COTU pia yaishtaki serikali kuhusu ushuru wa mafuta
ANITA CHEPKOECH Na PETER MBURU
MUUNGANO wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu) umeishtaki serikali kuhusiana na kulipisha ushuru wa asilimia 16 (VAT) kwenye bidhaa za mafuta, ukidai hali hiyo itafanya maisha kuwa magumu zaidi kwa Wakenya.
Katibu Mkuu wa muungano huo Francis Atwoli alisema walifika kortini kupitia wakili Ekwe Ashiando, wakiitaka iamuru sheria hiyo ibatilishwe ili kuokoa Wakenya wengi ambao wataumia zaidi.
Wameshtaki wizara ya fedha, mamlaka ya kukusanya ushuru (KRA) na tume ya kusimamia sekta ya kawi (ERC) kando na serikali.
“Bei za juu zitasababisha familia nyingi kukosa chakula kutokana na bei ya juu ya vyakula, huku zikiwa watu kutosafiri kutokana na nauli ghali. Hii ni kwa kuwa kila tunachofanya kinatokana na mafuta kwa hali moja ama nyingine,” akasema Bw Atwoli.
Alimlaumu waziri wa fedha Henry Rotich pamoja na hazina ya kimataifa ya fedha (IMF) na benki ya dunia kwa kushirikiana na kufanya maisha magumu kwa Wakenya.
“Lakini tunajua kuwa Jaji yeyote anayeelewa matatizo ya Wakenya atasitisha hatua hii. Tuko kortini ili kuhakikisha kuwa Wakenya hawatumiwi vibaya namna hiyo,” akasema.
Pamoja na viongozi wengine wa wafanyakazi wakiwa Kericho, Bw Atwoli alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati na kuwaokoa Wakenya.
“Tunatarajia kushuhudia gharama ya kazi ikipanda ajabu kufuatia kuongezeka kwa bei ya mafuta, tunamwomba Rais Kenyatta kutuhurumia na kutia saini mswada wa kuchelewesha kutekelezwa kwa sheria hiyo,” akasema Bw Atwoli.