• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
Crowe Global yawekeza kwa ‘blockchain’ kuimarisha ushindani

Crowe Global yawekeza kwa ‘blockchain’ kuimarisha ushindani

MILLICENT MWOLOLO na PETER MBURU

KAMPUNI ya ukaguzi na kutoa ushauri wa masuala ya ushuru Crowe Global imewekeza katika teknolojia ya ‘blockchain’ (BT) ili kuimarisha ushindani sokoni.

Kampuni hiyo imesema hatua hiyo inanuia kuchangamsha wateja pale wanaposhirikiana nao na kuhakikisha uadilifu katika biashara zake. Ilisema ikitumika vizuri, teknolojia ya blockchain itainua viwango vya ushindani vya Kenya katika dunia.

‘Blockchain’ ni mfumo wa kidijitali wa kukagua shughuli za kibiashara ambao unaweza kutumiwa kurekodi mambo yote yenye umuhimu, bali na ya kibiashara.

Tangu 2017, teknolojia hiyo imezidi kutumiwa nchini na baadhi ya kampuni za kibinafsi ya za umma, hasa ya usalama, usafiri, afya, bima na sekta ya magari.

Hata hivyo, soko lake nchini linasalia kutoguswa vikubwa, hivyo ikiwa nafasi yake kukua kwa kasi kwani ni kampuni nne tu zimewekeza kwake Jijini Nairobi hadi sasa.

“Tuko tayari kabisa kushauri kuhusu masuala kama hayo kwani kuna njia nyingi za kuyaangalia,” akasema Donald Odera, meneja mshirikishi, mpatanishi wa kimataifa na mshauri katika kampuni ya Crowe & Co Jijini Nairobi.

Awali mwaka huu, Benki Kuu (CBK) ilitahadharisha wafanyabiashara kuhusu BT kwani bado hakujawekwa taasisi yoyote ya kisheria kuongoza utendakazi wake.

Lakini Crowe imesema ina uwezo wa kutoa huduma za mwelekeo na ushauri kwa biashara ambazo zinataka kuwekeza katika BT.

Bw Odera alisema BT itarejesha uwazi na uwajibikaji katika bajeti kwenye sekta za umma na kibinafsi.

“Tumeingia katika ushirikiano ili kujiwezesha kuwahudumia watumizi na watoaji wa huduma za BT na Cryptocurrencies. Huu ndio wakati wa Kenya kuwa mbele katika hilo,” akasema.

Baadhi ya huduma inazopanga kutoa kampuni hiyo ni pamoja na ushauri kuhusu miundomsingi, kuhusu BT, namna ya kuzuia hatari za kimitandao na mengine.

Kampuni hiyo imesema kwa kuingia kwa mfumo huo sokoni, sekta kama za benki zitaadhiriwa kwani zitalazimika kubadili njia za awali za kuendesha shughuli zake.

Mataifa kama Uholanzi yameshuhudiwa kufanikiwa kwa mfumo huo, huku ukipanua nafasi za mapato.

“Kutokana na kuwa na uwazi na uwajibikaji, mfumo huu utazifaa serikali kuu na za kaunti kupunguza ufisadi,” akasema Bw Odera.

You can share this post!

Wanafunzi wadaiwa kumuua mwalimu kwenye purukushani za baa

Paa za majengo ya ubalozi wa Kenya ughaibuni zimetoboka...

adminleo