• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Kopa Ruto tulipe deni la Sh5 trilioni, Wakenya wamshauri Uhuru

Kopa Ruto tulipe deni la Sh5 trilioni, Wakenya wamshauri Uhuru

Na PETER MBURU

HATUA ya serikali kutoza Wakenya ushuru zaidi ili kulipia madeni ya Sh5 trilioni iliyokopa na kufadhili bajeti ya Sh3 trilioni sasa imeanza kuwakera wananchi, wakionyesha ghadhabu zao huku wakiionya vikali dhidi ya ukopaji kiholela.

Kero hilo Jumanne lilimwangukia Rais Uhuru Kenyatta alipotuma ujumbe kwenye mtandao wa Twitter kuhusu mradi wa serikali ya Uchina kutoa kitita cha Sh6 trillioni kwa mataifa ya Afrika, ambapo Kenya itanufaika.

Katika ujumbe wake, Rais Kenyatta ambaye amekuwa Uchina kwa kongamano la siku mbili alisherehekea hatua ya nchi hiyo kama ‘sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Uchina na bara la Afrika’.

Lakini Wakenya ambao wamekuwa wakimtaka atie saini mswada uliopitishwa na bunge kuchelewesha kutekelezwa kwa sheria ya kuongeza ushuru wa mafuta tangu bei ya bidhaa hiyo ilipopandishwa Septemba 1 walimvamia, wakionyesha kukerwa na tabia ya ukopaji.

Badala yake, watumizi wa mtandao wa kijamii wa Twitter walimtaka kiongozi wa taifa kutafuta mikopo ya kifedha kutoka kwa naibu wake William Ruto ambaye wanasema amedhihirisha kuwa na pesa kiasi cha haja.

Semi za Wakenya, nyingi zikiwa za kusisimua zilienea mitandaoni baada ya Bw Ruto kubeba Sh10 milioni kwenye mkoba Jumatatu katika kaunti ya Kajiado kununua mbuzi.

Hizi ni baadhi ya hisia za Wakenya mtandaoni:

@UKenyatta alichapisha “Nikiwa na Rais wa Uchina Xi Jinping wakati wa kongamano la ushirikiano wa Uchina na Afrika ambalo lilianza leo. Uchina ilizindua hazina ya $60bilioni kwa maendeleo ya Afrika na mbinu ya kuimarisha ushirikiano na Afrika.”

Lakini Wakenya hawakukawia kumpa wosia wao wa kuhusu walivyohisi.

“Badala ya kuomba Uchina deni, tafadhali zungumza na Ruto. Anaweza kufadhili bajeti ya mwaka huu. Ana tajriba ya kuzalisha pesa,” akaanza @jmwmut.

“Lakini Bw Rais kusema kweli maisha huku Kenya yamekuwa magumu tafadhali usikope pesa zingine, tayari tuna deni kubwa la Uchina…maisha huku hayakaliki,” akasema @Igneous.

Katika mjadala huo uliokua kwa kasi, @MangoPeter alihoji “Badala ya kuwakopa Wachina ambao watatwaa bandari zetu tukishindwa kulipa kama wanavyofanya Sri Lanka na kutufanya watumwa mbona Jubilee isikope pesa hizo kutoka benki isiyo kipimo ya Bw Ruto?”

“Hatutaki hizo pesa, wacha wakae nazo, mafuta yashapanda na mko huko mnaongelea madeni mengine, Wachina wabaki na pesa zao hatuzitaki,” @hillarybarsong akasema kwa ghadhabu.

You can share this post!

Mwanamume aandamana peke yake jijini kupinga bei ghali

Niliumizwa kila sehemu ya mwili, Bobi Wine asimulia...

adminleo