Kilipuzi cha Al Shabaab chaua maafisa 5 wa KDF Lamu
NA KALUME KAZUNGU
MAAFISA watano wa jeshi la Kenya (KDF) wameuawa ilhali wengine kumi wakijeruhiwa pale gari walimokuwa wakisafiria kukanyaga kilipuzi cha kujitengenezea kinachoshukiwa kutegwa ardhini na magaidi wa Al-Shabaab katika eneo la Sankuri, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki Jumatano.
Akithibitisha shambulizi hilo, Msemaji wa KDF Kanali Paul Njuguna, alisema maafisa hao walikuwa kwenye harakati za kuchota maji na kusambazia jamii eneo hilo wakati gari lao lilipokanyaga kilipuzi hicho majira ya saa mbili asubuhi.
Sankuri ni kijiji ambacho kinapatikana kwenye barabara kuu ya Kiunga kuelekea Hindi.
Bw Njuguna alisema maafisa wa kutosha wa usalama tayari wamesambazwa Sankuri na viungani mwake ili kuwasaka waliotekeleza shambulizi hilo ambao wanaaminika kutorokea kwenye msitu wa Boni.
“Leo majira ya saa mbili asubuhi maafisa wetu kumi wamejeruhiwa kwenye shambulizi la kilipuzi cha kujitengenezea eneo la Sankuri kwenye barabara ya Kiunga kuelekea Hindi.
Tunasikitika kwamba wakati wa shambulizi hilo, maafisa wetu watano waliuawa. Wale waliojeruhiwa tayari wamekimbizwa hospitalini kwa matibabu. Maafisa wetu walikuwa wakitekeleza jukumu la kuchota maji na kusambazia wakazi wakati waliposhambuliwa,” akasema Bw Njuguna kwenye ujumbe wake kwa vyombo vya habari.
Afisa huyo aidha aliwashukuru wakazi kwa ushirikiano wao na pia msaada waliotoa kwa wanajeshi eneo hilo wakati shambulizi hilo lilipotokea.
“Tumefurahia jinsi umma unavyoshirikiana nasi na hata jinsi walivyosaidia wanajeshi wetu punde shambulizi lilipotokea. Waendelee kushirikiana nasi ili kudhibiti usalama Lamu,” akasema Bw Njuguna.
Shambulizi hilo linajiri majuma matatu baada ya wanajeshi wengine sita kuuawa ilhali wengine watano wakijeruhiwa pale gari walimokuwa wakisafiria lilipokanyaga kilipuzi cha kujitengenezea kinachoshukiwa kutegwa barabarani na magaidi wa Al-Shabaab mnamo Agosti 8 mwaka huu.
Shambulizi hilo lilitekelezwa katika eneo la Kwa Omollo kwenye barabara ya Bodhei kuelekea Bar’goni, Kaunti ya Lamu.
Shambulizi la Jumatano ni pigo kubwa kwa maafisa wa usalama wanaoendeleza operesheni ya Linda Boni kwani wakazi tayari wameanza kujihoji sababu kuu zinazopelekea mashambulizi ya kigaidi kuendelea kushuhudiwa mara kwa mara hasa kwenye maeneo husika licha ya operesheni inayoendelea kudumu kwa takriban miaka minne sasa.