• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
JAMVI: Yatarajie haya Raila na Ruto wakimenyana debeni 2022

JAMVI: Yatarajie haya Raila na Ruto wakimenyana debeni 2022

Na MWANGI MUIRURI

BAADA ya wandani wa Kinara wa ODM, Raila Odinga kutangaza kuwa atawania urais 2022, kinyang’anyiro kikali kati yake na Naibu wa Rais, William Ruto kinanukia.

Wakiongozwa na Seneta wa Siaya, James Orengo wandani hao walisema kuwa hakuna cha kumzuia Odinga kuwa katika debe la urais 2022, huku naye Ruto akijitokeza hadharani kutangaza kuwa atamenyana naye kwa hali na mali.

Ni kinyang’anyiro ambacho kikiwadia, kitatifua kivumbi cha kipekee, wadadisi sasa wakisema kuwa sio vigumu kutabiri mshindi.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Prof Makau Mutua, hakuna vile Ruto anaweza akaibuka na ushindi akijipata katika ushindani na Odinga.

Lakini kwa mujibu wa mdadisi mwingine, Gasper Odhiambo ambaye ni mhathiri wa Somo la sayansi ya kisiasa, Odinga kuwindana na Ruto ni sawa na kumkabidhi naibu huyu wa rais ushindi wa moja kwa moja.

Hao wawili wakihitilafiana kimaoni, naye mchanganuzi wa kisiasa, Prof Ngugi Njoroge anasema kuwa kati yao wawili, kuna masuala mengi ambayo yatachangia kuamua mshindi atakuwa ni nani.

 

Uzoefu wa ‘Baba’

Prof Mutua anasema kuwa Odinga ataibuka mshindi kwa kuwa ako na tajiriba ya kuwania, ako na mitandao hapa nchini na ng’ambo kuhusu siasa na ni mweledi wa kupanga siasa za kukemea “walio na tabia kama za Ruto.”

Anashikilia kuwa wale wote ambao wamekuwa katika mrengo wake wa kisiasa wakiwa ni pamoja na Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula watajipata tu wamerejea katika merikebu ya Odinga kisiasa kwa kuwa wanajifahamu vyema kuwa hawana lao bila Odinga katika kambi yao.

Anasema kuwa uwezo kamili wa Odinga uko katika eneo la Magharibi “ambapo hata eneo hilo liwanie urais, wapiga kura wa eneo hilo bora tu Odinga ako kwa uwaniaji, watasusia wao na wampigie kura Odinga.”

Anasema kuwa Odinga ni mtetezi wa wanyonge nchini ambao ndio wenye hifadhi kubwa ya kura, anajipa guu mbele kimaeneo na historia yake ya kutetea demokrasia idumishwe itamweka pazuri.

Anasema kuwa ukigawa maeneo yote manane yaliyojumuika kama mikoa kabla ya kubadilishwa na mfumo wa ugatuzi na kubandikwa majina ya Kaunti, Odinga ako na guu mbele.

“Sio siri kuwa Odinga atatwaa Nairobi, Nyanza, Pwani, Magharibi, na Kaskazini Mashariki na kisha aibuke wa pili bila kupoteza kwa kura nyingi katika eneo la Mashariki. Ruto atwae Rift Valley na Kati mwa nchi. Ukijumuisha hesabu hiyo, mshindi wa moja kwa moja ni Odinga,” anasema.

Lakini Bw Odhiambo anasema kuwa hiyo ni hesabu ya dhana tu bila kuzingatia uwezo kamili wa Ruto kisiasa.

Anasema kuwa udadisi wake ni kuwa Ruto amejipa ukwasi wa kumwezesha kuteka Pwani, Kaskazini Mashariki, Nyanza atwae jamii ya Abagusii na hatimaye azidishe kura za Rift Valley na Mlima Kenya kuibuka na ushindi.

 

Injini ya Rais Kenyatta

“Ruto ndiye injini ambayo imemuweka rais Uhuru Kenyatta mamlakani katika uchaguzi wa 2013 na 2017. Ukitoa mchango wa Ruto katika hesabu ya serikali ya Jubilee, Odinga angekuwa rais anayekamilisha awamu yake ya pili kwa sasa,” asema.

Anashikilia kuwa Odinga alifanya makosa makuu ya kisiasa kutalakiana na Ruto baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 na ambapo ni wazi kuwa wangekwamiliana pamoja, Odinga angeibuka mshindi kwa urahisi.

Anasema kuwa ikiwa Ruto atasikizana na wapiga kura wa Mlima Kenya na awape unaibu wa urais, kisha agawe kura za Magharibi, hatimaye azindue siasa za jadi Mlima Kenya za kususia uwaniaji wa mgombezi wa Luo Nyanza, ushindi utakuwa wake.

