICHARD MUNGUTI na WANDERI KAMAU

VIONGOZI wa NASA waliokuwa kwenye hatari ya kukamatwa na polisi kuhusiana “uapisho” wa kinara wao Raila Odinga kama “rais wa wananchi” walipata afueni Jumanne baada ya Mahakama Kuu kuagiza Serikali isiwatie mbaroni.

Jaji Luka Kimaru alitoa agizo hilo baada ya kuelezwa na wakili Nelson Havi kwamba polisi wamekuwa wakiwawinda viongozi hao kwa nia ya kuwatia nguvuni. Viongozi hao ni pamoja na Seneta wa Siaya James Orengo, Gavana Hassan Joho wa Mombasa, Seneta Cleophas Malala wa Kakamega, Afisa Mkuu wa ODM Oduor Ogwen na mwenzake wa NASA Norman Magaya, David Ndii na Jimmy Wanjigi.

Wengine walio kwenye orodha hiyo ni wabunge Simba Arati (Dagoreti Kaskazini), Gladys Wanga (Homa Bay), George Aladwa (Makadara), , Babu Awino (Embakasi Mashariki).

Viongozi hao walikimbia mahakamani kuomba walindwe dhidi ya kukamatwa kufuatia misako iliyoanza dhidi ya wahusikan wakuu kwenye hafla ya “kuapisha” Bw Odinga.

Kati ya waliokamatwa kufikia sasa ni Mbunge wa Ruaraka TJ Kajwang’, Miguna Miguna na Mbunge wa Makadara George Aladwa.
“Walalamishi wanaishi na wasiwasi baada ya kupashwa habari kwamba wanasakwa ili wazuiliwe kwa kuhudhuria hafla ya kumwapisha Bw Odinga kuwa ‘rais wa wananchi’,” Bw Havi alimwambia Jaji Kimaru.

Jaji aliwapa viongozi hao dhamana ya Sh100,000 kila mmoja lakini akawataka wajisalamishe katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi (DCI) hapo kesho kuwasaidia wachunguzi katika upelelezi wao.

Katika mahakama nyingine, Wabunge wa mrengo wa NASA wapatao 141 nao walipata afueni baada ya Idara ya Polisi kuagizwa kuwarudishia walinzi na bastola walizokuwa wamepokonywa kuhusiana na msimamo wao wa kupinga Serikali.

Jaji Roselyn Aburili alisema kwamba hofu ya wabunge hao kwamba maisha yao yalihatarishwa na kupokonywa silaha na walinzi ni ya kweli.

Agizo hilo lilitolewa kwenye kesi ambapo Mbunge wa Homa Bay mjini Bw Peter Kaluma alikuwa amewashtaki Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Joseph Boinnet, bodi ya kuruhusu wanaomiliki silaha na katibu wa bodi hiyo Bw Samuel Kimaru akipinga kupokonywa bastola pamoja na walinzi.

Bw Kaluma alikuwa ameomba korti ifutilie mbali uamuzi huo na kuamuru warudishiwe walinzi na silaha. Serikali ilitwaa silaha za wabunge hao kwa madai walishiriki katika shughuli haramu ambapo Bw Odinga “aliapishwa” katika bustani ya Uhuru Park Jumanne wiki iliyopita.

Wabunge hawa walisema ni kinyume cha sheria na haki kunyang’anywa silaha na walinzi pasipo na arifa.

 

Kupokonywa paspoti
Matukio ya Jumanne yalijiri huku serikali ikifutilia mbali paspoti za viongozi kadhaa wa NASA kwa kushiriki katika hafla ya “kumwapisha” Bw Odinga kama “rais wa wananchi” wiki iliyopita.

Viongozi walioathiriwa na hatua hiyo ni mwenyekiti wa kamati tekelezi ya NASA Dkt David Ndii, Seneta Orengo, Gavana Joho, Bw Wanjigi na aliyekuwa seneta wa Machakos Johnstone Muthama.

Kwenye barua walizotumiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji, Jenerali Gordon Kihalangwa Jumanne, wanne hao waliagizwa kuwasilisha paspoti zao kwa idara hiyo katika muda wa siku 21 zijazo.

“Kulingana na Sheria ya Uhamiaji nchini mmeagizwa kuwasilisha paspoti zenu kwa idara hii mara moja,” akasema Jenerali Kihalangwa.

Na ijapokuwa barua hizo hazikueleza sababu halisi ya hatua hiyo, viongozi hao walionywa kuhusu “hatua kali” ikiwa hawatafanya hivyo. Hata hivyo, baadhi ya viongozi walipuuzilia mbali hatua hiyo.

Kwa upande wake, Dkt Ndii alisema kuwa serikali haina sababu yoyote ya kufuta paspoti yake kwani hajafanya kosa lolote.

“Hakuna sababu yoyote iliyotolewa kuhusu hatua hii. Haina umantiki wowote,” akasema Dkt Ndii, kwenye mtandao wa Twitter. Kauli hiyo pia ilitolewa na Bw Muthama aliyesema kuwa hatakubali kutishwa kwa vyovyote vile na Serikali ya Jubilee.

“Hakuna tishio lolote la Jubilee litakalobadilisha msimamo wangu wa kisiasa. Nitabaki imara,” akasema Bw Muthama.

Wiki iliyopita, Waziri wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’i alipiga marufuku vuguvugu la National Resistance Movement (NRM) akilitaja kuwa “hatari kwa usalama wa nchi.”

 

Habari zinazohusiana na hii

Msimu wa talaka

Nasa sinaswi tena

NASA ILIVYONASWA