Anasema kuwa ukitaka kuona jamii za Mlima Kenya kote nchini zimejitokeza zikiandamana na wagonjwa, walemavu na hata wafu wao kupiga kura, basi orodhesha Odinga katika kura hiyo ya urais.

Anasema kuwa ikiwa rais Kenyatta atatimiza ahadi yake ya kumuunga mkono Ruto 2022, basi “Odinga ajiandae kupangiwa zile njama tu ambazo amekuwa akikumbana nazo mikononi mwa mtandao wa Mlima Kenya ambao husemwa hununua ushindi kwa kila hali na mali.”

Anamkumbusha Odinga kuwa muungano wa Rift valley na Mlima Kenya ndio umemfungia nje ya ushindi 2013 na 2017 na hakuna ishara ambayo inajipa uhakika wa kubadilika 2022.

Hata hivyo, Prof Njoroge anasema kuwa imani kwa serikali inazidi kudidimia kiasi kwamba huenda 2022 kuzuke ususiaji mkuu wa upigaji kura hasa katika eneo la Mlima Kenya.

“Katika ushirika wa sasa wa Odinga na rais Kenyatta, watu wa Mlima Kenya ambao wanafahamika vyema na ujasiriamali wameshuhudia uthabiti ambao hata kwa wakosoaji sugu wa siasa za ODM, wanafurahia hatua ya salamu za maridhiano za Machi 19. Ni ushirika ambao umepanua mianya ya biashara na pia siasa za vurugu kutulia,” asema.

Anasema watu wa Mlima Kenya wamelegeza kamba kwa kiwango kikuu dhidi ya Odinga na huenda wasiwe na zile hisia za kujituma kumfungia nje ya kura 2022. Anaongeza kuwa kwa sasa Ruto ako na mengi ya kutimiza katika kujipakia upya kama mgombezi mwafaka wa urais.

 

Hasira, vitisho na mwizi wa mali ya umma

“Amejulikana kama mwanasiasa wa hasira, anayedhaniwa kuwa mwizi wa rasilimali za umma na pia anayehusishwa moja kwa moja na dhana kuwa huenda alichangia pakubwa kero la wakimbizi wa ndani katika ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Anajulikana kama anayetumia vitisho kujaribu kutwaa uungwaji mkono Mlima Kenya, suala ambalo linawafanya wengi kutaka kumkaidi ili waone ni lipi anawezaakatekeleza katika mazingara ya kuhatarisha Uhuru wake katika mahakama ya ICC kwa mara ya pili,” asema.

Katika hali hiyo, Prof Njoroge anasema kuna uwezekano mkubwa Odinga aibuke na ushindi ikiwa Ruto atalemewa kujiosha dhana hizo za ukatili wa kijamii, kisiasa na kiuchumi lakini mambo yabadilike kumfaa iwapo atafanikiwa kujitakasa.

Anaonya kuwa hesabu ya Odinga huwa na upekee ikizingatiwa kuwa wanaokiri imani yao ya kisiasa kwake, hata uwafanyie nini, uwachinjie au uwaleweshe, hawawezi wakang’atuka kutoka msimamo wao.

Nao wale ambao humchukia, au kumuogopa, hata uwafanyie nini, hawawezi wakabanduka katika ukaidi wao kwake.

Anasema hatari kuu ya siasa za Odinga ni kuwa huchachawisha safu ya kisiasa na usipokuwa makini, atakuandama kwa propaganda na ukwasi wa misamiati katika jukwaa la kisiasa.

Vile vile, anasema kuwa siasa za Ruto huwa sawa na haki jangwani ambapo ukatili, propaganda na ueledi wa kiuesmi ndio nguzo zake muhimu.

“Ukiangalia uchambuzi huo kuwahusu hawa wawili, hakuna wa kusukumika pembeni kwa urahisi na hiyo ndiyo taswira mimi nitasema itakumba siasa za 2022 ikiwa hawa wawili wataishia kuwa wagombezi wawili wakuu wa urais,” asema.

Odinga alizaliwa Januari 7, 1945 huku Ruto akizaliwa Desemba 21, 1966 tofauti yao kimiaka ikitarajiwa pia kuzua mjadala kuhusu ufaafu wa kila mmoja wao kuibuka rais wa tano nchini Kenya.

Kitaaluma, Odinga ni mhadisi huku Ruto akiwa na shahada kuhusu masuala ya mimea na wanyama

You can share this post!

TAHARIRI: Juhudi hizi nzuri za Uhuru zipigwe jeki

Sofapaka yabandua Tusker SportPesa Shield

adminleo